MTU ANAWEZA KUMILIKI PESA NA VITU NA AWE BADO HAJABARIKIWA
Nimepata msukumo wa kuandika ujumbe kwamba MTU ANAWEZA KUMILIKI PESA NA VITU VYA THAMANI NA AWE BADO HAJABARIKIWA
Sio wakati wote mtu anayeishi na laana anakuwa hana kitu. Kuna wakati mtu anakuwa na mali lakini bado yuko katika laana. Kimsingi, KUBARIKIWA SIO KUMILIKI PEKE YAKE, BALI NI KUFURAHIA UNACHOKIMILIKI! Mithali 10:22 ‘Baraka ya Bwana hutajirisha, Wala hachanganyi huzuni nayo.’ Ikiwa mtu anaonekana kwa nje kwamba amebarikiwa lakini bado ana huzuni, majuto, masononeko na simanzi bado hajapokewa baraka kutoka kwa Bwana. Ndiyo sababu tuna watu wengi wenye ‘happiness’ lakini hawana ‘joy’.
Happiness ni furaha unayoipata kutokana na matukio au mazingira fulani. Kwa kifupi unakuwa na happiness wakati tu mambo yakikuendea vizuri. Mhu 2:10 “Wala sikuyanyima macho yangu cho chote yalichokitamani; wala sikuuzuia moyo wangu katika furaha yo yote; maana moyo wangu ulifurahi kwa sababu ya kazi yangu yote, na hii ilikuwa sehemu yangu katika kazi yangu yote.”
Lakini joy ni furaha ya ndani inayokufanya uwe radhi na ulivyo navyo. Huna haja ya kushindana na dunia. Unaangalia Mungu amekupangia nini na kuishi katika mapenzi yake. Wafilipi 4:11 “Si kwamba nasema haya kwa kuwa nina mahitaji; maana nimejifunza kuwa radhi na hali yo yote niliyo nayo.” Waebrania 13:5 “Msiwe na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa.” Mtu anaweza kukufanyia jambo baya na lisikuumize bali uone kusudi la Mungu ndani yake. Mwanzo 50:20 “Nanyi kweli mlinikusudia mabaya, bali Mungu aliyakusudia kuwa mema, ili itokee kuokoa taifa kubwa, kama ilivyo leo.” Mtu mwenye JOY hawezi kusema amebarikiwa lakini hamfanyii Yesu chochote, hawi baraka kwa wengine na yeye mwenyewe anaishi kwa majonzi. JOY ni kifupi cha Jesus (Yesu), Others (Wengine) na You (Wewe).
Ngoja nikuonyeshe mifano michache ya watu wanaoonekana kwa nje wana baraka ila wako chini ya laana:
Kabla sijakuonyesha napenda ufahamu kwamba mtu anaweza kupata laana kutoka kwa Mungu, kwa wazazi wake, kwa wachawi au kutokana na dhambi zake mwenyewe.
1. Mtu ameoa mke mrembo au ameolewa na mume mtanashati lakini anatembea na watu wengine. Kum 28:30a “Utaposa mke na mume mwingine atalala naye”. Mke au mume anaitwa wa kwako kwa jina lakini wanaofaidika ni wengine. Anatamini muda mwingi awe mbali nawe au nyumba yako. Akitoka kazini au safari hakai. Anaweza kufika tu na kutoka au kutuma mtu alete begi yeye apitie mahali aje usiku wa manane.
2. Mtu anaanzisha miradi lakini faida inakwenda kwa wengine yeye anabaki tu na heshima kwamba mradi ni wa kwake. Kum 28:30 “….utajenga nyumba usiikae; utapanda mizabibu usitumie matunda yake.” Unapata kabisa pesa za kujengea nyumba na kupata mazao shambani, kazini au katika biashara lakini huwezi kunufaika na jasho lako. Kila unayemuweka akusaidie anajinufaisha na kukusahau wewe mmiliki.
