Ticker

6/recent/ticker-posts

Ninaishi peke yangu na ninashindwa kujizuia kuwaka tamaa

NINAISHI PEKE YANGU NA NIMESHINDWA KUJIZUIA KUWAKA TAMAA – Dr Lawi Mshana Ujumbe huu umetokana na mtu aliyekuwa ameniuliza swali kama unavyoliona hapo chini. Ingawa ni mwanamke nimejibu pia kumsaidia na mwanaume. Inawezekana upo mwenye swali kama hili ndiyo maana nikaona nitume hadharani na wewe usome pia na kujifunza. Mimi ni mwanamke niliyeokoka ninayeishi peke yangu. Inafikia wakati ninashindwa kujizuia katika kuwaka tamaa na Bibilia inasema kuwaka tamaa ni dhambi. Je nifanyeje ili kudhibiti hali hiyo? Je kama kuwaka tamaa ni dhambi na nimeshindwa kuzuia hali hiyo isinipate ina maana ninaweza nisiingie mbinguni kwa sababu hiyo? Kuna aina mbalimbali za tamaa ila nitazungumzia mbili ambazo wengi hawazitofautishi Tamaa ya mwili (sexual desire) Mtu yeyote aliye kamili kimaumbile (bila ulemavu wowote) Mungu amempa hali ya kumuhitaji mwenzi wa jinsi tofauti. Na wakati huo huo Mungu anataka uhitaji huo utoshelezwe ndani ya ndoa ya mume na mke mmoja (Mwanzo 2:24 “Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.”) na kuwaepuka wengine wote (l Korintho 6:18 “Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe.”). Kujiheshimu huku ndiko kunakomtofautisha mwanadamu na mnyama. Tamaa hii inaweza kujitokeza bila kushawishiwa na mtu yeyote tena bila kumfikiria mtu yeyote. Kwa kawaida tamaa hii inakuwa kali sana katika kipindi cha kubalehe au kuvunja ungo, kwa baadhi hata kipindi cha hedhi na katika kipindi cha umri wa makamo (miaka 45 hadi 60). (b) Tamaa mbaya (Lust) Anayeleta tamaa mbaya ni shetani kwa hiyo ni vigumu sana kuishinda kwa kutumia nguvu za mwili. Unaweza kujizuia usifanye uzinzi wa mwili (kitendo halisi cha zinaa) lakini hutaweza kuushinda uzinzi wa moyoni (mawazo). Mt 5:27-28 “Mmesikia kwamba imenenwa, Usizini; lakini mimi nawaambia, Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake.”. Tamaa mbaya ndiyo inayomfanya mtu atamani kufanya mapenzi na watu mbalimbali. Mtu aliyepagawa na pepo la tamaa mbaya, hawezi kuitawala tamaa aliyo nayo. Anaweza kumtamani mtu asiye na mvuto wowote mfano mtoto mdogo au bibi kizee. Tamaa hii ndiyo inayotengeneza wabakaji, makahaba, wasagaji, mashoga na wanaolala na wanyama. Mtu mwenye tamaa mbaya hawezi kutosheka hata kama ameoa au ameolewa. Kwa vile sijui ni tamaa ipi inakusumbua, nitakupa njia kadhaa za kudhibiti tamaa mbaya na tamaa ya mwili: 1. Kupata mume anayefanana nawe hasa hasa kimwili, kimaumbile na kimawazo Mwanzo 2:18 “Bwana Mungu akasema, Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye.” Mtu mwenye sifa za kiroho peke yake hafai kuwa mume wa mtu kwasababu lengo kuu la unyumba si kuwa roho moja tu bali ni kuwa mwili mmoja ( Mwanzo 2:24). Lazima awe na mvuto wa kimwili kwako. Mhu 9:9 “Uishi kwa furaha pamoja na mke umpendaye, siku zote za maisha yako ya ubatili, ulizopewa chini ya jua; siku zote za ubatili wako, kwa maana huo ni sehemu yako ya maisha; na katika taabu zako ulizozitaabika chini ya jua.”. Kuna mtu aliamua kumuoa msichana kwa vile ni mwambaji mzuri ingawa hamvutii. Kilichotokea, walipoishi pamoja alipata shida sana kumpenda mpaka ilibidi wakati mwingine amwambie, Hebu imba pambio. Alifanya hivi ili hisia za kumpenda zije. Hata hivyo upendo hautakiwi uwe wa hisia bali utokane na uamuzi ulioufanya. 