Ticker

6/recent/ticker-posts

Kwanini imani yetu haileti pesa?

KWANINI IMANI YETU HAILETI PESA? 

Limekuwa ni jambo la kawaida kuwaona watu wanaomcha Mungu au wanaomtumikia Mungu wakiwa masikini. Jambo hili sio tu kwamba linawazuia wengine kumgeukia Bwana bali pia linawapa maswali mengi waumini waaminifu. Ukisoma vizuri maandiko utaona kwamba imani haiwezi kujulikana kwa maneno bali kwa matendo. Yk 2:15-17 “Ikiwa ndugu mwanamume au ndugu mwanamke yu uchi na kupungukiwa na riziki, na mtu wa kwenu akawaambia, Enendeni zenu kwa amani, mkaote moto na kushiba, lakini asiwape mahitaji ya mwili, yafaa nini? Vivyo hivyo na imani, isipokuwa ina matendo, imekufa nafsini mwake.” Yakobo anahoji kwamba inawezekanaje mtu mwenye njaa amuendee mtu wa Mungu halafu badala ya kumsaidia yeye anamuombea tu na kumpa maneno ambayo hayana msaada wowote kv ubarikiwe na Bwana nk. Sikatai haya maneno lakini kuna wakati tunayatumia kwa kukwepa wajibu wetu. Yakobo aliendelea kusema kwamba kama imani yetu ni ya maneno tu hata shetani anatuzidi kwa vile sio tu kwamba anaamini kwamba Mungu yupo bali pia anatetemeka. Yak 2:19 “Wewe waamini ya kuwa Mungu ni mmoja; watenda vema. Mashetani nao waamini na kutetemeka.” Shetani anaamini na kutetemeka lakini hana matendo yanayothibitisha imani yake. Lazima sisi tumzidi shetani kwa kuwa na imani yenye matendo (imani itendayo kazi). Lazima tutende matendo yanayoendana na kutubu kwetu. Mdo 26:20 “bali kwanza niliwahubiri wale wa Dameski na Yerusalemu, na katika nchi yote ya Uyahudi, na watu wa Mataifa, kwamba watubu na kumwelekea Mungu, wakiyatenda matendo yanayopatana na kutubu kwao.” 

Napenda tujikosoe kwa kutumia kanuni zinazopatikana kwenye andiko la Mathayo 17:18-27. 

1. Hatuhoji kushindwa kwetu 

Mst 18,19 “Yesu akamkemea pepo, naye akamtoka; yule kijana akapona tangu saa ile. Kisha wale wanafunzi wakamwendea Yesu kwa faragha wakasema Mbona sisi hatukuweza kumtoa?” Ukisoma mistari iliyotangulia utaona kwamba wanafunzi wa Yesu waliletewa mtu mwenye pepo wakashindwa kumponya. Mst 15,16 “Bwana, umrehemu mwanangu, kwa kuwa ana kifafa, na kuteswa vibaya; maana mara nyingi huanguka motoni, na mara nyingi majini. Nikamleta kwa wanafunzi wako, wasiweze kumponya.” Lakini mtu huyo alipoletwa kwa Yesu pepo akatoka na kijana akapona tangu saa hiyo. Wanafunzi wa Yesu hawakuridhika kushabikia huduma ya Yesu bali wakamwendea Yesu kwa faragha (wakiwa peke yao na Yesu) ili wamuulize kwa nini wao walishindwa na Yeye akaweza. Waumini wengi wameridhika na maisha ya kubangaiza bila kuchukua hatua za kuuliza KWANINI hali hiyo haifikii mwisho wake. Ukiona maombi hayajibiwi lazima ubadilishe na kuuliza kwa nini. Unapoona mtu ukimpigia simu hapokei lazima ujiulize kwa nini na sio kuendelea tu kumpigia. Bila kutafuta faragha na Mungu utaendelea kufeli maisha bila huruma. Kwanini wenzako wanatoka lakini wewe hutoki. Usijifariji kwa kuwazushia mabaya. Chukua hatua ya kujihoji kibinafsi na kujua sababu halisi.

