Ticker

6/recent/ticker-posts

Mambo unayofanya yanayohujumu mustakabali wa maisha yako (Things you do that harm the future of your life) - Go to TRANSLATE and choose your language



MAMBO UNAYOFANYA YANAYOHUJUMU MUSTAKABALI WA MAISHA YAKO (THINGS YOU DO THAT HARM THE FUTURE OF YOUR LIFE)

1. U mvivu 

Watu wengi hawapendi kuitwa wavivu hata kama wako hivyo. Unaposhindwa kutumia muda na uwezo uliopewa na Mungu kikamilifu unakuwa ni mvivu. Walioanzisha muda wa ziada (overtime) walilenga kuhakikisha mambo yanafanyika kwa muda uliopangwa. UVIVU ni ndugu yake KUAHIRISHA. Mtu mvivu ni rahisi tu kuahirisha jambo lililotakiwa kufanyika leo alifanye siku nyingine bila sababu za msingi. Kijijini kwetu alikuwepo mtu mmoja ambaye anaamka asubuhi kwenda shamba lakini kutokana na maongezi na watu njiani, muda unamuishia na kuamua kurudi nyumbani akiwa na jembe lake begani. 

2. Huna shabaha 

Inawezekana una bidii ya kazi lakini huna shabaha hivyo unafanya mambo mengi sana kwa wakati mmoja. Matokeo yake yanakuponyoka na kujikuta hakuna jambo unamaliza. MTU ASIYEJUA AENDAKO HAWEZI KUPOTEA. Kwa vile huna shabaha unafanya chochote kilichoko mbele yako hata kama hakikufikishi unakotaka kwenda. Kabla ya kufanya kazi unatakiwa ujue kazi hiyo itakufanyia nini au itakusaidia kufika wapi. Wapo wengi wamefanya kazi fulani kwa miaka mingi na hawako tayari kuibadilisha hata kama wanaona maisha hayabadiliki. 

3. Umejitenga sana 

Hupendi kushirikiana na watu muhimu wakati huna uwezo wa kufanya kila kitu. Hii tabia ya kujitenga imesababisha wasomi wapitwe na wasiosoma katika mafanikio. Unajua kwa nini? Wasomi walijengwa kwa muda mrefu katika maisha ya ubinafsi kwamba usimsaidie mwanafunzi mwenzako ili asije akakupita. Kwa hiyo hata katika mitihani ya maisha bado wasomi wengine hawapendi kushirikiana na wengine wasije wakapitwa. Matajiri wakuu duniani ni wale wanaojenga mitandao na mahusiano yenye tija na watu. Tambua watu wanaofaa kujenga mahusiano yenye tija. 

4. Unaogopa kukataliwa 

Mungu amemuumba kila mmoja wetu na uwezo fulani ambao wengine hawana. Hivyo kama kila kitu unachotaka kufanya utaanza kwanza kuuliza watu wengine, watakuambia hakiwezekani. Kumbe ni wewe tu ungekiweza ili wengine wajifunze. Unapoogopa kwamba watu hawatakuelewa hutaweza kujaribu kufanya jambo jipya. Itabidi uendelee kurudia kufanya mambo ya kawaida yaliyozoeleka. Na kama unafanya mambo ya kawaida, utakuwa wa kawaida. Ukitaka kuleta tofauti katika maisha yako lazima uwe wa tofauti. 

5. Unakata tamaa haraka 

Unapenda kufanya mambo ambayo yatakupa matokeo ya haraka sana hata kama sio ya kudumu (quick fix). Hivyo ukiona jambo linachukua muda kidogo bila matokeo ya wazi unaacha na kuanza jingine. Kuna masuala yanahitaji hata miaka mitano kujiimarisha ndipo upate faida na faida yake itakuwa ya uhakika. Sio miti yote inatupatia mavuno mapema baada ya kupandwa. Mnazi unaweza kuanza mavuno ya kwanza kati ya miaka 6 na 10 na kuendelea kuzaa hadi miaka 20. Kwa hiyo huwezi kulinganisha mnazi na mchicha. Lazima ujiulize unataka mafanikio ya ukubwa gani na uwekezaji wake ni wa kiwango gani. 

