NINI KINASABABISHA MTU AMBAYE NI MTOAJI ASIBARIKIWE? – Dr
Lawi Mshana
Ni
kweli kwamba Biblia imejaa ahadi nyingi za baraka kamilifu kutoka kwa Mungu
kama tunavyoona katika Ebr 1:17 ‘kila kutoa kuliko kwema, na kila kitolewacho
kilicho kamili, hutoka juu, hushuka kwa Baba wa mianga; kwake hakuna
kubadilika, wala kivuli cha kugeuka-geuka’. Hata hivyo, baraka za Mungu zina masharti yake. Kum 28:2 “na baraka hizi
zote zitakujia na kukupata usikiapo sauti ya BWANA, Mungu wako.” Wengine hawamtii
Mungu bali wananyofoa mstari wa 13a unaosema “Bwana atakufanya kuwa kichwa, wala si mkia; nawe utakuwa
juu tu, wala huwi chini” na kusahau masharti yake
kwenye 13b yanayosema “utakapoyasikiza maagizo ya Bwana, Mungu wako, nikuagizayo
hivi leo, kuyaangalia na kufanya”. Afadhali
ukiona u mkia uwe muwazi kwa Mungu ili akusaidie kuliko kujifariji kwa maneno
ya uongo kwamba wewe ni kichwa. Yeremia 7:8 “Angalieni,
mnatumainia maneno ya uongo, yasiyoweza kufaidia.”
Usisahau kwamba kubarikiwa SIO KUMILIKI MALI PEKE YAKE BALI NI KUFURAHIA MALI UNAZOZIMILIKI. Kwa nje mtu anaweza kuonekana kama amebarikiwa lakini kiukweli hajabarikiwa. Ana mume au mke mzuri lakini hamfurahii, lipo gari zuri katik familia lakini anatamani asilipande bali atembee kwa miguu, ipo nyumba nzuri lakini kila mmoja ana chumba chake utafikiri ni wateja wa nyumba ya wageni wanaokutana tu asubuhi. Ndiyo sababu Mithali 15:17 anasema “Chakula cha mboga penye mapendano; Ni bora kuliko ng'ombe aliyenona pamoja na kuchukiana.” Amani na upendo ni baraka kubwa kuliko fedha na mali. Lakini pia Kum 28:30-32 anasema, “Utaposa mke na mume mwingine atalala naye; utajenga nyumba usiikae; utapanda mizabibu usitumie matunda yake. Ng'ombe wako atachinjwa mbele ya macho yako, usile nyama yake; utanyang'anywa punda wako mbele ya uso wako kwa jeuri, usirudishiwe; kondoo zako watapewa adui zako, usipate mtu wa kukuokoa. Wanao na binti zako litapewa taifa lingine, na macho yako yataangalia, na kuzimia kwa kuwatamani mchana kutwa; wala hapatakuwa na kitu katika uwezo wa mkono wako.” Maana yake ni nini? Unaonekana kwa nje kama mmiliki na tajiri lakini kwa ndani una simanzi, machungu, kilio, maumivu na vidonda moyoni. HUFURAHII UNACHOMILIKI AU ULICHO NACHO INGAWA NI CHA HALALI.
INAKUWAJE MTOAJI ASIBARIKIWE:
Watu wa Mungu wengi wana swali hili kwa vile wamekuwa wakimtolea Mungu lakini hawaoni baraka walizoahidiwa katika maandiko zikitimia maishani mwao. Hali hii imepelekea wengine kugoma kumtolea Mungu. Kama utaguswa na moja ya sababu nitakazozungumzia, ifanyie kazi bila kuipuuzia. Kwa Mungu hakuna dhambi kubwa na ndogo ingawa zipo dhambi zenye madhara makubwa kwa watu zinapotendwa kuliko zingine.
1. Mbegu mbaya
Gal 6:7 “Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho
atakachovuna.” Kuna uhusiano wa karibu kati ya
MBEGU na MAVUNO.
