Je inawezekana nina kifungo kinachozuia maendeleo yangu?
Mwaka 1996 (miaka 20 iliyopita), Mungu alinipa ufunuo wa dalili 20 za vifungo vinavyowatesa baadhi ya watu wake. Nililazimika kuandika kipeperushi kinachoitwa, UNAHITAJI HUDUMA MAALUM YA KUFUNGULIWA. Sambamba na kipeperushi hicho nikawa na vipindi vya maombezi maalum kwa watu wanaoteseka kimwili, kimaisha na kijamii ingawa baadhi yao rohoni wameokolewa. Roho wa Bwana amenisukuma wakati huu kukumbusha tena kuhusu dalili hizo ili tukiona mtu mwenye dalili hizo tumsaidie au tumuunganishe na huduma zinazoweza kumsaidia. Mungu anataka tuwe huru kwelikweli na kuanza kuionja mbingu tukiwa bado duniani.
Isa 10:27 ‘Tena katika siku hiyo mzigo wake utaondoka begani mwako, na nira yake shingoni mwako, nayo nira itaharibiwa, kwa sababu ya kutiwa (kupakwa) mafuta’. Mt 11:28-30 ‘Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha...kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi’.
Yafuatayo ni baadhi ya matatizo yanayoonyesha kwamba (kama unayo) bado uko katika kifungo na utumwa wa shetani. Hivyo, unahitajika kufuatilia huduma ambazo Bwana amezitia mafuta katika kufungua vifungo:
1.Kila inapofikia kipindi cha mahubiri ya Neno la Mungu au maombi, kichwa kinauma na unalala usingizi mzito hata kama hukukesha wala kufanya kazi nzito.
2.Unapopanga maombi ya kufunga, tumbo linakuuma sana kiasi kwamba unaamua kuahirisha au kama umeanza maombi unaamua kufungua (kula chakula) kabla ya muda uliopatana na Mungu.
3.Kila unapokusudia kuwahi ibada kama wenzako, unashindwa kutokana na dharura za wageni na kazi zako za mikono nyumbani.
4.Unapotaka kuombea mahitaji fulani, unayasahau kabisa na kuamua uombee mengine na mara zote unajitetea kwamba ni Roho Mtakatifu ameingilia kati.
5.Kila unapoomba au unapoombewa unajisikia kubanwa katika kifua, kuna kitu kinacheza tumboni na kutembea kwenye viungo vya mwili wako na mwisho unapoteza fahamu.
6.Muda wako mwingi katika maombi unapotea katika kumkemea shetani kuliko kuombea hitaji lako kwa sababu ya kikohozi cha ghafla, kupiga chafya, kupiga miayu au kichefuchefu.
7.Umeshajazwa nguvu za Roho Mtakatifu lakini mapepo yanakuingia kirahisi sana na hata yanapotolewa baada ya muda yanarudi tena.
8.Kila unapopata baraka za kifedha, matatizo kama vile magonjwa na misiba yanajitokeza na kuzimaliza fedha zote.
9.Tatizo ulilo nalo umelirithi katika ukoo wenu kwa sababu ya mkataba wa kimila na kwa vile haliondoki, shetani amekupa neno la kuhalalisha tatizo hilo kwamba umepewa mwiba kama mtume Paulo na unakiri hivyo.
10.Ingawa unajitahidi kutoa mali zako katika kanisa lako, bado shetani amefunga milango yote ya mafanikio katika kazi zako, biashara yako na mashamba yako. Mshahara wako hautoshi, biashara imesimama, wanyama na wadudu wanamaliza mazao yako na madeni yanazidi kuongezeka.
11.Unajisikia amani na furaha ukiwa kanisani lakini baada ya kutoka ibada na kurudi nyumbani kwako unajisikia kama vile unaingia kaburini na lazima patokee faraka kati yako na watu wa nyumbani mwako. Siku unapoomba na kufunga ndipo tatizo hili linapoongezeka zaidi.
12.Huna utajiri wa kudumu. Hivyo, kila unachonunua hakidumu kama unavyotarajia. Chakula kinaisha mapema sana, nguo zinachanika ovyo na vyombo vinavunjika tu.
13.Kuna watu husalimiani nao na umejitahidi kwa kila njia upatane nao lakini umeshindwa kabisa kuufuta huo uadui. Hata moyoni mwako unajisikia hukumu kwamba tatizo hili litakupeleka motoni.
