Ticker

6/recent/ticker-posts

Kwa nini ndoa nyingi za leo hazina furaha na amani?

Kwa nini ndoa nyingi za leo hazina furaha na amani? 

Mungu alipanga kwamba mtu anapoingia katika ndoa awe anaonja uzuri wa mbinguni na sio uchungu. Lakini kinyume chake, ndoa nyingi zimekuwa ni jehanamu ndogo. Wanandoa wana majuto, maumivu, simanzi, majeraha na hofu. Pamoja na ugumu huu, liko tumaini kwa Mungu aliyeanzisha taasisi hii ya ndoa.

Kwa utafiti wangu mdogo na kwa ufunuo wa Roho Mtakatifu napenda kukushirikisha sababu kadhaa za kukosekana kwa furaha na amani katika ndoa nyingi za leo:

1. Makosa katika uchaguzi wa mwenzi wa maisha.

Matatizo ya ndoa nyingi yanatokana na uchaguzi mbaya. Mungu anasema kwamba uzima na mauti vyote viko mbele yetu. Ni wajibu wetu kuchagua uzima kwa faida yetu na vizazi vijavyo. Kum 30:19 ‘nimekuwekea mbele yako uzima na mauti, baraka na laana; basi chagua uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako’ . Kama mtu alifumba macho asiangalie matatizo yanayojulikana wazi ya mchumba wake, lazima avune alichopanda. Tunatakiwa kuwa waangalifu sana kuruhusu moyo kummeza mtu ambaye hajulikani vizuri. Ukimpenda sana mtu macho yanapofuka hivyo huwezi kuona wala kukubali kwamba ana matatizo yanayoweza kukugharimu baadaye. Gal 6:7 ‘Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa chochote apandacho mtu, ndicho atakachovuna’. Pengine ulijua wazi tabia mbaya za mchumba wako lakini ukazipuuzia kwa vile tu ni tajiri au ni msomi au ni maarufu au umechoka kusubiri.

Kama Adamu hangekuwa na subira, angeoa sokwemtu kwa vile wanyama walishaumbwa. Sokwemtu ndiye alikuwa na sura inayokaribiana na mwanadamu. Isije ikawa umeoa au kuolewa na sokwemtu kutokana na kukosa subira au kushinikizwa na watu uoe au uolewe na mtu ambaye si chaguo lako la moyo na wala si mpango wa Mungu.

2. Msingi mbovu katika kuanza maisha ya ndoa.

Kama mlianza kukutana kimwili kabla ya ndoa kufungwa, lazima msingi utakuwa na nyufa ambazo baadaye zitaonekana hata kwenye kuta za ndoa yenu. Msingi wa ndoa yenu ni dhambi na kukosa subira ndiyo maana mnaishi kwa hatia na kutoaminiana. Tendo hilo linathibitisha kwamba mlikuwa na uwezo mdogo katika kusubiri na kutawala tamaa za miili yenu. Pia inadhihirisha mlikosa hofu ya Mungu.

Lakini pia inawezekana mlijiheshimu katika uchumba hadi ndoa lakini hamkuandaliwa vizuri kuwa mume na mke. Ndoa ni kiwanda cha kuzalisha watu kinachohitaji meneja mzuri. Lazima wanandoa wakae chini mapema  na kupanga wanataka nyumba yao iwe ya aina gani. Mjenzi hawezi kuamua baadae kuibadilisha nyumba iwe ya gorofa wakati msingi aliouweka awali ni wa nyumba ya miti. Kwa kuthamini hili mimi niliweka bajeti ya kukaa na mke wangu siku tano kwenye hoteli baada tu ya arusi yetu ili tuweke msingi wa nyumba yetu badala ya kulisha watu kifahari siku ya arusi. Lazima ndoa iwe na kanuni na dira ya kuiongoza.

Wengine walifichana uhalisi wa maisha yao. Pengine mume hakutaka mwenzake ajue kiwango chake cha maisha wakati wakiwa wachumba. Jambo hili linasababisha kujikwaa wakati wa kuishi pamoja. Inashindikana kumpa mke zawadi nyingi kama wakati wa  uchumba kwa vile sasa hakuna wa kukukopesha. Hivyo mke  anakosa hata mafuta ya kupaka. Ingekuwa bora zaidi kama mwanaume angekuwa muwazi ili mwanamke apige gharama kama ataishi naye au la badala ya kushtukizwa maisha ambayo hakuyategemea wala hakujiandaa kuwa nayo. Hata mwanamke pia anapaswa kuwa muwazi kwa mwenzake tangu mapema.

