KWANINI BADO SHETANI ANACHEZEA MAISHA YAKO NA KUKUKWAMISHA? – Dr Lawi Mshana
Ni ukweli usiopingika kwamba yapo maandiko mengi yanayothibitisha kwamba shetani ameshindwa na hana mamlaka tena. Mfano:
1. “Mimi sitasema nanyi maneno mengi tena, kwa maana yuaja mkuu wa ulimwengu huu, wala hana kitu kwangu.” Yohana 14:30
2. “Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.” Isaya 53:5
3. “akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani; akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo.” Kol 2:14,15
Pamoja na ukweli huu bado maisha ya wengi yako kwenye utumwa wa aina mbalimbali kv magonjwa, umasikini, madeni, dhambi na uonevu wa aina nyingi. La kusikitisha zaidi, baadhi yao wamemwamini Mungu na wengine wanamtumikia kabisa.
SABABU KADHAA ZA SHETANI ALIYESHINDWA KUWEZA KUCHEZEA MAISHA YAKO NA KUKUKWAMISHA:
1. Kutomjua Mungu na njia zake
Ni vigumu sana kupokea mema au baraka za Mungu aliye hai bila kumjua kwanza. Vinginevyo utafanikiwa kwa kuteseka sana, kwa masharti mengi au kwa njia zisizo halali. Ayubu 22:21 “Mjue sana Mungu, ili uwe na amani; Ndivyo mema yatakavyokujia.” Unapokataa kumjua Mungu anaweza kukuacha ufuate akili zako na kutenda yasiyokupasa. Ndiyo maana kuna watu wamekufa dhamiri zao na kuendelea kutenda maovu huku wakijidanganya kwamba nao ni watu wa Mungu.Warumi 1:28 “Na kama walivyokataa kuwa na Mungu katika fahamu zao, Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wayafanye yasiyowapasa.” Unaweza kushiriki ibada zote na semina nyingi na bado ushindwe kufikia ujuzi wa kweli. Ni lazima umruhusu Mungu akufundishe na uwe tayari kubadilika ndipo utapata mageuzi ya kweli katika maisha yako. 2 Timotheo 3:7 “wakijifunza siku zote, ila wasiweze kabisa kuufikia ujuzi wa kweli.”
2. Kutomjua shetani na hila zake
Shetani anajua kwamba hana mamlaka kwa Yesu Kristo pamoja na wote waliompokea Bwana Yesu. Kwa hiyo anachofanya ni kutudanganya ili tumuamini na kumkabidhi mamlaka yetu kwa hiari yetu. 2 Wakorintho 2:11 “Shetani asije akapata kutushinda; kwa maana hatukosi kuzijua fikira zake.” Shetani anataka umtilie mashaka Mungu ili iwe rahisi kukunasa. Kama ulishamhakikisha Mungu kwa jambo fulani, uwe makini sana kama unaendelea kuuliza. Shetani anaweza kujichomeka na kusema na wewe. Mwanzo 3:1 “Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa mwitu aliowafanya Bwana Mungu. Akamwambia mwanamke, Ati! Hivi ndivyo alivyosema Mungu, Msile matunda ya miti yote ya bustani?”
Kwa vile shetani alishang’olewa meno na Yesu anatafuta mtu aliyelala usingizi ili ammeze kwa wepesi. Kumbuka kumeza hakuhitaji meno. 1 Petro 5:8 “Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze.” Shetani anapomuingia mtu anaingiza moyo wa aina fulani kv kuiba, kugushi, kuzini, kusaliti nk kulingana na kazi anayotaka umfanyie. Yn 13:2 “Hata wakati wa chakula cha jioni; naye Ibilisi amekwisha kumtia Yuda, mwana wa Simoni Iskariote, moyo wa kumsaliti.”
