Ticker

6/recent/ticker-posts

Njia nyepesi ya kubadili maisha yako hata kama kiwango chako cha maisha ni cha kawaida

NJIA NYEPESI YA KUBADILI MAISHA YAKO HATA KAMA KIWANGO CHAKO CHA MAISHA NI CHA KAWAIDA 

Inawezekana kubadilisha maisha yetu hata kama kipato ni cha kawaida bila kuiba, kudhulumu, kujiunga na imani potofu kv Freemason au kuwaendea waganga wa kienyeji. Mungu ameahidi kutuinua kwa hiyo sio mpango wa Mungu tuishi maisha ya kubahatisha. 1 Samweli 2:8 “Humwinua mnyonge kutoka mavumbini, Humpandisha mhitaji kutoka jaani, Ili awaketishe pamoja na wakuu, Wakakirithi kiti cha enzi cha utukufu; Kwa maana nguzo za dunia zina Bwana, Naye ameuweka ulimwengu juu yake.”

Pengine mapato yako kwa mwezi hayatoshi kutimiza mahitaji yako ya msingi kwa mwezi. Kama hutakuwa na ziada, utakuwa katika madeni maisha yako yote na kamwe hutaona ndoto zako zikiwa kitu halisi.

1. Weka malengo yenye maana

Ninasema malengo yenye maana kwa vile kuna watu wana malengo ambayo hayaweza kuwa kitu halisi bali ni ndoto tu ya kusimulia kila siku. Mfano, Kusema Nataka kuwa tajiri, ni ndoto. Lakini kusema nataka nikusanye shilingi milioni kumi ni zaidi ya ndoto. Malengo yanawasaidia watu wenye kipato cha kawaida wafanye mambo makubwa. Kwa wale waliobahatika kujifunza masuala ya malengo yenye tija bila shaka wanajua sifa ya malengo hayo kwamba ni SMART. SMART ni vifupisho vya maneno ya kingereza yafuatayo: S – Specific (mahususi au kulenga jambo maalum badala ya kufanya mambo mengi kwa mpigo), M – Measurable (yanayopimika yaani uweze kujua umefika wapi au umebakiza nini), A – Achievable (yanayotekelezeka au yanayofikika yaani yasiwe kituko mf huna hata baiskeli ila unataka ununue ndege), R – Relevant/Realistic (yenye maana kwako mf kutaka ununue boti wakati hakuna mto mkubwa wala ziwa wala bahari haina maana) na T – Time bound (yenye muda maalum yaani tarehe ya mwisho ijulikane). Kumbuka KAMA HUJUI UENDAKO HUWEZI KUPOTEA (Mtu anajua amepotea kama tu alijua anakwenda wapi. Lakini kama mtu hajui anakokwenda njia yoyote ni sahihi kwake. Mtu wa aina hiyo hawezi kujisimamia bali anafanya kila kinachojitokeza mbele yake kwa kukurupuka. Badala ya yeye mwenyewe kuzipangia pesa zake, matukio ndiyo yanazipangia pesa zake. 

Najua mwingine anaweza kusema mimi ninaishi kwa imani kwa hiyo sina haja ya malengo. Tusisahau kwamba neno la Mungu linatuasa kwamba tutumie akili ipasavyo ila tusitende dhambi. 1 Wakorintho 15:34 “Tumieni akili kama ipasavyo, wala msitende dhambi; kwa maana wengine hawamjui Mungu. Ninanena hayo niwafedheheshe.” Lakini pia tunatakiwa kutumia imani kwa kuzingatia kipimo cha imani tulichopewa. Kujaribu kuishi kwa kuiga kiwango cha imani ya mtu mwingine ni kutafuta kifo. 2 Wakorintho 10:13,15 “Lakini sisi hatutajisifu zaidi ya kadiri yetu; bali kwa kadiri ya kipimo tulichopimiwa na Mungu, yaani, kadiri ya kufika hata kwenu. wala hatujisifu zaidi ya kadiri yetu, yaani, katika taabu za watu wengine; bali tukiwa na tumaini ya kwamba, imani yenu ikuapo, tutakuzwa kwenu kwa kadiri ya kipimo chetu, na kupata ziada.” Iga imani ya waliokutangulia lakini uzingatie kiwango chako. Waebrania 13:7 “Wakumbukeni wale waliokuwa wakiwaongoza, waliowaambia neno la Mungu; tena, kwa kuuchunguza sana mwisho wa mwenendo wao, iigeni imani yao.” Warumi 12:3 “Kwa maana kwa neema niliyopewa namwambia kila mtu aliyeko kwenu asinie makuu kupita ilivyompasa kunia; bali awe na nia ya kiasi, kama Mungu alivyomgawia kila mtu kiasi cha imani.”

