Ticker

6/recent/ticker-posts

UNATESWA NA SONONA NA HUJUI UFANYEJE? (sehemu ya kwanza)

JE UNATESWA NA SONONA (DEPRESSION) NA HUJUI UFANYEJE? (Sehemu ya kwanza)

UTANGULIZI

Kuwa mkristo hakumfanyi mtu aepuke matatizo ya kihisia kama vile sonona. Ingawa sonona ni neno la kitabibu ambalo halikutumika moja kwa moja kwenye Biblia, sonona ilionekana hata miongoni mwa viongozi wakuu wa kiroho. 

Wanamuziki wa zamani walioandika Zaburi 69, 88, na 102 walidhihirisha kwamba walikuwa na sonona ingawa ni katika muktadha wa matumaini. “Laumu imenivunja moyo, Nami ninaugua sana. Nikangoja aje wa kunihurumia, wala hakuna; Na wa kunifariji, wala sikumwona mtu….Nateswa mimi hali ya kufa tangu ujana…..Maana siku zangu zinatoweka kama moshi, Na mifupa yangu inateketea kama kinga. Moyo wangu umepigwa kama majani na kukauka, Naam, ninasahau kula chakula changu. Kwa ajili ya sauti ya kuugua kwangu Mifupa yangu imegandamana na nyama yangu. Nimekuwa kama mwari nyuni wa jangwani, Na kufanana na bundi wa mahameni. Nakesha, tena nimekuwa kama shomoro Aliye peke yake juu ya nyumba. Adui zangu wananilaumu mchana kutwa; Wanaonichukia kana kwamba wana wazimu Huapa kwa kunitaja mimi. Maana nimekula majivu kama chakula, Na kukichanganya kinywaji changu na machozi”.

MIFANO YA VIONGOZI MASHUHURI WALIOWAHI KUPATA SONONA

1. Musa, kiongozi wa watu wa Mungu aliyejulikana sana, aliwahi kumuomba Mungu amuue kwa sababu ameshindwa kubeba mzigo wa watu ambao Mungu alimpa awaongoze. Hes 11:14,15 “Mimi siwezi kuwachukua watu hawa wote peke yangu, kwa kuwa ni mzigo mzito sana wa kunishinda. Na kama ukinitenda hivi, nakuomba uniulie mbali, kwamba nimepata fadhili mbele ya macho yako; nami nisiyaone haya mashaka yangu”.

 2. Yona, mmishenari wa zamani, alikasirika kiasi cha kutamani kufa. Yona 4:9 “Mungu akamwambia Yona, Je! Unatenda vema kukasirika kwa ajili ya mtango? Naye akasema, Ndiyo, natenda vema kukasirika hata kufa”.

3. Eliya, kiongozi aliyekuwa nabii mkuu mwenye matendo ya miujiza, aliangukia kwenye kilindi cha sonona. Aliomba kufa tena mara tu baada ya ushindi mkuu wa vita ya kiroho dhidi ya uovu. Mungu aliitika maombi yake na kushuka kwa moto na akaweza kuwaua manabii 450 wa Baali lakini baada ya muda mfupi akapata sonona.  1 Fal 19:4 Lakini yeye mwenyewe akaendelea katika jangwa mwendo wa siku moja, akaenda akaketi chini ya mretemu. Akajiombea roho yake afe, akasema, Yatosha; sasa, Ee Bwana, uiondoe roho yangu; kwa kuwa mimi si mwema kuliko baba zangu’.  

Kwahiyo, hata watu wengi leo waliozama kwenye huduma wanaweza kupata sonona.  Ninao ushahidi wa watumishi wa Mungu wenye matatizo makubwa ingawa wanayakataa yasijulikane (suppress) kwa kisingizio cha ‘kukiri ushindi.’ Lazima tujifunze kutumia Neno la Mungu kutupatia ushindi badala ya kukiri bila kusimamia Neno lolote. Hatupaswi kukiri kwamba tunaumwa kwa shetani lakini kwa Mungu tujieleze vizuri ili tupate msaada wake. Ndiyo maana tuna watu wenye magonjwa ya kihisia yaliyovia ndani kwa sababu tu hayajawahi kushughulikiwa. Isaya 1:6 “Tangu wayo wa mguu hata kichwani hamna uzima ndani yake; bali jeraha na machubuko na vidonda vitokavyo usaha; havikufungwa, havikuzongwa-zongwa, wala havikulainishwa kwa mafuta.”

