Ticker

6/recent/ticker-posts

Maswali kuhusu jinsi ilivyo vigumu kuokoka duniani

Kwanini inakuwa vigumu kufanya maamuzi ya kuokoka hapa duniani? – Dr Lawi Mshana 

Ndugu mpendwa, Mungu anatupenda sana na ni mvumilivu sana kwetu. Katika watu wanaopendwa sana na Mungu wewe ni mmojawapo. Sio wote katika mtandao wamepata fursa ya kuuona ujumbe huu. Kumbuka mwisho wa msaada wa dhehebu lako ni katika kukuzika kaburini na baada ya kaburi ndipo maisha halisi yanaanza. Utakuwa wapi? Yafuatayo ni maswali 19 na majibu yake rahisi ambayo inawezekana hata wewe unayo kuhusu wokovu. Hakuna mtu aliyeamua kuokoka leo ambaye hakuwa na mojawapo ya maswali haya. Kwa hiyo wewe sio wa kwanza.

1. Ni wajibu wa Mungu kujifunua (kujiweka wazi) mwenyewe kwangu kwa hiyo sina haja ya kufanya chochote

Yer 29:13 anasema “Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote.”.

Mungu anasema ni wajibu wa mwanadamu kumtafuta kwa moyo wake wote. Sio busara kuhamishia wajibu huu kwa Mungu. Mungu ameahidi kwamba atajifunua kwetu pale tutakapomtafuta kwa dhati.

2. Nadhani Mungu ni mwema sana kiasi ambacho hawezi kumpeleka mtu yeyote motoni.

Eze 18:23 anasema “Je! Mimi ninafurahia kufa kwake mtu mwovu? Asema Bwana MUNGU; si afadhali kwamba aghairi, na kuiacha njia yake, akaishi?”.

Mungu anaonyesha wema wake kwa kusema hafurahii kifo cha mtu mwovu. Angependelea mtu mwovu aache njia zake mbaya. Mungu ni mwema. Hapendi kumuadhibu mwenye dhambi. Usiyeamini utahukumiwa kwa vile umekataa njia ya Mungu ya wokovu.

3. Ni vigumu kumwamini Mungu nisiyemuona.

2 Kor 5:7 “Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya” Ebr 11:6 “Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.

Kama ingekuwa tunatumia macho kumwamini Mungu, ingekuwa kazi ngumu. Lakini Mungu ametupa njia tofauti katika kumwamini. Tunaenda kwa imani na sio kwa kuona. Siwezi kuuona ubongo wako lakini hii haina maana kwamba huna ubongo. Siwezi kuuona umeme lakini tunajua upo kwa sababu ya matokeo yake. Kwa nini tunamwamini Mungu?

¨ Uumbaji unaonyesha kuna muumbaji

¨ Mungu anatenda miujiza hata leo.

¨ Mungu anabadili maisha ya watu

4. Ngoja nifurahie maisha sasa. Nitaokoka baadaye.

Lk 12:16-21 “Akawaambia mithali, akisema, Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana; akaanza kuwaza moyoni mwake, akisema, Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu. Akasema, Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu. Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi. Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani? Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu.

Usiyeamini unasahau kwamba maisha ya ushirika na Mungu yanaleta raha ya milele. Raha ya sasa bila Mungu ni ya muda tu. Mfano tuliousoma unawaonya wanaochagua kuishi kwa anasa za dunia hii. Biblia inasema, ‘itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake?’ (Mk 8:36). Lakini pia kuna raha ya aina yake unayoipata ukiwa ndani ya Yesu. Zaburi 34:8 “Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema; Heri mtu yule anayemtumaini.” 

5. Nitampokea Yesu kabla sijafa kwa vile bado ninao muda.

Mit 29:1” Aonywaye mara nyingi akishupaza shingo, Atavunjika ghafula, wala hapati dawa.” na Isa 55:6 “Mtafuteni Bwana, maadamu anapatikana, Mwiteni, maadamu yu karibu”.

Nabii Isaya aliwaonya watu wamtafute Bwana wakati bado anapatikana. Bwana anazidi kutuonya katika Zaburi kwamba tusiifanye migumu mioyo yetu tunaposikia Neno la Mungu. Huwezi kujua utakufa lini. Kifo hakichagua mkubwa wala mdogo. Wewe mwenyewe ni shuhuda kwamba tumekuwa tukishiriki mazishi ya wakubwa kwa wadogo mara nyingi.

