Ticker

6/recent/ticker-posts

Unaweza kuwa na tatizo usilolijua? (maandishi na video ya kuwekwa huru)

Unaweza kuwa na tatizo usilolijua? (video)

Unaweza kuwa na tatizo usilolijua?

Mtu mmoja alimpeleka ndugu yake hospitalini ili akapimwe macho. Madaktari wakamshauri na yeye pia apimwe. Alishangaa sana kugundua kwamba yeye ndiye mwenye matatizo makubwa ya macho kuliko yule ndugu yake aliyemsindikiza. Nimegundua kwamba nikiita wagonjwa mbele ili niwaombee kuna watu hawatapita kwa vile hawajui ni wagonjwa. Hivyo kuna wakati naombea kila mmoja kwa kumfuata pale alipo. Nimeshangaa mara nyingi kuona mapepo yakilipuka kwa watu ambao walidhani ni wazima na pengine ndio waliowasindikiza wagonjwa wanaohitaji maombezi. Ukiwafuatilia sana watu hawa ingawa wanadhani hawana tatizo utagundua wana matatizo mojawapo kati ya haya:

1. Ana woga na kuhisi kama kuna mtu anamfuatilia ingawa hamuoni kwa macho.

2. Kila anachoanzisha hakifanikiwa hata kama atapewa mtaji mzuri. Lazima apoteze kila kitu.

3. Hata anapopata pesa hawezi kutoka kwenye utumwa wa madeni na shetani anataka kumuaibisha.

4. Anaota ndoto za umaskini na kubakwa kwenye ndoto na watu anaowajua au asiowajua.

5. Kuna sehemu ya mwili inamuuma lakini ugonjwa hauonekani hospitalini au hausikii dawa. Wakati mwingine ugonjwa huo unampata katika msimu fulani kila mwaka.

6. Hana mahusiano ya kudumu. Lazima faraka itokee bila sababu ya msingi na kumuacha na maumivu. nk

Napenda kutumia Yohana 8:31-36, 39-42 kukushirikisha mambo ya msingi kuhusu maisha yako

1. Unaweza kumwamini Yesu lakini usikae katika Neno lake na usiwe mwanafunzi wake wa kuaminika

Mst 31 “Basi Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli.”

2. Unaweza kumwamini Yesu na bado hujaijua kweli na bado shetani anakutumikisha

Mst 32 “tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru.”

3. Unaweza kuwa na sifa zote za kidini lakini bado unamtumikia shetani

Mst 33 “Wakamjibu, Sisi tu uzao wake Ibrahimu, wala hatujawa watumwa wa mtu wakati wo wote; nawe wasemaje, Mtawekwa huru? Yesu akawajibu, Amin, amin, nawaambia, Kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi.”

4. Unaweza kuwa na dini nzuri lakini umeshindwa kutulia (dhambi zinakuhangaisha)

Mst 35,36 “Wala mtumwa hakai nyumbani sikuzote; mwana hukaa sikuzote. Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli.”

5. Unaweza kuwataja na kuwatambua manabii na mitume lakini bado unapingana na ukweli wa Neno la Mungu

Mst 39-40 “Wakajibu, wakamwambia, Baba yetu ndiye Ibrahimu! Yesu akawaambia, Kama mngekuwa watoto wa Ibrahimu, mngezitenda kazi zake Ibrahimu. Lakini sasa mnatafuta kuniua mimi, mtu ambaye nimewaambia iliyo kweli, niliyoisikia kwa Mungu. Ibrahimu hakufanya hivyo.”

6. Unaweza kumtaja Mungu lakini uko kinyume naye kwa matendo yako

Mst 41-42 “Ninyi mnazitenda kazi za baba yenu. Ndipo walipomwambia, Sisi hatukuzaliwa kwa zinaa; sisi tunaye Baba mmoja, yaani, Mungu. Yesu akawaambia, Kama Mungu angekuwa baba yenu, mngenipenda mimi; kwa maana nalitoka kwa Mungu, nami nimekuja; wala sikuja kwa nafsi yangu, bali yeye ndiye aliyenituma.”

Hivi karibuni tulikuwa na mafunzo na maombezi kwa ajili ya watoto. Tulimuona Mungu akiwagusa kipekee hata wamama walioamua kushiriki maombezi hayo. (angalia video)

Nashukuru kwa wale ambao mmeona umuhimu wa kutoa sadaka ya upendo kwa ajili ya safari ya umisheni Burundi. Nakukumbusha wewe pia kwa vile umebaki muda mfupi sana kabla ya kwenda kufanya umisheni huo.

Barikiwa na Bwana.

Dr. Lawi Mshana, +255712-924234 (sms au whatsapp), Korogwe, Tanga, Tanzania