Watu wengi wanajiuliza kwamba inakuwaje Mungu wa upendo na
mwenye nguvu zote anaruhusu tupitie magumu ya aina mbalimbali. Nitakupa mifano
hai ambayo inathibitisha kwamba Mungu anaruhusu mambo fulani yatokee kwa vile
ana kusudi jema mbele yako.
1.
Mungu hataki kumuua shetani ili ajue tunampenda kiasi gani na tuzidi kumtegemea
Mungu ametupa ‘utashi’ au ‘uwezo wa kuchagua maisha tunayotaka’ ili mradi tuwe tayari kwa matokeo yake badaye. Kama shetani hangekuwepo ingekuwa vigumu Mungu kujua tunampenda kiasi gani. Unaposhawishiwa na shetani halafu ukaamua kumtii Mungu, unakaribisha baraka kwako na kwenye uzao wako. Maisha yako leo ni matokeo ya uchaguzi ulioufanya au walioufanya watangulizi wako.
Kum 30:19 “Nazishuhudiza mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimekuwekea mbele yako uzima na mauti, baraka na laana; basi chagua uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako.”
2.
Mungu amempa mkuu wako au mumeo moyo mgumu ili aonyeshe nguvu zake
Hakuna Mwisraeli alifurahia kuteswa na Farao. Lakini kwa
upande mwingine Mungu aliruhusu hilo litokee ili atambulishe nguvu Zake katika
dunia yote. Israeli walijua umuhimu wa Mungu pale waliposhindwa kwa nguvu zao
wenyewe kujinasua katika makucha ya Farao. Kinachokuumiza zaidi sio KILE
UNACHOTENDEWA NA ADUI YAKO bali JINSI UNAVYOITIKIA BAADA YA KUTENDWA MABAYA.
Kinachokuumiza sio wewe kuitwa mbwa bali ni namna unavyoitikia. Ukikubali
kwamba unaweza kuwa mbwa utaumia sana. Lakini ukitambua kwamba huwezi kamwe
kuwa mbwa, utapuuzia na kuwa salama. Puuzia majina mabaya unayopewa na watu na
badala yake simamia jina jipya ulilopewa na Mungu wako.
Warumi 9:17,18 “Kwa
maana maandiko yasema juu ya Farao, ya kwamba, Nilikusimamisha kwa kusudi hili,
ili nionyeshe nguvu zangu kwako, jina langu likatangazwe katika nchi yote.
Basi, kama ni hivyo, atakaye kumrehemu humrehemu, na atakaye kumfanya mgumu
humfanya mgumu.”
3.
Mungu ameruhusu upite kwenye bonde la uvuli wa mauti ili uhitaji msaada Wake (gongo
lake na fimbo yake vikufariji)
Unaweza kujua maana ya faraja pale unapolia machozi. Faraja
haina maana sana kwa mtu anayecheka. Kwa hiyo kuna wakati Mungu anaruhusu upite
kwenye hali ngumu ili akikuvusha ujue Mteteaji wako yu hai. Ayubu 19:25 “Lakini mimi najua ya kuwa Mteteaji wangu
yu hai, Na ya kuwa hatimaye atasimama juu ya nchi.” Usikubali uongo wa shetani
kwamba Mungu amekuacha hata kama unapitia ugumu wowote. Mungu hajawahi kukuacha
ila wewe ndiye mara nyingi unamuacha. Waebrania 13:5 “….kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala
sitakuacha kabisa.”
Zaburi 23:4 “Naam,
nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe
upo pamoja nami, Gongo lako na fimbo yako vyanifariji.”
4.
Mungu anaweza kuruhusu adui wapigane na wewe lakini kamwe hataruhusu wakushinde
Hata kama kuna watu wanapigana na wewe, HAWATAKUSHINDA kwa
vile huko peke yako. Mwanzoni watajifariji kwamba wanakutesa lakini mwisho wao
utakuwa mbaya.
Yeremia 15:20 “Nami
nitakufanya kuwa kama ukuta wa boma la shaba juu ya watu hawa; nao watapigana
nawe; lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe, ili nikuokoe, na
kukuponya, asema Bwana.”
Mungu ameruhusu maji yafike shingoni lakini HAYATAWEZA
KUKUGHARIKISHA. Isaya 43:2 “Upitapo
katika maji mengi nitakuwa pamoja nawe; na katika mito, haitakugharikisha;
uendapo katika moto, hutateketea; wala mwali wa moto hautakuunguza.”
5. Pamoja
na mafanikio yaliyoko mbele yako, wengi hawafurahii
Katika mafanikio yako sio wote wanafurahia. Kuna watu
watahakikisha wanapinga juhudi zako kwa nguvu zote. Hivyo shetani aliyeshindwa
kuzuia mafanikio yako, sasa anatafuta watu wa kupinga mafanikio yako. 1
Wakorintho 16:9 “kwa maana nimefunguliwa
mlango mkubwa wa kufaa sana, na wako wengi wanipingao.” Kwa hiyo usichoke
kuomba ulinzi wake hata kama umefanikiwa. Zidi kuonyesha uaminifu wako kwa
Mungu ili baraka zako ziwe za kudumu na sio za msimu.
Wakati una hali ngumu kimaisha unapewa majina ya kimaskini. Unapofanikiwa usishangae ukiitwa Freemason hata kama hujui maana yake. Na usishangae wanaokuzushia hivyo wakiwa ni marafiki zako wa karibu uliowaamini sana, uliowasaidia sana na ambao hata hawajui Freemasonry ina maana gani. Zab 55:12-14 “Kwa maana aliyetukana si adui; Kama ndivyo, ningevumilia. Aliyejitukuza juu yangu siye anichukiaye; Kama ndivyo, ningejificha asinione. Bali ni wewe, mtu mwenzangu, Rafiki yangu, niliyejuana nawe sana. Tulipeana shauri tamu; na kutembea Nyumbani mwa Mungu pamoja na mkutano.”
Maombi
ya wiki hii
1. Ee Mungu naomba unifundishe kuishi maisha ya aina yoyote
bila kukuacha kama mtume Paulo alivyosema, “Najua
kudhiliwa, tena najua kufanikiwa; katika hali yo yote, na katika mambo yo yote,
nimefundishwa kushiba na kuona njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa.” (Fil
4:12).
2. Ee Mungu naomba unisaidie nijue sababu ya watu kunipinga
wakati sijawakosea ili nisipambane nao bali nikutazame Wewe.
3. Ee Mungu naomba ushughulike na watu wanaopigana nami. “Ee Bwana, utete nao wanaoteta nami,
Upigane nao wanaopigana nami.” (Zab 35:1)
Nakuombea
upokee baraka zifuatazo:
1. Mungu akufanye ukuta wa boma la shaba juu ya watu
wanaopigana nawe ili waumie wenyewe na kuachana nawe ili umtukuze Mungu wako.
2. Mungu akushike usianguke pale maadui zako wanapokusukuma. Zab 118:13 “Ulinisukuma sana ili nianguke; Lakini Bwana akanisaidia.”
Lawi Mshana, 0712-924234; Tanzania