Ticker

6/recent/ticker-posts

Sababu kuu nne zinazokufanya ukwame wakati u mwaminifu kwa Mungu

SABABU KUU NNE ZINAZOKUFANYA UKWAME WAKATI U MWAMINIFU KWA MUNGU 
Nimekutana na watu wa Mungu wenye maswali yasiyo na majibu kuhusu hali zao ngumu wakati wako vizuri kiroho na wanamtumikia Mungu kwa uaminifu kabisa. Napenda nikushirikishe sababu za kuteseka hata kama KIBINAFSI hujatenda dhambi. 

1. Uonevu wa mapepo 

Kuna watu tangu wamwamini Bwana hawajawahi kuombewa zaidi ya kuongozwa sala ya toba peke yake. Wameingia katika imani wakiwa na mapepo lakini hayajakemewa na kutolewa. Hata hivyo sio wote wanapoamini wanakuwa na mapepo lakini wapo ambao wanaendelea kutembea na mapepo huku wameshaamini. Mapepo hayatoki yenyewe bila kutolewa. Mojawapo ya dalili kwamba mtu ana mapepo ni pamoja na kushindwa kujizuia kufanya dhambi (hasira isiyotawalika, tamaa kali ya zinaa, msukumo wa kuua au kujiua nk), mateso ya kiakili (hofu, sonona, uzito moyoni, kusikia sauti akilini ambazo wengine hawazisikii, kuchanganyikiwa, nk), matatizo ya hisia (kushindwa kuwa karibu na watu wengine, kujisikia kukataliwa bila sababu za msingi nk), matatizo ya kiafya (magonjwa ambayo hayaelezeki na vipimo vya hospitali vinashindwa kuyatambua nk), uwezo wa kimizimu (kubashiri, kujihisi kunyanyuliwa hewani, kuvunja kitu kigumu kwa mkono tu, kujishangaa mfukoni kuna pesa nk), hisia zisizo za kawaida (kutamani kulala na wanyama, tamaa ya zinaa kinyume cha maumbile nk), uzoefu na mapepo (kujihisi kutembelewa na mapepo au kuyasikia, kupenda vitu vya kimapepo nk), kupata shida wakati wa maombi (kichomi cha ghafla, kuumwa kichwa ghafla, kichefuchefu ghafla, kutaka kukimbia, chuki kali nk) 