6. Unalalamika sana 

Mungu aliwahi kuwaangamiza waliokuwa wakinung’unika jangwani katika safari ya kutoka Misri kwenda Kanani. Matokeo yake katika watu takriban milioni 3 (wanaume, wanawake na watoto) waliotoka Misri wakafika wawili tu. Wengine walioingia Kanani ni wale waliozaliwa njiani au safarini. Kuna watu wanalaumu watu wote isipokuwa wao wenyewe. Hata matatizo waliyosababisha wao wenyewe, wanayahamishia kwa watu wengine. Ndiyo maana wengi wameshindwa kufikia Kanani yao waliyopangiwa na Mungu. Kinyume chake wanaendelea kuzunguka milima ya Seiri bila kwenda mbele na kufikia mpango waliopangiwa na Mungu. 

7. Unasubiri kazi nzuri 

Kuna watu hawajui kwamba kazi hazitafutwi bali zinatengenezwa. Unaangalia mahitaji na kutambua kazi inayoweza kulipa. Kazi ziko nyingi katika maeneo yetu lakini hatuzioni kwa vile tumuweka macho yetu kwenye ofisi tu. Tungeweka macho yetu kwenye mahitaji ya watu na raslimali tulizo nazo tungepata upenyo. Mtu angeweza kuanzisha darasa la chekechea kwenye eneo la makazi mapya lakini anaona elimu yake ni kubwa sana hivyo afadhali azunguke maofisini kutafuta kazi. Kumbe angeanzisha darasa la chekechea kwa mtazamo wa kisomi angeleta tofauti ambayo ingewafanya wengi wajiunge kwake. 

8. Unajidanganya na kutegemea mafanikio yako ya nyuma 

Kuna watu wanajidanganya kwamba wamefanikiwa wakati sio kweli. Mfano mtu anaweza kujidanganya kwamba amefanikiwa kwa vile ana smartphone lakini kusema kweli anayetumia simu ndogo ya tochi ndiye anaitumia vizuri na imemfanikisha. Unaweza kujidanganya kwamba umefanikiwa kwa vile nyumba yako ina mabati na madirisha ya hadhi kama ya jirani yako lakini kusema kweli maisha unayoishi sio sawa na ya kwake. Ni kujidanganya pale unapojaribu kuishi maisha ya mtu mwingine wakati kipato chako hakiruhusu kufanya hivyo. Kubali kiwango cha maisha yako na kujitahidi kukibadilisha kadri Mungu anavyokujalia. Usiendelee kutoa hadithi za maisha yako ya mafanikio uliyokuwa nayo zamani wakati haziakisi (haziendani na) hali ya sasa. Mfano unaelezea jinsi miaka 15 iliyopita ulivyokuwa Marekani wakati hakuna alama yoyote iliyobaki inayoendana na maisha yako ya sasa. 

9. Unajilinganisha na wengine 

Kujilinganisha na watu wengine kunakufanya ufanye kazi kwa ajili ya watu na sio kwa ajili ya mahitaji yako mwenyewe. Unaweza hata kununua kitu ambacho sio hitaji lako. Wapo wamama wengine wanajipamba kwa sababu ya wamama wenzao au wafanyakazi wenzao bila kuuliza waume zao kama wanapenda mapambo hayo. Matokeo yake mtu anashangaa pamoja na urembo wake anaachwa. Lakini pia ni hatari sana kuiga maisha ya mtu ambaye hujui vyanzo vyake vya mapato. Ni vizuri tutambue mahitaji na shauku zetu badala ya kutafuta kufanana na watu wengine. Wewe umeumbwa kwa jinsi ya ajabu ya kutisha. Mshukuru Mungu kwa vile ulivyo na kuendelea kutafuta mafanikio kwa njia halali. 

Ubarikiwe na Bwana! 

Dr Lawi Mshana, +255 712924234; Korogwe, Tanga, Tanzania