Ticker

6/recent/ticker-posts

BIBLIA INASEMA NINI KUHUSU MAPENZI YA JINSIA MOJA



BIBLIA INASEMA NINI KUHUSU MAPENZI YA JINSIA MOJA 

Kwanza napenda ufahamu kwamba hakuna dhambi mpya. Shetani anachofanya ni kuzihalalisha dhambi zikubaliwe kisheria ili hatua za kibinadamu zisichuliwe dhidi ya watu wanaotenda hayo. Kazi kubwa sio kukemea tu bali ni kuwafundisha watu ili wasiogope tu hatua za kisheria bali wamuogope Mungu. Kutamani tu kufanya dhambi hata kama mtu hajaifanya kimwili, mbele za Mungu ameshaifanya hivyo anatakiwa kutubu ili asiende Jehanamu. Kazi tuliyopewa na Mungu ni kuwasaidia watu WASHINDE KIU YA DHAMBI. Mathayo 5:28,29 “lakini mimi nawaambia, Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake. Jicho lako la kuume likikukosesha, ling'oe ulitupe mbali nawe; kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee wala mwili wako mzima usitupwe katika jehanum.”

Mfano tangu wakati wa Biblia kuna watu walifanya yafuatayo:

1. Kulala na wanyama (bestiality) Law 18:23 “Wala usilale na mnyama ye yote, ili kujitia unajisi kwake; wala mwanamke asisimame mbele ya mnyama ili kulala naye; ni uchafuko.” Kum 27:21 “Na alaaniwe alalaye na mnyama wa aina yo yote. Na watu wote waseme, Amina.”

2. Kulala na ndugu wa karibu (maharimu/incest). Kum 27:20,22 “Na alaaniwe alalaye na mke wa baba yake, kwa kuwa amefunua mavazi ya babaye. Na watu wote waseme, Amina. Na alaaniwe alalaye na umbu lake, binti ya babaye, au binti ya mamaye. Na watu wote waseme, Amina” Dhambi hii ilifanyika katika Kanisa la Korintho na ikahukumiwa I Kor 5:1 “Yakini habari imeenea ya kuwa kwenu kuna zinaa, na zinaa ya namna isiyokuwako hata katika Mataifa, kwamba mtu awe na mke wa babaye.”

3. Watu wa jinsi moja kufanya ngono. Law 20:13 “Tena mtu mume akilala pamoja na mtu mume, kama alalavyo na mtu mke, wote wawili wamefanya machukizo; hakika watauawa; damu yao itakuwa juu yao.” Law 18:22 “Usilale na mwanamume mfano wa kulala na mwanamke; ni machukizo.”

Biblia ya toleo la KJV na NASB katika 1 Kor 6:9 “Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa Mungu? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti,” imetaja maneno effeminate na homosexual yaliyotafsiriwa Kiswahili kama ‘wafiraji’ na ‘walawiti’. Effeminate ni mwanaume anayefanyiwa kitendo cha ngono katika ushoga (the passive male partner/men who are sodomized by other males). Walawiti (homosexuals) ni anayelala na mwanamme kama anayelala na mwanamke (sodomite).

Kwa hiyo ‘effeminate’ ni mtu ambaye alitegemewa kuwa na tabia za kiume badala yake anaonyesha tabia za kike (womanish). Hii ni pamoja na uvaaji. Mungu anachukizwa na watu wanaopenda kuonekana wameumbwa jinsi tofauti na waliyo nayo. Hata kama mume au mke au kiongozi wako hachukizwi, MUNGU ALIYEKUUMBA ANACHUKIZWA. Kum 22:5 “Mwanamke asivae mavazi yampasayo mwanamume, wala mwanamume asivae mavazi ya mwanamke; kwa maana kila afanyaye mambo hayo ni machukizo kwa Bwana, Mungu wako”

KWA NINI WATU WANAJIHUSISHA NA MAPENZI YA JINSIA MOJA:

1. Kufuata ‘ugumu wa mioyo’ bila kuzingatia msingi wa Neno la Mungu

Tabia ya wengi sasa hivi ni kuangalia mazingira badala ya Neno la Mungu. Wengi wamezoea kusema ‘haiwezekani,’ ‘sio rahisi kwa kizazi hiki’. Nk Wewe sio wa kwanza. Mitume walimuuliza Yesu mwenyewe wakimtaka ashushe viwango vya kwenda mbinguni. Mk 10:26,27 “Nao wakashangaa mno, wakimwambia, Ni nani, basi, awezaye kuokoka? Yesu akawakazia macho, akasema, Kwa wanadamu haiwezekani, bali kwa Mungu sivyo; maana yote yawezekana kwa Mungu.” Hata kama wewe unashindwa, wapo ambao wanaweza kwa msaada wa Mungu.

