JE UNATESWA NA SONONA (DEPRESSION) NA HUJUI UFANYEJE? (Sehemu ya pili)
Katika sehemu ya kwanza tulipata utangulizi, mifano ya viongozi mashuhuri waliokuwa na sonona na vyanzo vya sonona.
Nitajuaje kwamba nina sonona?
Tafsiri ya sonona inabadilika mara kwa mara, lakini kwa ujumla
lazima mtu awe na angalau moja ya dalili zifuatazo muda mwingi kwa
siku, takriban kila siku, kwa wiki mbili au zaidi ndipo
ahesabike kitabibu kwamba “ana sonona”.
· Kujisikia huzuni, kusononeka
au kuwa mtupu (empty)
· Kupoteza shauku au furaha
katika takriban shughuli zote.
Zaidi ya hayo, lazima mtu huyo awe na mambo zaidi ya matatu au
manne katika haya yafuatayo takriban kila siku kwa wiki
mbili au zaidi:
· Kuongezeka sana au
kupungua sana kwa hamu ya kula
· Kulala sana au kidogo sana
· Kufadhaika au kuwa goigoi
· Kuchoka au kukosa nguvu
· Kujihisi huna thamani au
hatia
· Kupungua uwezo wa kufikiri
au kuamua
· Kuwa na mawazo ya kufa au
kujiua
Dalili hizi lazima zikufikishe kwenye kudhoofika kwa utendaji wako
wa kila siku. Hata kama hujawa na sonona mafunzo haya yanaweza kukusaidia.
Nifanye nini kama nina sonona?
Wapo washauri wa afya wanaoweza kusaidia ingawa hawapatikani
maeneo mengi na unaweza kulazimika kulipia huduma hii. Lakini kama unajisikia
kuwa na mawazo ya kujiua, inaonyesha kwamba unahitaji msaada wa haraka kutoka
kwa mtu mwingine zaidi ya wewe mwenyewe.
Zifuatazo ni “Kanuni za Jumla za Uwakili wa Nafsi” ambazo mojawapo
inaweza kukusaidia katika kuanza kujihudumia.
1. Soma vifungu vya Maandiko vinavyofaa
katika kuelezea hisia na mawazo ya watu wanapokuwa na sonona. Kwa mfano, omba
Zaburi 13 pamoja Mfalme Daudi, kiongozi wa watu wa Mungu. Pia soma vifungu vya
Maandiko vilivyojaa matumaini, kama vile Zab 40, 42 au 2 Kor 1:3-11.
2. Tafuta mafunzo kuhusu
sonona kwenye Internet kama ilivyo kwenye huu ukurasa wangu wa
Facebook. Kumbuka tovuti zenye .gov na .edu zina taarifa za kuaminika zaidi.
3. Soma vitabu na majarida mazuri
kuhusu sonona.
4. Tunza orodha ya
dalili za sonona ili ugundue matukio yanayotokea kabla ya hali kuwa nzuri au
mbaya. Kisha epuka matukio yanayotangulia sonona na ongeza ushiriki wako katika
matukio au mawazo yanayozuia au kupunguza sonona.
5. Tafuta njia za kujizawadia kwa
kufikiri au kutenda katika namna inayopunguza sonona unapogundua kinachosaidia.
Kwa mfano, kama kwa kusema, “Hili pia litapita” kunasaidia, jipige kikofi cha
upendo (pat) mgongoni kwa kusema, “Naamua kusema na nafsi yangu namna hii
katika maombi yangu.”
6. Fanya shughuli ambazo
ziliwahi kukufurahisha, hata kama hudhani kama zitakupa furaha sasa. Kama
hukumbuki chochote, fanya mambo ambayo wengi wanayafurahia kama vile,
kusikiliza nyimbo, kufurahia uumbaji au kusoma kitabu kizuri.
7. Tenga muda wa kufanya
matembezi katika mwanga wa jua kwa vile mwanga wa jua mara
nyingi unasaidia kupunguza sonona.
8. Ungama kosa au dhambi kwa mtu
uliyemkosea ili kukabili hatia.
9. Kabili kwa namna
inayoonyesha kujali kama unataka kumkabili mtu kuhusu mambo anayofanya ambayo
yanakuumiza wewe au wengine.
10.Omba msaada kwa marafiki wanaoaminika,
familia, matabibu au wanasihi (washauri nasaha).
11.Fanya uchaguzi kuchukua hatua ya
kwanza katika kuweka miguu kwenye maombi yako kwa ajili ya kushinda sonona kwa
kuamua kufanya jambo unaloweza kulifanya mwenyewe leo.
12.Mwambie mtu fulani kuhusu uamuzi wako
wa kuchukua hatua uliyoamua katika kufanya jambo fulani. Mwombe mtu huyo kukuwajibisha kwa kuchukua hatua
hiyo.
