WEWE NI CHOMBO GANI CHA BWANA? JITAMBUE LEO!
2 Timotheo 2:20,21 “Basi katika nyumba kubwa havimo vyombo vya dhahabu na fedha tu, bali na vya mti, na vya udongo; vingine vina heshima, vingine havina. Basi ikiwa mtu amejitakasa kwa kujitenga na hao, atakuwa chombo cha kupata heshima, kilichosafishwa, kimfaacho Bwana, kimetengenezwa kwa kila kazi iliyo njema.”
Katika ‘nyumba kubwa’ (nyumba ya mtu tajiri) kuna vyombo vya aina nyingi kwa makusudi mbalimbali. Vingine vinapewa heshima vingine havipewi. Kuna vinavyotolewa kabatini siku akija mgeni maalum na vingine vinaweza hata kuwekwa popote tu. Tafuta kuwa chombo cha kuheshimiwa na Mungu na sio cha kudharauliwa kwa sababu ya kutawaliwa na dhambi na madhaifu mbalimbali.
Hivi karibuni nikiwa katika maombi nilitafakarishwa na Roho Mtakatifu kwamba tunatakiwa kujitambua sisi ni vyombo gani na kujikubali. Kama wewe ni sahani na unataka kufanya kazi za sufuria, unadhani utaziweza? Unadhani utaleta matokeo mazuri? Au kama wewe ni jaba la kujazwa maji halafu unataka uwe sufuria ya kupikia utastahimili moto wakati umetengenezwa kwa plastiki?
2 Kor 10:12 “Kwa kuwa hatuthubutu kujihesabu pamoja na baadhi yao wanaojisifu wenyewe, wala kujilinganisha nao; bali wao wenyewe wakijipima nafsi zao na nafsi zao, na wakijilinganisha nafsi zao na nafsi zao, hawana akili.”
Biblia inatuonya kuhusu kujilinganisha.
Aliyetuita ndiye anajua amekutengeneza kwa kazi gani na amekupa uwezo gani.
Mtume Paulo alijua ametumwa kwa makundi gani maalum. Kuna kundi au makundi maalum umetumwa kuyajenga kiroho na kijamii. Kuna watu watathamini huduma yako kwa vile umetumwa kwao.
Mdo 9:15,16 “Lakini Bwana akamwambia, Nenda tu; kwa maana huyu ni chombo kiteule kwangu, alichukue Jina langu mbele ya Mataifa, na wafalme, na wana wa Israeli. Maana nitamwonyesha yalivyo mengi yatakayompasa kuteswa kwa ajili ya Jina langu.”
Waefeso 3:7,8 “Injili hiyo ambayo nalifanywa mhudumu wake, kwa kadiri ya kipawa cha neema ya Mungu niliyopewa kwa kadiri ya utendaji wa uweza wake. Mimi, niliye mdogo kuliko yeye aliye mdogo wa watakatifu wote, nalipewa neema hii ya kuwahubiri Mataifa utajiri wake Kristo usiopimika.”
Kila mmoja wetu (na sio watu fulani wachache) ana kiwango fulani cha neema – una kipawa ulichopewa na Mungu kwa ajili yetu. Huna sababu ya kutumika kwa nguvu zako mwenyewe.
Waefeso 4:7,8 “Lakini kila mmoja wetu alipewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa chake Kristo. Hivyo husema, Alipopaa juu aliteka mateka, Akawapa wanadamu vipawa.”
Ukijua ukubwa wa kazi yako, utajua pia umeifanya kiwango gani, umebakiza kiasi gani na utalipwa nini. Mtume Paulo alijua amemaliza kazi na taji gani atapewa.
2 Timotheo 4:7,8 “Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda; baada ya hayo nimewekewa taji ya haki, ambayo Bwana, mhukumu mwenye haki, atanipa siku ile; wala si mimi tu, bali na watu wote pia waliopenda kufunuliwa kwake.”
Maombi ya wiki hii:
1. Ee Mungu nisaidie nijue mimi ni
chombo gani kwako ili nisijaribu kufanya kazi za wengine na kuacha ya kwangu.
2. Ee Mungu naomba unisaidie nijue
nimefanya kiasi gani kazi uliyonipa ili nijue nitautumiaje vizuri muda wangu
uliobaki.
Lawi Mshana