2. Kuepuka mazingira hatarishi au vitu vyenye ushawishi wa tamaa. Usipende kuwa karibu sana (bila sababu za lazima) na wapenzi wako wa zamani au wanaume wanaokuvutia sana, katika maeneo yaliyojitenga. Kila mtu ana aina ya watu wanaomvutia zaidi. Na hakuna mtu mwenye mvuto kwa watu wote hata kama ana sura nzuri. “ Hii ni kutokana na kwamba kila mtu ana maeneo tofauti yanayomvutia. Mwingine sura, mwingine umbile, mwingine, sauti, mwingine busara nk. Huwezi kutia moto kifuani pako na nguo zako zisiteketezwe!’’ Mit 6:27-28 “Je! Mtu aweza kuua moto kifuani pake, Na nguo zake zisiteketezwe? Je! Mtu aweza kukanyaga makaa ya moto, Na nyayo zake zisiungue?”. Usipende utani na kuzoeana kupita kiasi na watu wa jinsi tofauti. Unaweza kujaribiwa kwa wepesi zaidi au kumtia majaribuni mwenzako. 3. Kutambua udhaifu wako na kufanya uamuzi Ayubu alifanya agano na macho yake kuhusu kumwangalia msichana. (Ayubu 31:1 “Nilifanya agano na macho yangu; Basi nawezaje kumwangalia msichana?”). Ayubu alijua kwamba macho ndio mlango unaotumika kuingiza upendo au tamaa hasa kwa wanaume. Ayubu hazungumzii kumwangalia mwanamke kwa kawaida bali kumwangalia kwa tamaa. Kwa wanawake upendo unaweza kuingia kupitia masikioni. Maongezi na maneno ya kutia moyo yanaweza kuingiza upendo kwa baadhi ya wanawake hata bila kuvutiwa na sura ya mtu husika. Hata Bwana Yesu alisema jicho likikukosesha ling`oe (Mt 5:29 “Jicho lako la kuume likikukosesha, ling'oe ulitupe mbali nawe; kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee wala mwili wako mzima usitupwe katika jehanum.”). Usipodhibiti macho yako unaweza kwenda Jehanamu kwa kushindwa kujizuia kuangalia visivyofaa kupitia TV, kompyuta na simu yako. Tumepewa mamlaka ya kutoa pepo lakini siyo kutoa zinaa - zinaa inakimbiwa! (1Kor 6:18 “Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe.”). 4. Kufanya mazoezi ya mwili. Biblia haijasema mazoezi ya mwili hayafai kabisa bali inasema yanafaa kidogo 1Tim 4:8 “Kwa maana kujizoeza kupata nguvu za mwili kwafaa kidogo, lakini utauwa hufaa kwa mambo yote; yaani, unayo ahadi ya uzima wa sasa, na ya ule utakaokuwapo baadaye.”. Mwili usiofanya mazoezi unasisimka zaidi katika kufanya mapenzi. Mazoezi yanaweza kuwa kuruka, kukimbia, kutembea, kufanya kazi zinazokutoa jasho nk. Hata hivyo usifanye mazoezi mazito bila kuanza taratibu na kuzingatia afya na umri wako. Unahitaji ushauri wa wataalamu. Wapo wanaosema kuogea maji baridi kunasaidia pia ila sina jibu la kitaalamu. Lakini pia ulaji wako wa vyakula unaweza kukufanya uamshe tamaa za mwili. Pata ushauri wa watu wanaojua lishe ili uchague vizuri vyakula unavyokula. 5. Kutafuta chanzo halisi cha tamaa Usipigane vita usiyojua chanzo chake kiko wapi (Yak 4:1-3 “Vita vyatoka wapi, na mapigano yaliyoko kati yenu yatoka wapi? Si humu, katika tamaa zenu zifanyazo vita katika viungo vyenu? Mwatamani, wala hamna kitu, mwaua na kuona wivu, wala hamwezi kupata. Mwafanya vita na kupigana, wala hamna kitu kwa kuwa hamwombi! Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu.”). Usihangaike na mkia wa nyoka, tafuta kichwa cha nyoka kiko wapi. Pengine wanaume wanaokutamani wanakutumia nguvu za kichawi ili uwapende. Unapopunguza maombi nguvu hizo zinaweza kukuathiri katika mwili na kukufanya uwakwe na tamaa kali inayohamahama kwa watu tofautitofauti. Baadhi ya watu katika ukoo kila mtu awe ameokoka au hajaokoka anaanguka kwa zinaa kwa vile kuna maagano yalifanyika katika madhabahu za ukoo yanayohitaji kuvunjwa kwa damu ya Yesu Kristo. Hata hivyo vita ya kuvunja madhabahu ni kali sana. Tambua mamlaka yako na kushirikisha watu wanaojua jinsi ya kuvunja madhabahu. Ukifanya vita hii bila nguvu za kutosha wanaweza kukuua ghafla, kukufilisi au kukufanya kichaa. 