Tunahitaji kutambua mambo ya msingi katika ndoa. Katika Ukristo ndoa ni AGANO ambalo linahusisha Mungu, mume na mke. Hivyo mume na mke hawawezi kulivunja agano hilo isipokuwa Mungu tu. Mathayo 19:6 “Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe.” Kwa msingi huu kanuni ya ndoa ya Kikristo ni AGANO yaani 1+1=1 wakati ndoa zingine ni MKATABA ambapo 1+1=2. Mkataba unaweza kuvunjwa wakati wowote kwa vile Mungu hakuhusika bali serikali au wanadamu. Uhusiano wa mkataba ni wa watu wawili wanaoishi pamoja lakini kila mmoja ana haki zake tofauti (married singles) tofauti na agano ambapo wawili wanakuwa mwili mmoja (married couples).
Mahari ni suala linalotegemea maamuzi ya wazazi, wanandoa watarajiwa au utamaduni wao. Sio dhambi kama wazazi wataamua mahari ya pesa au mali isiwepo kabisa. Ili mradi wazazi wawaachilie watoto wao wakiwa wametimiza mambo ya msingi. Kuifunga ndoa kanisani wakati makubaliano hayakutekelezwa kunaweza kuleta madhara kwa wahusika.
Maandiko yanasema kwamba wanandoa wanatakiwa kuondoka kwao waende kuanzisha maisha yao. Mwanzo 2:24 “Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.” Mambo matatu muhimu yametajwa hapa. 1. Kuondoka kwa wazazi (kuacha utegemezi wa wazazi) 2. Kuambatana (kuwa na uhusiano wa karibu) 3. Kuwa mwili mmoja (kuunganishwa na Mungu).
Tuko katika kizazi kinachotafuta uhuru usio na mipaka (uholela) hivyo baada ya mtu kufikia umri fulani anakuwa na haki ya kufanya maamuzi hata kama bado anawategemea wazazi wake. Lakini ukweli ni kwamba maandiko yanamtarajia kijana akifikia kuoa au kuolewa aondoke nyumbani kwa wazazi akaanzishe familia yake na kizazi chake kipya. Sio mpango wa Mungu mtu aoe na kumleta mke wakae na wazazi wao. Wazazi wataendelea kuwapangia majukumu kwa vile mtoto kwa mzazi wake hakui. Matokeo yake wanandoa hao hawataweza KUAMBATANA. Ndoa inahitaji baraka za wazazi kabla ya baraka za mchungaji. Labda pale tu wazazi wanapopingana na kusudi la Mungu lililothibitishwa. Kuna wakati wazazi wanaweza kutofurahia mtoto wao kuoa au kuolewa na mtu fulani kutokana na sababu za msingi ambazo hazipaswi kupuuzwa. Maisha ya ndoa sio TUKIO LA MARA MOJA (EVENT) bali ni MCHAKATO (PROCESS) yaani, kuambatana na kuwa mwili mmoja.
Kama utaratibu au utamaduni unataka kulipa mahari, mhusika anapaswa kulipa mahari kama ilivyopangwa. La msingi tu wazazi tusitumie mahari kama kitega uchumi kiasi kwamba hayalipiki kirahisi.
1. Mtu akilipiwa mahari ndipo anakuwa mke rasmi
Kum 22:29 “yule mtu mume aliyelala naye na ampe baba yake yule kijana shekeli hamsini za fedha, kisha na awe mkewe, kwa kuwa amemtweza; hana ruhusa ya kumwacha siku zake zote.”
Kut 22:16-17 “Mtu akimshawishi mwanamwali, aliyeposwa na mume, na kulala naye, lazima atatoa mahari kwa ajili yake ili awe mkewe. Ikiwa baba yake huyo mwanamwali akataa kabisa kumpa, atalipa fedha kama hesabu ya mahari ya mwanamwali ilivyo.”
Kutolipa mahari kunaweza kufungua milango ya mapepo ya ngono (mke na mume wa kiroho) kwa vile shetani ni mshitaki kwa yale ambao hayajatekelezwa kwa mujibu wa Neno la Mungu.
2. Kwa vile kikao kilifanyika na makubaliano yakafanyika, ni dhambi kuvunja maagano au kutotimiza ahadi.
Warumi 1:31,32 “wasio na ufahamu, wenye kuvunja maagano, wasiopenda jamaa zao, wasio na rehema; 32 ambao wakijua sana hukumu ya haki ya Mungu, ya kwamba wayatendao hayo wamestahili mauti, wanatenda hayo, wala si hivyo tu, bali wanakubaliana nao wayatendao.”
