SI MPANGO WA MUNGU TUISHI KWA UTEGEMEZI NA UTUMWA WA MADENI BALI KWA IMANI – Lawi Mshana
Imekuwa ni jambo la kawaida kuishi kwa madeni kwa wasioamini na wenye imani. Hii inatokana na ukweli kwamba tumeamua imani ifanye kazi kanisani tu na sio katika maeneo yote ya maisha. Tumeamua KUHUBIRI imani lakini hatuko tayari KUISHI kwa imani. Biblia inasema, ‘Kwa maana haki ya Mungu inadhihirishwa ndani yake, toka imani hata imani; kama ilivyoandikwa, Mwenye haki ataishi kwa imani’ (Rum 1:17). Lakini pia Biblia hiyohiyo inasema moja ya ishara za kuwa mtu aliyebarikiwa ni kukopesha na sio kukopa. Kum 28:12 ‘Atakufunulia Bwana hazina yake nzuri, nayo ni mbingu, kwa kutoa mvua ya nchi yako kwa wakati wake, na kwa kubarikia kazi yote ya mkono wako; nawe utakopesha mataifa mengi, wala hutakopa wewe.’ Tangu tuchague kuishi kwa kutegemea kanuni za maisha ya dunia hii badala ya kanuni za ufalme wa Mungu, tumeshindwa kuitumia imani yetu katika kutatua matatizo yetu. Hatuoni kwamba ni dhambi kushindwa kuishi katika viwango alivyotuwekea Mungu. Kumbuka dhambi ina tafsri mbili; KUTENDA YASIYOKUPASA (mfano, uzinzi, wizi nk) na KUTOTENDA YANAYOKUPASA (mfano, kuhubiri Injili, kusaidia yatima na wajane katika dhiki yao, kusaidia masikini, kuishi kwa imani nk). Hii tafsiri ya pili inathibitishwa na Yakobo 4:17 ‘Basi yeye ajuaye kutenda mema, wala hayatendi, kwake huyo ni dhambi.’ Ni kweli tumeacha maovu na kumgeukia Mungu lakini hatutapona kama hatutatenda yale mema tunayotakiwa kutenda. Mfano, Mungu hapendi uende ibadani mikono mitupu Kut 34:20 “…Wala hapana atakayehudhuria mbele zangu mikono mitupu.” Pia hataki umtembelee mkwe wako mikono mitupu. Ruthu 3:17 “Akasema, Na vipimo hivi sita vya shayiri amenipa; maana akaniambia, Usiende kwa mkweo mikono mitupu.”
Pengine unajitetea kwamba huna cha kutoa kwa sababu ya ugumu wa maisha. Kitendo cha kukosa cha kumtolea Mungu kinaashiria kwamba kuna shida katika mahusiano yako na Mungu. Mtunga Zaburi anasema, ‘Nalikuwa kijana nami sasa ni mzee, Lakini sijamwona mwenye haki ameachwa Wala mzao wake akiomba chakula’ (Zab 37:25). Swali la kujiuliza U MWENYE HAKI ili Mungu asikuache na wanao wasiwe ombaomba? Kumbuka kila ahadi katika maandiko ina masharti yake. Tusipende kunyofoa mstari mmoja (text) na kuacha masharti ya utimilizo wake kwa kusoma kifungu kizima (context). Mfano wengi wetu tunapenda sana kusema, Mimi ni kichwa wala si mkia kwa kunukuu Kum 28:44 hata kama katika uhalisia ni kinyume chake. Wakati huohuo tunashindwa kusoma masharti ya kuwa kichwa katika Kum 28:1,2 “Itakuwa utakaposikia sauti ya Bwana, Mungu wako, kwa bidii, kutunza kuyafanya maagizo yake yote nikuagizayo leo, ndipo Bwana, Mungu wako, atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya duniani; na baraka hizi zote zitakujilia na kukupata usikiapo sauti ya Bwana, Mungu wako.” Je unatunza maagizo ya Bwana ili ustahili kutukuzwa na Bwana juu ya mataifa yote na baraka zake zikujilie badala ya wewe kuzitafuta? Unafika ibadani saa ngapi na unatoka saa ngapi? Una mchango gani katika utumishi wa kanisa lako? Kiasi gani unamshirikisha baraka zako mchungaji wako, au unamshirikisha matatizo tu? (Kumbuka Wagalatia 6:6 Mwanafunzi na amshirikishe mkufunzi wake katika mema yote.).