(i) Kama mbegu yako imeoza,
usitegemee mavuno mazuri. Biblia inatuonya tusitoe kilichopatikana kwa
udhalimu na kilema na kilicho kigonjwa. Mal 1:13 “Tena mwasema, Tazama, jambo hili linatuchokesha namna
gani! Nanyi mmelidharau, asema Bwana wa majeshi; nanyi mmeleta kitu kilichopatikana
kwa udhalimu, na kilema, na kilicho kigonjwa; ndivyo mnavyoleta sadaka; je!
Niikubali hii mikononi mwenu? Asema Bwana.” Wanadamu
wanataka pesa yako bila kujali imetoka wapi lakini Mungu anajali uliipataje.
Lakini pia hata kama uliipata kwa njia halali, Mungu hataki umpe mabaki, noti
zilizochoka, kuku anayechechemea nk. Wataipokea viongozi wako lakini Mungu
hajataikubali.
(ii) Panda mbegu ya
mavuno unayoyatarajia. Kama unataka kuvuna maharage, usipande mahindi. Kama
kuna baraka unaihitaji, tambua mbegu yake kama anavyofanya mkulima. Mkulima akihitaji
maharage anapanda maharage. Nilipohitaji Mungu anibariki vifaa vya elektroniki
nilimuomba Mungu sana. Siku moja Roho akanipa swali: Mbona hujapanda mbegu
yake? Chombo cha thamani nilichokuwa nacho miaka hiyo kilikuwa ni kamera ambayo
nilipewa na ndugu yangu. Ikabidi niitoe. Nilipoipanda ndipo nikafungua milango
ya vifaa mbalimbali vya aina hiyo. Kuna kipindi watu walikuwa wanajisikia sana
kunipa zawadi za mashati lakini nikawa sipewi suruali. Nilipotafakari sana
nikagundua kwamba niliwahi kuwapa watu mashati na sio suruali kwa hiyo navuna
nilichopanda.
2. Udongo mbaya
Lk 8:5 “Mpanzi alitoka kwenda kupanda mbegu zake; naye alipokuwa akizipanda,
nyingine zilianguka karibu na njia, zikakanyagwa, ndege wa angani wakazila.”
Yesu alitoa mfano kwamba mavuno mazuri yanategemea udongo mzuri na sio mbegu nzuri peke yake. Na alibainisha kwamba udongo wa njiani, mwambani na miibani hauna matokeo mazuri (Lk 8:4-8). Hakikisha shamba linafaa kabla ya kupanda mbegu yako nzuri. Kum 12:13,14 ‘Ujihadhari usitoe sadaka zako za kuteketezwa katika kila mahali upaonapo bali katika mahali atakapopachagua BWANA’. Tunahitaji uongozi wa Mungu tutoe wapi sadaka ambayo tunataka ilete matokeo fulani. Kumbuka kuna matoleo ya KUTIMIZA WAJIBU WA KIDINI ili huduma za kiroho ziendelee kutolewa lakini pia kuna sadaka unayoitamkia kwamba NAKUTOA UWE MBEGU YANGU YA UPENYO FULANI. Sadaka ya aina hii sio ya kila wakati. Nilipotaka kuanza ujenzi wa nyumba yangu nilipanda mbegu katika utaratibu nilioongozwa na Roho wa Mungu na nikamuona Mungu akifanikisha bila kukopa. Panda mbegu yako mahali sahihi alipopachagua Bwana ambapo sadaka hiyo itatumika kwa kazi ya Mungu na sio kutajirisha watu binafsi wakati kazi ya Mungu haiendi.
