
Mkristo wa kweli anapaswa kutambua tofauti ya misamiati ifuatayo: Kumpokea Yesu (kuokolewa na Yesu), kumpokea Roho Mtakatifu, kuongozwa na Roho Mtakatifu na kuvikwa uwezo utokao juu (Roho Mtakatifu kuwa juu yake kiutumishi) nk
KUMPOKEA YESU MOYONI
Kumpokea Yesu ni tofauti na kupokea au kujazwa Roho Mtakatifu. Yesu ana kazi yake na Roho Mtakatifu ana kazi yake ndani ya mwamini. Yesu mwenyewe aliweka bayana. Yohana 15:26 “Lakini ajapo huyo Msaidizi, nitakayewapelekea kutoka kwa Baba, huyo Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia.” Unaweza kuwa mwamini au muumini na uwe hujapokea Roho Mtakatifu. Mdo 19:2,6 “akawauliza, Je! Mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini? Wakamjibu, La, hata kusikia kwamba kuna Roho Mtakatifu hatukusikia. Na Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao; wakaanza kunena kwa lugha, na kutabiri.” Tunampokea Bwana Yesu kwa kutambua na kukubali kwamba tumemtenda Mungu dhambi na hatuwezi kushinda peke yetu bila msaada wa damu ya Yesu. Mtu anaweza kutupa mwongozo wa namna ya kutubu ili tupokee msamaha wa dhambi. Unapookoka jina lako linasajiliwa katika kitabu cha uzima mbinguni. Ukimuacha Yesu jina lako linafutwa. Usidanganywe kwamba ukiokoka umeokoka (huwezi kufutwa jina lako) hata kama unafanya madudu (ONCE SAVED, ALWAYS SAVED). Ufu 3:5 “Yeye ashindaye atavikwa hivyo mavazi meupe, wala sitalifuta kamwe jina lake katika kitabu cha uzima, nami nitalikiri jina lake mbele za Baba yangu, na mbele ya malaika zake.”
KUMPOKEA ROHO MTAKATIFU
Mtu anaweza kuokoka na awe hajampokea Roho Mtakatifu. Mtu hawezi kumpokea Roho Mtakatifu ‘kimyakimya’ lazima kutakuwa na ishara fulani zitakazotokea. Kuzaliwa rasmi kwa Kanisa (birthday) kulitokea siku ya Pentekoste ambapo Roho Mtakatifu alishuka na udhihirisho. Mdo 2:1-4 "Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja. Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka.“
Sio lazima udhirisho uwe wa kunena kwa lugha peke yake lakini lazima jambo jipya litokee katika maisha yako. Hata maandiko yanathibitisha hili. Mdo 2:17 “Itakuwa siku za mwisho, asema Mungu, nitawamwagia watu wote Roho yangu, na wana wenu na binti zenu watatabiri; na vijana wenu wataona maono; na wazee wenu wataota ndoto.” Hata hivyo mtume Paulo anahimiza watu wapende huduma ya kutabiri (kutoa maneno yanayoeleweka yanayotoka kwa Mungu) na WASIZUIE KUNENA KWA LUGHA. 1 Wakorintho 14:39 “Kwa ajili ya hayo, ndugu, takeni sana kuhutubu, wala msizuie kunena kwa lugha.” Kuna watu wanachanganya kati ya KUNENA KWA LUGHA na karama ya AINA ZA LUGHA. Kunena kwa lugha ni kuongea na Mungu (hakuna haja ya jirani mnayeomba naye kusikia maana huongei naye). Aina za lugha ni karama ambayo mtu anatoa ujumbe kwa lugha ambayo inabidi karama nyingine ya TAFSIRI ZA LUGHA isaidie ili watu waelewe. Kama hakuna wa kufasiri anyamaze maana kanisa halijengwi. 1 Kor 14:28 “Lakini asipokuwapo mwenye kufasiri na anyamaze katika kanisa; aseme na nafsi yake tena na Mungu.” 1 Wakorintho 12:10 “na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha.”
Angalizo: Hata kama unaona mtu ananena kwa lugha halafu ana tabia zake mbaya, hiyo haikufanyi upuuze utendaji wa Roho Mtakatifu. Unaweza kujikuta umemkufuru Roho Mtakatifu kwa tabia yako ya kubeza kunena kwa lugha. Neno linasema, MSIZUIE KUNENA KWA LUGHA. Mtume Paulo alitamani kila mtu ajaliwe kunena kwa lugha. 1 Wakorintho 14:5 “Nami nataka ninyi nyote mnene kwa lugha, lakini zaidi sana mpate kuhutubu, maana yeye ahutubuye ni mkuu kuliko yeye anenaye kwa lugha, isipokuwa afasiri, ili kusudi kanisa lipate kujengwa.” Ila Mtume Paulo anasema anatamani watu watabiri zaidi ili Kanisa lijengwe kwa vile anenaye kwa lugha anajijenga mwenyewe. 1 Wakorintho 14:4 “Yeye anenaye kwa lugha hujijenga nafsi yake; bali ahutubuye hulijenga kanisa.” Neno Kuhutubu hapa sio kuhubiri au kutoa hotuba ni KUTABIRI (kutoa unabii). Paulo mwenyewe anasema ananena kwa lugha kuliko wote katika kanisa la Korintho. Hivyo kama unamkubali mtume Paulo, kubali pia kwamba alitoa kipaumbele kikubwa katika kunena kwa lugha (hata kama bado hujajaliwa). Paulo hakupuuza kunena kwa lugha bali alitaka watu wajengane kiroho pia. 1 Wakorintho 14:18,19 “Namshukuru Mungu ya kuwa nanena kwa lugha zaidi ya ninyi nyote; lakini katika kanisa napenda kunena maneno matano kwa akili zangu, nipate kuwafundisha wengine, zaidi ya kunena maneno kumi elfu kwa lugha.”
