Mambo yanayosababisha wivu na matokeo yake (sehemu ya pili)
Sababu ya saba, Kutofurahia waliokukuta wakikubalika kuliko wewe.
1 Sam 18:6-9,11 “Hata ikawa, walipokuwa wakienda, hapo Daudi aliporudi baada ya kumwua yule Mfilisti, wanawake wakatoka katika miji yote ya Israeli, kwa kuimba na kucheza, ili kumlaki mfalme Sauli; wakatoka na matari, na shangwe, na vinanda. Nao wale wanawake wakaitikiana wakicheza, wakasema, Sauli amewaua elfu zake, Na Daudi makumi elfu yake. Basi Sauli akaghadhibika sana, na maneno haya yakamchukiza; akasema, Wamempa Daudi makumi elfu, na mimi wamenipa elfu tu; kuna nini tena awezayo kupata, isipokuwa ni ufalme? Sauli akamwonea Daudi wivu tangu siku ile. Mara Sauli akautupa ule mkuki; maana alisema, Nitampiga Daudi hata ukutani. Daudi akaepa, akatoka mbele yake, mara mbili.”
Daudi alikuwa kijana mdogo wakati Mungu alipomtumia kumuua Goliati. Ilipasa mfalme ajionee ufahari kwa kuwa na shujaa katika taifa lake. Pia alipaswa kutambua kwamba Daudi hawezi kumpindua katika nafasi yake kwa vile ni kijana tu na hana jeshi. Sifa alizopewa kwa kuleta ushindi, zilimfanya mfalme aanze vita naye. Kuna mtu amekukuta katika nafasi fulani lakini amepata kibali kwa watu kuliko wewe. Badala ya kuanzisha vita naye, jihoji kwamba una mapungufu gani halafu ujirekebishe. Vinginevyo utakuwa na uchungu na kutafuta njia za kumzushia mabaya au hata kumuua.
Sababu ya nane, kutoridhika na ulichopewa.
Yn 21:20-22 ”Petro akageuka akamwona yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu anafuata; (ndiye huyo aliyeegama kifuani pake wakati wa kula chakula cha jioni, akasema, Bwana, ni nani akusalitiye?) Basi Petro akamwona huyo, akamwambia Yesu, Bwana, na huyu je? Yesu akamwambia, Ikiwa nataka huyu akae hata nijapo, imekupasaje wewe? Wewe unifuate mimi.”
Petro alipewa huduma na Bwana lakini alidhani Yohana amepewa kubwa zaidi kuliko ya kwake. Akataka kujua zaidi habari zisizomhusu jambo ambalo halikumfurahisha Bwana. Kama roho ya wivu imekutawala, utapenda sana kujua mambo yasiyokuhusu. Unapopenda kujua mambo yasiyokuhusu, unaweza kujiumiza mwenyewe. Mfano, unapotafuta kujua mtu anayefanya kazi kama ya kwako analipwa shilingi ngapi, utaumia kama utagundua kwamba analipwa zaidi yako. Unasahau kwamba mkataba wako wa ajira hautegemei mtu mwingine bali ni wewe tu na mkuu wako. Biblia inatuonya kwamba tuwe radhi na vitu tulivyo navyo. Tusisahau maisha tuliyokuwa nayo awali kwa kujilinganisha na watu ambao hatujui hata historia ya maisha yao.
Sababu ya tisa, kuchukia mafanikio ya wengine kwa vile wewe hujajibiwa
Yak 4:2,3 “Mwatamani, wala hamna kitu, mwaua na kuona wivu, wala hamwezi kupata. Mwafanya vita na kupigana, wala hamna kitu kwa kuwa hamwombi! Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu.”
Watu wengi wenye wivu wanapenda kulalamika kuliko kuomba. Na hata wakiomba, wanaomba kwa nia mbaya. Mfano: Mtu ambaye hajajaliwa kupata mtoto anaweza kufurahia wenye watoto wanapokosa msaada wa watoto wao. Anasahau kwamba watoto wa wenzake wanaweza pia kumsaidia katika maisha yake. Hii ni roho mbaya inayomfanya mtu aendelee kuishi maisha duni yasiyo na majibu dhahiri. Ni bora zaidi kujua mpango binafsi tuliopangiwa na Mungu badala ya kutafuta kuwa na maisha ambayo yako nje ya mpango wa Mungu kwetu.
