Ticker

6/recent/ticker-posts

Kwanini baadhi ya "walokole" wakikopeshwa hawarejeshi?

KWA NINI “WALOKOLE” WAKIKOPESHWA HAWAREJESHI? 

Somo hili limetokana na maoni ya hadharani na ya kibinafsi ya wasomaji wangu wa makala iliyopita ya KWA NINI BAADHI YA WATU WANALEMEWA NA MADENI YASIYOLIPIKA.

Mmoja aliandika hivi: “Kwa upande wa ulipaji madeni walokole wengi sio waaminifu kabisa kwanza ni waongo sana Mungu atusaidie nyakati hizi za mwisho kila kitu ni feki.”

Na mwingine aliniandikia hivi: “Changamoto nyingine ambayo nimekutana nayo ni wakristo wanapokopa wanakuwa si waaminifu tofauti na watu wa mataifa wanakuwa na hofu na vitu vya watu. Changamoto nyingine baadhi ya wachungaji siyo waaminifu pia na kumdai zaidi unashindwa, sasa nikimkatalia wakati mwingine ni vibaya?”

Maswali haya yanadhihirisha wazi kuna shida katika maeneo yafuatayo:

1. Kuna watu wanategemewa waonyeshe njia na badala yake wanawazuia na kuwaumiza wengine. Luka 11:52 “Ole wenu, enyi wana-sheria, kwa kuwa mmeuondoa ufunguo wa maarifa; wenyewe hamkuingia, na wale waliokuwa wakiingia mmewazuia.

2. Baadhi ya waumini wanaumiza waumini wenzao na hawana ushuhuda mwema. Wamesahau kwamba tunatakiwa tusiwe kwazo bali tuwe barua au mfano wa kuigwa. 2 Kor 6:3 “Tusiwe kwazo la namna yo yote katika jambo lo lote, ili utumishi wetu usilaumiwe.” 2 Kor 3:3 “mnadhihirishwa kwamba mmekuwa barua ya Kristo tuliyoikatibu, iliyoandikwa si kwa wino, bali kwa Roho wa Mungu aliye hai; si katika vibao vya mawe, ila katika vibao ambavyo ni mioyo ya nyama.”

3. Baadhi ya watumishi sio mawakili waaminifu. Wakili ni mtu anayetunza mali ya mwingine. Ukishindwa kutunza mali ya mwingine, hutaweza kutunza ya kwako mwenyewe. 1 Kor 4:1,2 “Mtu na atuhesabu hivi, kuwa tu watumishi wa Kristo, na mawakili wa siri za Mungu. Hapo tena inayohitajiwa katika mawakili, ndiyo mtu aonekane kuwa mwaminifu.”

HISTORIA YA NENO WALOKOLE

Kwanza inasemekana asili ya neno walokole ni Uganda. Katika miaka ya 1940 hadi 60 waumini wenye msimamo mkali kwa wakati huo walikuwa wanajiita abalokole wakimaanisha waliookoka au ongoka. Na walikuwa na salamu zao wakikutana wanasalimiana kwa kugonganisha vifua na kuruka juu baada ya kugonganisha hivyo vifua.Wanawake walikuwa wanavaa magauni marefu sana hadi chini na walikuwa wanafunika vichwa vyao kwa vilemba vyeupe. Kitu cha pekee kwa jamii hiyo ni kuwa walikuwa hawapendi kufanya kazi wala kujishughulika na kutafuta mali wakiamini kuwa hayo ni mambo ya ulimwengu. Hali hiyo ilipelekea wengi kuwa maskini sana kiasi cha kuwa wahitaji wakubwa.Muda mwingi waliutumia kupeana shuhuda mbali mbali na walipenda kutumia neno kutendereza wakati wakikutana kwenye kitu kinaitwa faragha. Hivyo jamii hiyo ilikua kwa kasi sana hata watu wengine wa Afrika ya Mashariki hasa Tanzania waliojitangaza kuokoka wakaitwa "walokole" na jamii ya wasioamini. Lakini ikumbukwe kuwa jamii hiyo ya wasioamini iliwaita hivyo kama kwa namna fulani ya kuwadharau na kuwakebehi. Hivyo basi kila aliyeokoka miaka ya 50 hadi 80 aliitwa "mlokole" kwa kebehi ya wale wasioamini. Waliwaita hivyo wakiwafananisha na jamii hiyo ya Uganda ambao walipata sana nguvu baada ya mauaji ya "mashahidi wa uganda". Neno hilo hapo mwanzo halikupendwa kabisa na waamini wa Tanzania ila kadri miaka ilivyokwenda ndivyo jamii ya waliookoka walipoanza kulikubali na kulioana la kawaida hasa pale watu walipokuwa wakikebehi kuwa "walokole" huwa wanalia kanisani. Hali hiyo ikawa kama ni kumwagia petrol kwenye moto kwani waliookoka walilipokea kwa nguvu sana na kuanza kulitumia kama utambulisho wao kwa jamii nyingine ya wakristo.Utakuta mtu anasema "kwa hiyo wewe ni mlokole...ndio mimi ni mlokole bwana...!".