3. Msimu mbaya
Mhu 3:1 “Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu.” Kuna baraka zinapatikana kwa kutoa sdaka yako kipindi cha kampeni maalum za kazi ya Mungu kv mikutano ya injili, semina au ujenzi wa nyumba ya Bwana. Zek 10:1 ‘Mwombeni Bwana mvua wakati wa masika...kila mtu atapewa nyasi kondeni’. Huwezi kupanda mbegu kipindi cha kiangazi halafu uvune vizuri labda kama ni kilimo cha umwagiliaji. Lazima tutambue misimu ya kupanda ili tusipishane na baraka za Mungu. Mwanamke mjane alitaka kupishana na msimu wake wa kubarikiwa lakini baadaye akaelewa na alipotii hakufa njaa. Mwanamke huyu alisikia sauti ya Bwana (aliagizwa) kwamba kuna mtumishi atakuja amlishe lakini yeye akaangalia shida yake kuliko sauti ya Mungu. 1 Fal 17:9-15 “Ondoka, uende Sarepta ulio mji wa Sidoni, ukae huko. Tazama NIMEMWAGIZA mwanamke mjane huko akulishe. Basi, akaondoka, akaenda Sarepta; hata alipofika langoni pa mji, kumbe! Mwanamke mjane alikuwako akiokota kuni; akamwita, akamwambia, Niletee, nakuomba, maji kidogo chomboni nipate kunywa.Alipokuwa akienda kuleta, akamwita akasema, Niletee, nakuomba, kipande cha mkate mkononi mwako. Naye akasema, Kama Bwana, Mungu wako, aishivyo, sina mkate, ila konzi ya unga katika pipa, na mafuta kidogo katika chupa; nami ninaokota kuni mbili ili niingie nijipikie nafsi yangu na mwanangu, tuule tukafe. Eliya akamwambia, Usiogope; enenda ukafanye kama ulivyosema; lakini unifanyie kwanza mkate mdogo ukaniletee; kisha ujifanyie nafsi yako na mwanao. Kwa kuwa Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Lile pipa la unga halitapunguka, wala ile chupa ya mafuta haitaisha, hata siku ile Bwana atakapoleta mvua juu ya nchi. Basi akaenda, akafanya kama alivyosema Eliya; na yeye mwenyewe, na Eliya, na nyumba yake, wakala siku nyingi.” Kuna kipindi ambacho Mungu anakuagiza umtolee kitu fulani kwa faida yako mwenyewe wala si kwa faida ya huyo uliyemsaidia. Mungu anaweza kumleta mtu ili awe shamba kwa ajili ya baraka zako. Mungu hakushindwa kumlisha mtumishi wake Eliya kwa njia nyingine. Alikuwa tayari analishwa na kunguru. Ila Mungu akaamua amtume mbali kumbariki mjane anayekaribia kufa njaa.
Mimi sipendi kuandaa semina na mikutano ya Injili vipindi vya mvua na kilimo. Labda iwe ni maelekezo maalum ya Mungu. Sio busara kuomba mvua isinyeshe kwa sababu ya mkutano wakati ni msimu wa kilimo.
4. Mbegu chache
2 Kor 9:6 “Lakini nasema neno hili, Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu
atavuna kwa ukarimu.” Kama unapanda vichache utavuna vichache.
Ukipanda kwa wingi utavuna vingi.
(i). Zingatia uwiano kati ya mbegu unayopanda na mavuno unayotarajia. Ukipanda kopo la maharage usitarajie kuvuna magunia thelathini ya maharage. Mungu anabariki lakini hafanyi mazingaombwe. Baraka zake zinawiana na mbegu uliyopanda. Ukipanda kwa ukarimu, utavuna kwa ukarimu.
(ii). Zingatia uwiano kati ya pesa unazotoa na unazobakiza. Mtoaji mkuu katika Biblia ni mjane maskini aliyetoa senti mbili. Alitoa vyote alivyo navyo na sio ziada kama wengine walivyotoa . Lk 21:3,4 “Akasema, Hakika nawaambia, huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote; maana, hao wote walitia sadakani katika mali iliyowazidi, bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo.” Kama unaona aibu kwenye kikao cha harusi kutoa kiasi fulani kutokana na hadhi yako, ona pia aibu mtu kama wewe kutoa sadaka kwa Mungu ya kiwango hicho. Unapotoa sadaka Mungu analinganisha na ulichobakiza. Watu wakikuona ukitoa elfu 5, wanaweza kukuita mtoaji mzuri kwa vile wao wanatoa mia 5. Lakini tukizingatia uwezo wako uliojaliwa, hujatoa sadaka bado.
