JINSI YA KUSHINDA ROHO YA KUTOOA NA KUTOOLEWA (HOW TO OVERCOME ANTI-MARRIAGE SPIRIT)
Ninaamini kwamba kuna watu hawataoa au kuolewa hata kama tabia zao zitakuwa ni nzuri kama roho mbalimbali hazitashughulikiwa.
Isaya 10:27 “Tena itakuwa katika siku hiyo mzigo wake utaondoka begani mwako, na nira yake shingoni mwako, nayo nira itaharibiwa, kwa sababu ya kutiwa mafuta.” Neno hili linatia moyo kwamba upako wa Roho Mtakatifu unakwenda kuondoa mzigo uliokulemea na kuvunja nira iliyokufunga ili ufikie ndoto zako zilizoshikiliwa na maadui zako. Mungu anakupenda na anakuwazia mawazo ya amani.
Najua sio watu wote wanafahamu kwamba kuna vifungo vingi katika maisha ya watu. Nitakushirikisha mambo kadhaa ya kukusaidia kuwa huru. Na kama ujumbe huu umekufikia wewe unayewafunga watu wasioe na kuolewa, naagiza moto uteketeze kamba ulizowafungia ili wawe huru katika Jina la Yesu Kristo!
Nitakupa mambo kadhaa ya kukusaidia kutambua ukubwa wa hitaji lako kisha muendee Mungu au mtumishi wa Mungu mwenye mamlaka na neema ya kukuweka huru katika Jina la Yesu Kristo.
Mambo anayofanya shetani ili mtu asioe au kuolewa na mtu sahihi.
1. Shetani anaweza kukufanya uwe na dharau na kauli mbaya kwa kila mtu anayekuja mbele yako. Rebeka hangeolewa kama angekuwa si mkarimu kwa watu wa rika zote. Alimsaidia mtu mzima kunywesha ngamia na kumkaribisha nyumbani kwao. Kumbe huyo mtu alikuwa ametumwa kumtafutia Isaka mke. Kwa bahati mbaya, kuna wasichana wanachekea tu vijana wenzao lakini wanadharau sana watu wazima na wazee hivyo wanakuwa na sifa mbaya katika jamii. Napenda ujue kwamba hakuna mtu ataoa au kuolewa bila kuuliza jamii inayomzunguka kuhusu tabia ya mchumba wake. Mwa 24:12-54
2. Shetani anaweza kukufunga kupitia nguo unazovaliana na wenzako wenye tabia mbalimbali. Kama mwenzako ana tabia mbaya au ni mchawi anaweza kukushughulikia kupitia nguo yako uliyomuazima avae. Pia unaweza kupoteza nguo zako na kumbe rafiki zako wamezipeleka katika madhabahu za wachawi. Lakini pia shetani anaweza kupata nafasi kupitia nguo unazovaa ambazo zimetengenezewa kuzimu zenye majina ya majini au maneno ya makahaba.
3. Shetani anaweza kukulazimisha uoe au uolewe na mtu usiyempenda kwa vile tu huna mamlaka ya kiroho. Kuna dada aliwahi kupangiwa kazi kijijini mahali ambapo hakuna kanisa. Mganga wa kienyeji akamchumbia awe mke wake wa tatu. Yule dada akamshangaa sana na kumwambia huwezi kunioa mimi. Kilichotokea aliugua nusura angekufa ndipo akaambiwa na watu amkubalie yule babu asije akafa. Alipokubali kuolewa mke wa tatu ugonjwa ukaondolewa. Angekuwa na Yesu aliye hai moyoni na kujua kupigana vita vya kiroho haya hayangemkuta. Wapo watu leo waliolazimishwa kuolewa kwa njia za kichawi na sio kwa upendo. Hivyo wanaishi kama watumwa au wakimbizi katika nyumba zao wenyewe.
