Ticker

6/recent/ticker-posts

Mimi ni mjane mwenye watoto. Nikiolewa itakuwaje kuhusu watoto wangu? Naweza kuolewa na kijana? (go to TRANSLATE and select your language)

Mimi ni mjane mwenye watoto. Nikiolewa itakuwaje kuhusu watoto wangu? Naweza kuolewa na kijana?

Mimi ni mjane na nina watoto.

Nina maswali yafuatayo:

(1) Je, itakuwaje kama nitapata mtu wa kunioa wakati bado watoto wangu ni wadogo? Je, Mungu anafurahia jambo hilo ?

(2) Na huko ninakoolewa hawawezi kuninyanyasa kwa vile nilikuwa na watoto nikaolewa na kuwaacha ?

(3) Ninaogopa kuwatenganisha watoto wangu. Nifanye nini nisije nikamtenda Mungu dhambi ?

(4) Na kama nikipata ambaye hajaoa bado akinioa itakuwa ni mpango wa Mungu au ni lazima niolewe na mgane? Naomba ushauri.

USHAURI

Kama Mungu amehusika katika kumpata huyo mume, atakupenda pamoja na watoto wako. Kama hayuko tayari kuwalea watoto wako aliowakuta, hafai kuwa mume wako.

Lazima akubali kwamba familia yako imepungukiwa na mume (kwako mwenyewe) na baba (kwa watoto wako).

Kwa vile watoto wako ni wadogo, hupaswi kuwaacha peke yao baada ya kuolewa. Mume anayependa kuishi nawe wakati huu, anapaswa kukusaidia kuwalea. Mungu hapendi watoto wako wateseke kwa sababu ya wewe kuolewa.

Hakikisha unamjulisha waziwazi wajibu wako wa kuwalea watoto wako ambao bado ni wadogo. Usipuuzie chochote unachokigundua kwake kinachoweza kuwa tishio kwa watoto wako. Usisikilize tu maneno matamu yanayotoka kinywani mwake bali uhisi pia utayari ulioko moyoni mwake kwa ajili yako na watoto wako.

Usiolewe na mtu ambaye anataka ukaishi nyumba moja na wazazi wake kwa sababu kufanya hivyo ni kwenda kinyume na Neno la Mungu. Mwa 2:24 “Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.” Pia usiolewe na mtu mwenye maamuzi tegemezi yaliyoelemea sana kwa ndugu zake. Ni lazima mjadili mapema jinsi ndoa (nyumba) yenu itakavyohusiana na ndugu wa pande zote na mtakavyolea watoto wenu. Mkiweka msingi mzuri, hakuna kati yenu atakayenyanyasika. Lk 11:17 “Naye akajua mawazo yao, akawaambia, Kila ufalme uliofitinika wenyewe kwa wenyewe hufanyika ukiwa; na nyumba juu ya nyumba huanguka.”

Kutengana na watoto sio dhambi. Hakuna tatizo kama ndugu zako au wa mumeo aliyefariki watajitolea kukaa na watoto wako na kuwalea. Dhambi ni pale unapowatelekeza watoto sababu ya kuolewa. Lakini pia kukaa karibu na watoto hakuzuii kumtenda Mungu dhambi. Dhambi iko karibu na mwanadamu wakati wote kila mahali. Mwa 4:7,8 “Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde. Kaini akamwambia Habili nduguye, Twende uwandani. Ikawa walipokuwapo uwandani, Kaini akamwinukia Habili nduguye,akamwua.” Kuna watu wapo kwenye ndoa lakini bado wanamtenda Mungu dhambi kwa kutowasimamia vizuri watoto wao halafu wanamsingizia shetani. Pamoja na shetani kusababisha matatizo, lakini sio yote. Mengine tunayasababisha sisi wenyewe. Kutofuatilia mtoto amefika kwa bibi alikoenda likizo, anatakiwa arudi nyumbani saa ngapi, anafika kwenye darasa la tuisheni unayolipia nk ni matatizo yetu wenyewe.  Mithali 22:6 Mlee mtoto katika njia impasayo, Naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee”. Kutojali watoto kwa sababu ya kuolewa ni dhambi. Mtu asiyejali watu wa familia yake hata kama anajitahidi kufanya huduma za kanisani, amemkana Yesu tena ni mbaya kuliko mpagani au mtu asiye na dini. 1 Tim 5:8 “Lakini mtu ye yote asiyewatunza walio wake, yaani, wale wa nyumbani mwake hasa, ameikana Imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini.” Lakini pia kukataa kuolewa wakati unawakwa tama (kama fursa ipo) ni dhambi vilevile. 1 Kor 7:8-9 “Lakini nawaambia wale wasiooa bado, na wajane, Ni heri wakae kama mimi nilivyo. Lakini ikiwa hawawezi kujizuia, na waoe; maana ni afadhali kuoa kuliko kuwaka tamaa.” Kwa hiyo dhambi inakutamani katika pande zote mbili lakini ushindi upo katika kumtii Mungu.