6. Kuna wakati nilijaribu kuokoka nikashindwa.

Mit 3:5-6 “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako. Usiwe mwenye hekima machoni pako; Mche Bwana, ukajiepushe na uovu.” na Efe 2:8-9 “Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu.”.

Tatizo lako ni ‘kujaribu kuokoka’. Hatuwezi kujaribu kuwa wakristo kama ambavyo hatuwezi kujaribu kuwa watoto wa baba aliyetuzaa. Mtoto anazaliwa katika familia bila juhudi zake mwenyewe. Unapaswa kuacha kujitahidi kwa nguvu zako na uanze kumtumaini Mungu akuokoe kwa damu ya Yesu. Hilo pekee linaweza kukubadilisha uwe mkristo uliyeokoka na sio mkristo jina. 

7. Mimi ni mdogo sana kuhitajika kumpokea Kristo sasa.

2 Kor 6:2 “(Kwa maana asema, Wakati uliokubalika nalikusikia, Siku ya wokovu nalikusaidia;tazama,wakati uliokubalika ndiyo sasa; tazama siku ya wokovu ni sasa)”; Mhu 12:1 “Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, Kabla hazijaja siku zilizo mbaya, Wala haijakaribia miaka utakaposema, Mimi sina furaha katika hiyo.

Maandiko yanawaambia wote wanaodai kwamba bado ni vijana kwamba wamkumbuke muumba wao siku za ujana wao. Maandiko yanasema kwamba ukimgeukia Bwana utampata. Huu ndio muda muafaka kwa watu wa kila rika kuokoka.

8. Naogopa sitaweza kusimama katika wokovu.

Rum 14:4 “Wewe u nani unayemhukumu mtumishi wa mwingine? Kwa bwana wake mwenyewe yeye husimama au huanguka. Naam, atasimamishwa, kwa kuwa Bwana aweza kumsimamisha.”; 1 The 5:24 “Yeye ni mwaminifu ambaye awaita, naye atafanya.” na 2 Kor 12:9 “Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu.”.

Udhaifu usiwe kikwazo kwa vile la msingi ni kumuendea Kristo! Mungu ndiye anayetusimamisha. Mungu ni mwaminifu kwetu na nguvu zake zinatuimarisha katika udhaifu wetu. Ujumbe wa Injili ni kwamba Mungu anatushika kwa vile hatuwezi kujishikiza kwake.

9. Watu watanicheka. Marafiki zangu ni wa muhimu sana kwangu.

2 Tim 2:12 “Kama tukistahimili, tutamiliki pamoja naye; Kama tukimkana yeye, yeye naye atatukana sisi”; Yak 4:4 “Enyi wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa Mungu? Basi kila atakaye kuwa rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui wa Mungu.” na Mit 1:26 “Mimi nami nitacheka siku ya msiba wenu, Nitadhihaki hofu yenu ifikapo;”.

Kama kicheko cha watu kinakuumiza wewe usiyeamini, maumivu yatakuwa makubwa kiasi gani siku utakapochekwa na Mungu wakati ukipata uharibifu wa kujitakia? Lazima usiyeamini ufanye uamuzi kama rafiki zako wanastahili kuchukua nafasi ya Mungu au la. Nani katika rafiki zako unampenda kiasi kwamba ungestahimili  kifo cha msalaba  kwa ajili yake? Lazima usiyeokoka uwe jasiri kumchagua Mungu. Mtu yeyote akimkataa Mungu, Mungu naye atamkataa.

10. Nadhani nimetenda dhambi isiyosameheka.

Isa 55:7 “Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie Bwana, Naye atamrehemu; Na arejee kwa Mungu wetu, Naye atamsamehe kabisa.” na 1 Kor 6:9-11 “Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa Mungu? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang'anyi. Na baadhi yenu mlikuwa watu wa namna hii; lakini mlioshwa, lakini mlitakaswa, lakini mlihesabiwa haki katika jina la Bwana Yesu Kristo, na katika Roho wa Mungu wetu.”.

Unapaswa kujua rehema kuu ya Mungu. Orodha katika 1 Kor 6 ni ya dhambi nyingi. Mungu aliwasamehe wakorintho waliokuwa wamezitenda. Waliziacha dhambi zao na kumrudia Bwana. Mungu anaahidi kusamehe wanaotubu na kumgeukia.