3. Kutojitambua na tahadhari za kuchukua
Lazima tujitambue kwamba tunaweza sisi wenyewe kumpa shetani mamlaka juu yetu. Waefeso 4:27 “wala msimpe Ibilisi nafasi.” Kwa hiyo pamoja na kumkemea shetani tuhakikishe tunafunga milango yote ambayo anaweza kuitumia kuingia maishani mwetu. Kuna watu wanachezewa na shetani kwa vile wanamfukuza bila kufunga milango. Hata kama utamfukuza kuku atarudi tena kama hutafunga mlango. Jichunguze kuna mlango gani maishani mwako unaomfanya shetani arudishe tatizo lako mara kwa mara.
Hata kama una Mungu aliye hai lazima uepuke mazingira hatarishi. Biblia inasema, ‘Huwezi kumkumbatia kahaba mwili wako usisisimke!’ Mithali 6:27,28 “Je! Mtu aweza kuua moto kifuani pake, Na nguo zake zisiteketezwe? Je! Mtu aweza kukanyaga makaa ya moto, Na nyayo zake zisiungue?” Ni vizuri ujue ni dhambi gani inakuzinga kwa wepes kwa vile shetani anakujaribu baada ya kukusoma kwanza kwamba udhaifu wako uko wapi. Waebrania 12:1 “Basi na sisi pia, kwa kuwa tunazungukwa na wingu kubwa la mashahidi namna hii, na tuweke kando kila mzigo mzito, na dhambi ile ituzingayo kwa upesi; na tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu.” Lakini pia tusisahau kwamba tumepewa uwezo wa ajabu na Bwana wetu Yesu. Ila usisahau kwamba waliopewa mamlaka hii ni wale waliompokea Yesu na sio waumini wa ibadani au misa peke yake (wakristo wa Jumapili). Luka 10:19 “Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru.” Usije ukajichongea kwa shetani kwa kutumia Jina la Yesu wakati huna uhusiano binafsi na Yesu Kristo. Wengi wanahatarisha maisha yao kwa kutumia Jina la Yesu anayetajwa na wahubiri maarufu wakati hawamjua Yesu Kristo kibinafsi. Ni hatari sana kumtumia Yesu wa kuazima kwa wengine. Mdo 19:13-16 “Baadhi ya Wayahudi wenye kutanga-tanga, nao ni wapunga pepo, wakajaribu kutaja jina la Bwana Yesu juu yao waliopagawa na pepo wachafu, wakisema, Nawaapisha kwa Yesu, yule anayehubiriwa na Paulo. Walikuwako wana saba wa mtu mmoja Skewa, Myahudi, kuhani mkuu, waliofanya hivyo. Yule pepo mchafu akawajibu, akawaambia, Yesu namjua na Paulo namfahamu, lakini ninyi ni nani? Na yule mtu aliyepagawa na pepo mchafu akawarukia wawili, akawaweza, akawashinda, hata wakatoka mbio katika nyumba ile hali wa uchi na kujeruhiwa.”
4. Kutomtumikia Mungu ipasavyo
Sio kila ahadi kwenye Biblia ni ya kwako hata kama unaikiri. Lazima uwe na sifa zinazofanana na za huyo ambaye alipewa ahadi hiyo. Mara nyingi tunapenda kusema kila silaha itakayofanyika juu yangu haitafanikiwa na tunashangaa bado imefanikiwa. Unajua kwanini? Hii sio haki yako kama humtumikii Mungu bali unaingia tu kanisani na kutoka bila mpango kazi wala mpango wa utekelezaji. Isaya 54:17 “Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa na kila ulimi utakaoinuka juu yako katika hukumu utauhukumu kuwa mkosa. Huu ndio urithi wa watumishi wa Bwana, na haki yao inayotoka kwangu mimi, asema Bwana.” Unapokuwa humtumikii Mungu kama alivyokusudia, unakuwa chini ya laana ya kuwatumikia watu wengine. Kum 28:47,48 “kwa kuwa hukumtumikia Bwana, Mungu wako, kwa furaha na moyo wa kushukuru, kwa ajili ya ule wingi wa vitu vyote; kwa hiyo utawatumikia adui zako atakaowaleta Bwana juu yako, kwa njaa, na kwa kiu, na kwa uchi, na kwa uhitaji wa vitu vyote; naye atakuvika kongwa la chuma shingoni mwako, hata atakapokwisha kukuangamiza.” Lakini pia kama unamtumikia Mungu kwa ulegevu hatakuacha hivihivi. Lazima ujiulize Mungu ananufaika nini na wewe kwa wiki nzima ambayo unatumia pumzi yake na kufanya kazi zako. Yeremia 48:10a “Na alaaniwe mtu afanyaye kazi ya Bwana kwa ulegevu.”