Sonona na sababu zake

Ingawa wakristo wenye sonona wanaweza kudhihirisha dalili zisizofanana, zipo zinazojitokeza zaidi kama vile huzuni au kupoteza shauku. Pia wanaweza kuwa na mabadiliko kwenye kulala, mihemko na mawazo.  Zipo sababu nyingi. Hata hivyo nitataja chache tu.

Baadhi ya sababu za kupata sonona ni: 

1. Kurithi katika familia.

Kuna watu wana sonona kutokana na uovu wa mababu zao. Kwa hiyo wanarithishana hili tatizo. Kuna watu hata kama msiba haumhusu lazima azimie.

 

2. Madhara yanayotokana na matumizi ya dawa fulani au matatizo fulani ya kiafya. Ingawa madawa yanasaidia kuua viini vya magonjwa, yana madhara mengine (side effects) katika mwili kv kuua chembechembe hai za mwili. Lakini pia mtu akiugua muda mrefu ni rahisi kupata sonona.

 

3. Uzoefu fulani katika utoto.

Kama mtu alifanyiwa ukatili au unyanyasaji wa kijinsia kv kubakwa, kupigwa, kutelekezwa au kukataliwa katika utoto wake roho chafu inaweza kupata mlango wa kumtesa.

 

4. Msongo au kupoteza au mabadiliko

Mtu anaweza kupata sonona kama ameachana na mwenzi wake wa maisha (mume au mke) au amefiwa na mtu aliyemtegemea sana kimaisha. Lakini wakati mwingine mabadiliko ya maisha yanaweza pia kuleta athari kama vile kuachishwa au kufukuzwa kazi nk. Mabadiliko haya yanashusha kiwango cha maisha ya mtu na kuleta aibu katika jamii. Matokeo yake mtu anapata sonona.

 

5. Kukosa msaada katika nyakati ngumu.

Kama mtu anapopata matatizo magumu anakosa kimbilio sahihi ni rahisi kupata sonona. Ni muhimu kuwa na mtandao wa marafiki sahihi (kujizungushia watu sahihi wa kuaminika) ili kuepuka magonjwa kama haya. Lakini pia kupata washauri sahihi kunaweza kusaidia. Tatizo wengi wanamuendea mtu yeyote kwa ajili ya ushauri bila kuzingatia uwezo wake na uadilifu wake.

 

6. Kuwaza katika namna ambayo huna mtazamo chanya bali hasi.

Mtazamo ni jambo muhimu sana katika maisha ya mtu. Unaweza kupata matatizo kama mara nyingi unaone mabaya tu badala ya mazuri. Mfano mtu anakupa nguo halafu badala ya kushukuru unasema, Nadhani haipendi ndiyo maana ameamua anipe. Kwa kufanya hivi unakaribisha magonjwa mwilini mwako.

 

7. Kujikasirikia.

Kuna watu wanajikasirikia baada ya kukosea katika kufanya maamuzi halafu yakamgharimu. Kama alikatazwa kuolewa na mtu fulani halafu akalazimisha na kujikuta akiteseka, anajikasirikia kwa maamuzi aliyoyafanya.

 

8. Dhambi na hatia inayosababisha kujihukumu na kupoteza matumaini.

Mtu wa aina hii hata kama Mungu atamsamehe, atashindwa kujisamehe yeye mwenyewe. Lazima Mungu akikusamehe na wewe pia uupokee msamaha wake (uamini kwamba umesamehewa).

 

9. Kukosa uzoefu wa mambo yanayopendeza au kuvutia.

Kuna watu wana uzoefu wa mambo mabaya tu katika maisha yao. Hawajawahi kuonyeshwa upendo wa kweli. Ukifuatilia sana vijana wengi wanaodanganyika ni wale ambao hawakuonyeshwa upendo wa dhati na wazazi wao. Msicahana hajawahi kuambiwa na wazazi wake, Nakupenda mwanangu. Hivyo anasikia kwa mara ya kwanza neno hilo likitoka kwa watu wenye nia mbaya na yeye na kujikuta akiangukia mikononi mwa mawakala wa shetani.

 

10. Kupoteza maana na kusudi la maisha.

Lazima ujiulize kama unakula ili uishi au unaishi ili ule. Kila mmoja yupo hapa duniani kwa kusudi maalum la Mungu. Mafanikio yako yanategemea kiasi gani unalitambua kusudi hilo. Unaweza kuonekana kwa nje unamiliki mali lakini kama hutagundua kusudi la Mungu kwako hutafurahia unachokimiliki.

 Kipindi kijacho nitazungumzia, ‘Nitajuaje kama nina sonona?’ ‘Nifanyeje kama nina sonona?’ nk.

 Dr. Lawi Mshana, +255712924234, Tanzania