UNAJUA MANUFAA YA USHAURI NASAHA?
Ushauri nasaha ni fursa ya kujitambua na kutumia magumu yako ya maisha katika kutengeneza ukuaji na mabadiliko. Kuongea na mnasihi kunaweza kukusaidia kuainisha matatizo, kupata mtazamo mpya na kugundua njia mbalimbali ambazo awali hazikujulikana.
Ushauri unaweza kukusaidia kubadilisha hisia na kuponywa katika matatizo yaliyokupata zamani. Kuamua kuonana na mnasihi hakumaanishi kwamba u mtu dhaifu bali ni njia ya kutafuta kujengewa uwezo.
Ushauri nasaha ni mchakato ambapo watu wa rika zote wanasaidiwa kupata maono mapya, mtazamo mpya na hamasa.
Ni katika ushauri nasaha tu ndipo watu wanashirikishana mawazo na hisia kwa kusudi la kujenga. Ni mahali pekee ambapo watu wanajengewa uwezo kugundua majibu yao wenyewe na kujisikia wakitawala maisha yao na mahusiano yao wenyewe.
Nafasi ya ushauri nasaha ni pale mtu anapofikia kushindwa kukabiliana na hali fulani peke yake kwa ushindi.
Ushauri nasaha wenye matokeo makubwa unahitaji vipindi kadhaa visivyozidi saa moja kwa kila kipindi. Inapobidi, anayefanyiwa unasihi anaweza kujaza dodoso zinazosaidia kugundua chanzo cha tatizo kwa wepesi zaidi ili kupata ufumbuzi wa uhakika.
Ushauri nasaha sio tukio (event) bali ni mchakato (process). Kuna hatua kama 6 hizi ambazo mtu anapitia hadi kufikia ufumbuzi wa kudumu.
- Hatua ya kwanza ni kujenga uhusiano.
- Hatua ya pili ni kugundua tatizo.
- Hatua ya tatu ni kuweka malengo ya unasihi.
- Hatua ya nne ni kutafuta ufumbuzi wa tatizo.
- Hatua ya tano ni ufuatiliaji.
- Hatua ya sita ni utafiti na tathmini.
Hakikisha unaposhauriwa mnakuwa kwenye mazingira rafiki kwa kazi hiyo. Pamoja na kwamba faragha inahitajika, yawe mazingira ambayo hayana maswali.
Zipo sababu kadhaa za watu kutopenda kwenda kupata ushauri nasaha:
- ‘Kupata ushuri nasaha ni ishara ya udhaifu.’ Sio kweli kwa vile kuingia kwenye ushauri ni hatua ya kwanza katika kupata ufumbuzi wa hisia zilizokuumiza.
- ‘Wanaokwenda kushauriwa wamechanganyikiwa.’ Sio kweli kwa vile unaenda pale unapoona kwamba umejaribu kushughulikia tatizo lako wewe mwenyewe lakini mikakati yako haisaidii.
- ‘Kila mtu atajua ninachosema.’ Inatakiwa eneo hilo liwe na usiri. Lakini pia mshirikishe mnasihi ambaye anaweza kutunza siri. Hata kama anataka kukupa rufaa mahali pengine lazima aombe kibali chako.
- ‘Sijui hata nianzie wapi.’ Mnasihi anayejua kazi yake atakusaidia kujua la kufanya ili mazungumzo yawe na tija.
- ‘Siwezi kulipia huduma hiyo.’ Ni kweli huduma hii inalipiwa katika sehemu nyingine. Lakini mimi naitoa bure kwa vile ni huduma niliyopewa bure bila kuilipia. Neno la Mungu linasema, ‘Mmepewa bure, toeni bure’. Lakini pia wapo ambao walishagharamia ofisi inayotumika kwa huduma hiyo.
- ‘Naweza mara nyingi kuongea na rafiki. Sijui jinsi kuongea na mgeni kunavyoweza kusaidia.’ Unasihi ni tofauti na urafiki. Katika urafiki mahitaji ya pande zote lazima yashughulikiwe wakati kwenye unasihi, shabaha ni kwako tu na mnasihi ana mbinu za kiuponyaji za kukusaidia.
- ‘Siamini kama kuongea tu kunaweza kuleta jema lolote.’ Kujadili jambo na mtu fulani anayekujali na asiyekuhukumu kunasaidia kukupa ahueni kwenye msongo ulio nao. Unasihi ni zaidi ya hapo. Unapata njia ya kujua wewe ni nani na jinsi unavyohusiana na ulimwengu wako. Hii inakupa mtazamo mpya wa kushughulikia tatizo.
- ‘Nitakuwa naisaliti familia yangu.’ Wanasihi wako makini na wanaheshimu desturi na usiri. Hata hivyo inatakiwa kujadili katika kipindi cha kwanza kuhusu mipaka inayotakiwa kuzingatiwa kabla ya kuanza kushughulikia mambo ya kibinafsi zaidi.
- ‘Nikiongelea matatizo yangu, nitayafanya yawe makubwa zaidi au nitaharibikiwa kabisa.’ Kufanya uchunguzi wa hali inayokukandamiza, kunasaidia kuondoa maumivu na kusaidia kulielewa tatizo vizuri zaidi. Unasihi unatoa fursa ya kugundua chaguzi mbalimbali ambazo zitakufikisha kwenye maamuzi mazuri.
Ushauri unaweza kugusa maeneo ya kiakili, kimaisha, kiroho, kijamii nk.
Nadhani wengi wetu tunatambua jinsi ushauri nasaha ulivyochangia kuleta mabadiliko makubwa kuhusu kukabili VVU na UKIMWI. Hata sasa mwingine unapoona nikisema USHAURI NASAHA unadhani nataka ukapime VVU. Ukweli ni kwamba kuna matatizo makubwa katika maisha ya watu ambayo wanatembea nayo, wanalala nayo na kuamka nayo kuzidi hata yale ya VVU na UKIMWI.
Katika uzoefu wangu wa kufundisha na kushauri watu wanaoishi na VVU, viongozi wa dini, waumini na wafanyakazi maofisini nimegundua kwamba hisia zilezile wanazopitia wanaoishi na VVU ziko kwa wote.
Ni vigumu mtu kuwa tayari kusaidiwa kabla hajafikia hatua ya kulikubali tatizo lake. Hisia hizo ni kukataa tatizo (denial), hasira (anger), hatia (guilt), upweke (loneliness), sonona (depression) na kukubali tatizo (acceptance). Mtu anayeweza kusaidika ni yule tu ambaye amesaidiwa kufikia hatua ya kukubali kwamba ana tatizo lakini anataka kuendelea na maisha kama wengine walioshinda.
Dr Lawi Mshana, +255712924234, Tanzania