Baada ya kutambua wajibu wa jamii na taasisi za dini katika kukabiliana na majanga, Beyond Four Walls inatoa mafunzo kwa ajili ya kujihusisha kutoa huduma za kukabiliana na uhatarishi na majanga. Beyond Four Walls ni shirika lisilo la kiserikali ambalo kama jina lake lilivyo, linalenga kuwasaidia watu WATOKE NJE YA KUTA NNE yaani, kuacha ubinafsi na kujijali katika nyumba zetu binafsi, nyumba zetu za ibada na huduma zetu na kwenda kuwafikia wengine. Dhamira ya shirika hili ni KUJENGEA UWEZO JAMII ISHINDE UHATARISHI KWA KUTUMIA MBINU SHIRIKISHI.
Kuna mambo kadhaa yametupa msukumo wa kufanya huduma hii ambapo tumeanza kujengea uwezo taasisi za dini ambapo tuligundua mambo yafuatayo kupitia kanisani):
1. Jamii inajali mazishi na maziko kuliko matatizo yanayowakabili watu wakiwa bado wako hai. Mtu anaweza kutosaidiwa pesa za dawa, matibabu na lishe lakini mtu huyohuyo akifa pesa nyingi zinapatikana na mazishi yake yanakuwa ya kifahari. Kumbuka vifo vingine havitokani na majanga na wala sio dharura bali ni utaratibu unaompata kila mwanadamu. Pamoja na umaarufu wote wa Bwana Yesu alizikwa na watu wasiojulikana rasmi kwamba wanamuamini (wanafunzi wa siri). Yn 19:38-40 “Hata baada ya hayo Yusufu wa Arimathaya, naye ni mwanafunzi wa Yesu, (lakini kwa siri, kwa hofu ya Wayahudi), alimwomba Pilato ruhusa ili auondoe mwili wake Yesu. Na Pilato akampa ruhusa. Basi akaenda, akauondoa mwili wake. Akaenda Nikodemo naye, (yule aliyemwendea usiku hapo kwanza), akaleta machanganyiko ya manemane na uudi, yapata ratli mia. Basi wakautwaa mwili wake Yesu, wakaufunga sanda ya kitani pamoja na yale manukato, kama ilivyo desturi ya Wayahudi katika kuzika.”
2. Tunakabiliana na matatizo ya watu kiroho tu na kukwepa wajibu wetu tuliopewa na Mungu. Tunaridhika kuombea watu bila kujali mahitaji ya kimwili ambayo tunayamudu na wakati huohuo hatuoni majibu dhahiri ya maombi yetu kwao. Tunaona kabisa kwamba mtu tunayemuombea haponi lakini hatumuulizi kama kuna mahitaji ya kimwili ambayo tunaweza kumsaidia kv chakula, dawa nk. Yak 2:15-16 “Ikiwa ndugu mwanamume au ndugu mwanamke yu uchi na kupungukiwa na riziki, na mtu wa kwenu akawaambia, Enendeni zenu kwa amani, mkaote moto na kushiba, lakini asiwape mahitaji ya mwili, yafaa nini?”
3. Sadaka nyingi tunazotoa zinafanya kazi za kidini tu na sio kwa ajili ya wasiojiweza. Wakati huohuo tumeambiwa dini safi ni ile inayojali wasiojiweza. Yakobo 1:27 “Dini iliyo safi, isiyo na taka mbele za Mungu Baba ni hii, Kwenda kuwatazama yatima na wajane katika dhiki yao, na kujilinda na dunia pasipo mawaa.” Mtume Petro alikuwa akitoa sadaka (alms) kwa mwenye ulemavu mlangoni mwa hekalu. Siku moja akagundua hana kitu cha kumpa. Ndipo alihitaji mbingu iingilie kati na muujiza ukatendeka wa kumponya ili aende zake akafanye kazi ya kipato. Sina maana tusiwaombee watu uponyaji mpaka tukose dawa ya kuwapa! Hapana. Nakazia tu kwamba tufanye tunayoweza kibinadamu hadi pale tunapopata msukumo kwamba Mungu anataka kujibu kwa njia nyingine tofauti. (Mdo 3:1-9)
4. Tutaendelea kuishi maisha ya laana na badae tunaweza kuikosa mbingu kwa vile tunajali tu huduma za kiroho na hatuko tayari kuwa mkono wa Mungu wa kujali mahitaji ya KIMAISHA. Mt 25:41-46 “Kisha atawaambia na wale walioko mkono wake wa kushoto, Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari Ibilisi na malaika zake; kwa maana nalikuwa na njaa, msinipe chakula; nalikuwa na kiu, msininyweshe; nalikuwa mgeni, msinikaribishe; nalikuwa uchi, msinivike; nalikuwa mgonjwa, na kifungoni, msije kunitazama. Ndipo hao pia watajibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona wewe una njaa, au una kiu, au u mgeni, au u uchi, au u mgonjwa, au u kifungoni, tusikuhudumie? Naye atawajibu, akisema, Amin, nawaambia, Kadiri msivyomtendea mmojawapo wa hao walio wadogo, hamkunitendea mimi. Na hao watakwenda zao kuingia katika adhabu ya milele; bali wenye haki watakwenda katika uzima wa milele.”
