Mwongozo wa jinsi ya kufikiwa na huduma zetu mijini na vijijini
Nimekuwa nikipata mialiko ya kutoa huduma za kiroho na kijamii katika madhehebu mbalimbali. Napenda kutoa mwongozo mfupi hasa hasa kwa ajili ya kushirikiana na madhehebu na huduma za kiroho. Hata hivyo mwongozo huu sio sheria za Wamedi na Waajemi ambazo zilikuwa hazibadili bali katika mazingira fulani tunaweza kutozizingatia inapobidi. Danieli 6:8 “Sasa, Ee mfalme, piga marufuku, ukatie sahihi maandiko haya, yasibadilike, kama ilivyo sheria ya Wamedi na Waajemi, isiyoweza kubadilika.”
Napendelea zaidi kufanya semina za kujenga mwili wa Kristo kwa kuzingatia mambo yafuatayo:
1. Napenda zaidi kufundisha watu wanaoweza kushiriki tangu siku ya kwanza hadi ya mwisho. Niko tayari kufundisha watu 20 wanaoweza kushiriki siku zote kuliko watu 200 ambao kila mtu ana siku yake tofauti anayoshiriki. Najali zaidi ‘matokeo’ na ‘uendelevu’ kuliko ‘ushabiki’ kwa vile najua nitatoa hesabu siku ya mwisho kwa huduma nilizofanya. Masuala nyeti yanahitaji watu wachache wanaopatikana na waliomaanisha kuleta mabadiliko. Ikiwezekana wawe wakomavu wanaoweza kufundisha wengine na sio kujifunza kwa ajili yao wenyewe. 2 Tim 2:2 “Na mambo yale uliyoyasikia kwangu mbele ya mashahidi wengi, hayo uwakabidhi watu waaminifu watakaofaa kuwafundisha na wengine.”
2. Makanisa au madhehebu yanayoandaa semina, yapendekeze mada au masomo ambayo yatajibu changamoto zilizopo katika eneo lao. Hii inaepusha kurudia mambo yaleyale yaliyofundishwa tayari au kuzungumzia masuala ambayo hayana msaada wa moja kwa moja kwao. Sio vizuri kutumia vibaya raslimali tunazopewa na Mungu kwa kuita mtumishi kutoka mbali halafu anapofika anafundisha yaleyale tunayojifunza kila siku.
3. Semina ifanyike katika msimu mzuri ambapo watu hawajatingwa na shughuli muhimu kama vile matukio ya kitaifa mfano, uchaguzi, misimu ya mvua/kilimo au uvunaji, mkutano wa Injili katika makanisa jirani (labda tu kama hawakujua) nk. Sipendi kulaumu watu kwa kutohudhuria wakati ni kipindi cha Mungu cha kilimo ambacho hakijirudii tena kwa mwaka huo.
4. Napenda kufanya semina ambazo uongozi wa jimbo, kanda au dayosisi wametoa kibali au wana taarifa na nafarijika kuona baadhi ya viongozi hao wakishiriki. Hii sio tu kwamba inaepusha migogoro na uzushi lakini pia inarahisisha katika utekelezaji wa mafunzo baada ya semina kwa vile wafanya maamuzi walishiriki au waliwakilishwa. Mungu hapendi kufanya semina ili tu kujaza jedwali kwamba mwaka huu tumefanya semina kadhaa. Mungu anataka matunda ya kudumu. Yohana 15:16 “Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni.”
5. Pale inapowezekana, napenda semina za viongozi ziandaliwe kwa ushirikiano wa madhehebu tofauti yaliyo jirani na yenye utayari huo. Hii inasaidia kuondoa ubinafsi, kuleta umoja wa imani na kuujenga ufalme wa Mungu kwa vile ni vigumu misimamo ya dhehebu moja kutawala.
