Ticker

6/recent/ticker-posts

Kwanini baadhi ya watu walio karibu na watumishi wenye upako wana maisha duni?

KWA NINI BAADHI YA WATU WALIO KARIBU NA WATUMISHI WENYE UPAKO WANA MAISHA DUNI 

Kuna watu makanisani wamebaki kuwa mashabiki tu wa huduma zinazofanyika lakini wao wenyewe wana maisha duni. Wageni wamekuwa wakipokea majibu yao kwa wepesi zaidi kuliko wenyeji. Tutaangalia 2 Fal 4:1-7 kuona kwanini tunashindwa kuwatumia watumishi wenye neema za kipekee katika kupokea majibu dhahiri. 

1. Kujali huduma za kiroho na kupuuzia huduma za kifamilia na kimaisha 

Mst 1 “Basi, mwanamke mmoja miongoni mwa wake za wana wa manabii alimlilia Elisha, akasema, Mtumishi wako mume wangu amekufa; nawe unajua ya kuwa mtumishi wako alikuwa mcha Bwana; na aliyemwia amekuja ili ajitwalie wana wangu wawili kuwa watumwa.” Huyu mtumishi wa Elisha alikuwa MCHA BWANA lakini alitawaliwa na MADENI. Hakujali ataiachaje familia yake siku akitwaliwa na Bwana. Alichojali ni kumcha Bwana na kumtumikia Elisha. Hata leo wapo watumishi wanaopata baraka mbalimbali katika huduma lakini wanadhani wataendelea kuzipata siku zote hivyo hawaweki akiba yoyote wala kufanya maandalizi yoyote ya maisha yao ya baadaye. Wanachokazana kufanya ni kununua tu vyombo vikubwa vya Injili (huduma) na kusahau kwamba familia zao pia ni KAZI YA MUNGU. Matokeo yake mtumishi anajikuta akitumika peke yake kwa vile familia imemsusia. Watumishi wengine wanasahau kwamba Mungu alianzisha familia kabla ya kanisa. Kanisa au walioitwa (ekklesia) ni watu walioitwa na Mungu baada ya kumuasi. Huwezi kumuita mtu aliye karibu. Kabla Adamu na Eva hawajakosea Mungu alikuwa akiwatembelea wakati wa jua kupunga na kuwa na ushirika nao wa karibu sana. Mtu anaweza kuwa muumini safi ibadani wakati amemuacha Mungu siku nyingi. 1 Timotheo 5:8 “Lakini mtu ye yote asiyewatunza walio wake, yaani, wale wa nyumbani mwake hasa, ameikana Imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini.” Kimsingi mtu asiyetimiza mahitaji ya familia yake ameacha wokovu (kama alikuwa ameokoka) tena ni mbaya kuliko mpagani. 

