Ticker

6/recent/ticker-posts

Je naweza kupata mume kama yule wa mwanzo?

Je, naweza kupata mume kama yule aliyetangulia mbele ya haki? – Dr Lawi Mshana

Mungu anaweza kukupa mume kama yule aliyekuacha mjane kwa sababu mojawapo kati ya hizi:

1. Kama Mungu ndiye alihusika kukupa mume huyo.

Ikiwa una uhakika wa kutosha kwamba mume huyo ulimpata katika mazingira ya ki-Mungu, anaweza kukupa anayefanana naye katika maeneo ya msingi kv tabia. Si rahisi afanane naye kwa kila kitu mpaka sura nk. Yoeli 2:25 “Nami nitawarudishia hiyo miaka iliyoliwa na nzige, na parare, na madumadu, na tunutu, jeshi langu kubwa nililotuma kati yenu.” 

2. Kama umemuomba Mungu afanye hivyo.

Mungu anaweza kufanya hivyo kama una uhusiano mzuri na Mungu na umemuomba hivyo na kuwa na subira. Ili mradi usije ukamtangulia Mungu bali umpe muda. Neno la Mungu linasema ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa. . Yn 15:7 “Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa.”

3. Kama Mungu alimuona kwamba anakufaa kuliko wengine usiowafahamu.

Mungu anajua pengo lako kuliko wewe mwenyewe unavyolifahamu. Hivyo anaweza kuona anayekufaa zaidi ya huyo uliyekuwa umemzoea. Yeremia 29:11 “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.”

Hata hivyo ni vizuri kuzingatia yafuatayo:  

1. Ukipewa mume usimlinganishe na yule wa kwanza bali umlinganishe na Kristo  (kichwa cha kanisa) na ujali mpango wa Mungu kwa ajili yako wakati huu. Mara nyingi mume wa kwanza anakuwa kipimo hata kama alikuwa na matatizo kwa sababu hujui wengine wakoje. Kama ulijifunza kuishi na yule wa kwanza mpaka ukaweza kumkubali kama alivyo, utatakiwa pia kujifunza kuishi na mwingine utakayempewa.

2. Tambua udhaifu wako kabla ya kutaka mume mzuri ili na wewe utengenezwe na Bwana. Usitake tu kupata mume anayekupenda bali utake pia mume utakayemtii. Efe 5:22-25 “Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu…. Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake”. Mke akijitiisha kwa mumewe, huyo mume atampenda. Na Mume akimpenda mkewe, mke huyo atajitiisha kwake. Uhusiano huu unategemeana. Ukitaka mume mzuri na wewe uwe mzuri pia!

3. Inawezekana kwamba mume wa mwanzo alikuwa mzuri kwako kwa sababu tu alikupa uhuru kupita kiasi na alipuuzia madhaifu yako mengi bila kukukosoa. Je, ukipewa anayependa kukufundisha na kukukosoa pale inapobidi atakuwa ni mbaya? Mume mzuri ni yule atakayeweza kuziba pengo ulilo nalo na ambaye utaweza kuziba pengo alilo nalo. Hata kama utapata mume anayekufaa kuliko yule wa mwanzo ndoa yenu haitakuwa ya furaha kama Mungu hakuhusika na wewe siyo chaguo lake la kwanza, yaani havutiwi sana na wewe. Mume anaweza kuwa chaguo lako la kwanza (the best / unampenda kuliko wote), lakini wewe kwake ni chaguo la pili (the second best / hakupendi kama fulani).

4. Mume tofauti na yule wa mwanzo atakuwa mbaya kwako kama wewe sio mtu unayeweza kuishi na watu wenye tabia tofauti tofauti. Lazima uwe mtu unayeweza kuchukuliana na watu wa aina tofauti. Mume mzuri ni yule anayeshaurika na anayejali kukufahamu na kuelezea hisia zake kwako. Hutapata mtu aliyemaliza chuo cha ndoa. Mnachotakiwa kufanya ni kukubali kuwa wanafunzi wa chuo cha ndoa hadi pale kifo kitakapowatenganisha. Tabia zingine zinabadilika kadiri umri unavyosogea na maisha yanavyobadilika.

Nadhani maelezo haya yamekupa mwanga fulani ingawa swali lako haliko wazi sana kwamba mume wako wa mwanzo alikuwaje na ulimpendea nini. Pia sijui kama alikuwa ameokoka au la, ulimtawala au alikutawala, na sijui ulimpendea sura, umbile, tabia, huduma, mapenzi, au utajiri.

Hata kama Mungu atakupa kama wa mwanzo, hataangalia zaidi mambo ya kimwili bali ataangalia moyo. 

I Sam 16:7 “lakini BWANA  akamwambia Samweli, usitazame uso wake, wala urefu wa kimo chake, kwa maana mimi nimemkataa.  BWANA  haangalii kama binadamu aangaliavyo, maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali BWANA  huutazama moyo.”

Hata hivyo haina maana kwamba ni kosa kuitazama sura au mvuto wa nje. Andiko hili lina maana kwamba Mungu hafanani na sisi. Yeye anaangalia moyo wakati sisi alivyotuumba tunaangalia sura ya nje. Ukiwa mtu wa rohoni unaweza kujaliwa kuona moyo lakini haina maana upuuzie mambo ya nje unayoyapenda. Kama tungetakiwa kupuuza kabisa mambo tunayopenda hatungechagua nguo dukani wala aina ya kinywaji. Ingekuwa vyote sawa tu. Lakini Mungu ametupa utashi na uwezo wa kuchagua aina ya maisha tunayotaka. La msingi ni kuanzia moyoni kwa msaada wa Mungu na kumalizia nje kwa mtazamo wa kibinadamu (inside-out). Ni raha zaidi kuishi na mtu unayempenda ndani na nje kwa vile maisha ya ndoa ni ya kiroho na kimwili pia. Huoi au kuolewa na mtu ili aishi na Mungu bali kusudi aishi na wewe Mungu akiwa katikati yenu.

Kwa yeyote unayefanana na huyu aliyeuliza swali hili:

1. Nakuombea kwamba kabla Mungu hajakupa mume unayemtaka akurejeze na kukuandaa kwanza wewe mwenyewe. Yaani akupe uhusiano wa karibu na Yeye ili akuunganishe na mtu sahihi. 

Yeremia 15:19 “Kwa sababu hiyo Bwana asema hivi, Ukirudi, ndipo mimi nitakapokurejeza, upate kusimama mbele zangu; nawe ukitoa kilicho cha thamani katika kilicho kibovu, utakuwa kama kinywa changu; nao watakurudia wewe, bali hutawarudia wao.”

2. Lakini pia nakuombea kwamba usiwe na hofu ya maisha, usiaibike na Mungu awe faraja yako ya karibu sana.

Isa 54:4-6 “Usiogope; maana hutatahayarika; wala usifadhaike; maana hutaaibishwa; kwa kuwa utaisahau aibu ya ujana wako, pia mashutumu ya ujane wako hutayakumbuka tena. Kwa sababu Muumba wako ni mume wako; Bwana wa majeshi ndilo jina lake; na Mtakatifu wa Israeli ndiye Mkombozi wako; Yeye ataitwa Mungu wa dunia yote. Maana Bwana amekuita kama mke aliyeachwa na kuhuzunishwa rohoni, kama mke wakati wa ujana, atupwapo, asema Mungu wako.”

Pokea katika Jina lipitalo majina yote la Yesu Kristo!