2. Hatuna maombi yenye imani ing’oayo milima 

Mst 20,21 “Yesu akawaambia, Kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Kwa maana, amin, nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu. Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.” Bwana Yesu ni mwaminifu. Walipomuuliza kwa faragha aliwapa jibu. Aliwaambia tatizo lao liko kwenye eneo la imani na sio katika maombi. Watu wengi wana maombi mengi lakini hayana imani ndani yake. Kuna muda wa kumuomba Mungu atende na muda wa kutumia imani na mamlaka tuliyopewa. Ukishamuomba Mungu akakupa mamlaka unatakiwa wewe ndiye useme na milima iliyoko mbele yako. Yesu alisema kwamba mkiwa na imani MTAUAMBIA MLIMA HUU na hakusema mtamuomba Mungu auondoe mlima. Polisi wa usalama barabarani (traffic police) akishapewa mamlaka (kitambulisho, mavazi na silaha) hahitaji kupiga simu kwa kamanda mkuu wa polisi ili ampe kibali cha kusimamisha gari. Anatumia mamlaka yake na dereva atasimamisha gari tu. Tatizo jingine lililopo ni kwamba watu wengi hawafanyi maombi ya kufunga mara kwa mara. Wengine badala ya kufunga na kuomba wanafunga na kushinda njaa maana badala ya kuomba wanasoma magazeti na kuangalia tamthilia. Unapofunga na kupata muda wa kutosha na Mungu, imani inaongezeka na unapata maelekezo zaidi ya namna ya kumkabili adui. TUNAMUOMBA MUNGU LAKINI HATUSEMI NA MILIMA. Lazima tuseme na roho za umasikini, kupungukiwa na madeni na kuzihamisha kabisa zisiwepo katika maeneo yetu. 

3. Tunapenda mafanikio bila gharama 

Mst 22,23 “Nao walipokuwa wakikaa Galilaya, Yesu akawaambia, Mwana wa Adamu anakwenda kutiwa katika mikono ya watu, nao watamwua, na siku ya tatu atafufuka. Wakasikitika sana.” Yesu alipowaambia wanafunzi wake kwamba atauawa na siku ya tatu atafufuka, wakasikitika badala ya kufurahi. Kimsingi Yesu alikuwa anawaambia ninakwenda kupambana na shetani mpaka nimnyang’anye funguo za kuzimu na mauti. Lakini pia lazima tufahamu kwamba mbegu ikipandwa ardhini haiwezi kuhuika isipokufa kwanza. 1 Wakorintho 15:36 “Ewe mpumbavu! Uipandayo haihuiki, isipokufa.” Ilimlazimu Yesu kufa ili achipue na kuzaa mbegu nyingi zaidi yaani azae watumishi wengi zaidi. Kinyume chake wanafunzi wake waliwaza tu kwamba watam-miss sana. Hakuna mafanikio yanayokuja bila gharama. Wengi waliofanikiwa leo walilipa gharama kubwa kwa kubana matumizi, kufanya kazi za kudharaulika, kusoma mpaka wakaingiza miguu kwenye ndoo za maji baridi ili tu wasipate usingizi nk. Sio mafanikio yote yanahitaji usome sekondari lakini unapopata pesa lazima uwaze kujiongeza kwa kusafiri na kushiriki semina na kozi fupifupi za shughuli unayoifanya. Huwezi kujua unakwenda mbele, umesimama au unarudi nyuma kama hutapenda kuingia gharama ya kujifunza au kuwatumia wataalamu wakukague na kukushauri. 

