Ticker

6/recent/ticker-posts

Nimechoka kukaa peke yangu na sipati mume

Nimechoka kukaa peke yangu na miaka inasonga mbele bila mafanikio

Swali lenyewe nililokuwa nimepewa ni hili: “Nimechoka kukaa peke yangu na nimeshamwomba Mungu muda mrefu anipe mume lakini bado sijapewa na miaka inasonga mbele bila mafanikio Je, nifanyeje?” 

Ni kweli kwamba Mungu  anasema hapendezwi mtu awe peke yake kama unavyojisikia. Mwanzo 2:18 “Bwana Mungu akasema, Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye.” Lakini kutopewa  mume wakati umechoka kukaa peke yako kunaweza kuwa na sababu mbalimbali. 

Inawezekana kwamba:

1. Mungu ameona kwamba uchovu wako na upweke wako hautamalizwa na mume. Nimewahi kupata shuhuda za baadhi ya watu waliopitia hali hizi wakadhani ni tatizo la kimwili na kumbe ni tatizo la kiroho. Kama sio upweke wa kawaida mtu anaweza kuoolewa na bado asitosheke. Wakati mwingine mtu anahitaji kuombewa ili awekwe huru.

2. Mungu anaona kuwa mambo unayo pitia hata wengine walioolewa wanayapitia. Ndio maana wengine ingawa wameolewa bado wanashawishika kutoka nje ya ndoa zao. Kwa maneno mengine wapo wanandoa ambao bado ni wapweke ingawa Mungu alikusudia kuitumia ndoa kumaliza upweke. Ndoa yenye kasoro haiwezi kumaliza upweke.

3. Shetani alivuruga mpangilio wa maisha yako kwa sababu ya kuchelewa kuokoka  au kukufanya upishane na Mungu au maagano ya kishetani katika ukoo wenu. Kwa hiyo Mungu atauondoa upweke wako kwa maombi ya kimalengo, kuvunja hayo maagano au kwa njia zingine za ki-Mungu.  Mfano mpango wa Daudi kumuoa Merabu ulipovurugwa, ilibidi amuoe Mikali (I Sam 18:17-21).     Mikali akamsumbua sana Daudi mpaka ikabidi Bwana amuinulie Yonathani kuziba pengo la upendo alioukosa (2  Sam 1:26 “Nimesikitika kwa ajili yako, Yonathani, ndugu yangu, Ulikuwa ukinipendeza sana; Upendo wako kwangu ulikuwa wa ajabu, Kupita upendo wa wanawake.”) Kuna watu wanatafsiri vibaya andiko hili kwa vile wameharibika akili zao. Hivyo wanadhani walipendana kama mashoga. Maana yake halisi ni kwamba Mungu anaweza kukuinulia mwanamke mwenzako mwenye huduma ya kukutia moyo kuliko kuolewa na mwanaume anayetimiza  tamaa zako za mwili bila upendo wa kweli. Daudi na Yonathan hawakutamaniana kama mashoga bali walipendana katika upendo wa ki-Mungu.  1Sam 18 :  1 “…Yonathani akampenda (Daudi) kama roho yake mwenyewe?” Wanawake wenzako wana ushawishi mkubwa katika maisha yako. Wanaweza kujenga maisha yako au kuyabomoa.

4. Mungu hajamuandaa bado mume uliyemuomba katika mazingira yako. Inategemea unataka mume wa sifa gani. Pengine mazingira yako hayana mwanaume mwenye sifa ulizoomba. Mtumishi wa Ibrahim angempataje Rebeka kwa ajili ya Isaka kama hangeenda Mesopotamia? (Mwa 24:1-20 “…..Kisha huyo mtumishi akatwaa ngamia kumi katika ngamia za bwana wake akaenda zake, maana mali zote za bwana wake zilikuwa mkononi mwake, akaondoka, akaja mpaka Mesopotamia, mpaka mji wa Nahori.”). Unapokuwa unafanya maombi tu lakini hushiriki makongamano ya kukukutanisha na watu mbalimbali unajiwekea mipaka. Wengine wamepata shida zaidi kwa vile wanajuana kanisani kwao tu na hapo kanisani idadi ya wasichana ni mara mbili ya wavulana. Kinachotokea ni kugombania au kukosa kabisa mtu anayeendana naye. Lakini Mungu hajaishiwa kiasi hicho. Hata hivyo sina maana uzurure mitaani au makanisani ili kupata mtu wa kukuoa. Ninachotaka kusema ni kwamba lazima upanue wigo wa upatikanaji wa mwenzi wa maisha yako. Isa 54:2 “Panua mahali pa hema yako, na wayatandaze mapazia ya maskani yako; usiwakataze; ongeza urefu wa kamba zako; vikaze vigingi vya hema yako.” Kama maombi yako ni kuolewa na rubani sio rahisi kumpata katika mazingira yoyote labda Mungu mwenyewe aingilie kati. Hivyo unatakiwa ujue wanapatikana maeneo gani zaidi.

