Sikiliza pia ujumbe kuhusu hatari ya kutolipa madeni
KUOKOKA HAKUMPI MTU UHALALI WA KUBAKI NA VITU VYA WIZI
Ni ukweli usiopingika kwamba Bwana Yesu alikuja duniani kutafuta na kuokoka kile kilichopotea. Luka 19:10 “Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.” Tunapookolewa tunaanza mchakato wa kusafishwa hadi tuwe watu wa milki ya Mungu ili mradi tuonyeshe juhudi katika matendo mema. Tito 2:14 “ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, ili atukomboe na maasi yote, na kujisafishia watu wawe milki yake mwenyewe, wale walio na juhudi katika matendo mema.”
Tumeokolewa kutoka dhambini na tunaendelea kuokolewa na dunia hii mbovu iliyopo sasa halafu tukidumu katika matendo mema tutaokolewa na ghadhabu itakayokuja. Kwa hiyo kuokoka ni tukio la wakati uliopita, uliopo na ujao. 1 Wathesalonike 1:10 “na kumngojea Mwanawe kutoka mbinguni, ambaye alimfufua katika wafu, naye ni Yesu, mwenye kutuokoa na ghadhabu itakayokuja.”
Kuokoka ni zaidi ya kuongozwa sala ya toba. Lazima mabadiliko ya maisha yatokee baada ya kukutana na Bwana Yesu. 2 Wakorintho 5:17 “Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya.” Kimsingi andiko hili linatuambia kwamba mtu anapookoka anaanza safari ya maisha mapya. Andiko hili halina maana ameshafika mwisho wa safari yake bali ameanza safari ya kutoka Misri kuelekea Kanani. Anaweza kuanza hii safari na asifike mwisho. Hata wana wa Israeli wanaume laki sita (takriban milioni tatu ukihesabu na wanawake na watoto) walianza safari Misri lakini waliofika Kanani ni wawili tu, ukiacha wale waliozaliwa njiani. Hata hivyo nafuu aliyeamua kuanza safari kuliko yule ambaye ameamua kubaki Misri. Aliyebaki Misri anatangaza wazi kwamba amemkubali shetani na hatambui kazi aliyoifanya Bwana Yesu msalabani hata kama anasherehekea Pasaka na Kuzaliwa kwa Yesu.
Pengine unasema lakini si Yesu amenilipia deni la dhambi zangu msalabani? Uko sahihi kabisa. Lakini huyohuyo Yesu alisema uchukue msalaba wako umfuate. Kuna masuala ambayo yanakuhusu wewe mwenyewe. Tofautisha MSALABA WA YESU na MSALABA WA KWAKO! Mathayo 16:24 “Wakati huo Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate.”
Lazima toba iambatane na malipizo – huwezi kutubu kwa maneno tu
1. Zakayo
Lk 19:8-10 “Zakayo akasimama, akamwambia Bwana, Tazama, Bwana, nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyang'anya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne. Yesu akamwambia, Leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu. Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.”
Zakayo aliokoka kwa imani lakini alithibitisha kwamba ameokoka kwa matendo yake. Bwana Yesu alimpongeza kwamba kweli ameokoka kwa uamuzi wake wa kuwalipa aliowadhulumu. Unaloweza lifanye. Usiloweza Mungu atakurehemu. Lakini huwezi kupasua chupa ya mtu uliyomuomba na kusema tu nisamehe wakati una uwezo wa kumnunulia nyingine!
2. Waganga wa kienyeji
Waganga walipookoka walichoma vitabu vyao tena vyenye thamani kubwa. Nadhani ilikuwa ni zaidi ya tunguli kwa vile walivithaminisha wakajua vilivyokuwa vya bei kubwa. Hilo ndio tendo la toba ya kweli. Matendo ya Mitume 19:19 “Na watu wengi katika wale waliotumia mambo ya uganga wakakusanya vitabu vyao, wakavichoma moto mbele ya watu wote; wakafanya hesabu ya thamani yake, wakaona ya kwamba yapata fedha hamsini elfu.”
Je wewe?
Huwezi kuiona mbingu kama umeokoka lakini unaendelea kutumia vitu vya wizi au kuishi na mume au mke wa wizi! Najua unaweza kusema, “Mbona pamoja na kuishi naye nimejazwa Roho Mtakatifu, ninanena kwa lugha, Mungu amenibariki na ninatumiwa kwa miujiza?” Napenda ujue jambo la msingi kwamba Mungu hakumtuma Roho Mtakatifu kwa ajili ya watakatifu. Alimtuma kwa ajili ya kutututakasa. Kwa hiyo hayuko ndani yako kwa sababu ya utakatifu wako. Lakini pia tunatakiwa KUIAMINI KWELI yaani NENO LA MUNGU. 2 Wathesalonike 2:13 “Lakini imetupasa sisi kumshukuru Mungu sikuzote kwa ajili yenu, ndugu mliopendwa na Bwana, kwa kuwa Mungu amewachagua tangu mwanzo mpate wokovu, katika kutakaswa na Roho, na kuiamini kweli.” Usipoamua kubadilika, Roho Mtakatifu ataendelea kukutumia kama kibao cha kuelekeza wengine wakati wewe mwenyewe uko kwenye hali hiyohiyo siku zote. Mtume Paulo aliwahi kugundua ukweli huu akatutahadharisha. 1 Wakorintho 9:27 “bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha; isiwe, nikiisha kuwahubiri wengine, mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa.”
Kusema Bwana asifiwe na kutumiwa kwa miujiza hakutakuokoa kama huyafanyi mapenzi ya Mungu. Mt 7:21-23 “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.”