Je ni kweli kwamba maisha unayoishi ndiyo uliyopangiwa na Mungu au unajaribu kuwaiga watu ambao hawajasajiliwa katika ufalme wa Mungu? Fedha yenyewe sio tatizo. Mhu 10:19 “….Na fedha huleta jawabu la mambo yote”. Tatizo ni TABIA YA KUPENDA FEDHA “Ebr 13:5 Msiwe na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa.” Tunapungukiwa kwa vile tunajaribu kuishi maisha ya watu wengine! Saini ya dole gumba lako (finger print) haifanani na ya mtu yeyote kati ya watu karibia bilioni 7 duniani. Mpango wa Mungu kwako haufanani na wa yeyote duniani. Usipende kuwa fotokopi ya mtu fulani. Jitegemee maana wewe ni wa aina yake (you are unique).
Kukopa sio dhambi lakini maandiko hayapongezi kuishi kwa kutegemea kukopa. Baadhi ya maandiko machache yanayokatisha tamaa kukopa ni:
Kumbukumbu la Torati 28:12 Atakufunulia Bwana hazina yake nzuri, nayo ni mbingu, kwa kutoa mvua ya nchi yako kwa wakati wake, na kwa kubarikia kazi yote ya mkono wako; nawe utakopesha mataifa mengi, wala hutakopa wewe.
Mithali 22:7 Tajiri humtawala maskini, Naye akopaye ni mtumwa wake akopeshaye.
Zaburi 37:21 Asiye haki hukopa wala halipi, Bali mwenye haki hufadhili, hukirimu.
Lakini pia kukopa ni adui wa imani. Kwa vile una haraka sana unataka ukope leo ili usilazimike kumtegemea Mungu kwa kufanya hatua kwa hatua kadiri anavyokubariki. Lakini wakati mwingine unalazimika kuishi kwa hofu kwa vile hujui utalipaje deni lako. Unajiona kwamba unatumia mali ambayo haijawa ya kwako ingawa wanaokutembelea wanadhani ni ya kwako. Kwa mfumo huu kuna watu mpaka wanastaafu bado wanadaiwa wakati kuna watu wa kipato cha chini sana wamemtegemea Mungu na kujifunza kwa chungu (sisimizi) wakafanya makubwa. Mit 6:5-8 “Ujiponye kama paa na mkono wa mwindaji, Na kama ndege katika mkono wa mtega mitego. Ewe mvivu, mwendee chungu, Zitafakari njia zake ukapate hekima. Kwa maana yeye hana akida, Wala msimamizi, wala mkuu, Lakini hujiwekea akiba ya chakula wakati wa jua; Hukusanya chakula chake wakati wa mavuno.”
Nimejifunza kuishi kwa imani baada ya siku moja Roho Mtakatifu kunipa ufunuo kuhusu Waebrania 11. Niliangalia jinsi neno KWA IMANI lilivyorudiwa mpaka nikajifunza kitu na kugundua kwamba ninahubiri imani ila siishi kwa imani. Kila aliyetajwa alifanya kitendo kinachoonekana kwa macho ambacho kinathibitisha imani yake. Mfano, Kwa imani Habili alitoa dhabihu bora kuliko Kaini, kwa imani Nuhu aliunda safina apate kuikoa nyumba yake nk. Hebu jiulize UNA KITU GANI CHA KUONYESHA WATU KWAMBA ULIKIFANYA KWA KUMWAMINI MUNGU BILA KUOMBA MTU WALA KUKOPA? Hata kama huwezi katika maeneo yote, anza kufanya mazoezi ya jambo fulani. Yak 2:17 “Vivyo hivyo na imani, isipokuwa ina matendo, imekufa nafsini mwake.” Kama huna kitu cha kuielezea imani yako huna tofauti na mashetani. Yak 2:19 “Wewe waamini ya kuwa Mungu ni mmoja; watenda vema. Mashetani nao waamini na kutetemeka.” Kumbuka mashetani yakisikia Jina la Yesu yanaamini na kutetemeka lakini hayako tayari kumtii Yesu na kuifanyia kazi imani.