5. Mtu anayehitaji kuoa mtu kama wewe hajui kama unalo hitaji hilo na hajui kuwa huna mume. Kwa muda mrefu mataifa mengine yamekuwa na mitandao ya kuwaunganisha wakristo wenye mahitaji mbalimbali likiwemo la kupata mwenzi wa maisha. Ukweli ni kwamba, ni mara chache sana utampata mwenzi bila kukutana au kukutanishwa naye. Kijana  Adamu  alimletewa  msichana  Hawa akaachiwa uhuru wa kumpokea kama mke wake. Kamwe Mungu halazimishi mtu aolewe na mtu fulani. (Mwa 2:22-23 “na ule ubavu alioutwaa katika Adamu Bwana Mungu akaufanya mwanamke, akamleta kwa Adamu. Adamu akasema, Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanamume.”). Hata hivyo ni vizuri kuwashirikisha watumishi wa Mungu waaminifu walio karibu nawe kuhusu hitaji lako.

6. Kuna mambo ambayo Mungu anaendelea kukufanyia katika kipindi hiki cha ukimya ambayo yatakufaa baadaye. Yn 13:7. “Yesu akajibu, akamwambia, nifanyalo wewe hujui sasa, lakini utalifahamu baadaye?” Inawezekana katika kipindi hiki Mungu hakuandalii  mwenzi wako bali anakuandaa wewe mwenyewe. Mtu mwingine anataka kupata mume mwenye sifa nzuri wakati yeye mwenyewe ana sifa mbaya. Kubali utengenezwe kwanza kwa kumuomba Mungu akusaidie kutambua maeneo ambayo wewe ni kikwazo katika kupata mwenzi. Mfano, baba yako aliwahi kukulaani kwamba hutaolewa kutokana na jambo baya ulilomtendea au pengine u mvivu na kupika hujui au pengine u mchoyo. Mungu anaangalia pia kwamba utafanyika baraka kiasi gani kwa mumeo na sio tu kupata mume mzuri. Kama mume wako atatoka nchi nyingine inawezekana unasubiriwa ujue kingereza kwanza. Tambua maandalizi ya maisha unayotakiwa kufanya. Tatizo wengi tunaandaa arusi badala ya kuandaa maisha! Matokeo yake harusi inakuwa kubwa sana halafu kesho yake tunaanza kuishi maisha yasiyo na uhakika.

7. Pengine hali ya upweke na uchovu  unayopitia ni ya kipindi tu.  Una muda mfupi hali hiyo itaondoka yenyewe au itapungua kadri umri wako unavyosogea. Mabadiliko yanayoendelea katika mwili wako yanaweza kuchochea ashiki (tamaa ya mwili) wakati  fulani fulani. Jifunze pia kuikubali hali yako badala ya kujilinganisha na watu wengine. Mpango wa Mungu kwako ni tofauti na mtu yeyote duniani. Ndiyo maana dole gumba lako (fingerprint) halifanani na la yeyote kati ya watu takriban bilioni 7 duniani. Usisahau kwamba sio wakati wote wanandoa wanakuwa pamoja. Wakati mwingine mmojawapo anaenda masomoni au kuwa mbali na mwenzake sababu ya ajira nk na bado wanadhibiti tamaa na kutunza uaminifu wao. Ni suala la uamuzi tu na kuwa na hofu ya Mungu. Maisha yetu yanategemea tumeamua nini. Kum 30:19 “Nazishuhudiza mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimekuwekea mbele yako uzima na mauti, baraka na laana; basi chagua uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako.”

