Nikiwa katika maombi usiku wa leo, nimeona kwamba shetani anatengeneza silaha katika kiwanda chake kulingana na mtu anayemlenga. Anakusoma kwanza kabla ya kutengeneza silaha itakayoweza kukupiga vizuri. Pengine umetengenezewa panga au risasi au ugonjwa au ukame wa kimaisha au madeni yasiyolipika.
Isa 54:14-17 “14 Utathibitika katika haki; utakuwa mbali na kuonewa, kwa maana hutaogopa; na mbali na hofu, kwa maana haitakukaribia.15 Tazama, yamkini watakusanyana; lakini si kwa shauri langu. Watu wo wote watakaokusanyana juu yako wataanguka kwa ajili yako.16 Tazama, nimemwumba mhunzi avukutaye moto wa makaa, akatoa silaha kwa kazi yake; nami nimemwumba mharibu ili aharibu.17 Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa na kila ulimi utakaoinuka juu yako katika hukumu utauhukumu kuwa mkosa. Huu ndio urithi wa watumishi wa Bwana, na haki yao inayotoka kwangu mimi, asema Bwana.”
Andiko hili lina ahadi nyingi juu ya
ushindi wako kuanzia leo:
1. Haki ya Kristo ndiyo msingi wako wa
kusimama
2. Vinavyokutia hofu vimeondolewa
3. Wanaopambana na wewe wameanguka
tayari
4. Silaha zote kinyume na wewe
zimeharibiwa
5. Maneno ya laana juu yako yamefutwa na
kushindwa
6. Unastahili hivi kwa sababu umehesabiwa haki na u mtumishi wa Mungu (Hupokei kwa vile u mwema sana)
Hata hivyo nimeita moto wa Mungu uteketeze kiwanda hicho pamoja na kuharibu nguvu za mawakala wa shetani ambao amepanga kuwatumia kinyume chako. Uwe na moyo mkuu na kusimama katika Imani ili uuone mkono wa Bwana. Imani yako kwa Mungu imekuokoa. Luka 17:19 “Akamwambia, Inuka, enenda zako, imani yako imekuokoa.”
Maisha yako ya maombi yanahitaji Imani ili yawe na ufanisi na matokeo.
Waefeso 6:16 “zaidi
ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote
yenye moto ya yule mwovu.”
Lawi Mshana