Ticker

6/recent/ticker-posts

Mambo yanayosababisha mtu awe na wivu na matokeo yake (sehemu ya kwanza)

Mambo yanayosababisha mtu awe na wivu na matokeo yake (sehemu ya kwanza)

Ninapenda kukushirikisha ujumbe ambao Roho Mtakatifu alinipa kuhusu wivu. Ujumbe huu unaweza kukufaa wewe mwenyewe pamoja na kuushirikisha kwa wengine. Kama masomo haya yanakufaa au yanawafaa unaowapatia, usisite kunipa ushuhuda.

Sababu ya kwanza, mtu kutofurahia mwenzake akipata kibali kwa Mungu kuliko yeye. Mwa 4:4-5 “Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. Bwana akamtakabali Habili na sadaka yake; bali Kaini hakumtakabali, wala sadaka yake. Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana.” Badala ya Kaini kujifunza kwa mdogo wake ili naye ampendeze Mungu, yeye alikasirika. Matokeo yake akafanya hila ya kumuua ndugu yake. Wapo watu ambao wakiona maendeleo ya wenzao hawapendi kujifunza kwao bali wanatafuta njia za kuwakwamisha ili wabaki katika hali duni kama waliyo nayo. Sijui watu wote wakiwa duni au masikini nani atamuinua au kumkopesha mwenzake. Kama kuna mtu amepata kibali kuliko wewe na unajisikia vibaya, usisahau kwamba Mungu anakuona. 

Sababu ya pili, mtu kutowafurahia wenye maono asiyokuwa nayo. Mt 20:20-21, 24 “Ndipo mama yao wana wa Zebedayo akamwendea pamoja na wanawe, akamsujudia, na kumwomba neno. Akamwambia, Wataka nini? Akamwambia, Agiza kwamba hawa wanangu wawili waketi mmoja mkono wako wa kuume, na mmoja mkono wako wa kushoto, katika ufalme wako. Na wale kumi waliposikia, waliwakasirikia wale ndugu wawili.” Hakuna mwanafunzi wa Yesu aliwahi kukatazwa kuomba chochote kwa Bwana. Baada wanafunzi wawili kati yao kupata ufunuo wa maombi ya aina yake, wale wengine wakawakasirikia. Wapo watu wanakukasirikia kwa vile tu umewatangulia kuona jambo jema ambalo hawajaliona. Hata hivyo Bwana ni mvumilivu kwa vile hata hawa kumi ingawa waliwakasirikia wale wawili, hakuwafukuza katika utumishi. Mabadiliko na maendeleo yanaletwa na wenye maono makubwa. Hakuna kitu unachoweza kununua bila kukijua kwanza kupitia kwa mtu mwingine. 

Sababu ya tatu, mtu kuona kwamba tendo alilolifanya mwenzake linampa umaarufu kuliko yeye. Mk 14:3-9 “…Palikuwa na watu waliochukizwa katika nafsi zao wakisema, Kwani kupoteza marhamu namna hii? Maana marhamu hii ingaliweza kuuzwa kwa dinari mia tatu na kuzidi, wakapewa maskini. Wakamnung'unikia sana yule mwanamke….” Wanafunzi walitumika na Bwana Yesu muda mwingi wakasahau kwamba hata Bwana Yesu anahitaji huduma yao. Wapo watu ambao wamezama kwenye huduma mpaka wamesahau mahitaji ya msingi ya wachungaji wao. Matokeo ya watu wa aina hii ni kwamba wanachukizwa na kutoa ushauri mbaya wakiona mtu anasaidia watumishi wa Mungu. Wanajisikia vibaya wanapopitwa na mwingine katika utumishi hata kama walishindwa wenyewe kutoa mali zao. Mwanamke aliona thamani ya Yesu kuliko waliokuwa naye wakati wote. Wanafunzi walitakiwa kumshukuru kwa kuwakumbusha badala ya kumkasirikia. 