8. Pengine unaomba na kusubiri uote ndoto au mtu fulani akuote badala ya kujiweka katika hali inayofaa kuposwa. Hapa sina maana kwamba  ufanane  na kahaba. La hasha! Unatakiwa ufanane na  Rebeka. Rebeka alipokuwa na hitaji la kuolewa hakubakia katika  kuomba tu (kama aliomba kweli) bali alikuwa mkarimu  kwa  wageni na mwenye bidii (Mwa 24:17-20 “…Naye akasema, Unywe, bwana wangu, akafanya haraka, akatua mtungi wake mkononi mwake, akamnywesha. Hata alipokwisha kumnywesha akasema, Na ngamia zako nitawatekea, hata watakapokwisha kunywa…”). Kunywesha ngamia siyo kazi ndogo. Wanakunywa maji mpaka ya akiba wanayoyatumia mahali pasipo na maji. Ndio maana wanaweza kuishi jangwani. Rebeka alimpokea kwa ukarimu mtu ambaye hana sifa za kumuoa. Kumbe alikuwa ametumwa kumpatia Isaka mke na aliweka ishara zake. Kuna wasichana wanawachekea wanaume wanaotaka kuolewa nao na kuwadharau watu wengine. Matokeo yake wanakosa sifa kwa vile ili mtu aoe lazima aulize pia ndugu na majirani hasahasa wazee. Unatakiwa pia uwe  katika hali inayofaa kuwekewa tumaini kama mke nyumbani. Kwa kifupi, usiwe tu “mwanamke” bali uwe “mke”! Linda sana ushuhuda wako.     

9. Pengine u kigeugeu katika maombi yako. Ukijisikia tamaa unaomba sana upewe mume lakini tamaa ikipungua au ikitoweka na ukiona walioolewa wengine wanavyoteseka, unabadili maombi na kuomba utiwe nguvu tu ya kuendelea kuishi peke yako. Yakobo anasema, mtu wa nia mbili asidhani kuwa atapokea kitu kwa Bwana (Yak 1:6-7 “Ila na aombe kwa imani, pasipo shaka yo yote; maana mwenye shaka ni kama wimbi la bahari lililochukuliwa na upepo, na kupeperushwa huku na huku. Maana mtu kama yule asidhani ya kuwa atapokea kitu kwa Bwana.”). Maombi yako ya kupata mwenzi yasiongozwe na tamaa bali hitaji lako na ahadi za Mungu. Tumia neno la Mungu kudai haki zako badala ya msukumo wa tamaa. Mungu analiangalia neno lake apate kulitimiza na sio tamaa zako. Usiombe mambo mengi kwa wakati mmoja mpaka unasahau uliomba nini. Jifunze kudai haki yako mpaka uipate. Msumbue Mungu kama yule mwanamke mjane aliyedai haki yake mpaka kadhi dhalimu akampatia kwa shingo upande ili asisumbuliwe kila siku (Lk 18:1-8).

10. Pengine hicho ndicho kipimo chako cha kumpenda Mungu. Mwingine anaweza kuwa na  mume lakini kipimo chake kiwe kukosa watoto, kufarakana, magonjwa,  maisha magumu, kukosa uaminifu au ulemavu fulani. Sio wote wanafurahia ndoa zao. Wakati watu wengine wanataka kuingia kichwa kichwa kwenye ndoa (bila kujua majukumu yao), wengine wanataka kutoka (kwa kushindwa kufikia matarajio yao). Ndoa inahitaji kupaliliwa na kuhudumiwa ili isigeuke na kuwa ndoana. Zipo ndoa nyingi ambazo hazina “kanuni” yoyote ya kuiongoza ili kufikia malengo yake. Kila mtu anafanya lolote analoona ni jema kwake. Amu 21:25 “Siku hizo hapakuwa na mfalme katika Israeli; kila mtu alifanya yaliyokuwa ni mema machoni pake mwenyewe. 

