Ticker

6/recent/ticker-posts

“AGIZO KUU” SIO KWENDA KANISANI BALI NI “KUWA KANISA”


 “AGIZO KUU” SIO KWENDA KANISANI BALI NI “KUWA KANISA”

NB: Jipatie mafundisho ya UANAFUNZI na USHUHUDIAJI kwa Video na Audio

Napenda kukushirikisha somo hili kwa ‘miwani ya Neno la Mungu’ na sio kwa ‘miwani ya kidini na kimadhehebu.’ Wengi wetu tunafahamu uzito wa maneno ya mwisho ya mtu anayekaribia kuondoka duniani. Wengi wakiona mtu muhimu katika ukoo amezidiwa au anakaribia kufa, wanatamani sana kusikia atawapa wosia gani. Mtu akiupuuza maneno yake anakiona cha mtema kuni. Kama alisema akifa jambo fulani lisifanyike, watu wakilipuuza wanaweza kupata matatizo mbalimbali.

Kwa hiyo maneno ya mwisho ya Bwana Yesu kabla ya kuondoka duniani (kupaa), yana uzito mkubwa na yalipewa jina la AGIZO KUU (THE GREAT COMMISSION). Maneno hayo yanapatikana katika Mt 28:16-20 “…18 Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.19 Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; 20 na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.”

Baada ya Bwana Yesu kutambulisha mamlaka yake ilivyo kubwa baada ya kufa na kufufuka, aliwapa wanafunzi wake majukumu yafuatayo:

1. Enendeni (go) – Marko alielezea kwa upana kwamba watu waende wapi kufanya nini. Mk 16:15,16 “Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa.” WANAFUNZI WA KIPINDI HICHO NA SISI WA LEO, TUMEAGIZWA KWENDA DUNIANI KUHUBIRI INJILI. Rum 10:15b “Ni mizuri kama nini miguu yao wahubirio habari ya mema!” Bwana hakuagiza wanafunzi wake WAENDE KANISANI, bali aliwaagiza WAWE KANISA. Kanisa sio jengo bali ni walioitwa na Bwana kwa kusudi maalum (ekklesia). Watu hao ambao ni Kanisa wamepewa nguvu ya kushinda milango ya kuzimu. Mathayo 16:18 “Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda.” Kanisani ni kituo tu cha WALIOOKOKA kupeana mikakati, maelekezo, kumuabudu Mungu na kuonyana lakini kazi halisi ya Agizo Kuu inafanyika nje ya hapo. Waebrania 10:25 “wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia.” Wakolosai 3:16 “Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu.”

2.  Mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi – Tafsiri nzuri ya neno ‘ethnos’ au ‘ethnic groups’ liliotafsiriwa ‘mataifa’ ni ‘makabila’ (katika mazingira yetu) Kila kabila lifikiwe na Injili na kisha WAFANYWE au WATENGENEZWE KUWA WANAFUNZI. Agizo kuu sio kuongeza idadi ya washirika/washarika kwenye dhehebu ambao kazi yao ni kuombewa na kupiga makofi tu lakini hawana na wala hawatafuti uhusiano na Mungu. Washirika/washarika WANAJIUNGA na dhehebu kama wanachama lakini wanafunzi WANATENGENEZWA.

Kwa mujibu wa Maandiko Matakatifu mtu ambaye hajampokea Yesu kama Mwokozi sio mkristo na wala sio kanisa bali ni mshirika au msharika. Jina la msharika liko kwenye kitabu cha dhehebu lake lakini sio kwenye Kitabu cha uzima cha Mwanakondoo wa Mungu. Tuwe macho sana tunaoendelea kuabudu na kutumika kwa kuchunga makanisa, kuhubiri na kuimba wakati hatujampokea Yesu na kumuishia. Kuna siku tutaaibika hata kama tutazikwa vizuri kama hatutachukua hatua. Ufu 20:15 “Na iwapo mtu ye yote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto.”

Kipindi chetu tunapenda sana kupima matokeo ya huduma kwa idadi ya washirika/washarika lakini kipindi cha kanisa la kwanza walijali zaidi kuwa na wanafunzi. Hawa wanafunzi walianza kuitwa Wakristo huko Antiokia. Mdo 11:26 “hata alipokwisha kumwona akamleta Antiokia. Ikawa kwa muda wa mwaka mzima wakakusanyika pamoja na kanisa na kuwafundisha watu wengi. Na wanafunzi waliitwa Wakristo kwanza hapo Antiokia.” Mtume Paulo alidiriki kumwambia Timotheo asipoteze muda kufundisha mafundisho aliyopokea kwake kwa watu ambao sio waaminifu na hawayapeleki kwa watu wengine. Hata wewe utakufa na maono yako kama unafundisha tu watu ambao wanajijali wenyewe. 2 Tim 2:2 “Na mambo yale uliyoyasikia kwangu mbele ya mashahidi wengi, hayo uwakabidhi watu waaminifu watakaofaa kuwafundisha na wengine.” Sio mpango wa Mungu uingie na kutoka kanisani au uhubiri na kuimba siku za ibada tu. Kumfanya mtu kuwa mwanafunzi kunahitaji uhusiano wa mtu na mtu na sio kufundisha kikundi au semina. Sijui una wanafunzi wangapi ambao nao wana wanafunzi pia. Paulo alijali MTU MMOJAMMOJA na sio KIKUNDI katika kufanya uanafunzi. Angalia jinsi alivyotumia neno KILA MTU mara tatu. Wakolosai 1:28 “ambaye sisi tunamhubiri habari zake tukimwonya kila mtu, na kumfundisha kila mtu katika hekima yote, tupate kumleta kila mtu mtimilifu katika Kristo.”