5. Kutojua kupigana vita za kiroho
Watu wengi wanadhani tunatakiwa kuingia kwenye vita za kiroho wakati wowote tu hata bila maandalizi. Tunatakiwa kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake ndipo tuingie katika mapambano. Vinginevyo, tupambane pale tu vita inapojitokeza kwa dharura. Ikiwa hivyo naamini Mungu atatupatia neema yake. Tunatakiwa tuvae silaha zote ili shetani asipate mwanya au mlango wowote. Sio salama kujali tu maombi wakati wewe sio mkweli, huna imani, huna utayari nk. Lakini pia lazima utambue unapambana na ngazi ipi ya utawala wa shetani. Je ni falme au mamlaka au wakuu wa giza au majeshi ya pepo wabaya? Waefeso 6:10-12 “Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.” Bwana Yesu anasema kama utagundua kwamba hujajipanga vizuri kama adui yako alivyojipanga afadhali usitishe hayo mapambano kwanza. Huna haja ya kwenda kwenye huduma yenye vita kali bila kujipanga kwanza. Nimekutana na watu ambao wamejeruhiwa vibaya kwa kujiingiza kwenye vita kali za kiroho bila kutambua kwanza mamlaka yao, kufanya maandalizi na kutambua nguvu ya adui wanayemkabili. Lk 14:31,32 “Au kuna mfalme gani, akitaka kwenda kupigana na mfalme mwingine, asiyeketi kwanza na kufanya shauri, kwamba yeye pamoja na watu elfu kumi ataweza kukutana na yule anayekuja juu yake na watu elfu ishirini? Na kama akiona hawezi, hutuma ujumbe kutaka sharti za amani, mtu yule akali mbali.” Kama wote tungekuwa sawa, Biblia haingesema ukizidiwa uwaite watumishi wa Mungu. Yakobo 5:14 “Mtu wa kwenu amekuwa hawezi? Na awaite wazee wa kanisa; nao wamwombee, na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana.” Hata hivyo tutambue nguvu ya damu ya Yesu katika kutupa ushindi, ulinzi na utayari wa kuhatarisha maisha yetu kwa ajili ya Bwana. Ufu 12:11 Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa.