Imefika mahali katika programu za kusaidia watu waache zinaa, dunia inasema njia ya kusubiri hadi mtu aoe na kuolewa (abstinence) imeshindwa. Lakini haijafanyiwa utafiti wa kina. Hata kama ni wachache, wapo kwa vile WANAJITAHIDI. Biblia WENGI HAWATAIONA NJIA NYEMBAMBA. Luka 13:23,24 “Mtu mmoja akamwuliza, Je! Bwana, watu wanaookolewa ni wachache? Akawaambia, Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze.”

Bwana Yesu hakukubaliana na maamuzi ya Musa yaliyopingana na mpango wa Mungu tangu mwanzo kuhusu uumbaji.

Mk 10:4-9 “Wakasema, Musa alitoa ruhusa kuandika hati ya talaka na kumwacha. Yesu akawaambia, Kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu aliwaandikia amri hii. Lakini tangu mwanzo wa kuumbwa ulimwengu, aliwafanya mume na mke. Kwa sababu hiyo mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe. na hao wawili watakuwa mwili mmoja; hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe.”

2. Kushindwa kumtukuza Mungu hata kama unamjua

Rum 1:21 “kwa sababu, walipomjua Mungu hawakumtukuza kama ndiye Mungu wala kumshukuru; bali walipotea katika uzushi wao, na mioyo yao yenye ujinga ikatiwa giza.”

3. Kujiona una hekima sana za ugunduzi na uvumbuzi bila kumjali aliyekuumba

 Rum 1:22 “Wakijinena kuwa wenye hekima walipumbazika.”

4. Kumlinganisha Mungu na viumbe alivyoviumba (kutompa heshima anayostahili)

 Rum 1:23 “wakaubadili utukufu wa Mungu asiye na uharibifu kwa mfano wa sura ya binadamu aliye na uharibifu, na ya ndege, na ya wanyama, na ya vitambaavyo.”

5. Kuachwa na Mungu kiasi cha kudharau ulivyoumbwa kwa thamani – kutojua kwamba huo mwili sio wa kwako, hivyo huruhusiwi kuuchezea unavyotaka 

 Rum 1:24,25 “Kwa ajili ya hayo Mungu aliwaacha katika tamaa za mioyo yao, waufuate uchafu, hata wakavunjiana heshima miili yao. Kwa maana waliibadili kweli ya Mungu kuwa uongo, wakakisujudia kiumbe na kukiabudu badala ya Muumba anayehimidiwa milele. Amina.”

1 Wakorintho 6:20 “maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili yenu.”

6. Kuvamiwa na tamaa mbaya (lust) ya kufanya ngono kinyume na maumbile – hata wanandoa wanaofanya hivi watahukumiwa

Rum 1:26-27 “Hivyo Mungu aliwaacha wafuate tamaa zao za aibu, hata wanawake wakabadili matumizi ya asili kwa matumizi yasiyo ya asili; wanaume nao vivyo hivyo waliyaacha matumizi ya mke, ya asili, wakawakiana tamaa, wanaume wakiyatenda yasiyopasa, wakapata nafsini mwao malipo ya upotevu wao yaliyo haki yao.” 

7. Kumkataa Mungu katika fahamu – kuharibiwa akili

Rum 1:28 “Na kama walivyokataa kuwa na Mungu katika fahamu zao, Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wayafanye yasiyowapasa.”

Mithali 6:32 “Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa; Afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake.”

8. Kushindwa kuiheshimu ndoa takatifu – malazi machafu kwa wanandoa kv kufanya vitendo vya kishoga katika vyumba vya kulala, kulala na watoto wakubwa chumba kimoja, kuruhusu watoto wakubwa wa jinsi tofauti kulala chumba kimoja, kuruhusu mtoto alale na wageni wasiojulikana, kuvaa nguo za aibu mbele ya watoto nk

Ebr 13:4 “Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu.” 