Pamoja na kwamba jina hili halina historia nzuri, kwa kiasi kikubwa limeshakubalika katika jamii na lina maana tofauti na ile ya asili. Kwa hiyo mimi nimelitumia jina hilo kama jina ambalo jamii inawaita waumini wanaokiri wokovu.

KWA NINI WALOKOLE WAKIKOPESHWA HAWAREJESHI?

Sababu nitakazokupa si lazima mtu awe nazo zote. Hivyo usije ukawahukumu walokole wote. Zingine unaweza hata wewe uliyewakopesha zikakuhusu kwa vile Neno la Mungu ni upanga unaokata kotekote (kuwili). Ebr 4:12 “Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.”  Kwa miaka zaidi ya 20 katika kumtumikia Mungu nimegundua mambo kadhaa ambayo ni visababishi:

1. Kuwa muumini feki.

Wakati Mungu anaingiza watu katika ufalme wake, shetani naye anaingiza wa kwake. Leo hii tuna watumishi wa kweli na wa uongo. Hawa watumishi wa uongo wanafanana sana na watumishi wa kweli kiasi kwamba tunaonywa kwamba hiyo kazi ya kuwachambua na kuwaainisha Mungu ataifanya mwenyewe. Mt 13:24-30 “Akawatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika konde lake; lakini watu walipolala, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake. Baadaye majani ya ngano yalipomea na kuzaa, yakaonekana na magugu. Watumwa wa mwenye nyumba wakaenda wakamwambia, Bwana, hukupanda mbegu njema katika konde lako? Limepata wapi basi magugu? Akawaambia, Adui ndiye aliyetenda hivi. Watumwa wakamwambia, Basi, wataka twende tukayakusanye? Akasema, La; msije mkakusanya magugu, na kuzing'oa ngano pamoja nayo. Viacheni vyote vikue hata wakati wa mavuno; na wakati wa mavuno nitawaambia wavunao, Yakusanyeni kwanza magugu, myafunge matita matita mkayachome; bali ngano ikusanyeni ghalani mwangu.” Magugu yanayozungumziwa hapa ni mmea unaofanana sana na ngano kiasi kwamba ni vigumu sana kutofautisha. Hivyo wakati mwingine unawaonea wakristo wa kweli pale unapowajumuisha na mkristo feki aliyekutapeli. Kanisani ni mahali penye waovu na wema. Mt 22:10 “Watumwa wale wakatoka wakaenda njia kuu, wakakusanya wote waliowaona, waovu kwa wema; arusi ikajaa wageni.” Waovu wanaweza kubadilika wawe wema kwa sababu ya neema ya Mungu. Na wema pia wanaweza kubadilika kuwa waovu kwa vile shetani hajafa na halali usingizi. Huu ni uamuzi binafsi wa mtu ambao hautegemei kiongozi wake. Maisha ya mtu kwa kiasi kikubwa yanategemea uchaguzi anaoufanya mwenyewe. Kum 30:19 “Nazishuhudiza mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimekuwekea mbele yako uzima na mauti, baraka na laana; basi chagua uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako.” Kwa hiyo mkristo feki hashindwi kukupiga tarehe katika kukulipa deni bila aibu yoyote. Badala hata ya kuanza kupunguza deni yeye anaona ni kawaida tu na wala hahukumiwi moyoni. Anasahau kwamba mtu atakayekufa kabla ya kulipa madeni anayoweza ikiwa ni pamoja na kutolipa mahari hatakuwa salama. Kum 22:29 “yule mtu mume aliyelala naye na ampe baba yake yule kijana shekeli hamsini za fedha, kisha na awe mkewe, kwa kuwa amemtweza; hana ruhusa ya kumwacha siku zake zote.” 