Kwa nini malengo SMART ni muhimu?

a.     Yanakuchochea kuyafanyia kazi Mf Nataka niweke sh 10,000 kila mwezi ili kwa miaka 10 niwe na sh 1,200,000 za kitu fulani. Unaweza kuidharau hii pesa lakini miaka 10 itapita huna hata shilingi elfu 50 ya kumsaidia mtoto wako.

b.     Yanakufanya uwe na maandalizi Mf Ili uwe na shahada miaka 5 ijayo utajiandaa kwa ada na kukosa usingizi.

c.     Yanakusaidia ujue umefanikiwa wapi. Bila malengo huwezi kujipongeza wala kujikosoa baada ya muda fulani.

d.     Yanakusaidia ufanye ufuatiliaji. Utawajibika zaidi na kujua kama umeacha njia au uko sahihi.

e.     Yanakusaidia uwe na mipaka ya matumizi. Vinginevyo, pesa zitaishia katika masuala ya sherehe za kifamilia na kirafiki.

f.       Yanakusaidia utengeneze mpango. Mf ili niwe na sh 1,200,000 kwa miaka 10, itabidi nipunguze matumizi ya familia ili niwekeze sh 10,000 kila mwezi jambo ambalo sio rahisi sana kwa mtu asiye na mpango.

g.     Yanakusaidia ujue gharama utakayolipa. Mf sio kubana tu matumizi lakini unaweza kulazimika kuanzisha biashara fulani.

h.     Yanakutia hamasa ya kusubiri mafanikio makubwa ya mbele kuliko kuridhika na mafanikio madogo ya sasa.

i.       Yanakusaidia ujadiliane na familia jinsi ya kujipanga.

j.       Yanakusaidia uwe na tabia ya kuwekeza na kuweka akiba.

2. Badili mtindo wa maisha yako

·   Kama u mpangaji, hamia katika nyumba ya gharama nafuu. Usiige maisha ya watu wengine ambao hujui vyanzo vyao vya mapato ni vingapi.

·   Endelea kutumia chombo chako cha zamani mf baiskeli, pikipiki au gari kwa miaka mitatu au zaidi. Usiendekeze fashion bila sababu za lazima.

·   Nunua kitu kilichotumika (second hand). Baadhi ya vitu hivi ni imara sawa na vipya na bei yake ni nusu ya vipya. Sio lazima kila kitu ukinunue kikiwa kipya. Hata hivyo lazima uchunguzi wa kutosha ufanyike ili usije ukaingia gharama zaidi kwa kununua kitu kibovu.

·   Epuka kupeleka mtoto katika shule za bei kubwa bila sababu za msingi. Tambua kiwango chako cha maisha na uwezo wa mtoto wako. Kuna mtoto hata akipelekwa shule ya viwango anaweza asionyeshe tofauti ya maana.

2. Ongeza ujuzi wako

·   Soma zaidi upate cheti au stashahada au shahada. Kama una shahada pata shahada ya uzamili au hata shahada ya uzamivu.

·  Kaa na mtu mwenye ujuzi upate uzoefu zaidi. Sio watu wote wanahitajika kusoma elimu rasmi. Mtu anaweza kukaa na fundi na baada ya muda awe fundi. Mara nyingi ufundi hauhitaji cheti kama huna mpango wa kuajiriwa. Wangapi wanatengeneza simu na hawakumaliza shule ya msingi? Lini tumewauliza cheti? Je baadhi yao hawajajenga nyumba zao binafsi za kuishi kabla ya wenye ajira zao rasmi?