Sababu ya kumi, kukosa huduma yenye mvuto na upako.
Mdo 5:16-18 “Nayo makutano ya watu wa miji iliyoko kandokando ya Yerusalemu wakakutanika, wakileta wagonjwa, nao walioudhiwa na pepo wachafu; nao wote wakaponywa. Akaondoka Kuhani Mkuu na wote waliokuwa pamoja naye, (hao ndio walio wa madhehebu ya Masadukayo), wamejaa wivu, wakawakamata mitume wakawaweka ndani ya gereza”
Tumeshuhudia watu wengi wakiwazushia mabaya watumishi wa Mungu kwa sababu ya wivu tu. Wengine wamefukuzwa kwenye huduma kwa vile tu wana huduma zenye mvuto kuliko za viongozi wao wakuu. Hata wakuu wa dini wa kipindi cha huduma ya Yesu akiwa duniani kimwili walimzushia kwamba anatoa pepo kwa Belzebuli kwa vile tu wao wenyewe hawajawahi kutoa pepo. Unapotumiwa kwa viwango vya juu, wengine watakupaka matope bila hata kukuuliza wajue huduma yako ikoje na bila hata kukuombea.
Sababu ya kumi na moja, kutamani huduma zenye upako ili kujionyesha au kuonekana wa maana
Mdo 19:13-16 “Baadhi ya Wayahudi wenye kutanga-tanga, nao ni wapunga pepo, wakajaribu kutaja jina la Bwana Yesu juu yao waliopagawa na pepo wachafu, wakisema, Nawaapisha kwa Yesu, yule anayehubiriwa na Paulo. Walikuwako wana saba wa mtu mmoja Skewa, Myahudi, kuhani mkuu, waliofanya hivyo. Yule pepo mchafu akawajibu, akawaambia, Yesu namjua na Paulo namfahamu, lakini ninyi ni nani? Na yule mtu aliyepagawa na pepo mchafu akawarukia wawili, akawaweza, akawashinda, hata wakatoka mbio katika nyumba ile hali wa uchi na kujeruhiwa.”
Kuna watu wanatamani kufanya huduma ambazo hawajapewa kwa kutaka tu kujipatia sifa. Watu hawa walikuwa hawamtaki Yesu lakini wanataka umaarufu kwa kutumia jina Lake. Walimwonea wivu Paulo hivyo walitaka wajulikane kama yeye. Kama wangekuwa na nia ya kusaidiwa wangepeleka wenye pepo kwa Paulo wakafunguliwe. Matokeo ya kujiingiza kwenye huduma kwa namna hii ni kuvamiwa na mapepo na kuaibika mbele za watu.
Sababu ya kumi na mbili, kutofurahia huduma zenye upako zikiwa nje ya dhehebu lako.
Lk 9:49-50 “Yohana akajibu akamwambia; Bwana mkubwa, tuliona mtu anatoa pepo kwa jina lako; tukamkataza, kwa sababu hafuatani na sisi. Yesu akamwambia, Msimkataze, kwa kuwa yeye ambaye si kinyume chenu yu upande wenu.”
Kuna watu wanajisikia vibaya sana wanaposikia kwamba mtu fulani anatumiwa na Mungu wakati yuko nje ya dhehebu lao. Wanaona kwamba kama wataitambua huduma yake watu watawahama na kumfuata. Wanasahahu kwamba hakuna dhehebu linaloenda mbinguni hata moja. Madhehebu yanatusaidia tu kutambuana duniani na kutambulika serikalini. Kinachotambulika mbinguni ni majina ya wakristo walioshinda ambayo yako kwenye kitabu cha uzima. Yesu aliwaonya wanafunzi wake kwamba wasiangalie kufuatana au kutumika pamoja bali matokeo wakati jina lake linapotumika. Kimsingi, hakuna ‘hati miliki’ katika huduma za Mungu. Wengi wamebaki na mateso yao kwa vile tu wamekatazwa kukutana na huduma zenye funguo za matatizo yao. Wivu unasababisha kulinda dhehebu kuliko roho za watu.
Dr. Lawi Mshana, +255712924234, Tanzania