5. Kutotofautisha ‘mbegu’ na
‘mkate’
2 Kor 9:10 “Na yeye ampaye mbegu mwenye kupanda, na mkate uwe chakula, atawapa mbegu
za kupanda na kuzizidisha, naye atayaongeza mazao ya haki yenu.” Kuna vitu viwili vimetajwa hapa: MBEGU NA MKATE
(CHAKULA). Hivyo, zingatia mambo mawili: Usile mbegu na usipande mkate!
Mungu anakupa mbegu ili usife njaa msimu ujao na anakupa mkate ili ufurahie mbegu yako uliyoipanda msimu uliopita. SIO BUSARA KUHIMIZA TU WATU WATOE KILA WAKATI NA KUSAHAU KUHIMIZA WABORESHE MAISHA YAO. WAKATI WA KUTOA WATU WATOE. LAKINI PIA UWEPO WAKATI WA KUPUNGUZA MICHANGO ILI WAFURAHIE (WAJIPONGEZE) KWA UTOAJI WAO WA MSIMU ULIOPITA. Kuna wakati wa kupanda kwa machozi na wa kuvuna kwa sherehe. Zab 126:5 ‘wapandao kwa machozi watavuna kwa kelele za furaha’. Mungu akusaidie ujue Mungu amekupa pesa ili upande kama mbegu au ni mavuno ya ile mbegu uliyopanda katika huduma ili na wewe ununue au ugharamie kitu fulani cha familia yako. MUNGU ANATAKA FAMILIA IFANIKIWE KAMA KANISA LINAVYOFANIKIWA. Tusifike mahali waumini wanalalia maboksi huku wanahimizwa tu kuchangia huduma kwa michango isiyoisha.
6. Kutotoa kwa ukunjufu wa moyo
2 Kor 9:7 “Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu.” Mungu anataka ukitoa utoe kwa furaka na sio kwa hasira. Wakati ukimtolea Mungu, anaangalia moyo wako kabla ya kuangalia mkono wako. Yeye haangalii kama wanadamu waangaliavyo. 1 Sam 16:7 “Lakini Bwana akamwambia Samweli, Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. Bwana haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali Bwana huutazama moyo.”. Mungu hatakubariki kama unatoa kwa kufuata mkumbo yaani, kwa kutaka uonekane unatoa kama wengine wanavyotoa. Mungu anahitaji moyo wako kabla ya sadaka yako. Zab 51:17 “Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika; Moyo uliovunjika na kupondeka, Ee Mungu, hutaudharau.”. Mimi nafundisha watu wamtolee Mungu lakini sipendi watoe kwa kulazimishwa. Mungu hana njia moja ya kuiendeleza kazi yake. Anaweza kuamua ambariki mara dufu yule anayetoa kwa moyo ili afidie wale wasiopenda kumtolea Mungu.
7. Laana (roho) ya umaskini
Mtu anaweza kutoa sadaka vizuri
lakini ana roho ya umasikini na hasara katika maisha yake binafsi au ukoo wao.
Ishara mojawapo ya umasikini ni mgeni aliyekukuta kuinuka kiuchumi wakati wewe
unadidimia kiuchumi. Kum 28:43 “Mgeni aliye kati yako
atazidi kupaa juu yako; nawe utazidi kushuka chini.”
Dalili za roho ya umaskini ni:
·
Kutopata
kazi wala pesa wakati wenzako wanaofanana na wewe kitaaluma na kiujuzi
wanapata. Unaomba kazi pamoja na wenzako wenye elimu kama yako wanapewa lakini
wewe unanyimwa.
·
Kupata
pesa lakini hazikuwezeshi kufanya kitu cha maana. Mwingine anayepata pesa au
mshahara kama wa kwako anakuacha mbali sana kimaendeleo.