2. Kutowekwa huru kwelikweli baada ya kuamini

Mtume Paulo katika kipindi chake hakuridhika na toba (kuongoza sala ya toba) tu bali alifuatilia matendo yadhihirishe toba ya kweli. Mdo 26:20 “bali kwanza niliwahubiri wale wa Dameski na Yerusalemu, na katika nchi yote ya Uyahudi, na watu wa Mataifa, kwamba watubu na kumwelekea Mungu, wakiyatenda matendo yanayopatana na kutubu kwao.” Anayejua umetubu ni wewe mwenyewe, Mungu na shetani. Sisi wengine tunataka tuone matendo yanayotafsiri toba yako ingawa hatutatilia shaka imani yako. Mtume Paulo alipoitwa alipewa maelekezo ya kazi (job description). Mdo 26:18 “uwafumbue macho yao, na kuwageuza waiache giza na kuielekea nuru, waziache na nguvu za Shetani na kumwelekea Mungu; kisha wapate msamaha wa dhambi zao, na urithi miongoni mwao waliotakaswa kwa imani iliyo kwangu mimi.” Watu wengi wakishaongozwa sala ya toba hawaombewi zaidi. Matokeo yake wanaendelea na tabia za mapepo walizokuja nazo. Tangu nianze kuombea mtu mmojammoja katika ibada na semina ninazofanya nimekutana na vioja vingi. Mapepo yamelipuka kwa waumini wanaoaminika pamoja na watumishi wakiwemo mama wachungaji. Na mara nyingi mapepo haya kwa watu tofauti yamewahi kusema - tumekamata uchumi wake, tunazuia maendeleo yake, hatutaki afanikiwe, hatafanikiwa nk. Shetani anajua mtu akiwa masikini atampata kwa wepesi zaidi maana atashawishika kirahisi, atampa kazi isiyostahili afanye, atamtumikisha nk. Najua wapo wasioamini kufunguliwa baada ya kuamini. Lakini ukifika katika ibada zao utakuta watu waliochoka kimaisha, waliolemewa na madeni, wanaoanguka dhambini kila kukicha, wasiomtolea Mungu, wanaoteswa na tamaa, wanaobakwa kwenye ndoto, wenye magonjwa yasiyosikia dawa nk. Mdo 8:18-20 “Hata Simoni alipoona ya kuwa watu wanapewa Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mikono ya mitume, akataka kuwapa fedha akisema, Nipeni na mimi uwezo huu, ili kila mtu nitakayemweka mikono yangu, apokee Roho Mtakatifu. Lakini Petro akamwambia, Fedha yako na ipotelee mbali pamoja nawe, kwa kuwa umedhania ya kuwa karama ya Mungu yapatikana kwa mali.” Simoni alikuwa mchawi kisha akaamini. Ingawa alikuwa ameokoka rohoni, katika nafsi alikuwa bado hajafunguliwa ndiyo maana akataka kununua karama za Mungu ili arudishe ule umaarufu wake wa uchawi. Tunaokoka roho, nafsi inaendelea kuokoka na mwili hautakaa uokoke. Tutapewa mwili mpya. Matatizo ya wengi hayako kwenye “roho” bali yako kwenye “nafsi” (kuhisi, kufikiri na kuamua) na mwili. Ndiyo maana Neno la Mungu linasema kuna watu wameharibiwa akili zao. 1 Tim 6:5 “na majadiliano ya watu walioharibika akili zao, walioikosa kweli, huku wakidhani ya kuwa utauwa ni njia ya kupata faida.” 2 Tim 3:8 “Na kama vile Yane na Yambre walivyopingana na Musa, vivyo hivyo na hawa wanapingana na ile kweli; ni watu walioharibika akili zao, wamekataliwa kwa mambo ya imani.”

