Ticker

6/recent/ticker-posts

MTAFUTE MUNGU, NGUVU ZAKE NA UWEPO WAKE NDIPO UTAFURAHIA MAISHA


 MTAFUTE MUNGU, NGUVU ZAKE NA UWEPO WAKE NDIPO UTAFURAHIA MAISHA

Hata kama una nia njema ya kumtumikia Mungu, utaendelea kushindwa kwa sababu hutafuti kumjua Mungu na unategemea nguvu zako mwenyewe. Ikiwa Bwana Yesu alihitaji maombi mazito ili kutiwa nguvu wakati anakaribia mateso ya msalaba, je, wewe na mimi si zaidi? Luka 22:42-44 “akisema, Ee Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke. Malaika kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu. Naye kwa vile alivyokuwa katika dhiki, akazidi sana kuomba; hari yake ikawa kama matone ya damu yakidondoka nchini.” Nguvu zetu za mwili bila Roho wa Mungu hazitatufikisha popote. Hii kazi ina mwenyewe hivyo lazima tuhitaji msaada wake kuliko kuwakimbilia wanadamu. Zekaria 4:6 “Akajibu akaniambia, akisema, Hili ndilo neno la Bwana kwa Zerubabeli, kusema, Si kwa uwezo, wala si kwa nguvu, bali ni kwa roho yangu, asema Bwana wa majeshi.” Tambua kwamba kumtegemea mwanadamu ni laana. Yeremia 17:5 “Bwana asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha Bwana.”

Zaburi 105:4 “Mtakeni Bwana na nguvu zake, Utafuteni uso wake sikuzote.” Neno la Mungu linatusisitiza kwamba tumtafute MUNGU, NGUVU ZAKE na UWEPO WAKE. Mafanikio ya kweli yasiyo na majuto wala masharti ya kitumwa yanapatikana kwa kumjua sana Mungu. Ayubu 22:21 “Mjue sana Mungu, ili uwe na amani; Ndivyo mema yatakavyokujia.” Kuna mtu anaonekana kwa nje kama aliyetajirishwa na shetani lakini ni mtumwa na hafurahii mali alizo nazo. Mwingine amejenga majumba lakini haruhusiwi kulala ndani. Usiku ukifika anatoka nje kulala kwenye gari. Mwingine haruhusiwi kuvaa vizuri apendeze. Mwingine lazima usiku wa manane aende makaburini akalale akiwa uchi. Mwingine anamtoa ndugu anayempenda awe kafara kwa shetani. Kwa hiyo hawa watu wana utajiri wa kuonyesha watu lakini wao wenyewe hawaufurahii na baada ya maisha haya watahukumiwa na Mungu aliye hai.

Mtume Paulo naye alisema kwamba mahubiri yake sio ya kisomi na kiakili tu ya kushawishi watu bali yameambatana na dalili za Roho na nguvu. 1 Wakorintho 2:4,5 “Na neno langu na kuhubiri kwangu hakukuwa kwa maneno ya hekima yenye kushawishi akili za watu, bali kwa dalili za Roho na za nguvu, ili imani yenu isiwe katika hekima ya wanadamu, bali katika nguvu za Mungu.” Leo tuna watu wengi ambao imani yao iko katika misingi ya madhehebu na viongozi wao na sio kwa Mungu aliye hai. Wengi leo hawako tayari kupima mahubiri ya viongozi wao kama yanaendana au kupingana na Biblia. Mtume Paulo na timu yake waliwapongeza watu wa Beroya kwa kutathmini mahubiri yao ili wajiridhidhishe kama yanakubaliana na Biblia kabla ya kuyatekeleza. Mdo 17:11 “Watu hawa walikuwa waungwana kuliko wale wa Thesalonike, kwa kuwa walilipokea lile neno kwa uelekevu wa moyo, wakayachunguza maandiko kila siku, waone kwamba mambo hayo ndivyo yalivyo.”