4. Shetani anaweza kukufunga usioe au usiolewe ili nyota yako itumike kutajirisha watu. Kuna mtu kama ataoa au kuolewa na kuacha kazi aliyoajiriwa kuifanya, biashara hiyo inaweza kuanguka ghafla. Utagundua kwamba umefungwa kama unauza duka halafu akaja mteja wa jinsi tofauti (opposite sex) na kuonyesha kukupenda, huyo bosi wako anachukia sana. Anaweza hata kutishia kukufukuza kazi. Kuna dada alikuwa ameajiriwa kwenye kampuni fulani. Siku moja akamwambia bosi wake kwamba anataka kuolewa. Yule bosi alihamaki akamwambia nakuomba sana usiolewe maana nitafilisika. Niko tayari kukupa chochote lakini naomba usiolewe. Pengine hata wewe unatajirisha watu bila kujua.
5. Shetani anaweza kukufanya uolewe na mapepo. Utaona wanaume unaowajua au usiowajua wakikujia katika ndoto na kukuvalisha pete au kukubaka. Mapepo haya yanaweza kukufanya uwachukie sana wanaume. Kama u mwanaume unaweza kuwachukia sana wanawake. Mwingine anajiwa na jinni mchana kweupe likiwa na sura ya mwanadamu na wala si katika ndoto. Kuna dada alikuwa ameolewa na jinni la namna hii na lilikuwa linamletea shilingi laki moja kila siku asubuhi kwa ajili ya matumizi. Alipompokea Yesu likampokonya vitu vyote lilivyompa na kutoweka.
6. Shetani anaweza kukufanya upate wanaume ambao ni wa kukuchezea tu ila hawataki kukuoa ili kupoteza muda wako, hatimaye uangukie pabaya. Shetani anajua kwamba ni vigumu Mungu kukukutanisha na mtu sahihi wakati unafanya uasherati. Unapohitaji Mungu akusaidie lazima utubu na kuacha dhambi. Vinginevyo shetani kama mshitaki atakuwa kila wakati anamwambia Mungu, Huyu ni wa kwangu, unawezaje kumpa mume au mke kutoka kwako?
7. Shetani anaweza kukuvalisha kinyago uwe na sura ya jinsia nyingine. Kama u mwanaume shetani anakufanya uonekane mwanamke na kama u mwanamke uonekane mwanaume mbele za watu. Anajua kwamba hakuna mtu atapenda kuoa au kuolewa na mtu wa jinsia yake labda kama mtu huyo ni shoga au msagaji. Kuna kipindi niliombea mwanamke fulani ambaye ndoa yake ina mgogoro, pepo likalipuka ndani yake na kusema, “Kimada wa mume wake ametutuma tumvalishe kinyago huyu mama ili awe na sura mbaya kwa mumewe”. Huyu mama alikuwa mcha Mungu lakini pepo lilimuingia na kumtesa kwa vile aliruhusu kuwa na uchungu na mume wake.
8. Shetani anaweza kumtumia kiongozi wa dini mwenye tamaa. Kiongozi wako anaweza kukushinikiza uolewe na mtu kwa faida zake binafsi. Kwa mfano anaweza kukushurutisha uolewe na ndugu yake ambaye si chaguo lako na wala si mcha Mungu. Lakini pia kama uko vizuri kiuchumi na u mtoaji mzuri, mchungaji anaweza kuzuia usiolewe na mtu kutoka kanisa jingine kwa vile ukiondoka kipato kitashuka. Wapo wanaoishi kwa uchungu na majuto katika ndoa zao leo na wengine wamezeekea kanisani bila kuolewa kwa vile walifanywa mitaji ya wachungaji wao.