3. Kukosa kipato cha uhakika.

Mtu anapokuwa hana shughuli ya uhakika ya kumuingizia kipato anaweza kuishi maisha ya kubahatisha. Kuna watu hawafanyi kazi moja mpaka kufikia hatua ya kuielewe vizuri na changamoto zake. Hata ukimuuliza kuhusu kazi yake hasa anakuambia hajaamua bado kwamba atafanya shughuli gani katika maisha yake. Pamoja na kufanya kazi mbalimbali lazima mtu awe na kazi ya msingi na awekeze katika kazi hiyo. Utashangaa mtu ni fundi mzuri kwa miaka 20 lakini mpaka leo hana ofisi wala vitendea kazi (zana) muhimu. Ukimkopesha mtu wa aina hii hataweza kulipa maana anasubiri muujiza utokee. Hajui atapata nini wakati gani. Sio kazi zote zinahitaji raslimali fedha kama wengi wanavyotumia muda mwingi kutafuta wafadhili. Zingine zinahitaji zaidi muda, zingine nguvu, zingine kipaji, zingine elimu, zingine kuishi vizuri na watu nk. Mhu 9:10 “Lo lote mkono wako utakalolipata kulifanya, ulifanye kwa nguvu zako; kwa kuwa hakuna kazi, wala shauri, wala maarifa, wala hekima, huko kuzimu uendako wewe.” Unapokuwa huna kipato cha uhakika ni vigumu kuwa na kituo. Ukikosa kituo sio rahisi umiliki mali. Matokeo yake hutakopesheka. Watakukopesha wale tu wasio na vigezo katika kukopesha. Hata wafadhili walishashtuka. Hawawezi kuridhika na andiko la mradi (project proposal) wakati hakuna kazi inayoonekana kwa macho. Lazima mtu afanye maamuzi ya kufanya kazi fulani na kuielewa kwa kina. Kuna watu walidhani hata wasipojifunza watakuwa matajiri milele na kujikuta wameshuka ghafla. Hata kama Mungu amekupa utajiri kama hutakuwa mfuatiliaji unaweza kufilisika.  Mit 27:23,24 “Fanya bidii kuijua hali ya makundi yako; Na kuwaangalia sana ng'ombe zako. Kwa maana mali haziwi za milele; Na taji je! Yadumu tangu kizazi hata kizazi?”

4. Kutangaza vita na shetani bila kupigana vita na kushinda.

Ni jambo hatari sana kutangaza vita halafu hukai kivita. Efe 6:11 “Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.” Ukiendelea kusoma andiko hili utagundua kwamba utakuwa hatarini kama kuna eneo la maisha yako hujavaa silaha. Silaha hizo ni ukweli, haki, utayari wa Injili, imani, Neno, maombi na fikra sahihi. Hizi silaha zimegawanyika katika makundi mawili. Za kujilinda (defensive) na za kushambulia (offensive). Ukitumia muda mwingi kujiombea ulinzi kuliko kumshambulia shetani unakuwa hatarini zaidi. Hivyo lazima ufanye huduma zinazomkimbiza shetani ili mara nyingi awe mbali. Mtu ambaye hapigani vita vya kiroho anatekwa mpaka uchumi wake. Kila anachojaribu kufanya kinakwama hivyo analazimika kuishi kwa mikopo. Shetani anapenda kufilisi watu ili wamsujudie kirahisi. Hivyo yuko tayari awafunge wateja, akutie hasara na kukudhulumu ili uwe ombaomba na hatimaye akuingize katika himaya yake. Anaweza kukuacha utumike vizuri sana madhabahuni lakini anajua amekamata njia zako zote za uchumi kiasi kwamba unaweza kumkufuru Mungu. Hata kama mtu ni muumini kama hana muda wa kutosha na Mungu shetani anaweza kuvuruga mipango yake ya kiuchumi. Lakini pia kama mtu anaharibu kazi za shetani asisahau kufunika familia na mali zake kwa damu ya Yesu kwa vile shetani ana tabia ya kulipiza kisasi. Akiona umemshinda upande mmoja, anahamia upande mwingine.  