4. Tunakwepa majukumu yetu 

Mst 24-26 “Hata walipofika Kapernaumu, wale watozao nusu-shekeli walimwendea Petro, wakasema, Je! Mwalimu wenu hatoi nusu-shekeli? Akasema, Hutoa. Naye alipoingia nyumbani, Yesu alitangulia kumwuliza, akisema, Waonaje, Simoni? Wafalme wa dunia hutwaa kodi ama ushuru kwa watu gani? Kwa wana wao au kwa wageni? Naye aliposema, Kwa wageni, Yesu alimwambia, Basi, kama ni hivyo, wana ni mahuru.” Bwana Yesu hakukwepa kulipa kodi. Lakini kwa mtu wa Mungu kodi sio ile tu ya serikali ya hapa duniani bali pia kodi ya serikali ya Mungu. Kimsingi mtu wa Mungu ana uraia wa aina mbili (dual citizenship). Uraia wa nchi yake na uraia wa mbinguni. Waefeso 2:19 “Basi tangu sasa ninyi si wageni wala wapitaji, bali ninyi ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa nyumbani mwake Mungu.” Kama tunataka mafanikio ya uchumi wa serikali ya Mungu tunatakiwa kuishi kwa kanuni za ufalme wake. Tunatakiwa kutoa sehemu ya kumi (10%) ya mapato yetu, malimbuko na kuchangia kazi ya Mungu katika maeneo mbalimbali. Tusipomjali Mungu, kile tunachokipata hatutakifurahia au hakitatosha kwa mahitaji yetu. Kumbuka ni Mungu anatuepusha na majanga mengi na kutuponya magonjwa. Hagai 1:4-6 “Je! Huu ndio wakati wa ninyi kukaa katika nyumba zenye mapambo ya mbao, iwapo nyumba hii inakaa hali ya kuharibika? Basi sasa, Bwana wa majeshi asema hivi, Zitafakarini njia zenu.Mmepanda mbegu nyingi mkavuna kidogo; mnakula lakini hamshibi; mnakunywa lakini hamkujazwa na vinywaji; mnajivika nguo lakini hapana aonaye moto; na yeye apataye mshahara apata mshahara ili kuutia katika mfuko uliotoboka-toboka.” 

5. Hatutumii ujuzi na vitu tulivyo navyo kiufunuo 

Mst 27a “Lakini tusije tukawakwaza, enenda baharini ukatupe ndoana…” Bwana Yesu hakushindwa kuagiza pesa zije kimiujiza. Shetani ndiye anapenda kufanya mazingaumbwe kv kubadili anjifu iwe yai. Yesu alijua Petro ana taaluma ya uvuvi na ana ndoana. Alichohitaji Petro ni ufunuo tu wa kujua lini aende na itakuwaje akishavua hao samaki. Musa alipoonyesha mashaka kuhusu utume wake aliambiwa na Mungu, Una nini mkononi mwako. MUNGU ANATUMIA ULICHO NACHO KWA AJILI YA KUKUPA USICHOKUWA NACHO. Mara zote nilipomuomba Mungu anibariki aliutumia ujuzi nilio nao kv uandishi wa vitabu, kutafsiri vitabu, kutoa mafunzo kwa jamii kv kompyuta, UKIMWI, lugha nk. Lakini pia nimekuwa tayari kujifunza mambo mapya ili nifae kutumiwa zaidi. Lazima tujitambue kwamba tuna thamani kuliko pesa tunazozitafuta. Wakati mwingine unaomba Mungu akubariki lakini unayo ndoana tayari. Huna pesa lakini unakaa peke yako nyumba ya vyumba 6. Ungeweza kuvitumia vyumba visivyotumika kukuongezea kipato. 