5. Hatuna mikakati ya kukabiliana na majanga kibinadamu hata pale Mungu anaposema na sisi. Nabii Agabo alipotabiri kuhusu njaa, watu hawakufunga na kuomba kukemea hali hiyo bali walikusanya misaada na kuwapatia ndugu zao. Mitume hawakuzunguka na Biblia peke yake mkononi bali walipeleka misaada kwa wahitaji. (Mdo 11:28-30). Lakini pia Yusufu alipotafsiri ndoto ya Farao ya miaka 7 ya shibe na miaka 7 ya njaa hakusema watu wafunge bali iliwekwa mikakati ya kukabiliana na njaa. (Mwa 41:32-37). Pendekezo la Yusufu lilikubalika kwamba atafutwe mtu mwenye akili na hekima asimamie mpango huo. Tumekosa akili na hekima ndiyo maana tunatumbukia kwenye matatizo mengi kila wakati na mengine tulishaonywa na Mungu kwa njia ya ndoto.
6. Wakati mwingine tunajitoa sana kusaidia wahitaji kwa mipango ya dharura ambayo inawafanya watu wawe tegemezi wa misaada badala ya kuwajengea uwezo wajitegemee. Mfano, mhitaji anachangiwa pesa au chakula mara kwa mara lakini hakuna ufuatiliaji kwamba kwa nini halimi au kufanya kazi na kama hana shamba nani anaweza kumuazima. 2 The 3:10 “Kwa kuwa hata wakati ule tulipokuwapo kwenu tuliwaagiza neno hili, kwamba ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi, asile chakula.”
7. Tunaendelea kulazimisha matatizo ya watu yaishe kwa maombi tu wakati maandiko yanaonyesha kwamba mengine yanahitaji maelekezo maalum. Mfano, mwanamke mwenye madeni yasiyolipika alipomuona nabii wa Mungu hakumuombea bali alimuagiza atumie kidogo alicho nacho kama mtaji, atafute vyombo vya kuhifadhia na aende sokoni kuuza. Aliagizwa pia alipe kwanza madeni yake ndipo kinachobaki kiwe matumizi yake binafsi. (2 Fal 4:1-6). Harusi ya Kana ilipopungukiwa vinywaji Bwana Yesu hakuomba sala bali alitoa maelekezo ambayo yaliambatana na muujiza yalipofanyiwa kazi kibinadamu (Yn 2:4-10). Kwa sasa wengi wetu tumeamua kumuachia Mungu kila kitu wakati na Yeye alishatuachia wajibu huo. Matokeo yake ni kujikuta tukipigika kimaisha huku tunatangaza ukuu wa Mungu. Kuna mtu kila mara anaugua homa ya matumbo lakini anaombewa tu uponyaji bila kusaidiwa kuchunguza mazingira ya nyumbani yake kama yanazingatia usalama wa maji na mazingira ili tatizo lisijirudie. Tangu kipindi cha Biblia Mungu aliagiza kuwa na vyoo na kuvitumia vizuri. Kum 23:12,13 “Tena uwe na mahali nje ya kituo, kwa kutokea nje;nawe uwe na jembe dogo katika silaha zako; napo uotamapo nje uchimbe kwa lile jembe, na kugeuka na kukifunika kikutokacho.”
8. Tuna uwezo wa kufanya vitu vingi ila tumeamua tutafute wafadhili kwa kila hitaji wakati huohuo tunachangia sherehe zetu kwa pesa nyingi bila kutafuta wafadhili. Mambo haya yanatufanya tuwe maskini wa kutupa katika ufalme wa Mungu. Kama tunamtumaini Mungu ili tu atusaidie mambo fulani bila kuwekeza kwa ajili ya umilele wetu, SISI TU MASKINI KULIKO WATU WOTE. Yesu alikuja kwa ajili ya usalama wetu wa sasa na wa milele. 1 Wakorintho 15:19 “Kama katika maisha haya tu tumemtumaini Kristo, sisi tu maskini kuliko watu wote.”