· Kununua vitu halafu vinapotea au kuharibika mapema sana (havidumu). Chupa za chai zinavunjika ovyo, nguo nzuri uliyoanika nje inatafunwa na ng’ombe nk. Lengo hapa ni ili pesa itumike kinyume na mpango uliouweka.
Kumbuka Mungu wetu anatupa utajiri udumuo na sio wa muda
mfupi. Mt 8:18 “Utajiri na heshima ziko kwangu, Naam, utajiri udumuo, na
haki pia.”.
Unaweza kupata laana kutoka kwa
1). Mungu
mwenyewe.Yer 6:19 “Sikia, Ee nchi; tazama, nitaleta mabaya juu ya watu hawa,
naam, matunda ya mawazo yao, kwa sababu hawakuyasikiliza maneno yangu; tena kwa
habari ya sheria yangu, wameikataa.” Hata hivyo kimsingi ni watu wenyewe
wanaokaribisha laana kwa kutomtii Mungu na sio Mungu anayewalaani moja kwa
moja.
2). Wazazi
wako wa kiroho. Efe 6:1 “Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, maana
hii ndiyo haki.” Kushindana na baba zako kiroho waliokuzaa na kukulea au
kutowakumbuka na kuwajali unapobarikiwa.
3). Wazazi wako wa kimwili/kibaolojia. Efe 6:2,3 “Waheshimu baba yako na mama yako; amri hii ndiyo amri ya kwanza yenye
ahadi, Upate heri, ukae siku nyingi katika dunia.” Kuendelea kuchangia
arusi na misiba kwa pesa nyingi wakati umesahau kabisa wazazi na walezi wako
waliolima vibarua na kujinyima ili wakusomeshe.
4). Kwa
kurithi. Yn 9:2 “Wanafunzi wake wakamwuliza wakisema, Rabi, ni yupi aliyetenda
dhambi, mtu huyu au wazazi wake, hata azaliwe kipofu?” Laana za vizazi
(generational curses) kutokana na maagano ya kishetani yaliyokuwa yamefanyika
kwa niaba ya ukoo wenu.
5). Kwa kufungulia dhambi mlango. Mwa 4:7,11-12 “Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde. Basi sasa, umelaaniwa wewe katika ardhi, iliyofumbua kinywa chake ipokee damu ya ndugu yako kwa mkono wako; utakapoilima ardhi haitakupa mazao yake; utakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani.”. Kuishi maisha ya dhambi kunaleta laana katika kazi zako.
8. Matumizi mabaya
Tito 3:14 “Watu wetu nao wajifunze kudumu katika matendo mema, kwa matumizi yaliyo lazima, ili wasiwe hawana matunda.” Watu wengi wanaokesha wakiomba baraka za Mungu, hawajali kuomba Mungu awafundishe matumizi mazuri ya baraka za Mungu. Petro alijua atapataje pesa (shekeli) na atatumiaje shekeli hiyo. Mt 17:27 “Lakini tusije tukawakwaza, enenda baharini ukatupe ndoana, ukatwae samaki yule azukaye kwanza; na ukifumbua mdomo wake utaona shekeli ichukue hiyo ukawape kwa ajili yangu na kwa ajili yako.”. Matumizi mabaya yanaleta majuto, hatia na faraka katika familia. Watu wengi wana vitu vya thamani nyumbani visivyotumika kwa faida. Hii inatokana na kununua vitu kwa mashindano na kuiga maisha ya watu wengine. Matokeo yake manufaa ya baraka zao hayaonekani. Hivyo unaweza kubarikiwa na usione matokeo kwa vile unanunua vitu kwa pupa ambavyo sio mahitaji yako halisi. Mungu anatimiza mahitaji (needs) yetu na sio matamanio (wants) yetu.