13.Dhihirisha huzuni, simanzi na maumivu
ya kupoteza. Isaya mara nyingi anatafsiriwa kwamba anamzungumzia Yesu kama “Mtu
wa Huzuni” (53:3-4). Yohana pia aliandika kwamba “Yesu alilia” (11:35). Usizuie
kulia ili mradi usiwe kama watu waliopoteza tumaini.
14.Weka shabaha katika
kutafakari mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote
yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye
sifa njema, yaliyo mema (Fil 4:8). Haya ni mambo yanayotupa tumaini. Vua “miwani ya
giza” na tazama mema yanayotoka kwenye hali yako ngumu.
15.Unaweza pia kutumia tibalishe inayofaa
kushughulikia sonona.
16.Baada ya kuonana na
daktari, kama yupo, taratibu anza mazoezi kwa muda usiopungua
dakika 20 kama mara tatu hivi kwa wiki. Haya mazoezi yamethibitisha kusaidia
kupunguza sonona.
17.Jilazimishe kuwa
na watu hata pale unapokuwa hujisikii kufanya hivyo. Ukiwa na sonona
unajisikia kujitenga na wengine, lakini kuwa na watu sahihi kunasaidia sana
kupunguza sonona.
18.Kama huwezi kujichanganya
na watu kijamii, muombe mtu akupe msukumo wa kuwa na watu
wengine hata unapokuwa hujisikii kufanya hivyo.
19.Tafuta mtu au kikundi ambacho unaweza
kushirikisha mapito yako. Kama ambavyo umelia nao waliao, waruhusu wengine nao
walie na wewe. Ukiwa katika upweke, wapo watu wanaoweza kukutegemeza hata kwa
kupitia mtandao.
20.Dhibiti mawazo yako unayojisemea
ambayo yanapoteza tumaini lako. Kisha jiambie, “Acha!” Usiendelee kufikiri
namna hiyo lakini chagua kurudia mawazo ya kweli na yenye matumaini.
21.Soma au imba au sikiliza nyimbo au pambio au
muziki mwingine wa Kikristo ambao unaleta tumaini.
22.Tafakari mambo
yaliyosaidia zamani wakati ulipokuwa umesononeka. Kisha yafanye mambo
hayo tena.
23.Uliza watu wengine walifanya nini
waliposononeka. Kilichofanya kazi kwa wengine kinaweweza kufanya kazi kwako
pia.
24.Andika mawazo yako na hisia zako
kwenye karatasi. Tunga shairi. Tunga wimbo unaoelezea maumivu ya sonona yako na
tumaini la uponyaji.
25.Fanya kitu kusaidia
mwingine bila matarajio ya kurudishiwa chochote. Hii itakusaidia
kuondoa hali ya kujiwazia zaidi na kuanza kuwasaidia wengine.
26.Usiogope kuwainamisha
wengine kwako. Unaweza kuwapa fursa ya kukuhudumia – na unaweza kuwa mfano
mzuri kwamba na wewe unaweza kupata madhara usiposaidiwa.
27.Kipekee omba
mwongozo wa Roho Mtakatifu kuhusu kinachosababisha sonona na jinsi ya
kukishughulikia. Kumbuka kwamba Roho Mtakatifu ni Tabibu mkuu.
28.Waombe wengine wakuombee
kipekee kuhusu
sonona na athari zake.
29.Tumia vizuri huduma
za uponyaji zinazopatikana kanisani kwako.
30.Kama kila unachofanya
hakisaidii, jaribu kupambanua jinsi Mungu anavyoweza kutumia
sonona yako katika muktadha mpana wa ufalme wake.
·
Inaweza kukuandaa vizuri kwa wengine kwa kukupa ushirikeli
(empathy) (2 Kor 1:3-7).
·
Inaweza kukufanya uzidi kuwa mnyenyekevu na kumtegemea Mungu (2
Kor 12:7).
·
Inaweza kuzaa baraka za kiroho (Yk 1:12) au kudhihirisha nguvu ya
Mungu (Yn 9:1-7).
·
Inaweza kuwa ishara kwamba u mali ya Kristo (1 Pet 4:12-19).
·
Mungu anaweza kuitumia kupima uaminifu wako (Kitabu cha Ayubu).
Inawezekana usiweze kufanya mambo haya yote, na si lazima yote
yafanye kazi kwa kila mtu. Hata hivyo, unaweza kuhitaji mojawapo au baadhi
katika kushughulikia sonona yako.
Mungu akusaidie ili utoke katika kifungo hicho na kujiona kwamba
una thamani kubwa na unapendwa na Mungu.
Dr. Lawi Mshana, +255712924234, Tanzania