KIPANDE CHA USHAURI (A PIECE OF ADVICE)
KIJANA USIOMBE ‘MCHUMBA’, OMBA ‘MWENZI’
Napenda kukukumbusha kijana unayeomba Mungu akupe ndoa njema. Tambua kwamba kamwe Mungu hakupi mchumba bali anakupa mwenzi wa maisha. Uchumba ni mchakato tu wa kufahamiana ili hatimaye ndoa ifungwe. Katika kipindi cha kufahamiana unatakiwa kuhakikisha unamfahamu mwenzako katika uhalisia wake. Usidanganyike kwamba siku zote mtakuwa mnakubaliana mambo yote. Mnaweza kuwa na tofauti nyingi sana kama vile maumbile, urefu, rangi, kabila, malezi, dini, dhehebu, elimu, ujuzi, kipato nk. Usisahau kwamba kama hujamuona mtu akiwa amekasirika na anatawalaje hasira yake HUJAMFAHAMU bado.
Kijana fulani alitengeneza ‘crisis’ (ugumu fulani) ili amfahamu mchumba wake kabla ya ndoa kufungwa. Walipopatana kwamba watakutana mahali fulani (ambapo hakuna maswali kwa watu) kwa ajili ya mazungumzo zaidi, muda ulipofika alimpigia kwamba hataweza kufika kwa sababu ya dharura fulani. Yule dada alimtukana matusi ya nguoni akajisahau kwamba bado ni wachumba. Yule ndugu akavunja mahusiano hayo kwa kigezo kwamba amegundua kwamba hataweza kumvumilia akichelewa kazini. Sisemi uvunje uhusiano na mtu kwa kumjaribu mara moja tu lakini hakikisha mwenzako haigizi upendo wake kwako bali aweze kukuambia mambo ambayo hapendi bila kuogopa kwamba uhusiano utavunjika.
Kuna mtu Mungu amemuandaa kwa ajili yako. Kwa hiyo usimmeze kiasi cha kuona kwamba hutapata mwingine kama huyo. Kataa upendo wa zezeta ambao hauko tayari kubadilisha mwelekeo unapoona madhaifu ambayo hayatengenezeki. Kama mahubiri yameshindwa kumbadilisha mtu, usijidanganye kwamba wewe utaweza. Hakikisha madhaifu yanavumilika ndipo ukubali kwenda hatua nyingine.
Dkt. Lawi Mshana, +255712924234; Korogwe, Tanga, tanzania
Tafadhali toa maoni yako au uliza swali lolote hapo chini.