Kama
unaombewa na mtumishi wa jinsi tofauti na wewe, zingatia mambo yafuatayo:
1. Fahamu
historia ya mtumishi anayekuombea. Hakikisha huyo mtumishi
amepona katika maeneo ambayo anakuombea. Usimuendee mtumishi ambaye ndoa
yake mwenyewe imemshinda au yuko karibu na wanawake wengine kuliko mwenzi wake
wa maisha. Usimuamini mtumishi kwa kumtazama tu akiwa anahubiri
madhabahuni. Siku moja nikiwa nafanya semina mahali fulani, mama mmoja
aliniambia kuhusu mabaya yaliyomkuta. Hitaji lake lilikuwa kubwa kwa mchungaji
hivyo mchungaji huyo akampa rufaa aende kwa askofu kuombewa. Huyo mama
aliniambia kwa machozi kwamba alijikuta akianguka kwenye uzinzi na askofu huyo
badala ya kupata ufumbuzi wa tatizo lake. Kipofu akimwongoza kipofu mwenzake,
watatumbukia shimoni wote wawili (Mt 15:14).
2. Ombewa
mahali sahihi. Si vizuri kufanyiwa maombi mkiwa peke yenu kwenye chumba na mlango
umefungwa. Ni vizuri kuwa katika eneo ambalo madirisha na milango iko wazi kama
vile kanisani wakati wa mchana. Hii inasaidia msijaribiwe na muweze kulinda
ushuhuda. Hata hivyo kuna wakati shetani anapenda kuharibu ushuhuda kwa
kulifanya pepo lililolipuka limkimbize nje na kusema ananibaka. Ndiyo maana
katika huduma ya kukemea mapepo haifai mtu awe peke yake. Wakati nafanya semina
Dar, mapepo yalilipuka kwa dada mmoja wakati wa maombezi. Wahudumu walipokuwa
wamembeba wanamleta madhabahuni bila watu kutegemea akavua sketi na hakuwa
amevaa underskirt. Hivi ndivyo shetani anavyofanya ili kuaibisha watu na
kuvuvia wengine roho ya uzinzi. Unadhani hili lingetokea ofisini wakiwa wawili
tu nini kingetokea? Hata kama hawangezini kimwili, wangezini moyoni!
3.
Usipangiwe muda wa kuombewa mara kwa mara bila sababu. Mnapozoeana
kupita kiasi na mtumishi, adui anaweza kupata nafasi. Sio rahisi watu ambao
hawajazoeana kupanga mipango ya kufanya dhambi. Labda kwa waliobobea sana
katika dhambi ya zinaa. Mara nyingi watu wanaanguka wanapofikia hatua ya
kuzoeana sana na kuanza kutaniana kiasi kwamba hawaheshimiani tena. Jifunze
kuweka mipaka katika mahusiano yoyote hasa na watu wa jinsi tofauti na wewe.
Mfano, hakuna sababu ya kuitwa mara kwa mara ili uombewa labda kama katika
vipindi hivyo huendi peke yako. Maombi hayana mipaka hivyo mtu anaweza kuendelea
kuombewa hata akiwa mbali bila kukutana mara kwa mara.
4. Msiwe
na siri kati yenu bila sababu. Mfano msiwe na siri ambazo huwezi
kumwambia mumeo au mtu mwingine wa karibu na wewe. Labda tu kama ni siri ambazo
ukimjulisha mwenzi wako zitaleta madhara ya kiusalama. Mfano, kama umegundua
kwamba amehusika katika jambo fulani la kishirikina kuhusu wewe kv kutaka
kukutoa kafara. Lakini siri za masuala ya ndani ya ndoa mkiwa wawili tu
zinaweza kumsisimua mmoja wenu na kuanza kuvutiwa kimapenzi. Ni vizuri zaidi kuombewa
na mtumishi akiwa pamoja na mkewe au na wahudumu wengine wa jinsi mchanganyiko
(wanaume na wanawake).
5. Kuwa
macho na namna unavyoombewa. Mfano usiruhusu kuombewa kwa
kushikwa shikwa kila sehemu katika mwili wako. Pia omba kimoyomoyo ukivunja roho
zote zilizo kinyume na Mungu kabla hujawekewa mikono. Kuna mtu alibakwa baada
ya kuwekewa mikono. Alipowekewa tu mikono alilala usingizi na alipoamka akahisi
hali ambayo sio ya kawaida. Alihisi kama kuna mtu amemuingilia kimapenzi.
Alipouliza akaambiwa ni uponyaji unaendelea katika mwili wake. Mara nyingi watu
wa aina hii wana viapo ambavyo kama mteja atasema alichotendewa anaweza kufa.
Labda tu kama mteja huyo ataombewa na mtu mwenye mamlaka ya kuvunja maagano ya
kimapepo ndipo aseme alichofanyiwa.
6. Vaa
nguo za heshima unapoenda kuombewa ili uwe salama na usiwatie majaribuni
watumishi wa Mungu. Vaa gauni la heshima, refu ambalo halijakubana badala ya
sketi fupi na blauzi fupi kwa vile ni rahisi kufunuka hasa mapepo yakilipuka.
Hata hivyo ndani unaweza kuvaa nguo zilizokubana vizuri ili isiwe rahisi
ukikumbana na mtu anayetaka kukubaka. Sio tu katika kuombewa bali hata safarini
katika mazingira hatarishi. Kumbuka mtumishi anayeombea anaweza kuwa dhaifu
kiroho au anaweza kuwa amebobea katika kuzini na watu anaowaombea. Ukiwa
hujavaa nguo za heshima unaweza kumfanya ajaribiwe hata kama hakuwa amekusudia
kwa vile na yeye ni mwanadamu. Neno la Mungu limetuonya kwamba tusimpe Ibilisi
nafasi. (Efe 4:27)
Lawi Mshana, Freelance Facilitator & Public Speaker,
+255712924234, Tanzania