Wengi leo tunamtumikia Mungu bila dalili wala ishara zozote na tumeridhika na hali hiyo. Musa alimwambia Mungu kwamba kama hatamhakikishia kwamba yuko pamoja naye hataondoka mahali alipo. Unaweza kudhani alionyesha kiburi lakini sivyo. Alifanya kama mwajiriwa anayetumwa kwenda mahali. Lazima apewe barua inayoidhinisha kwamba ametumwa (endorsement). Wewe una kitambulisho gani kutoka kwa Mungu kuthibitisha kwamba amekutuma kufanya hicho unachokifanya? Kutoka 33:15,16 “Naye akamwambia, Uso wako usipokwenda pamoja nami, usituchukue kutoka hapa. Kwa maana itajulikanaje kuwa nimepata neema mbele zako, mimi na watu wako? Siyo kwa sababu unakwenda pamoja nasi, hata mimi na watu wako tutengwe na watu wote walio juu ya uso wa nchi?”

Kuna aina kuu mbili za uwepo wa Mungu. Aina ya kwanza ni ile hali kwamba Mungu yuko kila mahali wakati wote (omnipresence). Aina ya pili ni pale Mungu anapodhihirisha uwepo wake kwetu mpaka tunauhisi na hata kuuona (manifest presence). Hii ina maana kwamba Mungu anatuona wakati wote lakini sio wakati wote tunahisi uwepo wake. Hata hivyo kuna wakati Mungu anajidhihirisha mpaka tunajua yuko katikati yetu. Mwanzo 28:16,17 “Yakobo akaamka katika usingizi wake, akasema, Kweli Bwana yupo mahali hapa, wala mimi sikujua. Naye akaogopa akasema, Mahali hapa panatisha kama nini! Bila shaka, hapa ni nyumba ya Mungu, napo ndipo lango la mbinguni.”

Wakati wewe unamtafuta Mungu usisahau kwamba Mungu pia anatafuta watu wenye sifa fulani.

1. Wanaomuabudu katika roho na kweli – ambao hawaabudu kwa mazoea ya ibada

Yohana 4:23,24 “Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu. Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.”

2. Waliopondeka na kutetemeka mbele zake

Isaya 66:2 “Maana mkono wangu ndio uliofanya hivi vyote, vitu hivi vyote vikapata kutokea, asema Bwana; lakini mtu huyu ndiye nitakayemwangalia, mtu aliye mnyonge, mwenye roho iliyopondeka, atetemekaye asikiapo neno langu.”

Bila kuwa na nguvu za Mungu hatutaweza kuangusha ngome zinazozuia MAOMBI yetu na MAJIBU YA MAOMBI YETU katika ulimwengu wa roho.

2 Wakorintho 10:4 (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;)

Waefeso 6:10-12 “Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.?

Unaweza kupata ujumbe huu kwa audio kwa link hii https://on.soundcloud.com/wC76G

Maombi ya wiki hii

1.     Ee Mungu naomba uondoe mazoea katika maisha yangu na kunifanya upya katika uhusiano wangu na Wewe.

2.     Ee Mungu naomba udhihirishe uwepo wako katika maisha yangu ili niwe na uhakika kwamba ninakutumikia Wewe na sio miungu mingine.

3.     Ee Mungu naomba unipe moyo wa nyama uliopondeka ili niweze kutii sauti yako na maagizo yako.

4.     Ee Mungu naomba unipe nguvu za Roho wako ili niweze kuwa shahidi wako ambaye ni hodari na mwenye moyo wa ushujaa.

Kwa wale wenye mzigo wa kushirikiana nami kwa ajili ya kusaidia jamii inayoteseka kutokana na uhatarishi na majanga badala ya kutoa huduma za kiroho peke yake, karibuni mjiunge na group letu jipya la Vulnerability and Disaster Management (Kukabiliana na uhatarishi & majanga) ambalo liko Facebook.

Nimegundua kwamba kwa mujibu wa Mathayo 25:41-46 watu wengi wanaojali kutoa huduma za kiroho peke yake bila kutoa huduma za kugusa maisha ya kimwili kwa wasiojiweza wataenda motoni!  

Lawi Mshana, +255712-924234, Tanzania