5. Kukopa kwa ajili matumizi badala ya uzalishaji

Kuna watu ambao kila wanapohitaji mkopo ni kwa ajili ya matumizi.  Wanautumia wote wakati hawana uhakika wa kipato kwa ajili ya marejesho. Mtu anapokopa ili alipe ada au apate nauli au afanye sherehe na wakati hana kipato lazima akwame. Afadhali anayetumia sehemu ya mkopo kufanyia mradi ili asiendelee kuwa tegemezi wa mikopo. Watu wengi wa aina hii wana muda mwingi ambao hawana cha kufanya nyumbani. Hawangeshindwa kutumia sehemu ya mkopo huo kununua kuku wawili wa kufuga. Mtu makini anachakarika na kupanga majukumu kwa wasaidizi wake. Ni kosa kubwa kulala ukiwa hujui kazi zako ni zipi kwa siku inayofuata. Mit 31:15 “Tena huamka, kabla haujaisha usiku; Huwapa watu wa nyumbani mwake chakula; Na wajakazi wake sehemu zao.” Kazi sio laana. Mungu alimuweka Adamu kwenye bustani ya Edeni ili aitunze kabla hajatenda dhambi. Mwa 2:15 “Bwana Mungu akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza.” Ikiwa mtu anashindwa kurejesha hata nusu ya mkopo ambao hauna riba, unadhani huyu mtu kabla hajakopa alikuwa na mpango wowote wa jinsi atakavyorejesha? Huu sio wakati wa kuendelea kukopa pesa za chakula. Kopa mtaji wa kuzalisha kitu cha kukuondoa kuwa tegemezi. Watu wanaogopa kupokea simu zako maana ni za shida tu! Wakati mwingine na wewe wape zawadi hata ya mayai, machungwa au maharage. Unapovuna unakuwa kimya, mavuno yakiisha unaanza kupiga simu za kuomba msaada. Unaowaomba pesa nao wanahitaji maharage uliyovuna!

6. Kukopa watu wengi kwa wakati mmoja

Kuna mtu wakati anakuja kukukopa tayari anadaiwa na watu watano hivi. Na usishangae ingawa anakuambia hana chakula nyumbani, anataka pesa yote utakayomkopesha akalipe deni kwa mtu mmojawapo anayemdai. Unapoona haiwezekani kuishi bila kukopa watu wengi, maisha yamekushinda mahali hapo au katika kazi unazozifanya. Badilisha mazingira au kazi lakini usikimbie na madeni ya watu. Tuache tabia ya kung’ang’ania kazi tulizozoea tangu tuzaliwe! Tuwe wabunifu na tuwe na utayari wa kujifunza hata kazi mpya kabisa. Tujifunze kazi zenye fursa mbele yetu. Mara kadhaa nimekutana na fursa za ajira wakazikosa watu ambao hawako tayari kujiendeleza ingawa ni waombaji wazuri na wacha Mungu. Mwa 26:3 “Kaa ugenini katika nchi hiyo, nami nitakuwa pamoja nawe, na kukubariki, maana nitakupa wewe na uzao wako nchi hizi zote. Nami nitakifanya imara kiapo nilichomwapia Ibrahimu baba yako.” Mara nyingi ukikaa kama mwenyeji huwezi kuziona fursa. Ndiyo maana Mungu aliwabariki watu kadhaa kwa kuwapeleka ugenini. Ni vigumu mtu mwenye mikopo mingi kulipa pesa alizokopa kwa wakati. Jifunze kuomba kazi badala ya kuomba mkopo. Tatizo tunaendekeza urembo na utanashati kwenye maisha ya kiuchumi. Mara nyingi watu tunaoenda kuwakopa wana kazi ambazo tungeweza kuzifanya hata kama ni za hali ya chini.

7. Kuaminika bila mashahidi wala maandishi

Mtu anapokuja kukopa kama “mpendwa” mara nyingi sio rahisi kuandikishana unapomkopesha. Tabia hii inaondoa uwajibikaji. Matokeo yake kama amekopa wengi, ataanza kuwalipa wale wanaomkoromea (wale ambao ni mbogo) wanaotishia kumfunga au kumuaibisha. Na sio kwamba anafanya hili kwa makusudi. Uwezo wake mdogo wa kulipa wote kwa wakati mmoja, unamfanya aanze na ule upande unaohatarisha usalama wake. 2 Kor 13:1b “Kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatu kila neno litathibitishwa.” Watu wengi hawajui kwamba kuna madhara makubwa unapopoteza uaminifu kwa vile hujui anayekudai anasema nini kwa watu. Unaweza kupoteza fursa nyingi. Mtume Paulo aliamua kutumika na Timotheo baada ya kupata ushuhuda (sifa nzuri) kwa watu wa Listra na Ikonio. Hakuna mtu makini anayeweza kukupa kazi kubwa bila kuulizia historia yako ya nyuma. Mdo 16:1,2 “Basi akafika Derbe na Listra, na hapo palikuwa na mwanafunzi mmoja jina lake Timotheo, mwana wa mwanamke Myahudi aliyeamini; lakini babaye alikuwa Myunani. Mtu huyo alishuhudiwa vema na ndugu waliokaa Listra na Ikonio.” Lazima tutunze uaminifu badala ya kuwakwepa wanaotudai. Ukishindwa kurejesha nenda hata na kitu chako cha thamani ukamuachie anayekudai ili aone unajali.