9. Ushawishi na misaada

Mit 7:10,11,21 “Na tazama, mwanamke akamkuta, Ana mavazi ya kikahaba, mwerevu wa moyo; Ana kelele, na ukaidi; Miguu yake haikai nyumbani mwake. 21 Kwa maneno yake mengi na ulaini akamshawishi, Kwa ubembelezi wa midomo yake akamshinda.

10. Roho ya mpinga Kristo - kupagawa na mapepo (ni aina ya mapepo yanayolenga kuumiza moyo wa Mungu aliyemuumba mwanadamu amtukuze)

2 The 2:7-12 “Maana ile siri ya kuasi hivi sasa inatenda kazi; lakini yuko azuiaye sasa, hata atakapoondolewa. Hapo ndipo atakapofunuliwa yule asi, ambaye Bwana Yesu atamwua kwa pumzi ya kinywa chake, na kumwangamiza kwa ufunuo wa kuwapo kwake; yule ambaye kuja kwake ni kwa mfano wa kutenda kwake Shetani, kwa uwezo wote, na ishara na ajabu za uongo; na katika madanganyo yote ya udhalimu kwa hao wanaopotea; kwa sababu hawakukubali kuipenda ile kweli, wapate kuokolewa. Kwa hiyo Mungu awaletea nguvu ya upotevu, wauamini uongo; ili wahukumiwe wote ambao hawakuiamini kweli, bali walikuwa wakijifurahisha katika udhalimu.

UFAFANUZI KUHUSU MAKUNDI HAYA

1. Wasagaji - mwanamke anayemtamani mwanamke mwenzake kimapenzi

2. Mabasha/Mashoga – mwanaume anayemtamani mwanaume mwenzake kimapenzi

3. Wenye jinsi mbili – anaweza kuvutiwa na watu wa jinsia zaidi ya moja na sio lazima kwa wakati mmoja

4. Wasenge – jinsia yao ni tofauti na ya kuzaliwa na inayotafsiriwa na jamii husika – wanaweza kuingiziwa homoni au kufanyiwa upasuaji

5. Wasiotambua kundi lao hasa – Hawavutiwi na jinsia nyingine peke yake – kundi hili halikubaliki sana katika jamii hii. Ina maana wanaendelea kuchunguza wajue wanaangukia upande gani),

6. Wenye tabia za kuzaliwa ambazo zingine ziko nje ya tabia za jinsi yake. Mfano, mtu anaweza kwa nje kuwa mwanamke lakini kwa ndani ana tabia za kiume hata sauti yake ni nzito.

7. Wasiovutiwa kabisa na masuala ya mapenzi

8. Wenye utambulisho wa kijinsia mwingine wowote ambao bado hauwezi kuelezewa kwa maneno

Tabia za aina tofauti ndizo ziliwasababisha wachague nembo ya upinde wa mvua. Hata hivyo tusisahau kwamba hata kama wanatumia upinde wa mvua kama NEMBO yao DUNIANI bado upinde wa mvua ni AGANO LA MUNGU MAWINGUNI – Mungu hataiharibu tena dunia nzima kwa gharika hadi hukumu kwa kila mmoja wetu. Mwanzo 9:15,16 “nami nitalikumbuka agano langu, lililoko kati yangu na ninyi, na kila kiumbe hai katika wote wenye mwili, wala maji hayatakuwa gharika tena kuwaharibu wote wenye mwili. Basi huo upinde utakuwa winguni; nami nitauangalia nipate kulikumbuka agano la milele lililoko kati ya Mungu na kila kiumbe hai katika wote wenye mwili kilichoko katika nchi.”

Hata kama mambo haya yangehalalishwa na serikali zote duniani, Mungu hajayaruhusu na atawahukumu wote wanaoyafanya. Pambana na TABIA kuliko SHERIA kwa vile mambo haya yanafanyika sirini hata kwa wanandoa. Kanisa likinyakuliwa, waliobaki hawataweza kukwepa utendaji wa mpinga Kristo maana atafanya kazi kwa uwezo kamili (full capacity).

Maombi ya wiki hii:

1. Ee Mungu ponya nchi yetu na vizazi vyetu visijiingize kwenye tabia zilizokuchukiza mpaka ukaiangamiza Sodoma na Gomora.

2. Ee Mungu wasaidie viongozi wa nchi yetu wafanye maamuzi sahihi ambayo hayapingani na Maandiko Matakatifu.

Lawi Mshana