11. Kuna wanafiki wengi makanisani. Mtu fulani aliyedai ameokoka aliniumiza sana.

Isa 45:22 “Niangalieni mimi, mkaokolewe, enyi ncha zote za dunia; maana mimi ni Mungu; hapana mwingine.”; Rum 14:12-13 “Basi ni hivyo, kila mtu miongoni mwetu atatoa habari zake mwenyewe mbele za Mungu. Basi tusizidi kuhukumiana, bali afadhali toeni hukumu hii, mtu asitie kitu cha kumkwaza ndugu au cha kumwangusha.” na Mt 7:21-23 “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.”.

Kuna watu wengi wanaokwenda kanisani ambao ni wanafiki. Hata hivyo, wengi katika hawa sio wakristo wa kweli. Wote wanaodai wameokoka wakati sivyo, wanaliaibisha Jina la Bwana. Mungu atawahukumu kwa vitendo vyao, lakini mienendo yao haikupi tiketi ya kuikataa Injili. Usiyeokoka hutahukumiwa kwa vitendo vya wengine. Utatoa hesabu ya maisha yako binafsi mbele za Mungu. Mungu anatuagiza tumtazame Yeye na sio maisha ya watu wengine. Kama tungekuwa tunaangalia wanaofeli mitihani, hatungeendelea na masomo!

12. Nitatakiwa kumpokea Kristo hadharani?

Rum 10:9-10 “Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu.”, 1 Yn 4:15 “Kila akiriye ya kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu, Mungu hukaa ndani yake, naye ndani ya Mungu.” na Mt 10:32-33 “Basi, kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye mbinguni. Bali mtu ye yote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni.”. 

Jibu ni ndiyo. Wokovu unahusisha kuamini moyoni mwako na kukiri kwa kinywa chako. Ukiri huo lazima ufanyike mbele za watu wengine. Kama imani sio imara kiasi cha kukuwezesha kuisema hadharani, haitoshi kuwa imara unapokuwa peke yako. Hata ndoa hazifungwi kimyakimya. Hivi utamuelewaje mtu aliyeoa ambaye anashindwa kusema hadharani huyu ni mke wangu?

13. Mimi sio mwenye dhambi.

Isa 64:6-7 “Kwa maana sisi sote tumekuwa kama mtu aliye mchafu, na matendo yetu yote ya haki yamekuwa kama nguo iliyotiwa unajisi; sisi sote twanyauka kama jani, na maovu yetu yatuondoa, kama upepo uondoavyo. Tena hapana aliitiaye jina lako, ajitahidiye akushike; kwa kuwa umetuficha uso wako, nawe umetukomesha kwa njia ya maovu yetu.” Rum 3:10-12 “kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Hakuna mwenye haki hata mmoja. Hakuna afahamuye; Hakuna amtafutaye Mungu. Wote wamepotoka, wameoza wote pia; Hakuna mtenda mema, la! Hata mmoja.

 

Unaweza kuonekana msafi kwa watu lakini sio kwa Mungu. Mungu anajua njia zako, mawazo yako yote na mambo yako yote unayotenda sirini hata ukiwa peke yako. Ikiwa Mungu aliona hatuwezi peke yetu akamtuma Mwanae Pekee kwa ajili yetu unadhani utapona katika hukumu ya Mungu. Unapokataa wokovu wake maana yake unamwambia Mungu umekosea kumtuma Mwanao pekee. Kwa hiyo kumkataa Yesu kama sadaka ya Mungu kwako ni dhambi inayotosha kukupeleka motoni.  Waebrania 2:3 “sisi je! Tutapataje kupona, tusipojali wokovu mkuu namna hii? Ambao kwanza ulinenwa na Bwana, kisha ukathibitika kwetu na wale waliosikia”. 