9. Kumuibia Mungu Mal 3:9
Unapoamua kuacha kutoa zaka (fungu la kumi) katika ghala ya Mungu, kutotimiza ahadi zako na kutolipa madeni yako, unahesabika mwizi katika serikali ya Mungu. Mal 3:10 “Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema Bwana wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la.”. Sio rahisi watu wakuite mbarikiwa (heri) kama unakula sehemu ya Mungu. Mal 3:12 “Na mataifa yote watawaiteni heri; maana mtakuwa nchi ya kupendeza sana, asema Bwana wa majeshi.” Mungu anachukia wezi na wanyang’anyi (Yn 10:8). Ila wakitubu na kuwa waaminifu anawasamehe na kuwapokea (1 Yoh 1:9). Kumbuka AFADHALI KUWA NA SHILINGI 90 ILIYOBARIKIWA KULIKO SHILINGI 100 ILIYOLAANIWA. Ukitoa zaka (10%) ya pesa zako, pesa inapungua lakini inakuwa imebarikiwa. Kuliko ukiila yote na ya Mungu na kisha kupata matatizo yanayokula na kukupeperusha baraka zako.
10. Kutojali uhalali na ubora wa kazi
Kumbuka kazi ni baraka na sio laana. Mungu alianzisha kazi kabla ya laana. Mwa 2:15 ‘Bwana Mungu akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza’. Kazi ni heshima, sio taabu. Mungu angeweza kuitunza mwenyewe bustani lakini akamheshimu Adamu kwa kumpa wajibu huo.
i. Hakikisha unapata kazi kwa
msaada na uongozi wa Mungu na si kwa rushwa.
Kum 28:8 ‘ Bwana ataiamuru baraka ije juu yako katika ghala zako, na mambo yote
utakayotia mkono; naye atakubarikia katika nchi akupayo BWANA, Mungu wako’.
Bwana atabariki kazi yako kama ni yeye alikupa kazi hiyo, kama umeipata kwa
njia ya haki na ni kazi halali. Badala ya kuomba pesa, OMBA KAZI HALALI YENYE
PESA. Mungu hatupi utajiri bali anatupa NGUVU ya kupata utajiri. Kumbukumbu la Torati 8:18 “Bali utamkumbuka Bwana, Mungu
wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano
lake alilowapa baba zako, kama hivi leo.”
ii. Hakikisha unajali ‘bidii’ na
‘ubora’ wa kazi yako.
Mit 27:23,24
‘Fanya bidii kuijua hali ya makundi yako; na kuwaangalia sana ng’ombe zako. Kwa
maana mali haziwi za milele, na taji je! Yadumu tangu kizazi hata kizazi?
Mit 22:29
‘Je wamwona mtu mwenye bidii (utaalam/ujuzi) katika kazi yake? Huyo asimama
mbele ya wafalme; hatasimama mbele ya watu wasio na cheo.
Mit 20:4 ‘Mtu mvivu hataki kulima wakati wa baridi; hivyo wakati wa mavuno ataomba, hana kitu’.
Masaa yasipite bure bila kufanya kazi. Mungu hatoi mali za milele. Lazima tuzitunze ili zidumu. Mungu anawapandisha wanaojituma kufanya kazi. Kama unajiona kama huna kazi, nenda kajitolee kwa watu au maofisi bila kulipwa ili uuze ujuzi wako (ujulikane) lakini usikae nyumbani. Nikiwa mwanafunzi kuna mama alikuwa anauza chapatti nzuri sana. Wauzaji wengine walikuwa wanajua na wameridhika kabisa kwamba atauza za kwake ziishe kwanza ndipo zao zianze kununuliwa. Nikawa najiuliza kwanini hawataki kuongeza ujuzi wa mapishi. Chapatti zao zilikuwa ngumu sana hata kutafuna.
Mpendwa
masomo haya yanalenga kutusaidia tuweze kuishi viwango tulivyokusudiwa na
Mungu. Tujitahidi kuelewa kanuni za serikali ya Mungu ili tusifanane na mataifa
wasiomjua Mungu ambao wana kanuni zao za maisha ya dunia hii. Inawezekana
kuishi maisha yenye baraka tele yanayompa
Mungu utukufu. Naomba Mungu akufungue fahamu zako ili utambue baraka
ulizoandaliwa na Mungu na kuzipokea katika uhalisia.