2. Kuzoea matatizo kiasi cha kuyaona ya kawaida na kutoyashirikisha 

Mst 1 “Basi, mwanamke mmoja miongoni mwa wake za wana wa manabii alimlilia Elisha, akasema, Mtumishi wako mume wangu amekufa; nawe unajua ya kuwa mtumishi wako alikuwa mcha Bwana; na aliyemwia amekuja ili ajitwalie wana wangu wawili kuwa watumwa.” Inaonyesha huyu mtumishi wa Elisha alikuwa hajawahi kumshirikisha nabii kuhusu changamoto za familia yake. Alichagua mambo ambayo anaweza kumshirikisha nabii kwa kudhani sio yote yanaweza kutatuliwa na nabii. Matokeo yake hadi kufikia kifo chake akawa amekopa mpaka deni likawa halilipiki. Inaonyesha aliyemkopesha alikuwa anaweka kumbukumbu vizuri. Alipotoa mchanganuo wa mahesabu ya deni ikadhihirika kwamba deni ni kubwa kiasi ambacho mama mjane hawezi kulilipa zaidi ya kuwatoa watoto wake wawili wawe watumwa. Kuna watumishi wanazungumzia tu jinsi Mungu anavyowatumia kuponya watu lakini hawataki kushirikisha kuhusu ugumu wanaopitia ili waombewe na kusaidiwa. Wengine ndoa zimevunjika, chakula nyumbani hakuna hata kama ni msimu wa mavuno, kodi ya pango wameshindwa kulipa, wanakopa mijari ya mafuta dukani, kujenga nyumba imekuwa ni ndoto nk lakini wanaona aibu kushirikisha kanisa ili waombewe na kushauriwa. Wanadhani hawastahili kuombewa bali wanatakiwa kuombea tu wengine. Mtume Paulo alikuwa na huduma kubwa lakini bado alihitaji kuombewa na kanisa. Rum 15:30 “Ndugu zangu, nawasihi kwa Bwana wetu Yesu Kristo, na kwa upendo wa Roho, jitahidini pamoja nami katika maombi yenu kwa ajili yangu mbele za Mungu.” 1 Wathesalonike 5:25 “Ndugu, tuombeeni.” 

3. Kukimbilia duniani badala ya kushirikisha watumishi wa Mungu 

Mst 1 “Basi, mwanamke mmoja miongoni mwa wake za wana wa manabii alimlilia Elisha, akasema, Mtumishi wako mume wangu amekufa; nawe unajua ya kuwa mtumishi wako alikuwa mcha Bwana; na aliyemwia amekuja ili ajitwalie wana wangu wawili kuwa watumwa.” Inawezekana wengi katika wake za wana wa manabii walizoea kupambana na matatizo yao wenyewe bila kumwendea nabii wa Bwana. Wengi wanadhani masuala ya kifedha hayawezi kutatuliwa na Mungu hivyo wanaenda tu kutafuta ufumbuzi kwa majirani, marafiki na kwenye taasisi za fedha. Mjane huyu hakupenda kumuwekea mipaka Mungu bali alienda kumlilia bosi wa mume wake. Tusisahau kwamba kuna watu hata kama watapewa pesa nyingi bado watatawaliwa na madeni. Tatizo lao sio la kimwili bali ni la kiroho. Ipo roho ya madeni ambayo haiwezi kumruhusu mtu awe na uhuru wa kiuchumi (financial freedom). Lakini Mungu anaweza kututoa kwenye utumwa wa madeni yasiyolipika tukidhamiria na kumuomba kwa bidii. Hakuna deni kubwa zaidi ya dhambi zetu ambazo zilimgharimu Bwana Yesu uhai wake. Hata hivyo Bwana Yesu alilipia deni lote la dhambi zetu kwa utimilifu. 

4. Kuona mahitaji yako tu na kutoona uwezo wako 

Mst 2 “Elisha akamwambia, Nikufanyie nini? Niambie; una kitu gani nyumbani? Akasema, Mimi mjakazi wako sina kitu nyumbani, ila chupa ya mafuta.” Watu wengi wanaohitaji kusaidiwa hawaoni uwezo wao wala raslimali walizo nazo. Kanuni ya Mungu ni kumuongezea aliye na kitu. Mathayo 13:12 “Kwa maana ye yote mwenye kitu atapewa, naye atazidishiwa tele; lakini ye yote asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang'anywa.” Kabla ya kuhitaji msaada lazima uangalie kwanza una uwezo gani. Vinginevyo unaweza kukopa kwa riba wakati una kitu cha thamani ambacho ungekiuza tu maana hukitumii sana kwa sasa. Muujiza wako unategemea ulicho nacho na sio usicho nacho. Ndiyo maana ingawa wanaokopesha wanajua una mahitaji, bado wanaulizia dhamana. Kama huna dhamana maana yake hukopesheki. Elisha alijua kanuni ya muujiza wa Mungu ilivyo ndiyo maana alimuuliza, una kitu gani nyumbani. Mwanamke alianza kwa kusema sina kitu lakini akataja chupa ya mafuta ambayo alidhani haiwezi kusaidia kitu. Kumbe tayari alikuwa na kitu cha kusababisha muujiza. Kabla ya kuomba msaada jieleze vizuri una uwezo gani ili hata ikibidi upewe ngwe ya shamba ukalime. Sio vizuri kila wakati usaidiwe bure wakati ungeweza kupunguza gharama kidogo hata kwa kulimia nyumba yake, kufyeka (kupunguza) maua, kufundisha mwanae Hisabati, kusimamia ujenzi wa nyumba yake nk. Hukosi kitu cha kuchangia kwa ujuzi wako, nguvu zako au muda wako. 