·   Pata ujuzi zaidi wa shughuli yako Mf mama wa nyumbani anaweza kujifunza kupika keki nzuri zaidi ya keki aliyozoea kupika. Hakuna shughuli ambayo haihitaji kuongezwa ujuzi. Lazima kuangalia mahitaji ya soko na kuwa tayari kujifunza ujuzi mpya. Lakini pia upendo wa familia utakua kama mapishi nyumbani yanakuwa kiubinifu zaidi badala ya kupika mtindo uleule kwa miaka mingi.

·    Kuna njia tatu za kupata ujuzi:

o  Kusoma – chagua kifungu na soma kwa sauti (sio kimyakimya).

o  Kusikiliza – sikiliza mafundisho, masomo yaliyorikodiwa nk

o  Kutazama (observing) – mtazame mtu anayefanya jambo linaloweza kuboresha maisha yako.

·    Kuna mambo 3 yanayoathiri sana maisha yako: vitabu unavyosoma, jumbe unazosikiliza na watu unaokutana nao.

3. Badilisha kazi

Hukuandikiwa kufanya kazi unayoifanya maisha yako yote wala hukuzaliwa nayo. Kuna watu tu waliokutangulia walikufundisha au ulijikuta umechaguliwa na taasisi za elimu kuisomea. Hata hivyo kama kazi hiyo itakulazimu kutoka kijijini kwenda mjini, unatakiwa kuwa mwangalifu. Mshahara wa sh 500,000 Dar unaweza kuwa sawa na mshahara wa sh 100,000 kijijini kutokana na tofauti ya gharama za maisha. Kubadilisha kazi kunaweza kusaidia kama kuna marupurupu mbalimbali au kama hakuna gharama za ziada kv usafiri. Kwa hiyo lazima kuzingatia masuala mbalimbali kabla ya kuhamia mahali kwa ajili ya ajira au biashara. Vinginevyo pesa zitaishia kwenye nauli au kodi kubwa ya pango.

4. Anzisha shughuli yako mwenyewe

·  Shughuli yenye mafanikio ni ile ambayo imeanza na kitu unachokipenda (hobby). Shughuli yako mwenyewe inaweza kuongeza kipato chako.

·    Faida za shughuli yako binafsi

o   Unapata faida yote badala ya kumegewa na bosi.

o   Unaweza kuamua muda wa kufanya kazi, wa kupumzika na wa ibada.

o   Unaweza kuvaa nguo yako yoyote kazini.

o   Huwi na hofu ya kuachishwa kazi na bosi wako. Unakuwa bosi wewe mwenyewe.

o   Unaweza kuamua hata kwenda na mbwa wako kazini (kulingana na mazingira ya eneo husika). Kwa kifupi unakuwa na uhuru mkubwa zaidi.

5. Pangilia raslimali zako

Kama una raslimali ambazo hazitumiki ni bora kuziuza ili upate pesa za kuwekeza.

Mfano, kama una TV mbili na moja huitumii. Au una magari mawili na moja unalitumia mara chache sana. Kwa nini usiamue kubadili chombo kimoja kiwe pesa badala ya kutafuta mkopo wa riba ya muda mrefu? Chunguza raslimali ulizo nazo ambazo hazikusaidii kwa sasa ila zinakutambulisha tu kwa wageni kwamba una uwezo wa kiuchumi wakati hunufaiki nazo.

6. Ongeza kasi ya kulipa deni lako

Kama ulikopa lazima kila pesa unayoipata uimege kwa ajili ya kupunguza deni. Watu wengi wana mapango wa kukopa lakini hawana mpango wa kupunguza madeni. Matokeo yake wanapoteza kuaminika na mwisho hawakopesheki tena. Ukimaliza deni mapema utaweza kuendelea na uwekezaji. Usipende kuwa mtumwa wa madeni wakati tayari umeshapata mtaji wa kutosha kuzungusha katika biashara yako!