Narudia kusema muombe Mungu akupe mume atakayekupenda wewe pamoja na watoto wako. Hakuna masharti kwamba ni lazima uolewe na kijana ambaye hajawahi kuoa au mgane kama wewe. 

La msingi, kama unaolewa na kijana unatakiwa:

1. Umpime kama kweli yuko tayari kulea watoto wako. Je, anazungumzia nini kuhusu watoto wako kila mnapopata nafasi ya kuongea?

2. Uhakikishe amekomaa kimawazo anapoamua kukuoa. Asiamue kukuoa kwasababu ya kushawishiwa na misaada yako au kwa kuwa umejenga ukaribu sana na yeye mpaka akakutamani.

3. Uwe na umri unaofaa kuzaa naye kama ana malengo ya kupata watoto. Mueleze waziwazi kama huwezi kuzaa tena ili kuepusha migogoro inayoepukika. Kuna kijana alioa mwanamke aliyemficha kwamba amefungwa kizazi. Kijana akawa anahangaika na matibabu mpaka alipojulishwa na mtu wa pembeni. Namna hii ndoa inaweza kutodumu au kuwa ndoa ya maonyesho tu kwa watu lakini katika uhalisia haipo.

Kama ni mgane atakuwa na uzoefu kama wa kwako. Hata hivyo uzingatie kwamba:

1. Mkewe alikufa kwa ugonjwa gani na maisha yao yalikuwa na ushuhuda gani. Ni vizuri mkapime afya zenu kv Virusi vya UKIMWI, magonjwa ya ngono nk.

2. Anakutaka tu kama mjane mwenzake wa kuweza kumlelea watoto wake au anakupenda kweli uwe mkewe.

3. Uamuzi wa kukuoa unatoka kwake binafsi kwa kanuni za kibiblia au alishawishiwa tu na watu wanaokufahamu. Usisahau kwamba hata kama anayetaka kukuoa ni kijana au mgane ni lazima muwe na imani moja. 2 Kor 6:14 “Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza?”.

4. Vilevile, mnapaswa kufuata taratibu zote za Kanisa katika kuwaunganisha kuwa mume na mke. Ulizia utaratibu wa kanisa lenu ukoje katika suala la uchumba hadi ndoa.

Tahadhari katika kumpata mtu anayekiri wokovu kama wewe. 

Usimuamini mtu kwa sababu ameongozwa tu sala ya toba au anaabudu kanisa lenye misingi mizuri ya imani. Kuna dada alimwambia kaka fulani kwamba hawezi kumuoa kwa vile hajaokoka. Alichofanya yule kaka ni kuamua KUMUOKOKEA yule dada. Aliamua kujiunga na kanisa lao na kukubali kuongozwa sala ya toba. Hakuishia hapo akajiunga na kwaya na kuimba kwa miaka kadhaa. Kisha alipomuuliza yule dada kama yuko tayari kuolewa naye, dada akadhani sasa ameiva kiroho na kumkubalia. Ndoa ilipofungwa usiku uleule alishangaa kaka akivuta kreti la bia chini ya kitanda na kumwambia tunywe pombe.

Muda wa ibada au huduma kanisani hautoshi kumfahamu mtu kwa vile wengi wanajikausha wasigundulike. Maombi ni muhimu pamoja na ufuatiliaji kupitia kwa watu wanaomfahamu kwa karibu zaidi.

Lakini pia usijidanganye kwamba ukiolewa na mtu utamhubiri ili baadaye aokoke. Wengi waliofanya hivyo wameishi kwa majuto makubwa. Hakuna mume anayeweza kumuokoa mkewe. Ni Bwana Yesu peke yake aliimwaga damu Yake akatununua kwa bei kubwa ya uhai wake. Afadhali kuishi peke yako kuliko kumkaribisha shetani katika maisha yako hadi kifo kitakapowatenganisha.

Mungu akusaidie usifanye makosa katika eneo hili muhimu la mustakabali wa maisha yako!

Dkt. Lawi Mshana, Freelance Facilitator & Public Speaker, +255712924234, Tanzania