14. Sijali hata kama nitakwenda motoni. Marafiki zangu wengi watakuwa huko pamoja nami.

Lk 16:19-26 “Akasema, Palikuwa na mtu mmoja, tajiri, aliyevaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi, na kula sikuzote kwa anasa. Na maskini mmoja, jina lake Lazaro, huwekwa mlangoni pake, ana vidonda vingi, naye alikuwa akitamani kushibishwa kwa makombo yaliyoanguka katika meza ya yule tajiri; hata mbwa wakaja wakamramba vidonda vyake. Ikawa yule maskini alikufa, akachukuliwa na malaika mpaka kifuani kwa Ibrahimu. Yule tajiri naye akafa, akazikwa. Basi, kule kuzimu aliyainua macho yake, alipokuwa katika mateso, akamwona Ibrahimu kwa mbali, na Lazaro kifuani mwake. Akalia, akasema, Ee baba Ibrahimu, nihurumie, umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake majini, auburudishe ulimi wangu; kwa sababu ninateswa katika moto huu. Ibrahimu akasema, Mwanangu, kumbuka ya kwamba wewe uliyapokea mambo mema yako katika maisha yako, na Lazaro vivyo alipata mabaya; na sasa yeye yupo hapa anafarijiwa, na wewe unaumizwa. Na zaidi ya hayo, kati yetu sisi na ninyi kumewekwa shimo kubwa, ili wale watakao kutoka huku kwenda kwenu wasiweze; wala watu wa kwenu wasivuke kuja kwetu.”  na Zab 112:10 “Asiye haki ataona na kusikitika, Atasaga meno yake na kuyeyuka, Tamaa ya wasio haki itapotea.”.

Usiyeamini anadhani utakuwa na ushirika na marafiki zako motoni. Kinyume chake, utakuwa na ushirika na moto na kiberiti. Hakuna ushirika unaoweza kuwepo wakati watu wanaungua moto. Hebu jaribu kuongea na rafiki yako wakati unamsogezea njiti ya kiberiti inayowaka moto uone kama mazungumzo yataendelea.

15. Namtafuta Yesu lakini simpati.

Yer 29:13 “Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote.” 1 Yn 3:22 “na lo lote tuombalo, twalipokea kwake, kwa kuwa twazishika amri zake, na kuyatenda yapendezayo machoni pake.”.

Usiyeamini anashindwa kumpata Yesu kwa vile humtafuti kwa moyo wote. Kwa sehemu unamtafuta Mungu na kwa sehemu unatafuta kujipendeza mwenyewe. Ili kupokea wokovu, ni lazima kumgeukia Mungu kwa moyo wako wote. Lakini pia wapo wafuasi wake ambao wanaweza kukutambulisha kwake.

16. Siwezi kumuelewa Mungu wala Biblia.

Rum 11:33 “Jinsi zilivyo kuu utajiri na hekima na maarifa ya Mungu! Hukumu zake hazichunguziki, wala njia zake hazitafutikani!”, Zab 25:14 “Siri ya Bwana iko kwao wamchao, Naye atawajulisha agano lake.” na 1 Kor 2:14 “Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni.

Ni kweli kwamba kuna maeneo ambayo hatuwezi kuyaelewa vizuri kuhusu Mungu. Hata hivyo, kila mtu anaweza kuelewa Injili ya Kristo na kuokoka. Usiyeamini ukimcha Mungu (ukiwa na hofu ya Mungu), unaweza kuuelewa mpango wa Mungu wa wokovu. Ukishaokoka, unaweza kuanza kuwa na ufahamu wa rohoni kuhusu maeneo mengine yaliyokuwa magumu kuyaelewa. Vinginevyo masuala ya wokovu yatakuwa upuzi kwako kwa vile hujapenda kuyajua.  

17. Siwezi kujitenga (kujinasua) na dhambi zangu.

Lk 13:3 “Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo.” na Ebr 7:25 “Naye, kwa sababu hii, aweza kuwaokoa kabisa wao wamjiao Mungu kwa yeye; maana yu hai sikuzote ili awaombee.”. 

Kila mtu anaweza kuacha dhambi zake kwa msaada wa Roho wa Mungu. Mungu aliyeagiza tutubu, ndiye anayetupa uwezo wa kuacha uovu. Mungu anaweza kuwaokoa wote wanaomjia. Mavuno ya kuishi katika dhambi ni uharibifu na mauti. Ukimgeukia Mungu, utavuna uzima wa milele. Warumi 6:23 “Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.” 