14.Umepoteza furaha ya kwenda nyumbani kwa Bwana (Zab 122:1) na hujisikii kuhuishwa wala kumfurahia Bwana (Zab 85:6).
15.Bwana anapokuagiza kumtumikia kwa huduma fulani, anasimama mtu mbele yako kukuzuia na kwa kumtii unashindwa kufikia kusudi la Mungu.
16.Unajiuliza kwamba utaendelea mpaka lini kuabudu, wakati hutendewi ishara au muujiza wowote wala husikii/hujui sauti ya Mungu kiasi kwamba hutofautiani na mpagani ambaye hana dini wala hajui kuabudu.
17.Kila unapozungumza unatoa maneno machafu, ya kihuni, yasiyo na maana, ambayo hayana neema kwa wanaosikia na unajisikia aibu lakini umeshindwa kuyaacha.
18.Kila jambo unalofanya au unalosema hata kama ni zuri linapuuzwa na watu, na watu wanakuchukia bila sababu hata wasiokujua ambao mnakutana kwa mara ya kwanza tu sokoni, hotelini, dukani au safarini. Mwenzako anaweza kuomba kitu chema apewe lakini wewe unyimwe.
19.Kila mara unapotaka kufanya jambo fulani, unaanza vizuri lakini katika kumaliza shetani anavuruga mipango yote. Mfano unasoma shuleni au chuoni vizuri kwa mafanikio lakini unapofikia wakati wa mtihani unaugua ghafla au matokeo yakitolewa umeshindwa kabisa.
20.Kila unapoombea watu wabarikiwe, Mungu anaitika mara moja lakini wewe mwenyewe roho ya umasikini inazidi kukufilisi kiasi kwamba umefikia hatua ya kuacha au kutojali kuombea wengine.
Tangu nimeanza huduma hii kiupya kupitia kipindi kinachoitwa UHURU KAMILI nimeona mateka wakiwekwa huru.
Ngoja nikupe mambo machache ambayo tangu mwaka jana niliyaona kwa watu wa Mungu:
1. Kuna watu hawana amani katika ndoa zao kwa vile wameolewa na mapepo mahaba kwa njia ya ndoto na wengine hawakutakiwa kuolewa kutokana na maagano ya ukoo au wachawi.
2. Kuna watu uchumi wao umekamatwa kiasi kwamba hata wanapoongezewa mtaji au mkopo bado wanapata hasara tu.
3. Kuna watu wamechukuliwa nyota (nuru) zao tangu siku ya kuzaliwa kupitia ndugu au marafiki wa karibu waliochukua kitovu na kukipeleka kwenye madhabahu za wachawi hivyo wanashindwa kuwa na hatua hata kama wana kazi nzuri au bidii ya kazi.
4. Kuna watu wameachiwa mfuko wa uganga (uchawi) na kwa vile wameukataa bila kuwa na mamlaka ya kiroho wanateswa pamoja na familia zao.
5. Kuna watu wakifanya kazi za wengine zinafanikiwa sana lakini wakijaribu za kwao wenyewe hakuna matokeo wanayopata.
6. Kuna watu wametolewa kafara na ndugu zao au mabosi wao ili watajirike hivyo wanachofanya hakifanikiwi ingawa wana kazi zao – wamefanywa misukule ya ofisi za watu bila kujua. Nk
Haya ni baadhi tu ya matatizo ambayo pengine umeyazoea.
Ndugu mpendwa, usifungwe na roho ya dini. Kutana na watumishi wa Mungu wenye funguo za milango ya upenyo wa mafanikio yako. Mungu anakuwazia mawazo ya amani na mafanikio. Usijitetee kwa kutumia maandiko wakati katika uhalisia shetani anachezea maisha yako mahali fulani. Muweke wazi shetani ili kazi zake zivunjwe katika Jina la Yesu. Unapoendelea kumtumikia Mungu na ulemavu fulani, hutakuwa na matokeo dhahiri yanayompa Mungu utukufu na kuwavuta watu katika ufalme wa Mungu.
Mk 9:20,21 “Wakamleta kwake; hata alipomwona, mara yule pepo alimtia kifafa; naye akaanguka chini, akagaa-gaa, akitokwa na povu. Akamwuliza babaye, Amepatwa na haya tangu lini? Akasema, Tangu utoto.”
Yohana 8:36 “Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli.”
Nakushauri ukiona kipengele ambacho unateseka umuombe Mungu, utafute ushauri au uombewe ili uwe huru.
Dr Lawi Mshana, +255712924234; Korogwe, Tanga, Tanzania