Mkikubaliana halafu mkapuuza kutimiza ahadi mtahukumiwa. Andiko linatuonya kwamba tusivunje maagano kama tunataka kuepuka mauti. Hata mwanamke atahukumiwa kwamba kwanini alikubali kuolewa bila mahari kulipwa. Labda kama makubaliano yalionyesha wazi kwamba hakuna kulipa mahari yoyote. Kwa mujibu wa andiko hapo juu, mwanamke anahukumiwa kwa kukubaliana na makosa ya mume wake. La kusikitisha, tunaandaa harusi za kifahari bila kujali kulipa mahari.
3. Kama ulikubali kwamba utamaliza kiasi cha mahari kilichobaki, tambua kwamba unadaiwa. Kwa kifupi, umeoa kwa mkopo. (Dawa ya deni ni kulipa).
Kama mtu anadaiwa na halipi anatambulika kwamba sio mtenda haki. Zaburi 37:21 “Asiye haki hukopa wala halipi, Bali mwenye haki hufadhili, hukirimu.” Mtu asiyetenda haki hawezi kuwa salama baada ya kuondoka duniani kwa vile moja ya sifa za mbingu mpya na nchi mpya ni HAKI. 2 Petro 3:13 “Lakini, kama ilivyo ahadi yake, mnatazamia mbingu mpya na nchi mpya, ambayo haki yakaa ndani yake.”
Kama ulisema ndiyo nitalipa mahari, maanisha hivyo. Biblia inasema kinyume cha hapo unaongozwa na yule mwovu. Mathayo 5:37 “Bali maneno yenu yawe Ndiyo, ndiyo; Siyo, siyo; kwa kuwa yazidiyo hayo yatoka kwa yule mwovu.”
Mhubiri 5:4,5 “Wewe ukimwekea Mungu nadhiri, usikawie kuiondoa; kwa kuwa yeye hawi radhi na wapumbavu; basi, uiondoe hiyo uliyoiweka nadhiri. Ni afadhali usiweke nadhiri, Kuliko kuiweka usiiondoe.” Watu wanaoahidi halafu wanapobarikiwa hawatimizi ahadi zao, mbele za Mungu wanaitwa WAPUMBAVU. Jiulize kama wapumbavu wana nafasi katika ufalme wa Mungu.
4. Ndoa ni siri ambayo huwezi kuielewa kibinadamu (beyond human comprehension) kiasi kwamba inafananishwa na uhusiano wa Kristo na Kanisa
Waefeso 5:31,32 “Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake, ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja. Siri hiyo ni kubwa; ila mimi nanena habari ya Kristo na Kanisa.”
Ukitaka kuelewa uzito wa ndoa ya Kikristo, jifunze uhusiano wa KRISTO na KANISA. Kristo hadaiwi bali amelipa deni lote kwa ajili ya dhambi zetu. Kanisa nalo tuna wajibu wa kutambua bei (gharama) ya uhai wa Yesu alioutoa ili kulipia dhambi zetu.
Shuhuda
Kuna mtu alipewa neema ya kupelekwa kuzimu na mbinguni (Kwa wale wanaoamini kwamba Mungu aliyempeleka mtume Paulo hadi mbingu ya tatu akiwa duniani, anaweza hata leo kufanya hivyo). Huko kuzimu aliona wanawake wanaoteseka kwa sababu hawakulipiwa mahari. Lakini pia aliona mtu akiteseka kuzimu kwa sababu aliahidi kununua gitaa la kanisa na hakufanya hivyo hadi kifo chake. Ikiwa aliyeahidi kununua gitaa alihukumiwa, Je wewe uliyeahidi kulipa mahari na hukufanya hivyo?
Ushauri
wangu
1. Hata kama mwenzi wako amefariki au
wazazi wake wamefariki, kalipe mahari unayodaiwa. Waone ndugu zao ambao bado
wako hai.
2. Kama ni miaka mingi tangu upangiwe
mahari, nashauri uzingatie thamani ya fedha kwa sasa. Sio sawa kulipa kiasi
kilekile cha shilingi elfu 10 uliyopangiwa miaka 30 iliyopita.
3. Mahari haitofautiani sana na
nadhiri. Kama hukuweza kulipa mahari yote kabla ya ndoa kufungwa, usiendelee
kufurahia matunda ya ndoa na kusahau kwamba malipo hayajakamilika. Usiweke
kipaumbele katika madeni mengine na KUKAWIA kulipa mahari kwa vile hujui
utaondoka lini duniani. Afadhali ugome
kuoa kuliko kupuuza kulipa mahari uliyokubali katika kikao rasmi.
4. Nashauri wazazi wasipange mahari kubwa ambayo inawafanya watoto wao waoe na kuolewa kwa madeni ambayo yanawanyima baraka na kuwakosesha mbingu. Mahari isiwe ni njia ya kupata kipato bali iwe tu kama zawadi ya kuunganisha familia mbili.
Kama unataka nikutumie hizi makala kwa email nipatie anuani yako ya barua pepe kwa kuniandikia kupitia CONTACT US (WASILIANA NASI).
Lawi Mshana, +255-712924234, Tanzania,