6. Hatujui watu wenye baraka zetu 

Mst 27a “.,..ukatwae samaki yule azukaye kwanza.” Bwana Yesu alimuelekeza Petro kwamba baraka zipo kwa samaki yule atakayezuka kwanza. Kama Petro hangejua nani ameandaliwa kwa ajili yake angehangaika kuwapekua samaki wote aliowavua. Wapo watu wengi matajiri lakini sio lazima wawe na pesa zako. Wana pesa kwa ajili yao wenyewe na kwa ajili ya watu wengine. Muombe Mungu akujalie kumtambua mtu mwenye baraka zako badala ya kutaka kila mtu aguswe kukusaidia. Tangu Mungu anipe ufunuo huu nimekuwa silazimishi waumini wachangie kiasi kinacholingana. Matokeo yake samaki mmoja au wachache wanaweza wao wenyewe kuchangia kiasi chote kinachohitajika. 

7. Hatujui jinsi ya kuvuta pesa 

Mst 27b “…ukifumbua mdomo wake utaona shekeli ichukue hiyo…” Bwana Yesu hakumwambia Petro kwamba samaki huyo azukaye kwanza atatema au kutapika shekeli. Alimwambia ukifumbua mdomo wake utaona shekel ichukue hiyo. Mtu anaweza kuwa na pesa zako na bado asikupe. Mpaka pesa itoke ni lazima ujue jinsi ya kusababisha itoke. Kuna tofauti kati ya KUTOA MATANGAZO YA KUOMBA MSAADA na KUHAMASISHA WATU WACHANGIE. Hata hivyo sio vizuri kutumia udanganyifu na ujanja katika kuwafanya watu watoe pesa. Ila ni muhimu maono yaeleweke ili kumfanya mtu avutiwe kuchangia. Habakuki 2:2 “Bwana akanijibu, akasema, Iandike njozi ukaifanye iwe wazi sana katika vibao, ili aisomaye apate kuisoma kama maji.” Watu hawahitaji kujua uliota nini usiku. Wanahitaji kujua maana yake na faida yake katika ufalme wa Mungu na katika maisha yao. Usiwaambie watu mambo ambayo ni SIRI wape UFUNUO. Mambo ambayo yamefichika sio kwa ajili yetu bali ni kwa ajili ya Mungu mwenyewe. Kum 29:29 “Mambo ya siri ni ya Bwana, Mungu wetu; lakini mambo yaliyofunuliwa ni yetu sisi na watoto wetu milele, ili tuyafanye maneno yote ya sheria hii.” 

8. Tunatumia pesa za Mungu kwa matumizi yetu binafsi 

Mst 27b “…..ukawape kwa ajili yangu na kwa ajili yako.” Bwana Yesu aliweka wazi lengo la pesa hizo kwamba ni kwa ajili ya kulipa kodi yake na ya Petro. Hakushindwa kusababisha zipatikane shekeli 10. Ni muhimu sana kujua pesa ulizopewa ni za nini na kuzitumia kwa matumizi husika. Unapotumia pesa za Mungu kwa matumizi binafsi unaingiza laana kwenye nyumba yako. Mfano waumini wamechangia pesa za ujenzi wa kanisa halafu wewe unazitumia kujengea nyumba yako binafsi. Hata kama utakaa kwenye nyumba hiyo ikiwa ni nzuri sana, utaishi maisha ya laana, mikosi na hasara nyingi kiasi kwamba hutaifurahia nyumba hiyo. Wanaokuona watadhani una raha sana lakini mwenyewe utakuwa unajua jinsi unavyopata shida. Mtu aliyelaaniwa hawezi kufurahia wala kufaidi alicho nacho. Kumbukumbu la Torati 28:30 “Utaposa mke na mume mwingine atalala naye; utajenga nyumba usiikae; utapanda mizabibu usitumie matunda yake.” 

MAOMBI YANGU KWA AJILI YAKO: 

Naomba Mungu akupe maombi yenye imani ing’oayo milima, ujue baraka zako zilipo na jinsi ya kuzipata na utumie pesa unazopata kwa utukufu wa Mungu. 

Dr Lawi Mshana, +255712924234; Korogwe, Tanga, Tanzania