3. Mtu anadhulumiwa haki zake bila kupata mtetezi. Kum 28:31,33 “Ng'ombe wako atachinjwa mbele ya macho yako, usile nyama yake; utanyang'anywa punda wako mbele ya uso wako kwa jeuri, usirudishiwe; kondoo zako watapewa adui zako, usipate mtu wa kukuokoa. Matunda ya nchi yako, na taabu yako yote, vitaliwa na taifa usilolijua; utaonewa tu, na kupondwa chini daima;” Utalaumu sana serikali, hakimu, bosi, mchungaji, shehe, nk lakini ni laana inayokufanya ukose mtetezi. Usije ukashangaa ukinunua kitu dukani, mwenye duka akakataa pia kukurudishia chenji akisema nilishakurudishia.
4. Mtu amezaa au kulea watoto wakapata kazi na mafanikio lakini hawamkumbuki tena au hawaolewi/hawaoi/hawazai. Wako tayari wachangie arusi ya mtu sh 200,000 lakini kumtumia mzazi sh 10,000 inashindikana. Tatizo hili haliko kwao zaidi bali liko kwako. Usiongeze laana nyingine kwa kuwatamkia mabaya. Kum 28:32,41 “Wanao na binti zako litapewa taifa lingine, na macho yako yataangalia, na kuzimia kwa kuwatamani mchana kutwa; wala hapatakuwa na kitu katika uwezo wa mkono wako. Utazaa wana na binti, lakini hawatakuwa wako wewe; kwa sababu watakwenda utumwani.”
5. Mtu anapata mshahara mzuri na faida kubwa lakini wageni wanaomkuta wanainuka kiuchumi wakati yeye hafanyi cha maana zaidi ya kuwaonea wivu na kuwaita Freemason. Anasahau kwamba Yesu ni zaidi ya Freemason maana fedha na dhahabu ni mali yake. Kum 28:43 “Mgeni aliye kati yako atazidi kupaa juu yako; nawe utazidi kushuka chini. Yeye atakukopesha, wala wewe usimkopeshe; yeye atakuwa ni kichwa, wewe utakuwa mkia.”
Tafuta karatasi uchore mstari katikati kuanzia juu. Upande mmoja andika mambo ambayo wewe ni kichwa hapo ulipo na upande mwingine andika mambo ambayo wewe ni mkia hapo ulipo. Ukiwa mkweli kabisa utashangaa na utaanza maombi kiupya. Usijifariji kwa kuwa tu na Yesu bali mtumie amalize matatizo yako. Ilikuwa kidogo tu wanafunzi wa Yesu wazame ingawa walikuwa na Yesu kwenye mashua. Na nataka nikwambie kama wangezama Yesu angeondoka zake awaache maiti zikiwa zinaelea. Ila walishtuka wakamuamsha. Lk 8:23,24 “Nao walipokuwa wakienda, alilala usingizi. Ikashuka tufani juu ya ziwa, chombo kikaanza kujaa maji, wakawa katika hatari. Wakamwendea, wakamwamsha, wakisema, Bwana mkubwa, Bwana mkubwa, tunaangamia. Akaamka, akaukemea upepo na msukosuko wa maji, vikakoma; kukawa shwari.”
Wewe ambaye Mungu amekuona unayopitia mpaka akanipa ujumbe huu leo, NAVUNJA LAANA ZOTE ZINAZOKUFUTAILIA KATIKA MAISHA YAKO NA UKOO WAKO KATIKA DAMU YA YESU KRISTO. MUNGU AKUJALIE KUTAMBUA CHIMBUKO LA MATATIZO YAKO NA KUKUWEZESHA KUCHUKUA HATUA YA IMANI ILI UFIKIE HATIMA YAKO ULIYOPANGIWA NA MUNGU. BWANA YESU AKUGUSE NA KUPONYA KILA ENEO KATIKA MAISHA YAKO!
Dr Lawi Mshana, +255712924234; Korogwe, Tanga, Tanzania