Riba unayolipa kwa kukopa ungeiepuka kama ungeweka akiba ndipo ugharamie kitu unachohitaji. Ukitaka kushinda roho ya kukopa ni kuwa na subira. Kukopa sio dhambi lakini kopa kwa sababu za lazima baada ya kushindikana kwa njia zingine zote. Usizoee kukopa kama mtindo wa maisha maana Biblia inasema kukopa ni utumwa. Mithali 22:7 “Tajiri humtawala maskini, Naye akopaye ni mtumwa wake akopeshaye.”

7. Geuza ongezeko liwe uwekezaji

Mara nyingi ongezeko la mshahara na faida halitumiki vizuri. Kuna watu hawawezi kugundua kama Mungu amewabariki kwa vile pesa zikiongezeka, wanaongeza matumizi. Kama pesa itaongezeka halafu matumizi yabaki vilevile, unaweza kutumia ongezeko hilo kwa ajili ya akiba au uwekezaji wa muda mrefu. Hebu jiulize tangu uongezewe mshahara au faida iongezeke, umefanya nini kinachoonekana nyumbani kwako! Kama hakuna, huu ujumbe umekuja kwa ajili yako.

8. Jipatie kipato cha ziada 

Pamoja na kazi au shughuli yako ya sasa unaweza kufanya kazi nyingine ya ziada kv kufundisha tuisheni baada ya muda wa kazi, kuuza magazeti, kuwa mlezi wa watoto nk

Ili mradi kutafuta kwako pesa kusiwe mbadala wa muda wa mahusiano na Mungu au na familia. Kuna watu wameamua kutafuta pesa kuliko mahusiano mpaka unajiuliza hizo pesa zina malengo gani kama imani inapotea na familia inabomoka kwa kutafuta pesa. Kuna baba alikuwa anajali pesa kuliko mahusiano. Hivyo anaposafiri anatuma pesa nyingi nyumbani akidhani ni mbadala wa mahusiano. Siku moja mke wake akamwambia nashukuru kwa pesa zako lakini nataka ujue kwamba sikuolewa na pesa zako!

9. Epuka gharama zisizo za lazima

·    Piga simu zisizo za lazima muda wa usiku.

·    Hakikisha bomba halivuji maji.

·    Tumia balbu za watts ndogo kama sio chumba cha kusomea au bulb za energy saver. Taa za mshumaa zinakula umeme robo ya ulaji wa balbu.

·    Nunua vitu vizuri vilivyotumika badala ya vipya ili mradi uzingatie ubora wake.

·    Piga pasi nguo nyingi kwa mara moja na ikibaki nguo ya mwisho zima umeme.

·    Usiache vyombo vya umeme vimechomekwa kwenye soketi au havijazimwa. 

Nimependa kukupa ushauri huu kwa vile hatukuagizwa kufundisha na kuhubiri peke yake. Kuna wakati tunatakiwa kuwashauri watu ili wawe na matumizi ya lazima na hatimaye matokeo yaonekane. Tito 3:14 “Watu wetu nao wajifunze kudumu katika matendo mema, kwa matumizi yaliyo lazima, ili wasiwe hawana matunda.”

Nakuombea Mungu akusaidie ili maendeleo yako yawe dhahiri kwa watu wote. 1 Timotheo 4:15 “Uyatafakari hayo; ukae katika hayo; ili kuendelea kwako kuwe dhahiri kwa watu wote.” Mungu ameahidi kwamba majirani zetu watatuita wabarikiwa. Mal 3:12 “Na mataifa yote watawaiteni heri; maana mtakuwa nchi ya kupendeza sana, asema Bwana wa majeshi.”

Leo sijazungumzia sana utoaji kwa vile zipo makala nyingi ambazo nimezungumzia utoaji kwenye ukurasa huu wa VLM. Na nimegundua wapo watu ambao wamebarikiwa baada ya kuwa watoaji wazuri lakini baraka zao hazionekani kwa vile si waangalifu katika mtindo wao wa maisha.

Unapochukua hatua kupitia masomo haya na ukaona matokeo usisite kunipa ushuhuda ili tumshukuru Mungu pamoja. Kuna wakati wa kuombewa, wa kujifunza na wa kushuhudia matendo makuu ya Mungu.

Ubarikiwe!

Dr Lawi Mshana, +255712924234, Tanzania