3. Kutegemea ndugu na kushindwa kuambatana.

Kuna wana ndoa ambao hawana maamuzi binafsi katika masuala ya nyumba zao. Kwa nje wanaonekana kama mume na mke lakini katika uhalisia ni ‘remote control’ ya ndugu zao. Wanaongozwa kwa mbali kama mtu anayewasha TV kwa rimoti. Kwa maneno mengine, ni bendera fuata upepo. Hawajaweza kutekeleza maagizo makuu matatu ya Mungu ya  kuacha, kuambatana na kuwa mwili mmoja. Mwa 2:24 ‘Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja’.  Haiwezekani kuwa mwili mmoja (kuunganishwa kimwili, kiroho na kimawazo) kabla ya kuwaacha wazazi na kuambatana. Kuacha wazazi sio kuwasahau bali ni kujitegemea katika kuiongoza nyumba yako. Si lazima mfumo wako wa kuongoza ufafanane na wa wazazi wako. Kuambatana ni kuwa marafiki wa karibu kuliko yeyote mwingine. Kuna msemo unaosema, ‘Out of sight, out of mind’, yaani, ukiwa humuoni mtu kwa karibu, anatoka kwenye mawazo yako. Kadiri wanandoa wanavyokuwa mbali, ndivyo kila mmoja anavyomsahau mwenzake na wakati huohuo mwingine aliye karibu anaingia moyoni kuziba pengo lililopo. Hatimaye, mlango wa zinaa unakuwa wazi. Lazima jitihada zifanyike za kuhakikisha hakuna mwanya au ufa unaotokea kwa watu waliounganishwa kuwa mwili mmoja.

4. Kumsahau aliyeanzisha ndoa.

Watu wengine hawakumshirikisha Mungu katika kupata mwenzi wa maisha isipokuwa wanataka tu Mungu aibariki ndoa yao. Mungu alianzisha ndoa kwa malengo ya kusaidiana katika kumtumikia. Mungu hakuwaumba Adamu na Hawa kwa faida zao wenyewe bali watawale, wamiliki na kuitiisha nchi. Mwa 1:28 “Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi.” Kinyume chake wengi wanadhani ndoa ni kwa ajili ya kujifurahisha tu wao wenyewe. Na hii ndiyo sababu watu wengi wakioa au kuolewa wanaacha kufanya kazi ya Mungu na matokeo yake wanaishi katika laana. Kum 28:30a, 47 ‘Utaoa mke na mtu mwingine atalala naye...kwa kuwa hukumtumikia BWANA, Mungu wako, kwa furaha na moyo wa kushukuru, kwa ajili ya ule wingi wa vitu vyote’. Yeyote anayetaka Mungu aiponye na kuisimamia ndoa yake ajiulize kwanza swali hili: ‘Mungu ananufaika nini na ndoa yangu?’

5. Kuthamini pesa kuliko utu (ubinadamu).

Kuna wanandoa ambao wamejenga upendo wao katika mafanikio ya kimwili. Kwa hiyo, mwenzi ana thamani kama tu ana pesa. Msingi huu unasababisha ndoa iyumbe hali ya uchumi inapobadilika. Ndoa inatakiwa ithamini mpango wa Mungu na utu kuliko kitu kingine chochote. Vinginevyo, mtu atatafuta zaidi pesa kuliko kuwa na faragha na mwenzi wake. Matokeo yake ukaribu (intimacy) unapungua, upweke alioukimbia unajitokeza tena na maana halisi ya ndoa inatoweka. Kumbuka Mungu anawaunganisha mume na mke ili kudhibiti upweke (Mwa 2:18). Kuna watu wengi siku hizi ni ‘married singles’ badala ya kuwa ‘married couples’. Yaani, mtu anaonekana kwa nje kwamba ameoa au kuolewa lakini kwa ndani yuko peke yake. Mtu yuko tayari atafute pesa na kusahau umuhimu wa mahusiano. Lazima pesa tunazozipata ZITUTUMIKIE NA SIO SISI KUZITUMIKIA. Pesa zisaidie kuijenga familia na sio kuibomoa. Mama mmoja alikuwa mkweli kwa mumewe aliyekuwa anajali tu kutuma pesa lakini harudi nyumbani. Alimwambia, “Nashukuru kwa pesa unazotuma lakini naomba usisahau kwamba sikuolewa na pesa zako!”

6. Kuingia katika ndoa kabla ya kujua kwamba ndoa ni majukumu.

Wapo wanaoingia katika ndoa kichwakichwa bila maandalizi ya msingi ya maisha. Mungu hakumpa Adamu mke hadi pale alipohakikisha amempa bustani ya kulima na kuitunza (Mwa 2:15-17). Ni kweli kwamba Mungu hapendi mtu awe peke yake lakini alishughulikia upweke wa Adamu baada ya kumpa kwanza bustani na majukumu. Hawa naye aliumbwa ili kumkamilisha Adamu. Ndiyo maana Mungu alitoa ubavu wa Adamu akautumia kumuumba Hawa. Mungu alitaka kila mmoja amuhitaji mwenzake.