Nitafurahi siku moja kama Mungu atasema, KWA IMANI LAWI ALIFANYA HILI NA HILI BILA KUMTEGEMEA MWANADAMU.
Mithali 29:25 “Kuwaogopa wanadamu huleta mtego; Bali amtumainiye Bwana atakuwa salama.” Wapo waumini leo wameikana imani na kuanguka kwa sababu ya kuogopa maisha, ajira zao na mabosi wao. Wapo wachungaji, mitume na maaskofu leo wameshindwa kuwakemea waumini fulani kwa vile wana uwezo kiuchumi na ndio walioshika maisha yao.
Nilisikitika kupata kisa kimoja cha mchungaji fulani ambaye alimtenga muumini wake kwa sababu ya uasherati. Msichana huyo akamwambia mchungaji lakini naomba ujue kwamba anayetufanyia hivi ni mzee wa kanisa unayekaa naye mbele madhabahuni. Mchungaji hakuweza kuchukua hatua zozote maana mzee huyo ni mfadhili wake mkuu. Tusipokuwa waangalifu tutahubiri wengine na mwisho sisi wenyewe tukataliwe.
Hatari ya kuishi bila imani ni kubwa sana katika kipindi hiki ambacho mpinga Kristo anajiandaa kutawala dunia kwa fedha moja, dini moja na serikali moja. Ufu 13:15-18 “Akapewa kutia pumzi katika ile sanamu ya mnyama, hata ile sanamu ya mnyama inene, na kuwafanya hao wote wasioisujudu sanamu ya mnyama wauawe. Naye awafanya wote, wadogo kwa wakubwa, na matajiri kwa maskini, na walio huru kwa watumwa, watiwe chapa katika mkono wao wa kuume, au katika vipaji vya nyuso zao; tena kwamba mtu awaye yote asiweze kununua wala kuuza, isipokuwa ana chapa ile, yaani, jina la mnyama yule, au hesabu ya jina lake. Hapa ndipo penye hekima. Yeye aliye na akili, na aihesabu hesabu ya mnyama huyo; maana ni hesabu ya kibinadamu. Na hesabu yake ni mia sita, sitini na sita.”
Mpinga Kristo ameshajipanga tayari kwa kutumia kile tunachoshabikia kwamba ni MAENDELEO YA KITEKNOLOJIA. Mwenye hekima ndiye tu atagundua mikakati hii. Je tutakapolazimika kukataa kadi fulani kwa vile ina chapa na hatujajifunza kuishi kwa imani tutaweza kweli kupona?
Sikuhukumu ndugu yangu bali nakukumbusha tu kwamba, turudi kwenye Neno la Mungu. Tusiwe na upako wa kuimba na kuhubiri tu madhabahuni bali upako huo ufanye kazi katika maeneo yote ya maisha. Yaani, kazini , shambani, nyumbani na katika bishara zetu.
TUOMBEANE ILI TUMALIZE MWENDO SALAMA NA KUILINDA IMANI KAMA MTUME PAULO. 2 Timotheo 4:7 “Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda”.
Dr Lawi Mshana, Korogwe, Tanga, Tanzania
Unauthorized use and/or duplication of this material without express and written permission from this site’s author and owner is strictly prohibited.
Excerpts and links may be used, provided that full and clear credits is given to Lawi Mshana and www.lawimshana.com with appropriate and specific direction to the original content.