Sababu ya nne, mtu kuomba bila kujiandaa na matokeo ya maombi yake. Mwa 16:1-2,5-6 “Basi Sarai mkewe Abramu hakumzalia mwana, naye alikuwa na mjakazi, Mmisri, jina lake Hajiri. Sarai akamwambia Abramu, Basi sasa, Bwana amenifunga tumbo nisizae, umwingilie mjakazi wangu labda nitapata uzao kwa yeye. Abramu akaisikiliza sauti ya Sarai. Sarai akamwambia Abramu, Ubaya ulionipata na uwe juu yako; nimekupa mjakazi wangu kifuani mwako, naye alipoona kwamba amepata mimba, mimi nimekuwa duni machoni pake. Bwana na ahukumu kati ya mimi na wewe. Naye Abramu akamwambia Sarai, Tazama, mjakazi wako yu mkononi mwako, mtendee lililo jema machoni pako. Sarai akamtesa, naye akakimbia kutoka mbele yake.” Sarai alimuomba mumewe afanye jambo ambalo hakuwa amejiandaa na gharama ya majibu yake. Alitaka tu apate mtoto kupitia kwa mjakazi wake bila kujiandaa kwamba heshima yake itakuwaje. Matokeo yake, mtoto alipopatikana akahofu kwamba atapoteza heshima na kuanza kumtesa mjakazi wake. Wapo watu wengi wa aina hii makazini, majumbani na makanisani. Walikuhurumia ukiwa duni lakini ulipofanikiwa tu wameanza kukuzushia mabaya na kukufitini. Tena usishangae mtu akikuombea upate kazi au pesa na ukishapata awe wa kwanza kukufitini. Wengine walishukuru kupata mfanyakazi (house girl) baada ya kuteseka muda mrefu, lakini je ni wote wanajali kuwalipa mishahara yao kwa wakati? La kusikitisha wengi wanaowanyanyasa kama si waumini ni viongozi wa kanisa. 

Sababu ya tano, mtu kuona aliyoshindwa yamefanywa na wengine. Mwa 26:19-21 “Watumwa wa Isaka wakachimba katika lile bonde, wakapata kisima cha maji yanayobubujika. Wachungaji wa Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaka wakisema, Maji haya ni yetu. Ndipo akakiita jina la kile kisima Eseki, kwa sababu waligombana naye.Wakachimba kisima kingine, wakagombania na hicho tena. Akakiita jina lake Sitna.” Wachungaji wa Gerari waligombana na wachungaji wa Isaka kwa vile walikuwa na wivu. Wapo watu wengi wanashindana nawe kwa vile tu wameshindwa kufanya kama wewe. Matokeo ya watu wa aina hii ni kutafuta kuwanyang’anya, kuwaibia na kuwapokonya wenzao. Pia hawashindwi kukuzusha mabaya kwa vile tu umepata upenyo ambao wao hawana. Wanadhani wakisifia mafanikio yako, watadharauliwa na kupuuzwa. Wapo pia waliomzushia Bwana Yesu kwamba anatoa pepo kwa Belizebuli ili tu wafunike hali yao ya kutotumiwa na Mungu. Ukiwafuatilia sana watu wengi wanaowasema vibaya watumishi wa Mungu, wao wenyewe hawana majibu ya mahitaji ya watu. Kama mtumishi fulani anatumiwa na shetani, basi wewe tumiwa na Mungu! 

Sababu ya sita, mtu anapofanikiwa zaidi kuliko waliomtangulia. Mwa 30:31-34 “Akamwuliza, Nikupe nini? Yakobo akasema, Usinipe kitu; ukinifanyia neno hili, nitalisha wanyama wako tena na kuwalinda. Nitapita katika wanyama wako wote leo, na kutoa huko kila mnyama aliye na madoadoa na marakaraka, na kila mnyama mweusi katika hao kondoo, na aliye na marakaraka na madoadoa katika mbuzi; nao watakuwa mshahara wangu. Na haki yangu itanishuhudia katika siku zijazo, utakapokuja kwa habari ya mshahara wangu ulioko kwako. Kila asiye madoadoa au marakaraka katika mbuzi, au asiye mweusi katika kondoo, akionekana kwangu, itahesabiwa kuwa ameibiwa. Labani akasema, Tazama, na iwe hivi kama usemavyo.” Mwa 31:1,2 “Basi Yakobo akasikia maneno ya wana wa Labani, wakisema, Yakobo amechukua mali yote ya baba yetu; na kwa mali ya baba yetu amepata fahari hii yote. Yakobo akaona uso wa Labani, ya kuwa hakumtazama vema kama jana na juzi.” Labani alikubaliana vizuri na Yakobo kwamba mshahara wake utakuwa wa aina gani baada ya utumishi wa muda mrefu tena bila malipo. Kilichotokea wakazaliwa mifugo mingi ya marakaraka jambo lililomfanya Labani asimtazame Yakobo vizuri. Mara ngapi watu wamekubaliana malipo na mtu akabadilika njiani kwa vile tu ameona mwenzake amebana matumizi na kufanya mambo makubwa? Mara ngapi mtumishi mwenye mshahara ambao ni robo ya ule wa mkuu wake ametendewa vibaya kazini na mkuu wake kwa vile tu amevaa nguo nzuri kuliko yake? Usipolipa watu haki zao, na wewe hutalipwa haki zako. Kanuni ya Mungu ya kuvuna na kupanda inafanya kazi kwa mema na mabaya. Ukipenda, utapendwa; ukidhulumu, utadhulumiwa. 

........ Somo litaendelea

Dr. Lawi Mshana, +255712924234, Tanzania