KUONGOZWA NA ROHO MTAKATIFU
Lakini mtu anaweza kumpokea Roho Mtakatifu lakini haongozwi na Roho Mtakatifu. Ameridhika na kunena kwa lugha lakini haendi hatua nyingine. Mtu anapookolewa anakuwa mtoto (baby). Yohana 1:12 “Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake.” Halafu mtu akiongozwa na Roho anakuwa mwana (son or daughter). Warumi 8:14 “Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu.” Kuongozwa na Roho maana yake ni KUTAWALIWA NA ROHO MTAKATIFU. Unamsikiliza Roho Mtakatifu katika kila unalotaka kufanya. Unaweza kukatazwa, kuruhusiwa au kuambiwa usubiri. Mtume Paulo aliwahi kukatazwa kuhubiri na akatii hadi pale aliporuhusiwa. Mdo 16:6-10 “Wakapita katika nchi ya Frigia na Galatia, wakikatazwa na Roho Mtakatifu, wasilihubiri lile neno katika Asia. Walipofika kukabili Misia wakajaribu kuenda Bithinia, lakini Roho wa Yesu hakuwapa ruhusa, wakapita Misia wakatelemkia Troa. Paulo akatokewa na maono usiku; alimwona mtu wa Makedonia amesimama, akimsihi, na kumwambia, Vuka, uje Makedonia utusaidie. Basi alipokwisha kuyaona yale maono, mara tukataka kutoka kwenda Makedonia, kwa kuwa tuliona hakika ya kwamba Mungu ametuita tuwahubiri Habari Njema.”
ROHO MTAKATIFU KUWA JUU YAKO
Isa 61:1 “Roho ya Bwana MUNGU i juu yangu; kwa sababu Bwana amenitia mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao.”
Nikukumbushe tu kwamba siku ya Pentekoste, Roho Mtakatifu aliposhuka alijaza mpaka chumba walipokuwepo. Nyumba tunazokaa zinahitaji pia kujazwa Roho Mtakatifu ili mapepo yasitawale na kutufanya tuote ndoto mbaya. Kwa vile maandalizi yalifanyika kwa siku 10, ilikuwa siku maalum kwa Kanisa na kulikuwa na uhitaji wa watu wa lugha zingine kupata ujumbe, neema ilikuwa kubwa kiasi cha kuwezeshwa kuongea lugha za watu hao bila kuzijua. Mungu anafanya kila jambo kwa sababu za msingi. Hata Bwana Yesu hakutembea juu ya maji ili kujionyesha bali ilibidi afanye hivyo kwa vile alikuwa mbali wakati wanafunzi wake wanahangaika baharini. Wahubiri waliojaribu kuonyesha watu kwamba wanaweza kutembea juu ya maji kama Yesu walizama.
Roho Mtakatifu akiwa JUU yako ni zaidi ya kumpokea au kujazwa Roho Mtakatifu. Hapa huduma yako inapewa uwezo wa KUFUNGUA WALIOFUNGWA na KUWAWEKA MATEKA WAWE HURU. Kama mtumishi hajafikia hatua hii huduma yake haitaweza kutatua changamoto za watu anaowaombea. Bwana Yesu alienda nyikani akiwa amejaa Roho (Lk 4:1) lakini alipomaliza majaribu kwa ushindi akarudi akiwa na NGUVU ZA ROHO NA USHAWISHI MKUBWA. Lk 4:14,15 “Yesu akarudi kwa nguvu za Roho, akenda Galilaya; habari zake zikaenea katika nchi zote za kandokando. Naye alikuwa akifundisha katika masinagogi yao, akitukuzwa na watu wote.” Bila Roho Mtakatifu kuwa juu yako utalalamikia na kulaumu watu na hata serikali kwa vile hujui kalenda ya Mungu na huna mamlaka dhidi ya shetani.
USHUHUDA
Wakati tunaokoka miaka ya 80 watu hawakuridhika kuabudu bila kujazwa Roho Mtakatifu. Hivyo kulikuwa na vipindi vya mara kwa mara vya maombezi ya ujazo wa Roho Mtakatifu. Sasa hivi tunajali tu idadi ya washirika/washarika ambao hawajui kuomba wala hawajui karama yoyote waliyopewa na Mungu. Matokeo yake hawana msukumo wowote wa kumtumikia Mungu. Biblia imesema kila mtu (sio kila mchungaji) ana angalau karama moja kwa ajili ya kumtumikia Mungu. Sijui tangu umjue Bwana unafahamu karama gani umepewa kwa ajili yetu! 1 Petro 4:10 “kila mmoja kwa kadiri alivyoipokea karama, itumieni kwa kuhudumiana; kama mawakili wema wa neema mbalimbali za Mungu.” Hata kama ulishajazwa Roho Mtakatifu bado unahitaji kujazwa tena kwa vile hata gari linaishiwa mafuta na kuhitaji kujazwa tena.
Maombi ya wiki hii:
1. Ee Mungu naomba uniwezeshe kutambua
umuhimu wa Roho Mtakatifu katika maisha yangu na kuwa na ushirika naye.
2. Ee Mungu naomba unihuishe tena kwa
kunijaza Roho na kunisaidia nisimzimishe Roho katika maisha yangu. 1
Wathesalonike 5:19 “Msimzimishe Roho.”
Lawi Mshana