TATIZO LAKO NI KUBWA LAKINI MUNGU AMEKUTENGENEZEA UTARATIBU MAALUM WA MAJIBU YAKO
Ni ukweli usiopingika kwamba kuna mahitaji hatupokei majibu yake kwa sababu tu hatujaweza kuzingatia kanuni fulani. Wakati mwingine tunapokea majibu kwa muda mfupi tu lakini hayawi ya kudumu.
Tuangalie andiko la Yn 5:1-11 kwa ajili ya kanuni muhimu za kutusaidia:
1. Tambua mahali sahihi pa kusubiria
Mst 3-4 “Ndani ya hayo jamii kubwa ya wagonjwa walikuwa wamelala, vipofu, viwete, nao waliopooza, wakingoja maji yachemke. Kwa maana kuna wakati ambapo malaika hushuka, akaingia katika ile birika, akayatibua maji. Basi yeye aliyeingia wa kwanza baada ya maji kutibuliwa, akapona ugonjwa wote uliokuwa umempata.”
Hawa watu walijua mahali sahihi pa kusubiria kwa vile walipata ushuhuda wa majibu ya wengine waliowatangulia. Ukifuatilia sana utagundua kwamba watu wenye mahitaji maalum katika maeneo mbalimbali hawakai popote tu. Wanakaa mahali ambapo wanapita watu wengi na pengine wanaotoka benki, sokoni au ibadani kwa maana kwamba kuna uwezekano wana pesa ya ziada au ni watu wenye huruma wanaoenda kuabudu. Hii ndiyo sababu hata kipindi cha Biblia kiwete aliwekwa na ndugu zake katika mlango wa kuingilia hekaluni. Mdo 3:2 “Na mtu mmoja aliyekuwa kiwete toka tumboni mwa mamaye alichukuliwa na watu, ambaye walimweka kila siku katika mlango wa hekalu uitwao Mzuri, ili aombe sadaka kwa watu waingiao ndani ya hekalu.”
Hata Zakayo hakupanda mkuyu wowote tu. Alijiridhisha kwanza kwamba Yesu atapitia njia hiyo. (Lk 19:4 “Akatangulia mbio, akapanda juu ya mkuyu apate kumwona, kwa kuwa atakuja kuipitia njia ile.”)
Swali la kujiuliza: Ni kweli hapo ndipo mahali sahihi pa kusubiria majibu yako? Kuna uwezekano wa kupata mwenzi wa maisha wa vigezo ulivyoomba hapo unaposubiria?
2. Ukubwa wa tatizo lako usikukatishe tamaa
Mst 5-7 “Na hapa palikuwa na mtu, ambaye amekuwa hawezi muda wa miaka thelathini na minane. Yesu alipomwona huyu amelala, naye akijua ya kuwa amekuwa hali hiyo siku nyingi, alimwambia, Wataka kuwa mzima? Yule mgonjwa akamjibu, Bwana, mimi sina mtu wa kunitia birikani, maji yanapotibuliwa; ila wakati ninapokuja mimi, mtu mwingine hushuka mbele yangu.”
Hapa kuna mambo kadhaa ya kujifunza:
(i). Huyu mtu alikuwa na tatizo la miaka mingi ambalo lilimzuia kuwahi maji
yanapotibuliwa lakini hakukata tamaa na kurudi nyumbani. Alichojali ni
kusubiria mahali sahihi. Hata wewe usikate tamaa, unakaribia kukumbukwa na
Mungu.
(ii). Yesu alijua tatizo lake siku nyingi na kwamba hawezi kuwahi maji yakitibuliwa. Hivyo siku moja akaamua kumtengenezea utaratibu mwingine maalum (upendeleo wa Mungu). Yeremia 31:22 “Hata lini utatanga-tanga, Ee binti mwenye kuasi? Kwa maana Bwana ameumba jambo jipya duniani; mwanamke atamlinda mwanamume.”
(iii). Huyu ndugu alieleza kikwazo chake cha kupokea majibu na wala hakumlaumu Mungu. Aliona ni haki Mungu kuponya mtu mmoja anayewahi maji yanapotibuliwa na kuacha wengine wasubiri. Ila akasema tatizo lake ni kukosa mtu wa kumuwahisha – inawezekana ndugu zake walishakata tamaa wakamtelekeza.
(iv). Huyu ndugu aliwaza njia moja tu ya majibu yake. Pengine alidhani Yesu ni mtu fulani tu ambaye anataka kumsaidia maji yakitibuliwa amuwahishe. Kumbe ndiye Mponyaji Mkuu aliyepanga ratiba ya malaika kushuka siku fulani. Hata wewe unadhani baraka zako ziko kwenye hiyo shughuli unayofanya tu. Pengine Mungu anataka kukupa kazi mpya ambayo hujawahi kuiwaza wala kuifanya.
Kumbuka Yesu alipitia pale kwa ajili ya KUMPONYA YEYE TU akitokea kwenye sikukuu ya Wayahudi na hakuhangaika na wagonjwa wengine ambao wanaweza kufuata utaratibu wa kuwahi malaika akitibua maji (Yn 5:1-2). Sio lazima unachotendewa wewe na mwenzako atendewe hivyohivyo. Hakuna mtu anaweza kutembea na muujiza wako.