6. Kukosa uaminifu kwa Mungu
Kuendelea kupambana na shetani wakati si mwaminifu kwa Mungu ni kuhatarisha maisha yako. Lazima tuhakikishe kwamba tunampa Mungu sehemu yake katika baraka anazotupatia. Tunapotoa zaka kwa uaminifu madirisha ya mbinguni yanafunguliwa. Funguo za hayo madirisha ni zaka na sio maombi peke yake. Shetani akikugundua kwamba u mwizi kwa Mungu wako atakuchezea bila huruma yoyote kwa vile anajua wewe ni halali yake. Malaki 3:9,10 “Ninyi mmelaaniwa kwa laana; maana mnaniibia mimi, naam, taifa hili lote. Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema Bwana wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la.” Ni kazi yetu makuhani kuwafundisha watu kutofautisha vitakatifu na vya kutumiwa siku zote. Eze 22:26 “Makuhani wake wameihalifu sheria yangu, wametia unajisi vitu vyangu vitakatifu; hawakuweka tofauti ya vitu vitakatifu na vitu vya kutumiwa sikuzote; wala hawakuwafundisha watu kupambanua vitu vichafu na vitu vilivyo safi, nao wamefumba macho yao, wasiziangalie sabato zangu, nami nimetiwa unajisi kati yao.” Usipende kukaa na sehemu ya Mungu kwenye nyumba yako, kazi yako au biashara yako. Utakaribisha laana katika nyumba yako, kazi yako na biashara yako. Ukikosa uaminifu kwa Mungu, utapigwa na kukimbizwa na adui zako. Unaweza kuwalaumu wanaokukimbiza lakini inawezekana ni Mungu ameruhusu ukimbizwe na kufanywa mtu asiye na kikao duniani. Kila unachoshika kinakuponyoka. Kum 28:25 “Bwana atakufanya upigwe mbele ya adui zako; utawatokea juu yao kwa njia moja, lakini utakimbia mbele yao kwa njia saba; nawe utatupwa huko na huko katika falme zote za duniani.” Unajikuta unatawaliwa na maadui zako na kukimbia bila kufukuzwa na mtu. Law 26:17 “Nami nitauelekeza uso wangu kinyume chenu, nanyi mtapigwa mbele ya adui zenu; hao wawachukiao watatawala juu yenu; nanyi mtakimbia wakati ambao hapana awafukuzaye.”
7. Kutohudumiwa na watumishi sahihi
Bwana Yesu hakufundisha na kuhubiri Neno peke yake bali pia aliponya wanaoteseka. Alifanya hivyo kwa vile Mungu alimtia mafuta kwa kazi hiyo. Sio wote wametiwa mafuta kwa ajili ya kuwaweka watu huru. Mdo 10:38 “habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye.” Hata hivyo unatakiwa kuwa makini sana usije ukaangukia kwa watumishi feki ambao utawatambua kwa matunda yao. USIANGALIA MIUJIZA PEKE YAKE BALI ANGALIA PIA MWENENDO WAO. Ebr 13:7 “Wakumbukeni wale waliokuwa wakiwaongoza, waliowaambia neno la Mungu; tena, kwa kuuchunguza sana mwisho wa mwenendo wao, iigeni imani yao.” Ukiona nabii au mtumishi anatumiwa kwa miujiza lakini hana ushuhuda mwema huyo hakutumwa na Mungu. Ishara hizo zitakuwa zinatoka kwa yule mwovu. Kum 13:1-3 “Kukizuka katikati yako nabii, au mwotaji wa ndoto, akikutolea ishara au ajabu, ikatukia hiyo ishara au hiyo ajabu aliyokuambia akisema, Na tuifuate miungu mingine usiyoijua, tuitumikie hiyo; wewe usiyasikize maneno ya nabii yule, au yule mwotaji wa ndoto, kwa kuwa Bwana, Mungu wenu, yuawajaribu, apate kujua kwamba mwampenda Bwana, Mungu wenu, kwa mioyo yenu yote na roho zenu zote.” Wengi wanapotea leo kwa vile wanaangalia MATOKEO tu na kusahau CHANZO. Biblia inasema katika nyakati za mwisho hata wateule watadanganyika kwa vile shetani atafanya maajabu makubwa ya udanganyifu. Marko 13:22 “kwa maana wataondoka Makristo wa uongo, na manabii wa uongo, watatoa ishara na maajabu, wapate kuwadanganya, kama yamkini, hata hao wateule.”
Nakuombea Mungu akupe macho na masikio ya kiroho ili uweze kupambanua na kuepuka mitego ya Ibilisi na kuishi maisha ya ushindi tele katika Kristo Bwana.
Uwe na siku njema!
Dr Lawi Mshana, Korogwe, Tanga, Tanzania
Unauthorized use and/or duplication of this material without express and written permission from this site’s author and owner is strictly prohibited.
Excerpts and links may be used, provided that full and clear credits is given to Lawi Mshana and www.lawimshana.com with appropriate and specific direction to the original content.