5. Kutoimarisha mahusiano na watu wengine 

Mst 3 “Akasema, Nenda, ukatake vyombo huko nje kwa jirani zako wote, vyombo vitupu; wala usitake vichache.” Mara nyingi Mungu hafanyi kila kitu peke yake bali anawatumia watu katika utendaji wake. Kwa hiyo unaweza kukwama maisha kama unajali tu kuwa mwombaji mzuri wakati unadharau watu unaokutana nao. Kama ulivyo msalaba unahitaji uhusiano na Mungu (wima/vertical) na uhusiano na watu (mlalo/horizontal). Kuna watu wakiona wanajuana na mtu maarufu wanajisikia sana na kudharau watu wengine. Wanasahau kwamba maisha yanabadilika. Wengine hawajali kuwapokea wateja wao hata kama hawajui wanafanya kazi gani. Wanasahau kuna siku watastaafu au kuna siku wataenda ofisi zingine kuhitaji msaada na kuwakuta waliowapuuza ndio mabosi huko. Wewe ni bosi kwako lakini kwenye ofisi nyingine wewe ni mteja. Unaweza kushangaa siku moja unaenda kuomba kazi mahali ambapo bosi wake ni yule kijana aliyekuwa chini yako ukamnyanyasa sana. Elisha akamwambia kaombe vyombo vingi vitupu kwa majirani zako. Unadhani kama huyu mwanamke angekuwa hana mahusiano mazuri na wenzake ingekuwaje? Watu wote unaokutana nao katika maisha yako wanaweza kuwa raslimali wakati fulani hivyo usiwapuuze. Huwezi kuona thamani ya wakili mpaka utakapokuwa na kesi au hitaji fulani la kisheria. Pokea vizuri watu na kuwaheshimu kwa vile hujui watakusaidieje kesho au watakuwa na nafasi gani kesho. 

6. Kutofuata vizuri au kupuuzia maelekezo 

Mst 4,5 "Kisha uingie ndani, ukajifungie mlango wewe na wanao, ukavimiminie mafuta vyombo vile vyote; navyo vilivyojaa ukavitenge. Basi akamwacha, akajifungia mlango yeye na wanawe; hao wakamletea vile vyombo, na yeye akamimina."  Huyu mjane alipewa maelekezo na akayafuata bila maswali. Ni rahisi kupuuzia ushauri unaopewa na kujikuta ukiumia au ukikosa baraka zako. Unadhani tukio kama hili angelifanya hadharani ingekuwaje? Angekatishwa tamaa na kujikuta akiingia mashaka. Yapo mambo ambayo yanahitaji wewe peke yako, mengine wewe na mwenzi wako na mengine wewe na familia yako. Kuna watu wanapotembelea watumishi wa Mungu, wanapewa maelekezo fulani lakini wanaporudi nyumbani wanayaacha na kutafuta mahali pengine pa kwenda kuombewa. Unapochanganya maelekezo ya watumishi unahatarisha maisha yako. Hakuna tofauti na kwenda kwa madaktari tofauti kwa ugonjwa huohuo mmoja na kuamua kunywa dawa ulizoagizwa na madaktari tofauti kwa wakati mmoja. Fanyia kazi maelekezo unayopewa mpaka ufikie mwisho. Usipende mafanikio kwa njia za mkato. Hutapata uponyaji au baraka za kudumu kwa kufanya hivyo. Matokeo yake utakuwa unazunguka tu na kuanza moja kila wakati. 