3. Tii maelekezo hata kama huna uzoefu nayo na hutaeleweka
Mst 8-9 “Yesu akamwambia, Simama, jitwike godoro lako, uende. Mara yule mtu akawa mzima, akajitwika godoro lake, akaenda. Nayo ilikuwa ni sabato siku hiyo.”
Uzoefu ni jambo muhimu sana katika maisha. Lakini wakati mwingine uzoefu ni adui wa ufunuo wa Mungu. Unapozoea sana maisha fulani unaweza kushindwa kutumia imani yako katika kukufanyia mambo makubwa. Daktari anayejua ini liko upande gani na tafsiri ya maumivu anayopata, anaweza kufa kwa wasiwasi wakati mgonjwa asiyesoma anapachukulia kawaida tu. Hebu jiulize, unaishi na ulemavu kwa miaka 38 halafu unaambiwa, Jitwike godoro lako uende. Ni rahisi kusema siwezi. Huyu ndugu alipotii na kujaribu kulinyanyua godoro, akashangaa akitiwa nguvu za Mungu. Hata wewe kuna mambo unaweza ambayo hujasomea shuleni wala chuoni lakini akili yako inakuambia huwezi kwa vile hujasomea. Badilika leo! Usiruhusu chuo kikuwekee mipaka katika maisha yako. Wala usiogope watu wakiona umebeba godoro siku ya sabato. Hawana msaada na wewe siku unapolala njaa. Usikubali waidharau kazi yako ambayo ni ya halali na inasaidia kutimiza mahitaji yako.
4. Huwezi amini - kuna watu wanatamani na wanaomba ubaki na tatizo lako milele
Mst 10-11 “Kwa sababu hiyo Wayahudi wakamwambia yule aliyeponywa, Leo ni sabato, wala si halali kwako kujitwika godoro. Akawajibu, Yeye aliyenifanya kuwa mzima ndiye aliyeniambia, Jitwike godoro lako, uende.”
Tangu huyu ndugu ahamishiwe birikani ili kusubiri muujiza wake inawezekana kuna ndugu zake wanalima mashamba yake. Unadhani watafurahi kusikia kwamba amepona? Kuna mtu akifufuka leo ndugu zake watatafuta njia ya kumuua kwa vile alipokufa tu walibadilika kabisa na kupokonya familia yake mali zote.
Hebu jiulize badala ya mtu kukusindikiza ukamshukuru Mungu kwa kukuponya baada ya ulemavu wa miaka 38, yeye anakuambia LEO SIO SIKU YA KUBEBA MAGODORO. Utamuelewa kweli! Umezungukwa na watu kama hawa wengi sana. Hawezi kufurahi kwamba umejenga nyumba yako, umeingiza bomba la maji katika nyumba yako, umechumbiwa, umeolewa/umeoa, umepata kazi, biashara yako inakua, ndoa yenu ina amani na upendo nk. Hata hivyo Mungu ameumba jambo jipya kwa ajili yako leo – POKEA UPENDELEO WA MUNGU WALIOPOKEA WANA WA ISRAELI WAKATI WAKITOKA MISRI.
Kutoka 11:2,3 “Basi nena wewe masikioni mwa watu hawa, na kila mtu mume na atake kwa jirani yake, na kila mwanamke atake kwa jirani yake, vyombo vya fedha, na vyombo vya dhahabu.Bwana akawapa watu hao kibali machoni pa Wamisri. Zaidi ya hayo, huyo Musa alikuwa ni mkuu sana katika nchi ya Misri, machoni pa watumishi wa Farao, na machoni pa watu wake.”
Hata hivyo nikutahadharishe kwamba unapopewa kibali (favor) lazima ufanye kitu. Anza kusalimia watu na kuwabariki hata kwa kidogo ulicho nacho ili ujenge mahusiano. Hakuna mtu hata kama ni tajiri asiyefurahi akipewa zawadi. Acha mtazamo wa kutaka tu kusaidiwa bila wewe kufanya chochote.
Maombi ya
wiki hii:
1. Ee Mungu nifunulie nijue mahali
sahihi pa kusubiria majibu yangu ili nisipishane na muujiza wangu.
2. Ee Mungu nisaidie nisione kwamba
tatizo langu limekuwa kubwa kuliko uwezo wako wa kuliondoa.
3. Ee Mungu niwezeshe kutii maelekezo
yako hata kama hayaingii akilini ili nisijicheleweshe mwenyewe
4. Ee Mungu nisaidie kujua kwamba sio wote wanasikitika wanapoona tatizo langu. Wengine wanashangilia ninavyoteseka. Ila umemtuma Yesu ili niwe na uzima tele.
Tangazo
Download (pakua) na install (sakinisha) App yangu kwenye
simu yako ili upate masomo yote kwa maandishi na kwa video (Kiswahili na
Kingereza) bure na kwa wepesi kupitia kiungo hiki https://www.appcreator24.com/app2584201-q514wi. Usiache kutoa ushuhuda wa yale Mungu
anayokutendea kupitia huduma hii ili tumpe Mungu utukufu.
Lawi Mshana