Lazima kila mmoja ajue majukumu yake katika ndoa. Pamoja na ukweli kwamba wanandoa wanapaswa kusaidiana lazima  kila mmoja ajue majukumu yake. Wapo watu wanaosema kazi zote ni za mume ikiwa ni pamoja na kupika na kudeki na mke ni msaidizi anayesaidia tu pale inapobidi. Tatizo hili linatokana na kutafsiri neno msaidizi kwa lugha ya kiswahili au kingereza badala ya lugha ya kiebrania iliyotumika katika kuandika Agano la Kale. Neno msaidizi ni EZER KENEGDO – mwanamke ni mtu mwenye nguvu wa kumuokoa mwanaume. Kumbuka hata Roho Mtakatifu anaitwa pia msaidizi lakini haina maana kwamba ni mdogo kwetu wala haina maana kwamba anatusaidia tu pale tukishindwa. Roho Mtakatifu ni msaidizi kwa maana ya ‘kuwa karibu kututia nguvu ya kutenda’. Mke anayejua vizuri wito wake anatakiwa awe mfariji au muwezeshaji. Mwanamke ana hadhi sawa na mwanaume isipokuwa tu majukumu yao yako tofauti. Kama kuumbwa kabla kunasababisha mume awe wa maana zaidi kuliko mke (kwa wanaoamini waliumbwa kwa nyakati tofauti), basi itabidi sokwe mtu naye awe wa maana zaidi kuliko mume kwa vile aliumbwa kabla ya Adamu. Hata hivyo tusisahau kwamba mfumo dume ulianzishwa na Mungu mwenyewe ingawa hauna maana ya kumnyanyasa mwanamke. Ndiyo maana Mungu alichagua kuitwa baba na sio mama. Huu sio udhalilishaji bali ni ugawaji wa majukumu kwa utukufu wake mwenyewe. Maumbile yenyewe yanaonyesha kwamba Mungu alikusudia tofauti ziwepo kwa ajili ya mume na mke kuhitajiana. Ingawa wote wana haki sawa, lazima pawe na kiongozi. Hakuna ‘authority sharing’ yaani, kugawana madaraka. Ndiyo maana mke akaitwa msaidizi na sio msimamizi. Mungu aliweka tofauti kati ya mke na mume kwa vile mtu anavutiwa zaidi na kitu asicho nacho ili akamilike (opposites attract). Tofauti hizi za kimaumbile ni kwa ajili ya kukamilishana na sio kushindana. Hivyo tuufurahie na kuulinda uumbaji wa Mungu wetu bila kuukosoa. Kuna vitu mwanaume anaweza zaidi kuliko na mwanamke na kuna vitu mwanamke anaweza zaidi kuliko mwanaume. Sina haja ya kusema uwezo wa mwanaume maana unajulikana. Lakini mwanamke ana uwezo wa ajabu aliopewa na Mungu ili kumuokoa (kumlinda mwanaume). Na shetani kwa kulijua hilo anawatumia baadhi yao vibaya. Mfano, mwanamke ana uwezo wa kuhisi kitu kwa haraka bila kufikiri kwanza (intuition). Mke anaweza kukuambia huyu mtu unayetaka kufanya naye biashara atakudhulumu. Ukipuuzia halafu ukadhulumiwa, unaanza kumlaumu mkeo kwamba amekulaani. Tuutumie huu uwezo wao kwa faida ya familia zetu.

7. Kutotambua kwamba shetani aliyevuruga ndoa ya kwanza hajafa

Shetani anabuni mbinu mpya usiku na mchana kwa ajili ya kuharibu ndoa na familia. Siku moja ndugu mmoja aliyeokoka alikuwa safarini kwenye ndege. Alipoona jirani waliyeketi naye anaomba kwa bidii alimuomba washirikiane maombi. Yule ndugu akamwambia, “Mimi ni muabudu shetani (satanist) na siku ya leo tunaomba ndoa za watu wa Mungu zivunjike.” Ndoa yenu inayumba kwa vile shetani amefanyia kazi maombi ya watu wake (waabudu shetani). Watu wengi wanaoanguka kwenye ndoa hawafanyi makusudi bali wanalishwa limbwata. Wanakamatwa mioyo yao kwa uchawi mpaka wanajikuta wanamfuatilia mtu ambaye hakuwa na mvuto wowote kwake na hatimaye kutelekeza familia zao. Unashangaa mtu anang’ang’ana na mtu na kumkabidhi pesa zote huku familia inateseka. Lazima maombezi yenye nguvu na mamlaka yafanyike ili kuwatoa watu katika mashimo walikowekwa ndipo watakumbuka familia zao na kujutia dhambi zao.

Hata kama kuna makosa yalifanyika huko nyuma, Mungu anaweza kuponya na kuhuisha ndoa za watu wake wanaomkimbilia kwa imani bila kukata tamaa.

Naomba kwamba:

1. Mungu akusaidie ukubali makosa uliyofanya na kuuendea msalaba bila kuficha dhambi zako ili ndoa yako iponywe na kurejezwa.

2. Mungu akusaidie kuwa karibu na mwenzi wako kuliko mtu mwingine yeyote hata kama umelazimika kuwa mbali naye kikazi au kimasomo.

3. Mungu akupe macho ya kuwatambua majini-watu ambao unadhani wanavutia kumbe ni mawakala wa kukuingiza katika ufalme wa giza.

4. Mungu ahuishe tena ndoa yako iliyochoka ili usiishi mazingira hatarishi na ambayo hayampi Mungu utukufu.

Pokea majibu ya maombi haya katika Jina la Yesu Kristo!

Dr. Lawi Mshana, +255712924234, Tanzania