6. Kujitia nguvu kwa neno la Mungu lisiloshindwa. Biblia imejaa maneno mengi yanayoonyesha jinsi Mungu anavyowajali wajane na wapweke. Mungu wa miujiza hafungwi na ndoa aliyoianzisha mwenyewe. Anaweza kulifanya jangwa liwe ziwa la maji Isa 41:18 “Nitafunua vijito vya maji juu ya vilima, na chemchemi katikati ya mabonde; nitageuza jangwa kuwa ziwa la maji, na mahali pakavu kuwa vijito vya maji.”; Isa 54:6-8 “Maana Bwana amekuita kama mke aliyeachwa na kuhuzunishwa rohoni, kama mke wakati wa ujana, atupwapo, asema Mungu wako. Kwa kitambo kidogo nimekuacha; lakini kwa rehema nyingi nitakukusanya. Kwa ghadhabu ifurikayo nalikuficha uso wangu dakika moja; lakini kwa fadhili za milele nitakurehemu, asema Bwana, Mkombozi wako.”. Mungu anaweza kukufanya wewe uliyeachwa au kutelekezwe uwe na maisha ya utoshelevu bila kuolewa tena. Unaweza kuwa peke yako na ukatoshelezwa na Mungu (2 Kor 3:5 “Si kwamba twatosha sisi wenyewe kufikiri neno lo lote kwamba ni letu wenyewe, bali utoshelevu wetu watoka kwa Mungu.”). Mungu huwakalisha wapweke nyumbani. (Zab 68:6 “Mungu huwakalisha wapweke nyumbani; Huwatoa wafungwa wakae hali ya kufanikiwa; Bali wakaidi hukaa katika nchi kavu.”). Mungu anajua mapito yako na yuko tayari kuziba pengo lako kuanzia leo. 7. Kuenenda kwa Roho. Kama huongozwi na Roho Mtakatifu, unaongozwa na mwili wako au shetani kwa hiyo, lazima uteswe na tamaa. Ukitaka usitimize kamwe tamaa za mwili, enenda kwa Roho (Gal 5:16-21 “Basi nasema, Enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili. Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka. Lakini mkiongozwa na Roho, hampo chini ya sheria. Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu.”). Ukimtumia vizuri Roho Mtakatifu uliyempokea, atakupa ushindi katika vita hii. Unaweza KUMPOKEA Roho Mtakatifu na ushindwe kumruhusu KUKUONGOZA. Rum 8:14 “Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu.” Unapookoka unakuwa MTOTO wa Mungu na unapoongozwa na Roho unakuwa MWANA wa Mungu. Kwa tafsiri ya Kiyunani kuna hatua za ukuaji. Mtoto ni mchanga lakini mwana ni mtoto ambaye amekua. 8. Kuweka wazi kazi za shetani ili zivunjwe kwa maombi Kumbuka Yesu alidhihirishwa ili azivunje kazi za Ibilisi. Lakini swali ni je, unazijua kazi za ibilisi katika maisha yako? Epuka kuwa na vitu vinavyoalika mapepo ya tamaa mfano, mavazi ya makahaba (Mith 7:10 “Na tazama, mwanamke akamkuta, Ana mavazi ya kikahaba, mwerevu wa moyo”). Epuka pia kujipamba kama Yezebeli. 2Fal 9: 30 “Hata Yehu alipofika Yezreeli, Yezebeli akapata habari; akatia uwanja machoni mwake, akapamba kichwa chake, akachungulia dirishani.”; Ufu 2:20 “Lakini nina neno juu yako, ya kwamba wamridhia yule mwanamke Yezebeli, yeye ajiitaye nabii na kuwafundisha watumishi wangu na kuwapoteza, ili wazini na kula vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu.”). Yapo mavazi ya WACHA MUNGU na MAVAZI YA MAKAHABA. Na kibaya zaidi baadhi ya mavazi hayo yametengenezewa kuzimu ili ukiyavaa mapepo nayo yakuvae na uwakoseshe wengine. Jiulize kwa nini unajisikia kuvaa nguo inayotamanisha watu. Unapata faida gani kama unampenda Mungu. Hiyo ni roho ya Yezebeli. Pia tumia Jina la Yesu kuharibu ndoto chafu unazoota mfano kuota uko uchi mahali pasipostahili, kuota unazini au kubakwa na watu unaowajua au usiowajua n.k. Ndoto hizi usizipuuzie maana ni jambo halisi linalofanyika katika ulimwengu wa roho maishani mwako. Madhara yake: kama hujaolewa unaweza usiolewe tena, kama umeolewa unaweza usizae au umchukie mwenzi wako au yamuue mwenzi wako nk. Haya mapepo yanapomuoa mtu yanakuwa na wivu sana asimpende mtu mwingine. Yuda 1:8 “Kadhalika na hawa, katika kuota kwao, huutia mwili uchafu, hukataa