Ticker

6/recent/ticker-posts

KIPANDE CHA USHAURI - USILEMAZWE NA UJUZI RASMI WA CHUO


KIPANDE CHA USHAURI (A PIECE OF ADVICE)

USILEMAZWE NA UJUZI RASMI WA CHUO

KAZI zipo nyingi ila AJIRA ni chache na zitaendelea kuwa chache kwa vile vyuo havijasimama kutoa mafunzo. Kila mwaka mamia ya watu wanamaliza vyuo. Miaka ya zamani ilikuwa kabla mtu hajamaliza chuo ameshabukiwa kwa ajili ya kuajiriwa mahali fulani.

Tusisahau kwamba pamoja na ajira kupungua, mahitaji yanazidi kungezeka kwa vile idadi ya watu inaongezeka. Hata hivyo, ingawa mahitaji yanaongezeka, yako tofauti na yale ya miaka iliyopita. Lazima tubadilike kwa haraka sana kama soko linavyobadilika. TUSITAFUTE KAZI BALI TUTAFUTE KUJUA MAHITAJI YALIYOPO NDIPO TUWEKEZE MITAJI YETU. Mfano, watu walikuwa wanauza CD na DVD, sasa watu wanatumia flashi. Hivyo watu wamehamia mtandaoni kulipwa kadiri idadi ya wafuasi inavyokuwa kubwa nk. Zamani tulijitahidi sana kujua kompyuta (computer application), sasa kuna watu hawajui kompyuta ila wanajua teknolojia ya kidijitali (digital technology) na wanapata pesa kupitia simu janja tu. Simu yako inaweza kuwa ni mtaji mkubwa sana ila umeamua kuitumia tu kwa kuchati na kujipiga picha.

Zipo kazi ambazo zinaweza kukutoa kimaisha na hakuna siku utaulizwa cheti. Wanachotaka walaji wako ni ubora na upatikanaji wako tu. Hebu jiulize, lini ulimuuliza fundi simu akuonyeshe cheti chake? Umemuamini kwa vile tu rafiki au majirani zako walikupa sifa yake katika kukarabati simu.

 Hata hivyo tatizo lako una ujuzi wa juujuu wa masuala mbalimbali. Hutaki kubobea katika kazi fulani hata kama ni kwa kozi fupi. Kazi zisizo rasmi hazihitaji cheti lakini zinahitaji sana UWEZO na UMAHIRI. Mtu mwenye cheti anaweza kuajiriwa bila kuwa na uwezo mkubwa. Anaweza kujificha nyuma ya wafanyakazi wenzake wenye uwezo. Lakini kazi isiyo rasmi cheti chake ni uwezo wako wa kumshawishi mteja wako kwamba unaweza. Jitahidi kuijua shughuli yako kwa kina hata kwa kulipia kozi fupi! Usifanye shughuli yako kienyeji. Hata kama ni shughuli ya mtaji mdogo sana, IFANYE KISASA NA KWA UBORA ILI IHESHIMIKE.  

 Lawi Mshana