8. Kuelewa vibaya kanuni za Mungu kuhusu utajiri.

Kuna watu wanafunga na kuomba ili Mungu awape utajiri. Wanadhani pesa zitashuka kutoka mbinguni kama mvua. Hawajui kwamba kuna kanuni za kupata utajiri wa ki-Mungu. Maombi yanakupa mwongozo au dira. Kimsingi Mungu hatoi utajiri bali anatupa NGUVU ZA KUPATA UTAJIRI. Na hatupi utajiri ili tujifurahishe tu bali tutimize kusudi lake. Kum 8:18 “Bali utamkumbuka Bwana, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo.” Utashangaa mtu anafunga na kuomba ili aokote pesa. Maana yake anataka wenzake waliofanya kazi waangushe pesa njiani ili yeye aokote. Mara nyingi nimemuomba pia Mungu anibariki lakini siombi pesa bali naomba KAZI zenye pesa kwa vile najua Mungu anabariki kazi za mikono. Lakini pia ni muhimu kujua kazi yenye baraka zako. Nilijaliwa kumjua Mungu nikiwa kidato cha pili. Na wakati huo nikajua kwamba Mungu atanibariki bila kufanya kazi za kuajiriwa. Kum 28:8 “Bwana ataiamuru baraka ije juu yako katika ghala zako, na mambo yote utakayotia mkono wako; naye atakubarikia katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako.” Hivi unajua kazi au nchi aliyokupa Mungu wako? Kazi nzuri ni ile ambayo umekalishwa na Bwana kuliko kujikalisha mwenyewe. Yer 7:3,7 “Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Tengenezeni njia zenu, na matendo yenu, nami nitawakalisha ninyi mahali hapa.  ndipo nitakapowakalisha mahali hapa, katika nchi hii niliyowapa baba zenu, tokea zamani hata milele.” Wengine wanadhani kuwa tajiri ni dhambi. Wanasahau kwamba fedha na dhahabu ni mali ya Bwana na sio ya shetani. Hagai 2:8 “Fedha ni mali yangu, na dhahabu ni mali yangu, asema Bwana wa majeshi.”

9. Kushindwa kuwa na mahusiano yenye tija na watu wenye imani tofauti.

Kuna watu wanadhani ukiwa mtu wa imani unatakiwa ujitenge kabisa na watu wengine. 2 Kor 6:14 “Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza?” Andiko hili wakati mwingine limetumika vibaya. Kwa upande mmoja tunatahadharishwa tusipitilize katika mahusiano yetu na wasioamini kiasi cha kujikuta tumeingizwa katika maagano ya kishetani pasipo kujua. Lakini kwa upande mwingine tunaambiwa kwamba kuna namna tunaweza kuhusiana na wasioamini. Kama kuna jinsi isivyo sawasawa, basi kuna jinsi iliyo sawasawa. Yapo mahusiano ambayo hayagusi imani wala umilele wako hivyo unaweza kushirikiana nao. Ndiyo maana hakuna mtu wa imani anabagua mteja akija dukani kwake labda kama biashara yake ni ya kishetani ndipo anaweza kutopenda kupokea pesa za mtu wa Mungu. Lakini pia kuna mafanikio unaweza kupata kupitia watu wa dini tofuati na ya kwako. Mimi nimeshuhudia Muislamu akinitambua na kunisaidia kwa moyo mweupe na Mkristo akinibagua na kunikwamisha. La msingi tujue mipaka ya mahusiano yetu na kila mtu. Mtu anaweza kuwa mzuri katika kuomba naye na wakati huohuo awe hatari sana katika kufanya naye biashara. Kila mtu ana uwezo fulani na udhaifu fulani. Ukiwa na marafiki sahihi wanaweza kufanyika baraka kwako na kukufanya usitegemee mikopo peke yake. 