kutawaliwa, na kuyatukana matukufu”. Omba au ombewa na kuchukua hatua zinazostahili nawe utaishi maisha ya ushindi katika Yesu Kristo. Nataka pia ujue kwamba Mungu ameweka ashiki (tamaa ya mwili) kwa makusudi mema ili watu waone umuhimu wa kuoa na kuolewa na kwa jinsi hiyo washiriki katika uumbaji (kuzaa watoto) na kufarijiana. Tamaa inakuwa dhambi pale: 1. Mtu anapoendekeza tabia ya kumtamani mtu ambaye sio mume wake wala mke wake. Kama ndege anapita juu yako na kwa bahati mbaya akakuchafua kichwani haitafanana na kuruhusu ajenge kiota kichwani mwako. Ninachotaka kusema hapa ni kwamba mwanaume yeyote akimwona mwanamke aliye uchi anaweza kumtamani lakini je, anakimbia au anakemea pepo huku amemkodolea macho? 2. Mtu anapoilisha tamaa na kuilea – inazaa dhambi. Yakobo 1:15 “Halafu ile tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa dhambi, na ile dhambi ikiisha kukomaa huzaa mauti.” Tamaa ikichukua mimba huzaa dhambi. Kama una ashiki na halafu kipindi hicho unakaa karibu na wanaume wanaokuvutia bila sababu za msingi, unaweza kutenda dhambi. Shetani atatumia nafasi hiyo kuwafanya wayatawale sana mawazo yako. Kwa hiyo, utatumia muda mwingi kuwafikiria, hasa hasa ukiwa peke yako. 3. Mtu anapotamani kukutana kimwili na mtu bila kumuoa au kuolewa naye Mungu hakukusudia tendo la mwili lianzishe upendo bali alikusudia likamilishe upendo aliouanzisha. Mara nyingi mtu wa tamaa anajifikiria mwenyewe bila kujali upande wa pili. Anataka tu kumtumia mtu kutimiza tamaa zake binafsi. Na mara nyingi hajali maisha ya baadae ya mtu huyo (2Sam 13:11-15 “Naye alipokwisha kuileta karibu naye, ili ale, Amnoni akamkamata, akamwambia, Njoo ulale nami, ndugu yangu. Naye akamjibu, La, sivyo, ndugu yangu, usinitenze nguvu; kwani haifai kutendeka hivi katika Israeli; usitende upumbavu huu. Nami nichukue wapi aibu yangu? Wewe nawe utakuwa kama mmoja wa wapumbavu wa Israeli. Basi, sasa, nakusihi, useme na mfalme; kwa maana hatakukataza kunioa. Walakini yeye hakukubali kusikiliza sauti yake; naye akiwa na nguvu kuliko yeye, akamtenza nguvu, akalala naye. Kisha Amnoni akamchukia machukio makuu sana; kwa kuwa machukio aliyomchukia yakawa makuu kuliko yale mapenzi aliyokuwa amempenda kwanza. Amnoni akamwambia, Ondoka, nenda zako.”). Hata hivyo mkristo wa kweli hapaswi kushindwa na tamaa. 1. Mtu yoyote hata asiyeamini amepewa uwezo wa kujitawala au kujizuia. Anaweza kuupa mwili wake sababu ya kuukatalia jambo lolote na ukatii. 2. Aliyeokoka akizungumza na watu wa jinsi tofauti mambo ya lazima tu bila utani uliozidi na faragha zisizo za lazima, haitakuwepo nafasi ya tamaa mbaya kumtawala. 3. Aliyeokoka anaagizwa kuusulubisha mwili, tamaa zake na mawazo yake (Gal 5:24) badala ya kusubiri akatumie mamlaka yake kwa mapepo yaliyopagaa watu wengine. Kumbuka mbinguni hawaingii wanaotenda dhambi kwa kukusudia ( Ebr 10:26-27) wala wanyonge na wazinzi ( Ufu 12:27; 22:15). Mbinguni wanaingia waliotunza vazi la wokovu ( Ufu 16:15; 3:4) na walioshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo na neno la ushuhuda wao (Ufu 12:11). Nataka kukutia moyo kwamba hakuna jambo ambalo huwezi kulishinda ukiwa na Yesu Kristo. Rum 8:37 “Lakini katika MAMBO HAYO YOTE tunashinda na zaidi ya kushinda, kwake yeye aliyetupenda!” Tamaa inaweza kumsababisha mtu asiende mbinguni kama hachukui hatua zozote za kuikabili ikiwa ni pamoja na kuichukia na kutumia mamlaka ya Jina la Yesu kuidhibiti. Naomba Mungu akutetee katika mapito yoyote unayopitia na eneo lolote ambalo unashindwa. Hakuna lisilowezekana Kwake. Dr Lawi Mshana, Korogwe, Tanga, Tanzania