18. Siwezi kutoa maisha yangu kwa Yesu kwa sababu nitawaumiza walio karibu nami.

Mt 10:34-39 “Msidhani ya kuwa nimekuja kuleta amani duniani; la! Sikuja kuleta amani, bali upanga. Kwa maana nalikuja kumfitini mtu na babaye, na binti na mamaye, na mkwe na mkwe mtu; na adui za mtu ni wale wa nyumbani mwake. Apendaye baba au mama kuliko mimi, hanistahili; wala apendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili. Wala mtu asiyechukua msalaba wake akanifuata, hanistahili. Mwenye kuiona nafsi yake ataipoteza; naye mwenye kuipoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataiona.”, Mt 19:29 “Na kila mtu aliyeacha nyumba, au ndugu wa kiume au wa kike, au baba, au mama, au watoto, au mashamba, kwa ajili ya jina langu, atapokea mara mia, na kuurithi uzima wa milele.”.

Maandiko yanatupa faraja na changamoto. Mungu anatuahidi baraka tele tunapojitoa kwake. Ukipoteza marafiki na familia kwa ajili ya Kristo, anaahidi kukupa marafiki wapya na familia mpya. Injili wakati mwingine inatenga waaminio kutoka katika familia zao zisizoamini. Wakati mwingine, mpasuko huu wa mahusiano ni gharama kwa ajili ya kumtumikia Kristo. Mk 10:29-30 “Yesu akasema, Amin, nawaambieni, Hakuna mtu aliyeacha nyumba, au ndugu waume, au ndugu wake, au mama, au baba, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, na kwa ajili ya Injili, ila atapewa mara mia sasa wakati huu, nyumba, na ndugu waume, na ndugu wake, na mama, na watoto, na mashamba, pamoja na udhia; na katika ulimwengu ujao uzima wa milele.

19. Itakuwaje kwa ajili ya watu ambao hawajawahi kusikia Injili?

Rum  2:12-16 “Kwa kuwa wote waliokosa pasipo sheria watapotea pasipo sheria, na wote waliokosa, wenye sheria, watahukumiwa kwa sheria. Kwa sababu sio wale waisikiao sheria walio wenye haki mbele za Mungu, bali ni wale waitendao sheria watakaohesabiwa haki. Kwa maana watu wa Mataifa wasio na sheria wafanyapo kwa tabia zao yaliyo ndani ya torati, hao wasio na sheria wamekuwa sheria kwa nafsi zao wenyewe. Hao waionyesha kazi ya torati iliyoandikwa mioyoni mwao, dhamiri yao ikiwashuhudia, na mawazo yao, yenyewe kwa yenyewe, yakiwashitaki au kuwatetea; katika siku ile Mungu atakapozihukumu siri za wanadamu, sawasawa na injili yangu, kwa Kristo Yesu.”.

Kwa mujibu wa maandiko haya, kila mtu anajua vya kutosha kuhusu Mungu kiasi cha kuwajibika kwa matendo yake. Mungu amejifunua kwao kupitia uumbaji na dhamiri zao. Uumbaji mzuri unathibitisha kwamba kuna Muumbaji mzuri. Mungu ameweka dhamiri ndani ya kila mwanadamu. Dhamiri hii inamtia moyo mtu akitenda jema na kumfanya ajisikie hatia anapotenda baya. Mungu anaahidi kwamba atahukumu kwa haki kulingana na kiwango cha uelewa na ufunuo alichoweka ndani ya mwanadamu. 

Pengine baada ya kuusoma ujumbe huu umeguswa na uko tayari kumpa Bwana maisha yako. Omba hivi kwa imani:

Ee Bwana Yesu, nakiri kwamba mimi ni mwenye dhambi. Naliitia Jina lako. Nisamehe dhambi zangu zote. Naamini ulikufa kwa ajili yangu. Naamini ulifufuka kutoka kwa wafu kama yanenavyo maandiko. Nakupokea katika maisha yangu uwe Bwana na Mwokozi wangu binafsi.  Asante Yesu kwa kuniokoa. Amen.” 

Kama umeomba sala hii kwa kumaanisha kabisa, UMEOKOKA LEO. Unachotakiwa kufanya ni kuanza kusoma Biblia, kumwomba Mungu na kushiriki ibada katika kanisa lenye mafundisho sahihi ya kibiblia linaloamini kwamba tunaokolewa tukiwa hapahapa duniani. Wokovu katika ukamilifu wake sio tukio (event) la mara moja tu bali ni mchakato (process) hadi tutakapofikia hatua ya kutukuzwa (glorification). Rum 8:30 Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki; na wale aliowahesabia haki, hao akawatukuza.Katika roho umeokoka leo, nafsi inaendelea kuokoka na mwili hauokoki, siku moja tutapewa mwili wa utukufu.