7. Kutojiandaa kwa ajili ya baraka kubwa 

Mst 6 “Ikawa, vilipokwisha kujaa vile vyombo, akamwambia mwanawe, Niletee tena chombo. Akamwambia, Hakuna tena chombo. Mafuta yakakoma.” Mungu anaangalia uwezo wako kabla ya kukupa kitu fulani. Ndiyo maana katika mfano wa talanta watu wote hawakupewa kiasi kinacholingana. Mathayo 25:15 “Akampa mmoja talanta tano, na mmoja talanta mbili, na mmoja talanta moja; kila mtu kwa kadiri ya uwezo wake; akasafiri.” Mungu hana upendeleo hivyo atakupa kulingana na uwezo wako. Ndivyo ilivyo hata leo. Hata kama unatamani kupata kazi yenye mshahara mkubwa hutapeleka maombi ya kazi kama unajijua huna sifa. Mfano unaona tangazo la kazi ya udaktari (medical doctor) hutaiomba tu kwa vile una shida ya pesa. Unajua wazi kwamba huna taaluma hiyo. Mungu alijaza vyombo vitupu vilivyokuwepo. Vilipoisha muujiza ukakoma. Ukitaka Mungu akutendee mambo makubwa usifunge na kuomba peke yake bali chukua hatua ya kujiongeza katika uwezo wako. Soma zaidi, wekeza zaidi, pata maono zaidi, pata marafiki sahihi nk ili uwe na sifa za kupata zaidi. Isaya 54:2 “Panua mahali pa hema yako, na wayatandaze mapazia ya maskani yako; usiwakataze; ongeza urefu wa kamba zako; vikaze vigingi vya hema yako.” 

8. Kutokuomba ushauri wa jinsi ya kutumia pesa au baraka unazopata 

Mst 7a “Ndipo akaja akamwambia yule mtu wa Mungu.” Watu wengi wanapenda kushirikisha tu mahitaji ya kuombewa lakini wanapojibiwa hawakumbuki kushirikisha majibu. Wanasubiri wapate tatizo jingine ndipo wawatafute tena watumishi wa Mungu. Hata Mungu anaweza kukuchoka kama siku zote unamuendea kwa maombi tu. Unatakiwa wakati mwingine umuendee Mungu kwa SHUKRANI na KUMSIFU. Biblia inaonya kuhusu kushirikisha mahitaji au matatizo tu na kusahau kushirikisha baraka. Wagalatia 6:6,7 “Mwanafunzi na amshirikishe mkufunzi wake katika mema yote. Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna.” Mshirika anapaswa kushirikisha baraka anazopata kwa wazazi wake wa kiroho na sio matatizo peke yake. Ndiyo maana sio busara kutembelea nyumba ya mchungaji wako siku zote bila baraka yoyote. Sio lazima ununue vitu vya thamani na sio lazima ufanye hivyo kila siku unapoenda. Huyu mjane alikuwa na busara sana. Aliuliza afanyeje baada ya mafuta kupatikana. Mwingine angejiamulia mwenyewe kufanya anayotaka na kujuta baadaye. Kuna watu wanahitaji ushauri makini kuhusu nini wafanye baada ya kupata pesa kubwa vinginevyo watalizwa na wajanja au kujifunza kwa makosa yao wenyewe. Kama tunahitaji ushauri wa kisheria kwa mawakili, tunahitaji pia ushauri wa kitaalamu (consultancy) katika maeneo mengine ya maisha. 