9. Shetani anaweza kukufanya uchelewe kuombea hitaji la kuoa au kuolewa kiasi kwamba unapoanza kuliombea muda umeenda sana. Unapochelewa sana unaweza kukosa subira na kukosea katika kufanya maamuzi. Utashindwa kumpa Mungu muda wa kumtengeneza mtu ambaye ni chaguo lako. Mungu alipanga kuumba mwanadamu siku nyingi na hakumuumba mpaka alipomtengenezea mazingira. Ilipofika siku ya sita ndipo akamuumba mwanadamu. Hitaji hili linahitaji kuomba mapema ukiwa na mwongozo fulani ili umpe Mungu muda wa kukuandaa, kukuandalia mwenzi anayekufaa na kukukutanisha naye. Mungu ametupa utashi na uhuru wa kuchagua hatima yetu. Ukikosea kuchagua usimsingizie Mungu wala shetani.
10. Shetani anaweza kuhakikisha siku moja unazini na jinni ili uingizwe katika maagano ya kuzimu. Hata kama hutalala na jinni, anaweza kuwa wakala wa shetani ambaye baada ya kuzini naye anachukua mbegu au majimaji na kuyapeleka kufanyiwa kazi kuzimu. Sio wote tunaokutana nao barabarani ni watu. Wengine ni majini yaliyovaa tu sura za watu. Matokeo yake unasaidia kuzimu ipate watoto na kuwaleta duniani kutesa watu wakati huohuo wewe mwenyewe hupati upenyo wowote.
11. Shetani anaweza kutumia maneno ya laana yaliyotamkwa juu yako. Inawezekana kuna siku mzazi au mlezi wako alisema hutafanikiwa, hutaoa, hutaolewa! Usiyapuuzie maneno hayo. Kama alikuwa na sababu inayokubalika katika kusema maneno hayo, laana inaweza kukupata. Laana isiyo na sababu haimpigi mtu (Mit 26:2). Maana yake ni kwamba kama laana ina sababu inampiga mtu. Panapohitaji toba katubu, panapohitaji kufuta kwa damu ya Yesu kafute lakini usikae kimya ukidhani matatizo yataisha yenyewe kwa “kumuachia Mungu”.
12. Shetani anaweza kutumia maagano ya ukoo wenu ambayo hayajavunjwa. Mfano kama katika ukoo wenu waliwahi kuchanjiana damu kwamba mtu asioe mpaka apate ridhaa ya wazee wa ukoo, kitakachotokea kwa mtu anayejaribu kuoa bila kufuata utaratibu huo ni kutofanikiwa. Lazima kuna tatizo litampata kama vile kuzaa mtoto nje kwanza ndipo aoe au kutopata mtoto au ndoa kuvunjika nk. Kuna ukoo ilikuwa mtu akizaa watoto wanne lazima afe mtoto au mama. Iliendelea hivyo mpaka walipogundua ni laana ya shangazi. Walipomuendea na kutubu alitamka maneno ya kufuta laana hiyo ndipo tatizo likakoma.
MAOMBI YANGU KWA AJILI YAKO:
1. Naifuta historia yako mbaya na kuweka sura mpya ya ki-Mungu ndani yako na kibali cha Bwana katika Jina la Yesu Kristo!
2. Nakutoa katika madhabahu za wachawi walioiba nyota yako na
kutangaza mwaka wa Bwana wa kukutana na haja ya moyo wako katika Jina la Yesu
Kristo!
3. Nakutoa katika mitego yote iliyokunasa na kukufanya utende
usiyoyataka katika Jina la Yesu Kristo!
4. Navunja nira ya kutooa na kutoolewa kwa upako wa Roho
Mtakatifu. Nakufungua macho na kukukutanisha na mwenzi wako sahihi katika Jina
la Yesu Kristo!
5. Navunja maagano yanayokufanya uteseke katika ndoa yako katika Jina lipitalo majina yote la Yesu Kristo!
Pokea majibu ya maombi yako uliyomlilia Mungu kwa muda mrefu
katika Jina la Yesu Kristo aliye hai!
Lawi Mshana, Freelance facilitator & Public speaker, +2557129242434, Tanzania