Neema kimaandiko ni neno lenye tafsiri pana. Hata hivyo tafsiri rahisi ni ‘kupata usichostahili’ na ‘uwezesho kutoka kwa Mungu’ Kuna vitu Mungu ametupa ambavyo hatukustahili na hutuwezi kuvilipia. Mojawapo ni wokovu wa roho zetu. Hivyo tunahitaji kuthamini sana zawadi hii iliyogharimu uhai wa Bwana wetu Yesu Kristo. Yeyote anayekataa zawadi hii au kuipuuza anamaanisha kwamba Yesu aliteseka bure msalabani. Hivyo maandiko yanasema hatakuwa salama. Waebrania 2:3 “sisi je! Tutapataje kupona, tusipojali wokovu mkuu namna hii? Ambao kwanza ulinenwa na Bwana, kisha ukathibitika kwetu na wale waliosikia.” NI yule aliyepokea zawadi hii halafu anarudia matapishi anakuwa kwenye hatari kubwa zaidi. Waebrania 10:30,31 “Maana twamjua yeye aliyesema, Kupatiliza kisasi ni juu yangu, mimi nitalipa. Na tena, Bwana atawahukumu watu wake. Ni jambo la kutisha kuanguka katika mikono ya Mungu aliye hai.”
Lengo la ujumbe huu ni kuzungumzia tafsiri ya ‘uwezesho kutoka kwa Mungu.’ Hii ina maana kwamba hii neema haipo tu kwa ajili ya maisha baada ya kifo bali pia ipo kwa ajili ya maisha yetu tukiwa bado duniani. Tusipofahamu tunaweza kushindwa kunufaika nayo.
Tupateje huu uwezesho wa Mungu?
1. Tuwe na juhudi ya kuhubiri nguvu ya ufufuo ya Bwana Yesu
Mdo 4:33 “Na mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwake Yesu kwa nguvu nyingi, na neema nyingi ikawa juu yao wote.”
Tukiendelea kuhubiri tu mafanikio ya duniani (prosperity gospel) na kusahau kwamba maisha haya ni kivuli cha maisha yajayo, neema nyingi haitakuwa juu yetu. Hata kabla Yesu hajafa msalabani matajiri walikuwepo. Yesu alipofufuka alifungua ukurasa mpya wa Paradiso (Edeni) ambapo Adamu alifukuzwa awali. Luka 23:43 “Yesu akamwambia, Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami peponi.” Uzima wa milele unaanzia hapa duniani tunapomwamini Yesu. Yohana 17:3 “Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma.”
2. Tusitegemee nguvu zetu wala ujanja wetu wa kimwili
2 Wakorintho 12:9 “Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu.”
Huwezi kuthamini nguvu za Mungu kama tayari unadhani una nguvu. Unapoona udhaifu wako mbele za Mungu ndipo utahitaji nguvu za Mungu. Lazima ujione kwamba huwezi bila msaada wa Mungu. Wafilipi 4:13 “Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.” Hakuna jambo utashindwa kulifanya kama Mungu atakutia nguvu.
3. Tusisubiri tuwe na ziada ndipo tumtolee Mungu
2 Kor 8:1- 4 “Tena ndugu zetu, twawaarifu habari ya neema ya Mungu, waliyopewa makanisa ya Makedonia; maana walipokuwa wakijaribiwa kwa dhiki nyingi, wingi wa furaha yao na umaskini wao uliokuwa mwingi uliwaongezea utajiri wa ukarimu wao. Maana nawashuhudia kwamba, kwa uwezo wao, na zaidi ya uwezo wao, kwa hiari yao wenyewe walitoa vitu vyao; wakituomba sana pamoja na kutusihi kwa habari ya neema hii, na shirika hili la kuwahudumia watakatifu.”
Watu waliopewa neema ya utoaji hawasubiri wawe na ziada. Wanaweza kumpa mtu kitu ambacho wao wenyewe wanakihitaji sana. Huwezi kumuiga mtu wa aina hii. Hamtolei Mungu ili tu abarikiwe duniani. Anatoa akijua anawekeza kwa ajili ya maisha yake yajayo. Kuna watu wamejilimbikizia mali hapa duniani lakini watakuwa maskini sana baada ya maisha haya kwa vile wamechangia dunia tu na sio kumtolea Mungu. Mathayo 6:19,20 “Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wevi huvunja na kuiba; bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi.”
4. Tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri
Waebrania 4:16 “Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.”
Hatutapokea kwa vile tu tumekubali wito. Tunahitaji kukaribia kiti cha neema kwa ujasiri ndipo tutapata NEEMA YA KUTUSAIDIA WAKATI WA MAHITAJI. Hutaweza kukaribia kiti cha neema kwa ujasiri kama kuna mambo fulani unahukumiwa moyoni (mashitaka ya shetani). Dhambi ambayo huiungami na kuiacha Yohana 5:24 “Amin, amin, nawaambia, Yeye alisikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani.”
Usjidanganye kwamba unavyomficha kiongozi wako dhambi zako, na Mungu hazioni. Unazuia mafanikio yako na hupokei rehema za Mungu. Mithali 28:13 “Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema.”
5. Tuwatumikie wengine kwa moyo safi
1 Petro 4:10 “kila mmoja kwa kadiri alivyoipokea karama, itumieni kwa kuhudumiana; kama mawakili wema wa neema mbalimbali za Mungu.”
Neema ya Mungu sio kwa ajili ya watu
wabinafsi na wachoyo. Ni kwa ajili ya watu wanaohudumia wengine. Jiulize
unamhudumia nani bila kutazamia malipo au shukrani yoyote kutoka kwake!
Unapotafuta sifa na heshima za duniani, unakuwa umeshalipwa tayari. Malipo ya
mbinguni ni kwa ajili ya wale ambao hawakulipwa duniani.
Mathayo 6:1 “Angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu, kusudi mtazamwe na wao; kwa maana mkifanya kama hayo, hampati thawabu kwa Baba yenu aliye mbinguni.”
Maombi
ya wiki hii
1. Ee Mungu naomba unifundishe kuhubiri Neno lako kwa
usahihi ili neema nyingi iwe juu yangu.
2. Ee Mungu naomba uondoe mazoea ndani yangu ili
nisitegemee nguvu zangu, akili yangu na elimu yangu bali nikutegemee Wewe
unayeweza yote.
3. Ee Mungu naomba uniwezeshe kukutolea sadaka yenye kazi
maalum kwangu badala ya kukutolea mabaki na ziada.
4. Ee Mungu naomba unirehemu na kuniponya roho yangu ili
nisihukumiwe moyoni kwamba sistahili kupokea majibu yangu.
5. Ee Mungu naomba uniwezeshe kuwatumikia wengine bila
kutarajia kitu kutoka kwao ili nipate thawabu kutoka kwako.
Nakuombea Mungu akuwezeshe kuishi maisha aliyokupangia ili
utimize kusudi lake la kukuleta duniani bila kusahau kwamba kuna siku utaondoka
duniani kama walivyoondoka wengine na kusahaulika. Ujue kuna maisha mengine ya
uhakika zaidi kuliko haya tuliyo nayo hapa duniani.
Lawi Mshana, +255712-924234, Tanzania.