10. Kutokuwa na utaratibu wa kuweka akiba

Kuna watu hawajali kuweka akiba ya chakula wala pesa. Kisingizio chao katika kufungua akaunti ni kukwepa makato ya benki. Biblia inasema tujifunze kwa sisimizi wanavyojituma na kuweka akiba ili tusivamiwe na umasikini. Mit 6:6-11 “Ewe mvivu, mwendee chungu, Zitafakari njia zake ukapate hekima. Kwa maana yeye hana akida, Wala msimamizi, wala mkuu, Lakini hujiwekea akiba ya chakula wakati wa jua; Hukusanya chakula chake wakati wa mavuno. Ewe mvivu, utalala hata lini? Utaondoka lini katika usingizi wako? Bado kulala kidogo, kusinzia kidogo, Bado kukunja mikono upate usingizi! Hivyo umaskini wako huja kama mnyang'anyi, Na uhitaji wako kama mtu mwenye silaha.” Kukosa tabia ya kuweka akiba kunawafanya watu wakope kwa ajili ya chakula. Mtu mwingine anapopata pesa kubwa hawi na wazo la kununua mahindi au vyakula visivyoharibika kwa bei ya jumla. Anaendelea kununua visadolini vya unga na mijari ya mafuta kila siku wakati huohuo pesa kubwa inaishia kwenye nguo, kujipamba na sherehe. Lazima tujifunze kuweka akiba ya mahindi hata kwa mwaka mzima tunapojaliwa maana kuna mabadiliko mengi ya tabia nchi. Hapa naongea na wakulima wanaovuna mahindi na kuuza yote pamoja na watu wanaopata pesa lakini hawana vipaumbele (priorities) katika maisha. Hata kama pesa inakatwa benki kuna siku itakunusuru na tatizo kwa vile huwezi kuitumia kwa haraka kama uliyo nayo nyumbani. Kumbuka benki kuna wafanyakazi wanaohitaji mishahara kwa kukutunzia pesa zako.  Akiba yako inaweza kupunguza kutegemea kukopa watu kila unapopata dharura. 

11. Kutojali muda

Unapokuwa hujali muda wa kuanza na kumaliza huwezi kufikia malengo yako. Na kama huwezi kufikia malengo yako mwenyewe, huwezi pia kufikia malengo ya kulipa pesa za watu ulizokopa. Watu wengi wasiojali muda wanapenda kuahirisha mambo. Ni jambo la kawaida kazi iliyotakiwa kukamilika wiki hii kukamilika mwezi ujao. Efe 5:15-17 “Basi angalieni sana jinsi mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima bali kama watu wenye hekima; mkiukomboa wakati kwa maana zamani hizi ni za uovu. Kwa sababu hiyo msiwe wajinga, bali mfahamu ni nini yaliyo mapenzi ya Bwana.” Unaweza kuwa mtu wa rohoni vizuri lakini kwa upande mwingine u mjinga. Lazima tujue jinsi ya kuukomboa wakati. Tujue kazi ngapi zinatakiwa kuisha leo na sio kesho. Kanisani kwetu inajulikana kabisa kwamba kama muda wa kuanza ibada umefika na sijafika nitakuwa na dharura au niko safarini. Tukipatana saa 8 ukaja saa 8.30 unaweza usinikute. Kwangu kutojali muda ni dhambi. Kama sipendi Mungu acheleweshe maombi yangu, kwa nini mimi nimcheleweshe? Najua kanuni ya Mungu – unachopanda ndicho utakachovuna. Huwezi kupanda mahindi uvune mtama. Wag 6:7 “Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna.” Ukijali muda na majukumu yako kwa siku, utafanya kazi nyingi na baraka zitaongezeka. Kuna watu wanasema wanatumia muda wao mwingi katika maombi lakini ukifuatilia sana wanaomba maombi ambayo hayana maelekezo wala majibu yoyote. Mwingine ameamua asifanye kazi ili awe kwenye maombi, lakini ukimkuta chumbani anaangalia tamthilia, anasoma magazeti ya udaku, anasukwa masaa 3, anapiga soga nk. Tuacheni ubabaishaji hatuwezi kufanikiwa kwa mtindo huo. Lazima tubadilike ili tupokee baraka kamilifu. Kama ni muda wa kuomba omba kweli; kama ni muda wa kazi fanya kazi!

Dr. Lawi Mshana, +255712924234, Tanzania