9. Tunataka watu watujali na kutusaidia wakati sisi wenyewe hatujali wengine. Luka 6:31 “Na kama mnavyotaka watu wawatendee ninyi, watendeeni vivyo hivyo.” Ukiumwa unatamani mtaa mzima ukutembelee na unalaumu sana wasiokutembelea. Je wewe umetembelea wangapi ukiwa na chochote mkononi? Unataka kupongezwa na kusaidiwa lakini hata tu kutia moyo wengine huwezi. Mf. Waimbaji wengi wa Injili wanatuma nyimbo kwenye magroup mtandaoni ili wasaidiwe lakini sidhani kama wamewahi kutoa maoni yoyote au kupongeza huduma za makundi hayo. Nadhani wala hawasomi chochote wanachokikuta humo. Tunatakiwa kuwa na busara kama nyoka na wapole kama hua (Mt 10:16).
Nimeona umuhimu wa kushirikiana na jamii kwa kuzingatia vigezo mbalimbali kv ujuzi, upatikanaji, utayari, mzigo moyoni, huruma, misaada ya vitu, nguvu, kipaji, fedha nk
Unajua hata wewe unaweza?
Daudi alikimbilia kwenye pango asiuawe lakini watu takriban 400 wakamkimbilia ili awasaidie. Sifa za hao watu ni hizi WENYE DHIKI, WENYE MADENI na WENYE UCHUNGU MOYONI. Hivi angekuwa wewe ungewapokea au ungewafukuza ukizingatia kwamba unapambana na hali yako ya kutafutwa na mfalme ili uuawe? Hata kama unaonekana kama huna kitu, tunaamini kuna sehemu yako katika mpango huu!
1 Sam 22:1-2 “1 Basi Daudi akaondoka huko, akakimbilia pango la Adulamu; na ndugu zake na watu wote wa mbari ya baba yake waliposikia habari hiyo, wakamwendea huko. 2 Na kila mtu aliyekuwa katika hali ya dhiki, na kila mtu aliyekuwa na deni, na watu wote wenye uchungu mioyoni mwao, wakakusanyika kwake; naye akawa jemadari wao; nao waliokuwa pamoja naye walipata kama watu mia nne.” HATUTAJALI TENA HALI ZETU TU BALI TUTAWAFIKIA WENGINE PIA KADIRI TUNAVYOJALIWA NA MUNGU.
KAMA UMEHAMASIKA NAKUKARIBISHA USHIRIKIANE NASI KATIKA HUDUMA HII AMBAYO TUNAIFANYA BILA UBAGUZI WA AINA YOYOTE
Tujulishe kama una utayari wa KUJITOLEA katika eneo lolote na Mungu atakukumbuka kwa yale mengine unayohitaji akufanyie.
Mfano wa namna unavyoweza kuhusika (popote ulipo):
1. Nina uzoefu wa kutoa mafunzo ya namna
ya kukabiliana na majanga mf moto, mafuriko, matetemeko nk
2. Nina uzoefu wa kuwanusuru au kuwaokoa
watu kwenye majanga (eleza kwa vipi na kwa muda gani)
3. Nina uzoefu wa kutoa huduma ya kwanza
kwa waliopata majanga (eleza kwa vipi na kwa muda gani)
4. Ninapenda kujitolea kuazima kwa muda
vitu vyangu wakati wa majanga (mfano, gari, pikipiki, nyumba, kiwanja, hema,
turubai, viti, vipaza sauti, mtumbwi, godoro, vifaa vya uokozi nk)
5. Ninapenda kutoa elimu kwa jamii ili
kuitahadharisha na majanga (eleza kwa namna gani) mf. Kutumia vipaza sauti,
redio yangu, TV yangu, mtandao wa jamii nk
6. Ninapenda kutoa fedha kwa ajili ya
kazi ya kukabiliana na majanga
7. Nina uzoefu wa kufanya utafiti,
ufuatiliaji na tathmini katika majanga
8. Ninapenda kujitolea ujuzi wangu
katika majanga Mfano, Ufundi, utaalamu nk (utaje)
9. Tunapenda mpango huu ufike kwenye taasisi yetu ili nayo ihusike kv kanisa, msikiti, shirika nk
Kumbuka unaweza kushirikiana nasi hata ukiwa mbali kwa sababu ya maendeleo ya kiteknolojia ya sasa.
Wasiliana nasi sasa bila kusita ili tufanye kazi hii pamoja yenye thawabu kubwa mbele za Mungu. Tuma taarifa zako tukufahamu zaidi inapowezekana.
Dr Lawi Mshana (Mkurugenzi Mtendaji), 0712-924234 (whatsapp); mshanalawi@gmail.com; beyond4wallstanzania@gmail.com
Akaunti ya Beyond Four Walls Namba 0133621816400 iko tawi la CRDB Bank Korogwe