Ndoa inaanzia kwa wazazi na sio kanisani
Ezra 10:3 “Haya basi! Na tufanye agano na Mungu wetu, kuachana na wake zetu, na wale waliozaliwa nao, tukilifuata shauri la bwana wangu, na shauri la hao wanaoitetemekea amri ya Mungu wetu; mambo haya na yatendeke kwa kuifuata torati.”
Kazi ya Kanisa ni kuibariki tu. Ndiyo maana tunafunga ndoa baada wachumba kumalizana kwa wazazi wao. Hivyo kuishi na mtoto wa watu bila kumlipia mahari au kumaliza mahari kunaweza kukugharimu hata kama una cheti cha ndoa. Labda tu kama ulipewa mke bure bila kutajiwa mahari ya kulipa. Hapo unawapa zawadi tu kama unavyojisikia. Usipende kuishi na deni la kuoa kwa sababu mizimu inaweza kuwa na haki ya kuifuatilia ndoa yenu. Afadhali usioe kama umetajiwa gharama usiyoimudu kuliko kuitikia tu halafu badae ushindwe kulipa. Kumbuka ndoa ni agano na sio kama watu waliopanga (cohabiting).
Usipolipa gharama ya wizi kimwili utailipa kiroho
Kut 22:1-5 “1 Mtu akiiba ng'ombe au kondoo, na kumchinja, au kumwuza; atalipa ng'ombe watano badala ya ng'ombe mmoja, na kondoo wanne badala ya kondoo mmoja. 2 Mwivi akipatikana akiwa yu hali ya kuvunja mahali, naye akapigwa hata akafa, hapatakuwa na malipizo ya damu kwa ajili yake. 3 Lakini kama jua limekucha juu yake, ndipo patakuwa na malipizo ya damu kwa ajili yake; ingempasa kutoa malipo kamili; akiwa hana kitu, na auzwe kwa ajili ya wivi wake. 4 Kama hicho kitu kilichoibwa chapatikana hai mkononi mwake, kama ni ng'ombe, au punda, au kondoo; atalipa thamani yake mara mbili. 5 Mtu akilisha katika shamba, au shamba la mizabibu, akimwacha mnyama wake, akala katika shamba la mtu mwingine; atalipa katika vitu vilivyo vizuri vya shamba lake mwenyewe, au vya mizabibu yake.”
Lipi deni la watu. Usiishi na mkopo nyumbani kwako! Zaburi 37:21 “Asiye haki hukopa wala halipi, Bali mwenye haki hufadhili, hukirimu.” Nilijua ukweli huu hivyo nilihakikisha nalipa mahari yote kabla ya kuoa.
Najua utasema haya mambo ni ya Agano la kale. Lakini je mbona unanukuu Agano la Kale kwamba wewe ni kichwa na sio mkia? Tambua Agano la Kale ni kivuli cha mambo yajayo. Mambo pekee ya Agano la Kale ambayo hatuyafanyi ni yale ambayo Bwana Yesu ameyakamilisha alipokuja kama vile kuomba ukombozi kwa kuchinja wanyama. Tayari Yesu ni mwanakondoo wa Mungu aliyechinjwa. Yohana 1:29 “Siku ya pili yake amwona Yesu anakuja kwake, akasema, Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu!”
Maswali ya kujiuliza
1. Hivi unaweza kutubu na kumuomba Mungu
atakase kitu ulichoiba halafu uendelee kukitumia na bado uwe na amani ya kweli
moyoni?
2. Hivi unaweza kumuomba Mungu akurehemu kwa dhambi yako ya kuishi na mume au mke wa mtu bila kufanya maamuzi ya kumuacha?
Lakini napenda pia ujue kwamba ukishaizoelea dhambi DHAMIRI YAKO INAKUFA hivyo hujisikii hatia tena moyoni. Hii haina maana kwamba uko salama bali ina maana kwamba Roho wa Mungu amekuacha. Rum 2:14,15 “Kwa maana watu wa Mataifa wasio na sheria wafanyapo kwa tabia zao yaliyo ndani ya torati, hao wasio na sheria wamekuwa sheria kwa nafsi zao wenyewe. Hao waionyesha kazi ya torati iliyoandikwa mioyoni mwao, dhamiri yao ikiwashuhudia, na mawazo yao, yenyewe kwa yenyewe, yakiwashitaki au kuwatetea; katika siku ile Mungu atakapozihukumu siri za wanadamu, sawasawa na injili yangu, kwa Kristo Yesu.” 1 Samweli 18:12 “Sauli akamwogopa Daudi, kwa sababu Bwana alikuwa pamoja naye, ila amemwacha Sauli.”
Hakuna jambo lolote tunaloweza kumficha Mungu. Hata kama wanaokuzunguka hawajui, shetani ambaye ni mshitaki wetu anajua ni kitu gani unachokifanya ambacho kitazuia lango la mbinguni kufunguka kwa ajili yako. Kumbuka shetani anajua sana mbinguni na vigezo vya kuingia huko. Mungu si zaidi? Waebrania 4:13 “Wala hakuna kiumbe kisichokuwa wazi mbele zake, lakini vitu vyote vi utupu na kufunuliwa machoni pake yeye aliye na mambo yetu.”
Najua makala kama hizi hazipendezi wengi. Lakini kuna siku utatamani kuambiwa ukweli huu lakini utakuwa umechelewa.
Mungu atusaidie sana!
Niulize maswali kibinafsi kama una nia ya kujifunza kuijua kweli na sio kujilinda kana kwamba uliwahi kufika mbinguni. Hukumu ya Mungu itazingatia Neno la Mungu na sio tafsiri ya dini yako wala kiongozi wako.
Dr. Lawi Mshana, +255712-924234 (sms au
whatsapp), Korogwe, Tanga, Tanzania