Eneo hili la mchakato wa kupata mwenzi wa maisha lina changamoto nyingi sana hasa kwa yule ambaye anataka kuoa au kuolewa na sio kuokota au kuokotwa. Wanaume na wanawake ni wengi lakini mume au mke anayekufaa ni mmoja tu. Adamu alipewa mke wa kufanana naye kwa hiyo tusipuuze kuwa na tabia au maisha yanayoendana (compatibility) kama tunataka ndoa ya furaha. Kumbuka mke au mume huyo hataishi na Mungu bali ataishi na wewe. Kwa hiyo, vigezo visiwe vya kiroho tu bali vizingatie maeneo yote ya maisha. Mtu anaweza kuwa mchungaji mzuri, mwimbaji mzuri au kiongozi mzuri wa taasisi na asiwe mume mzuri au mke mzuri. Taasisi ya ndoa ni kubwa sana hivyo haihitaji tu mtu kuonekana amevaa suruali au gauni lazima vigezo vizingatiwe!
Sio mazingira yote utakutana na mwenzi ambaye ni chaguo lako na ambaye mnakamilishana (complementing each other). Ukishafumba macho wakati wa kuomba, ufike mahali ufungue macho wakati wa kuchagua ukiongozwa na Mungu. Hatima yako haitegemei kuchaguliwa na Mungu kwa vile amekupa utashi. Anataka uchague aina ya maisha unayotaka na ujiandae na matokeo ya uchaguzi wako. Ukikosea kufanya uchaguzi wa mwenzi wa maisha, sio tu kwamba utaharibu hatima (destiny) yako na mustakabali wa maisha yako bali na wa kizazi chako. Kum 30:19 “Nazishuhudiza mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimekuwekea mbele yako uzima na mauti, baraka na laana; basi chagua uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako.” Nadhani wewe mwenyewe unaona jinsi watu wanavyoteseka leo kutokana na maamuzi mabaya ya wazazi wao ya kutowasomesha au kutoandaa maisha ya mbele.
Usikubali kulazimishwa kuoa au kuolewa na mtu kwa sababu za maslahi binafsi hata kama ni ya kidini. Kuna mtu anazuiwa kuolewa na mtu sahihi kwa kisingizio kwamba huduma yake inahitajika sana kanisani hapo au kwa vile ni mtoaji mzuri. Ikiwa na maana kwamba akiolewa na mtu wa kanisa jingine, kipato cha kanisa kitapungua wakati ni chaguo lake na ni mpango wa Mungu. USIKUBALI KUWA MTAJI WA MIRADI YA WATU. Utajuta bure badae. Mimi nilioa mke ambaye alikuwa anategemewa sana kanisani kama mwimbaji na katibu wa kanisa. Lakini kanisa halikuchanganya ndoa na maslahi binafsi. Mchungaji akamuachilia kwa amani kabisa bila kujali tofauti zetu za kimadhehebu.
Lakini pia hata Isaka na Rebeka tunaowanukuu mara kwa mara tunapofundisha uchumba na ndoa, hawakuwa wanafahamiana kwa karibu ila mifumo ilitumika ili kuhakikisha wanajiridhisha kwamba ni mpango wa Mungu kuwa wanandoa. Sio busara kukutana mtandaoni, kazini au kwenye basi halafu mnapanga kuoana bila juhudi zozote za kufahamu ndugu wa karibu. Ndoa inaunganisha familia na sio wanandoa peke yake. Lazima muachiliwe kwa baraka za wazazi au kifamilia. Kwa kufanya hivyo mtagundua kama kuna utapeli wowote. Hili ni jambo muhimu na la lazima sana kabla ya ndoa kufungwa kanisani. Mwanzo 2:24 “Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.” Mimi nilioa mke ambaye anatoka zaidi ya kilomita elfu mbili kutoka mahali nilipo lakini bado nilihakikisha nafahamu kwanza wazazi wake, ndugu zake na kanisa anakoabudia. Unatakiwa kuwa macho sana na mtu ambaye anakusifia wewe tu lakini haulizi kwenu wapi, ndugu zenu ni kina nani na wala hatafuti kufahamiana nao.
Wapo vijana wengi wanaoniuliza maswali mbalimbali mtandaoni. Hata hivyo nakushauri kwenye hii blog yangu usome kwanza makala nilizoandika kuhusu MAHUSIANO ndipo utauliza vizuri maswali yako ambayo utaona hujajibiwa bado. Makala zimekusanywa kwa mpangilio kama wa maktaba. Pia unaweza kudownload App yangu ya LAWI MSHANA ili iwe rahisi kujisomea mara kwa mara.
Huu ni wakati wako wa kukutana na yule ambaye Mungu amemuandaa kwa ajili yako ambaye ataziba pengo ulilo nalo na ambaye utakuwa msaada kwake auone umuhimu wako (ambaye mtahitajiana).
Barikiwa.
Lawi Mshana, Free Facilitator & Public Speaker, +255712924234, Tanzania