6. Napenda semina au warsha hasa iliyoandaliwa na madhehebu tofauti isifanyike siku za ibada kuu za madhehebu hayo kv Ijumaa, Jumamosi na Jumapili. Kufanya hivi kutaepusha waumini wa kanisa moja kufuata walimu wageni katika kanisa jingine kwa vile waumini wengi wanavutiwa zaidi kusikiliza wageni kuliko wenyeji hata kama ujumbe ni uleule. Tunapenda huduma yetu ijenge ufalme wa Mungu. Lakini pia mchungaji, katekista au kasisi ataweza kufanyia kazi mafunzo mapema kwenye ibada kuu inayofuata.
7. Semina ilenge mafundisho ya Neno la Mungu na sio mafundisho yanayowagawa watu kimadhehebu (doctrine). Misingi ya imani ya dhehebu itafundishwa na wachungaji katika makanisa yao. Ninakuja kama mwalimu na sio mchungaji. Ndiyo maana sipendi kujitambulisha wala kutambulishwa kwenye semina kama mtumishi wa dhehebu tofauti. Hili halina faida yoyote kwa washiriki wa semina. Lina faida tu kwa waandaaji wa semina.
8. Inapofanyika semina ya dhehebu moja ni vizuri zaidi wakishirikisha matawi mbalimbali hata kama ni kwa uwakilishi wa viongozi tu. Tumeona matokeo mazuri tulipotoa mafunzo katika kambi za wamama na za vijana ambapo washiriki walitoka matawi, parish au sharika tofauti.
9. Kama tumeombwa kutoa mafunzo ya kijamii, tunapenda ushirikishwaji wa watu kutoka dini zote na tunapendekeza mafunzo yafanyike mahali ambapo hakuna maswali (neutral) badala ya kanisani au msikitini kama vile ukumbi wa jamii au shule.
10. Tunaomba kujulishwa maadili ya mahali husika ili kama hayapingani na Neno la Mungu tuyazingatie na kuyaheshimu. Kila kanisa lina taratibu, miiko na utamaduni wake ambapo mambo fulani yanatiliwa mkazo zaidi. Mfano, utaratibu wa ibada, uvaaji nk
Ngoja nikuambie nilichowahi kukutana nacho katika umisheni nje ya nchi:
Mwaka fulani nilienda nchi fulani (sipendi kuitaja) kufanya semina ya viongozi wa dini kwa siku kadhaa za katikati ya wiki. Mchungaji mmojawapo alipogundua kwamba Jumapili inayofuata nitakuwa sijaondoka, akaniomba nikahubiri kanisani kwake. Siku ilipofika akaja kunichukua. Njiani akaniambia, “kanisani kwangu hasimami mtu mwingine madhabahuni isipokuwa mimi mwenyewe maana ni mimi Mungu ameniita kwa kazi hiyo. Kwa hiyo watu watashangaa sana kuona nimekuruhusu wewe usimame leo. Nimekusikiliza katika semina ya viongozi nikaona una kitu kinachoweza kusaidia kanisa letu.”
Ingawa nilishangaa kidogo, alifanya jambo jema sana kunijulisha hata kama msimamo wake ni tofauti na ninaouamini mimi. Huoni kwamba ningemkwaza sana kama ningemuita mtu pale madhabahuni wakati kwake ni mwiko?
Inashauriwa pia hata kwenye nyumba za watu ukikaribishwa sebuleni usikimbilie tu kukaa. Tulia kidogo upate maelekezo, usije ukakalia kiti cha mwenye nyumba ambacho hakikaliwi na wengine bila sababu za msingi. Unaweza kumkosesha amani au kunyanyuliwa na wanaojua taratibu. (Ziko nyumba za aina hii).
Nahitaji sana maombi yako ili niendelee kufanya hii kazi ya ufalme wa Mungu bila hila wala ujanja wowote. 1 The 2:3 “Kwa maana maonyo yetu siyo ya ukosefu, wala ya uchafu, wala ya hila.” 2 Kor 11:13 “Maana watu kama hao ni mitume wa uongo, watendao kazi kwa hila, wanaojigeuza wawe mfano wa mitume wa Kristo.”
Kama una swali au unahitaji ufafanuzi zaidi unaweza kuwasiliana nami kibinafsi kupitia kitufe cha Whatsapp kwenye ukurasa wetu.
Barikiwa
na Bwana.
Dr Lawi Mshana, 0712-924234