9. Kutojituma katika kazi 

Mst 7b “Naye akasema, Enenda ukayauze mafuta haya, uilipe deni yako.” Baraka hii ilimlazimu huyu mjane kwenda sokoni kuuza mafuta. Haikuwa rahisi kubeba hizo ndoo au madebe yote na kukaa sokoni hadi mafuta yote yanunuliwe. Kuna watu wanaishi maisha magumu kwa vile tu wanapenda urembo na utanashati. Wanataka maisha mazuri bila kufanya kazi. Kuna watu wanaishi maisha magumu kwa vile tu wanachagua kazi. Utakuta mtu anasema, MIMI SIWEZI KUFANYA KAZI KWAKO HALAFU UNILIPE! AFADHALI NIBAKI NA TAI YANGU SHINGONI. Watu wa aina hii wanakufa masikini wakiwa na tai zao shingoni. Hakuna sababu ya kuona aibu kufanya kazi yoyote ikiwa huna pesa ili mradi iwe ni ya halali. Kuendelea kulelewa na ndugu na kutumia pesa yote unayopata kwenye mitandao ya kijamii wakati una nguvu za kufanya kazi, kuna siku utajuta wakati umri wako ukiwa umesogea sana. 

10. Kubadili matumizi kiholela 

Mst 7bc “Naye akasema, Enenda ukayauze mafuta haya, uilipe deni yako; nayo yaliyosalia uyatumie wewe na watoto wako.” Huyu mjane alielekezwa kwamba kipaumbele cha matumizi ya pesa itakayopatikana kwa kuuza mafuta ni kulipa deni. Kiasi kitakachobaki ndicho atumie kwa ajili yake na watoto wake. Kuna watu wanalia machozi ili wapate pesa ya kulipa deni lakini wakishapata wanasahau na kununua vitu vingine. Tabia hii inaleta laana kubwa katika maisha. Ndiyo maana kuna watu wanazunguka tu kwenye kazi, biashara na mikopo lakini hawaendi popote kwa vile wanadaiwa na hawataki kulipa pale wanapokuwa na uwezo. Wanakuwa kwenye mzunguko usio na mwisho wa umasikini (vicious cyle). Unakuta mtu amewapa watu kazi na wakaifanya vizuri lakini anagoma kuwalipa posho zao. Usifikiri utakuwa salama hata kama una pesa nyingi. Utakutana na hasara nyingi katika maisha hata kama una pesa na mwisho utakwenda motoni hata kama unaficha tabia yako kwa kufanya kazi za kidini. Yak 5:1-4 “Haya basi, enyi matajiri! Lieni, mkapige yowe kwa sababu ya mashaka yenu yanayowajia. Mali zenu zimeoza, na mavazi yenu yameliwa na nondo. Dhahabu yenu na fedha yenu zimeingia kutu, na kutu yake itawashuhudia, nayo itakula miili yenu kama moto. Mmejiwekea akiba katika siku za mwisho. Angalieni, ujira wa wakulima waliovuna mashamba yenu, ninyi mliouzuia kwa hila, unapiga kelele, na vilio vyao waliovuna vimeingia masikioni mwa Bwana wa majeshi.” 

MAOMBI YANGU KWA AJILI YAKO 

Leo najisikia msukumo wa kukuombea wewe unayedhalilika na kudhalilishwa kwa ajili ya madeni. Unatumikishwa na watu kwa sababu tu ya madeni. Umeuzwa na kupoteza uhuru wako. Unalazimika kufanya mambo usiyoyataka. Mwamini Yesu na kumuishia ili uwe na miaka ya uheri na kuuona wema wa Mungu siku zote. Nakutangazia kwamba Mungu amekuona na anakutoa sasa katika makucha ya watu waliokushikilia. Roho za madeni, hasara, kudhulumiwa na kushindwa zikuachie sasa katika Jina la Yesu Kristo aliyeshinda kifo na mauti! 

Dr Lawi Mshana, +255712924234; Korogwe, Tanga, Tanzania