Kwa hiyo nakushauri mambo yafuatayo:

Kwanza, muombe Mungu akuondolee upweke wako bila kumchagulia kwamba auondoe kwa   kukupa mume. Mungu aliyekuumba kwa mfano wake anaweza kukusaidia kwa njia nyingi.  

Pili, tambua nia ya Mungu kwa ajili ya maisha yako. Pengine kuna jambo kubwa analotaka kukufanyia au kukutumia kulifanya kwanza ukiwa bado unaishi peke yako.

Tatu, kubali katika maisha yako kwamba kuwa peke yako sio tatizo. Mungu mwenyewe akiona haja atakupa mume kwa sababu u mtoto wake. Mtume Paulo alipewa karama ya kutokuoa. 1 Kor 7:8 “Lakini nawaambia wale wasiooa bado, na wajane, Ni heri wakae kama mimi nilivyo.

Nne, jipatie marafiki katika wanawake wenzako wenye mawazo sahihi (chanya) ambao hawatakuamsha tamaa za mwili. Unapaswa kuzungumza zaidi na watu wanaoona mafanikio yako kuliko upungufu wako. Usipoteze muda na watu ambao kila saa wanakuambia, “Hivi unawezaje kuishi peke yako!” Wanatakiwa waone pia maendeleo yako yaliyotokana na wewe kuwa peke yako.

Tano, mtumikie Bwana kwa bidii ili Mungu akuheshimu (Yn 12:26 “Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Tena mtu akinitumikia, Baba atamheshimu.”). Uwepo wa Mungu pamoja na shughuli nyingi za ki-Mungu vinaondoa mawazo potofu. Kuna msemo unaosema, ‘akili isiyo na la kufanya ni karakana ya shetani’. Kama kichwa chako kimejaa taarifa za Mungu,  shetani hatapata nafasi ya kurekodi vya kwake.

 Sita, utese mwili mara kwa mara kwa kufunga na kuomba, kukesha na kutumika. Mwili ukinyimwa madai yake, unapoteza pia tamaa ya mwili. Ndio maana ukiwa mgonjwa tamaa pia inatoweka. Kumbuka, ukifanya uamuzi wa kufanya jambo au kutolifanya, baadaye hisia zako zitakubaliana nawe. Hatimaye, itakuwa ni mtindo wa maisha yako. Mwili una tabia ya kukubaliana na hali ambayo umeuzoeza. Ukizoea kula chakula muda fulani, tumbo litaanza kunguruma muda huo ukifika. 

Saba, vunja maagano ya kishetani (kama yapo) ili shetani asizuie kusudi la Mungu juu ya maisha yako. Nimewahi kuombea dada mmoja pepo likalipuka na kusema halitaki aolewe. Pepo hilo lilipotoka tu ndani ya wiki moja alichumbiwa na wanaume watatu. Wazazi wake wakaniambia kwamba alikuwa hachumbiwi kabisa. Unajua shetani hashindwi kukuvalisha kinyago uonekane u mvulana badala ya msichana ili tu usichumbiwe.

Mwisho, nakusihi uungane na kile Paulo alichowaambia Wagalatia. Gal 6:17    ‘Tangu sasa mtu asinitaabishe, kwa maana ninachukua mwilini mwangu chapa zake Yesu!’ Kama unaye Yesu rohoni, sasa chukua CHAPA ZAKE YESU mwilini mwako. Ukimvaa Yesu tamaa za shetani hazitaweza kukugusa wala kukutesa. Rum 13:14 “Bali mvaeni Bwana Yesu Kristo, wala msiuangalie mwili, hata kuwasha tamaa zake.” 

Naamini lipo jambo mojawapo litaweza kukusaidia ili na wewe uwe na maisha ya furaha kama watu wengine. Mungu anakuwazia mawazo ya amani hivyo usikate tamaa na wala usichoke. Yeye ni mwaminifu na wa haki atafanya kila jambo kwa wakati unaofaa.

Uwe na moyo mkuu.

POKEA HAJA YA MOYO WAKO KATIKA JINA LA YESU KRISTO!

Dr. Lawi Mshana, +255712924234, Tanzania