2. Laana za vizazi 

Kut 20:3-6 “Usiwe na miungu mingine ila mimi. Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, Bwana, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao, nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri zangu.” Kuna watu wanateseka kwa vile babu zao waliabudu miungu mingine. Mungu anachukizwa sana na tabia ya kuabudu miungu mingine kiasi kwamba alisema kama watu watafanya hivyo ATAWAPATILIZA WANA MAOVU YA BABA ZAO HATA KIZAZI CHA TATU NA CHA NNE. Omb 5:7,8 “Baba zetu walitenda dhambi hata hawako; Na sisi tumeyachukua maovu yao. Watumwa wanatutawala; Hakuna mtu wa kutuokoa na mikono yao.” Kumbuka hapa hazungumzii DHAMBI (SIN) bali anazungumzia UOVU (INIQUITY). Jiulize uko kizazi cha ngapi na utambue babu zako waliamini nini. Mfano Danieli alikuwa mcha Mungu tena mwenye karama za Mungu lakini bado alichukuliwa utumwani akiwa kijana. Unajua kwa nini? Alikuwa miongoni mwa watu waliobeba laana iliyotokana na babu zake kutomtii Mungu. Kum 28:36 “Bwana atakupeleka wewe, na mfalme wako utakayemweka juu yako, kwa taifa usilolijua wewe wala baba zako; nawe huko utatumikia miungu mingine ya miti na mawe.” Eze 21:3 “uiambie nchi ya Israeli, Bwana asema hivi; Tazama, mimi ni juu yako, nami nitautoa upanga wangu alani, nami nitamkatilia mbali nawe MTU MWENYE HAKI NA MTU MBAYA.” Wakati Danieli amekuwa mzee akafuatilia kitabu cha nabii Yeremia na kugundua kwamba muda wa laana umeisha lakini hatua hazijachukuliwa. Dan 9:2 “katika mwaka wa kwanza wa kumiliki kwake, mimi Danieli, kwa kuvisoma vitabu, nalifahamu hesabu ya miaka, ambayo neno la Bwana lilimjia Yeremia nabii, ya kuutimiza ukiwa wa Yerusalemu, yaani, miaka sabini.” Kimsingi Danieli alisoma Yer 25:11 “Na nchi hii yote pia itakuwa ukiwa, na kitu cha kushangaza; nayo mataifa haya watamtumikia mfalme wa Babeli miaka sabini.” Bila kufuatilia babu zetu waliambiwa nini au walifanya maagano gani kuna matatizo hayataisha kirahisi. Huwezi kujitenga na uovu wa baba zako uwe salama hapa duniani. Ni kweli uovu wao hauwezi kukuzuia kwenda mbinguni lakini unaweza kuzuia baraka zako za hapa duniani. Danieli alijihusisha na dhambi za mababu kana kwamba alikuwepo. Badala ya kusema WAMEFANYA DHAMBI, yeye alisema TUMEFANYA DHAMBI. Dan 9:5 “tumefanya dhambi, tumefanya ukaidi, tumetenda maovu, tumeasi, naam, hata kwa kuyaacha maagizo yako na hukumu zako.” Huwezi kupuuza uovu wa babu zako wa kuabudu mizimu, kufanya matambiko na uchawi hata kama wewe umeokoka. Danieli pia alikuwa mcha Mungu lakini akawa uhamishoni au mateka kwa miaka mingi ingawa huko uhamishoni alipata upendeleo fulani wa Mungu. Baraka kamili zinakuwa nchini kwako ambapo uko huru na sio uhamishoni. Utajuaje kuna laana ya vizazi kwenu? Utaona matatizo yanayojirudia au kurithiwa kv matatizo ya kiakili, magonjwa, matatizo ya uzazi (utasa nk), kuvunjika kwa mahusiano kv ndoa, umasikini au kupungukiwa kifedha, ajali, vifo vya ghafla, ukosefu wa amani nk. KUMBUKA NI PALE TU MATATIZO HAYA YANAPOJIRUDIA KWENYE VIZAZI KADHAA NDIPO INAKUWA NI LAANA. Kama ni wewe tu mwenye matatizo, hiyo sio laana ya vizazi bali kuna sababu nyingine kv dhambi uliyofanya nk. 

3. Imani potofu 

Hizi ni imani potofu zilizojengwa katika maisha kutoka kwa wazazi na walezi kiasi kwamba hatuzioni kwamba ni mbaya. Kumbuka imani ina uwezo wa kuweka mipaka ya mafanikio yako. Ndiyo maana Biblia inasema, “Maana aonavyo nafsini mwake, ndivyo alivyo.” Mit 23:7. Kwa maneno mengine WEWE UKO VILE UNAVYOFIKIRI. HUWEZI KUFANYA MAMBO ZAIDI YA FIKRA ZAKO. Hii ndiyo sababu pamoja na kuwa na maisha mazuri kiroho, Neno la Mungu linasema tugeuzwe na kufanywa upya fikra zetu. Rum 12:2 “Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.” Kuna watu wengine wako vizuri kiroho lakini fikra zao zimeharibiwa na shetani. Matokeo yake wanashindwa kufanya maamuzi sahihi ya maisha yao na kujikuta wakimsingizia shetani au kumlaumu Mungu kwa makosa yao wenyewe. Hata kama tutakemea mapepo yatoke kuna watu hawatabadilika sana kwa vile bado wana fikra za mapepo. Ndiyo sababu Biblia inasema tunatakiwa kuangusha ngome. 2 Kor 10:3-4 “Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;) tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo.” Pepo linaweza kutoka lakini mtu aendelee kuishi kama mtumwa kwa vile bado ngome ipo kwenye maisha yake. Lazima uwe tayari kujikosoa kama fikra zako ni sahihi kama Mungu anavyotaka. Unaomba vizuri Mungu akubariki lakini je ni kweli unajiona kwamba unastahili kuwa tajiri kama Mungu anavyotaka? Teka nyara fikra zako zimtii Kristo ndipo utaona mabadiliko dhahiri ya maisha yako yanayoendana na utii wako wa kiroho. 