3. Mkiwabatiza kwa jina la Baba, Mwana na Roho Mtakatifu – Ubatizo ni tendo linalotakiwa kufanyika baada ya mtu kumwamini Yesu na kusajiliwa katika kitabu chake cha uzima. Marko 16:16 “Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa.” Hata kipindi cha safari ya Wana wa Israeli kutoka Misri kwenda Kanani, hawakubatizwa wakiwa Misri. Walihesabika kuwa wamebatizwa baada ya kuamini Musa ni kiongozi wa kuwapeleka Kanani na walipovuka bahari ya Shamu. 1 Wakorintho 10:2 “wote wakabatizwa wawe wa Musa katika wingu na katika bahari.” Hata Bwana Yesu alifuata utaratibu huu wa kubatizwa. Lk 3:21,22 “Ikawa, watu wote walipokwisha kubatizwa, na Yesu naye amebatizwa, naye anaomba, mbingu zilifunuka. Roho Mtakatifu akashuka juu yake kwa mfano wa kiwiliwili, kama hua; sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe.” Jiulize kwanini siku Yesu alipobatizwa ndipo mbingu zilifunguka na sauti kutoka mbinguni ikasema, HUYU NDIYE MWANANGU MPENDWA, NIMEPENDEZWA NAYE!

4. Muwafundishe yote niliyowaamuru 

Tuhakikishe mafundisho tunayofundisha hayapingani na Biblia. Usichague maneno unayotaka kusikia kwa vile tu yamesemwa na kiongozi mkubwa. Ni Yesu peke yake aliyeshinda kifo na mauti na atakayetuhukumu. Fuata mafundisho yenye uzima (sound doctrine) badala ya kutafuta wahubiri wanaokufurahisha wakati hawakusaidii kufikia viwango vya Mungu. 2 Timotheo 4:3 “Maana utakuja wakati watakapoyakataa mafundisho yenye uzima; ila kwa kuzifuata nia zao wenyewe watajipatia waalimu makundi makundi, kwa kuwa wana masikio ya utafiti.”

Kila tunachofundisha leo tutatoa hesabu yake siku ya mwisho na tutapata hukumu kubwa kama tunawapotosha watu au kuwaambia watu wafanye mambo ambayo hatuna uhakika nayo. Yakobo 3:1 “Ndugu zangu, msiwe waalimu wengi, mkijua ya kuwa mtapata hukumu kubwa zaidi.” 2 Timotheo 3:14 “Bali wewe ukae katika mambo yale uliyofundishwa na kuhakikishwa, kwa maana unajua ni akina nani ambao ulijifunza kwao.” 

Kumbuka Bwana Yesu ameahidi kwamba hatawaacha wote watakaofuata haya maelekezo na maagizo yake hadi atakaporudi tena kwa ajili yao. Tusipoangalia Mungu atatuacha tupambane wenyewe na maisha yetu. Mt 28:20b “na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.”

Usisahau pia kwamba hata watoto ambao wanajua mema na mabaya watapotea kama hawajaokoka. Waliookoka wana malaika maalum kwa ajili yao. Hukumu ya watu wanaokosesha watu waliomuamini Yesu ni kubwa sana. Mt 18:6,10 “bali atakayemkosesha mmojawapo wa wadogo hawa waniaminio, yamfaa afungiwe shingoni jiwe kubwa la kusagia, na kutoswa katika kilindi cha bahari. Angalieni msidharau mmojawapo wadogo hawa; kwa maana nawaambia ya kwamba malaika wao mbinguni siku zote huutazama uso wa Baba yangu aliye mbinguni.”

Tangazo

Wewe unayehitaji kufanya huduma ya USHUHUDIAJI na UANAFUNZI kwa utaratibu ulioelekezwa katika Neno la Mungu unaweza kuagiza masomo hayo utumiwe kwa mtandao kwa Tsh 12,000 (yote kwa pamoja). Yanapatikana kwa Video na Audio. Somo la jinsi ya kufanya ushuhudiaji ni video/audio 3 na uanafunzi ni video/audio 4.

 

Lawi Mshana, 0712-924234; mshanalawi@gmail.com