4. Maumivu ya nafsi au rohoni 

Moja ya kazi ya Yesu hapa duniani ni kuwaponya waliovunjika moyo. Isa 61:1 “Roho ya Bwana MUNGU i juu yangu; kwa sababu Bwana amenitia mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao.” Kuna watu wana maumivu ambayo shetani anayatumia kuwatesa. Maumivu haya yanatokana na mambo waliyotendewa na watu kv kunyanyaswa kijinsia, kutelekezwa, kukataliwa nk wakiwa wadogo au ndani ya ndoa. Kutokana na kuruhusu maumivu yakutawale unafungua mlango kwa shetani. Shetani hawezi kumtesa mtu bila kupewa mlango au haki ya kisheria (legal right). Waefeso 4:26,27 “Mwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka; wala msimpe Ibilisi nafasi.” Utajuaje kwamba una kifungo cha nafsi kisicho salama? Unakuwa katika mahusiano ya kinyanyasaji lakini huko tayari kufanyia kazi, umevunja uhusiano na mtu zamani lakini unashindwa kumtoa akilini mwako, unapofanya jambo fulani au kufanya maamuzi unajihisi kama mtu fulani yuko na wewe au anakuona, unapokuwa kwenye tendo la ndoa na mwenzi wako wa maisha lazima umuwazie mtu mwingine, unajiona umechukua tabia mbaya za mtu uliyewahi kuwa na mahusiano naye ungawa hutaki hizo tabia, unatetea haki yako ya kuwa na uhusiano na mtu hata kama kwa kufanya hivyo unaleta madhara kwenye ndoa na familia yako, unapata uzoefu wa matatizo kama ya mtu uliyewahi kuwa karibu naye sana kv magonjwa, ajali, utumwa fulani nk. Tambua kwamba unaweza kuunganishwa na kahaba kwa kiwango cha kuwa mwili mmoja hata kama sio mke au mume wa ndoa. 1 Kor 6:16 “Au hamjui ya kuwa yeye aliyeungwa na kahaba ni mwili mmoja naye? Maana asema, Wale wawili watakuwa mwili mmoja.” Wewe jitetee tu kwamba uko salama kwa maandiko ambayo hujui maana yake kama hujafa masikini au kuwa mtu asiye na maana hapa duniani! 

Tujiulize maswali machache: 

1. Bwana Yesu alikufa kwa ajili ya ulimwengu wote? NDIYO. 
2. Ulimwengu mzima umemuamini na kuokoka? HAPANA 
3. Bwana Yesu alichukua magonjwa yetu yote pale msalabani? NDIYO 
4. Watu wote ni wazima ikiwa ni pamoja na watu wa Mungu? HAPANA 

Nataka ujue kwamba kuja kwa Yesu na kufa msalabani hakufanyi matatizo yaondoke yenyewe (automatic). Ni lazima tumuendee na kutumia Jina lake na damu yake kwa ajili ya kupata haki zetu na kufuta hati za mashitaka kwenye familia zetu. MUNGU AMEMTOA MWANAE YESU KAMA SADAKA YA UKOMBOZI WETU LAKINI HATUTAFAIDI CHOCHOTE KAMA HATUTAMPOKEA KAMA ZAWADI KUTOKA KWA MUNGU. Hata kama mimi nitakupa zawadi nzuri kiasi gani, haitakuwa ya kwako kama hutanyoosha mkono kuipokea. 

TAFAKARI NA KUCHUKUA HATUA ILI UWE HURU KWELIKWELI. 

Dr Lawi Mshana, +255712924234; Korogwe, Tanga, Tanzania