KWA NINI INAKUWA VIGUMU LEO KUPATA MKE/MUME SAHIHI (SEHEMU YA TATU)
Vijana wa kike na wa kiume wanakuwa na wakati mgumu sana kipindi hiki katika kupata mwenzi sahihi wa maisha. Wengine wanaomba Mungu awape mchumba badala ya mwenzi wa maisha. Matokeo yake wanachumbiana kila kukicha bila kufikia ndoa takatifu. Uchumba ni mchakato tu kuelekea kwenye ndoa kamili. Mungu hajaahidi popote kwamba atakupatia mchumba mwema bali mume au mke mwema.
Nitatumia ndoa ya Isaka na Rebeka ilivyokuwa tangu uchumba hadi ndoa. Hata hivyo ninapozungumzia MWENZI SAHIHI sina maana ya MWENZI MKAMILIFU. Bado mwanadamu ana mapungufu yake ambayo yanaweza kutumiwa kama fursa za kuhitajiana. Mungu anaunganisha watu ili wakamilishane (complement each other).
Nimepata msukumo wa kuisoma Mwanzo 24 kiufunuo ili kukupa kanuni za msingi za kukusaidia. Sio lazima zimfae kila mtu. Bado wapo wenye maisha mazuri bila kanuni hizi zote. Huu ni mwongozo tu kwa wacha Mungu (wanaomhofu Mungu kuliko kufuata tamaa zao za mwili na wanaojua kuna siku tutatoa hesabu ya matendo yetu mbele za Mungu).
NB: HII NI SEHEMU YA TATU. FUATILIA SOMO LA KWANZA (NA 1-5) NA SOMO LA PILI (NA 6-10)
Sababu za ugumu wa kupata mwenzi sahihi:
11. Kuandaa sherehe za kulisha watu bila kutoa shukrani kwa Mungu
Mst 26,27 “Yule mtu akainama akamsujudu
Bwana. Akasema, Na atukuzwe Bwana, Mungu wa bwana wangu Ibrahimu, ambaye
hakuacha rehema zake na kweli yake kwa bwana wangu. Bwana akaniongoza mimi nami
njiani hata nyumba ya nduguze bwana wangu.”
Vijana wengi wakishaona Mungu amewakumbuka na kuwapa mwenzi wa maisha wanasahau waliomba nini. Hawamtolei Mungu chochote kama shukrani kwa matendo yake makuu. Wanaanza tu mikakati ya sherehe za kifahari ili wafurahi na ndugu zao na marafiki zao. Huyu mtumishi wa Ibrahimu kabla hata hajawaona wazazi wa Rebeka akamsujudia Bwana kwa kumuongoza na kumfanikisha katika safari yake. Kwa vile hakuna shukrani wala maombi wakati mwingine shetani anavamia uchumba huo na kuupeperusha. Wengine hata hawana wapendwa waaminifu wa kuomba nao katika kila hatua. Shetani hafurahii kuona mtu anapata mwenzi kutoka kwa Bwana maana anataka kuvuruga maisha ya watu. Tangu shetani aivuruge ndoa ya kwanza pale bustani ya Edeni, hajajiuzulu. Mithali 19:14 “Nyumba na mali ni urithi apatao mtu kwa babaye; Bali mke mwenye busara, mtu hupewa na Bwana.” Jihoji mwenyewe kama unataka KUOKOTA/KUOKOTWA au KUOA/KUOLEWA. Wewe ni wa thamani sana machoni pa Mungu. Ili ujue kuna vita kali hata ndani ya ndoa, siku moja mtu wa Mungu alikuwa anasafiri kwa ndege. Akaona jirani yake akiomba kwa uzito. Hivyo akamuomba washirikiane maombi. Huyo jirani yake akamwambia, ‘Mimi ni muabudu shetani (satanist) na leo ni siku ya kuombea ndoa za Wakristo zivunjike.’ Lazima tujue kwamba kuna vita vikali sana katika mchakato wa kuoa na kuolewa pamoja na ndani ya ndoa.
12. Kutotafuta kibali cha ndugu
Mst 28-33, 49-54 “Basi yule msichana akapiga mbio, akawaambia watu wa nyumba ya mama yake mambo hayo. Na Rebeka alikuwa na kaka, jina lake Labani. Labani akatoka mbio kumwendea yule mtu kisimani. Ikawa, alipoiona ile pete, na vikuku mikononi mwa nduguye, akasikia maneno ya Rebeka nduguye, akisema, Hivyo ndivyo alivyoniambia mtu huyo, basi akamjia mtu yule, na tazama, amesimama karibu na ngamia kisimani. Akasema, Karibu, wewe uliyebarikiwa na Bwana, mbona unasimama nje? Kwa maana nimeiweka nyumba tayari, na nafasi kwa ngamia. Na mtu yule akaingia katika nyumba, akawafungua ngamia; naye akatoa majani na malisho kwa ngamia, na maji ya kuoshea miguu yake, na miguu ya watu waliokuwa pamoja naye. Akaandaliwa chakula, lakini akasema, Sili mpaka niseme kwanza maneno yangu. Akamwambia, Haya, sema. Basi, kama mnataka kumfanyia rehema na kweli bwana wangu, niambieni kama sivyo, niambieni; ili nigeuke upande wa kuume au wa kushoto. Ndipo Labani na Bethueli wakajibu wakasema, Neno hili limetoka kwa Bwana, wala sisi hatuwezi kukuambia neno jema wala baya. Tazama, huyo Rebeka yuko mbele yako, umchukue, ukaende zako awe mke wa mwana wa bwana wako, kama alivyosema Bwana. Ikawa mtumishi wa Ibrahimu aliposikia maneno yao, akainama hata nchi mbele za Bwana. Kisha huyo mtumishi akatoa vyombo vya fedha, na vyombo vya dhahabu, na mavazi, akampa Rebeka; na vitu vya thamani akampa nduguye na mamaye pia. Wakala wakanywa, yeye na watu waliokuwa pamoja naye, nao wakakaa usiku. Wakaondoka asubuhi, naye akasema, Nipeni ruhusa niende kwa bwana wangu.”
Ni raha sana kupata kibali kwa ndugu wa mume wako au mke wako. Hata Labani kaka yake Rebeka akamlaki Eliezeri na kumkaribisha nyumbani kwa ukarimu mkubwa na kuihudumia mifugo yake. Tena akamtambua kwamba ni mtumishi wa Mungu. Hizi ni ishara kwamba Mungu amekubali uhusiano huu. Nilipotaka kuoa mmojawapo kati ya wasichana ambao wako karibu nami nilipata vikwazo sana. Lakini nilipopata yule ambaye ni chaguo la Bwana ingawa alitoka umbali wa nauli ya shilingi laki 2, nilipata pesa hiyo bila kukopa na kuweza kulipa mahari yote bila kudaiwa. Kumbuka usipomaliza mahari mizimu ya ukoo itawafuatilia na hamtaenda mbinguni. Ni rahisi kupata gari kama Mungu amekuahidi kuliko kupata baiskeli ambayo Mungu hajakuahidi. Hata katika maisha ya kawaida haiwezekani kuimarisha mahusiano bila vizawadi vya hapa na pale. Haingekuwa busara kwa mtu tajiri aliyekuja na ngamia kumi kukosa zawadi (kwenda mikono mitupu). Hata Biblia inaonya kwenda kwa wakwe zako mikono mitupu. Ruthu 3:17 “Akasema, Na vipimo hivi sita vya shayiri amenipa; maana akaniambia, Usiende kwa mkweo mikono mitupu.” Ni aibu sana kumtembelea mtu ambaye hamjaonana naye kwa siku nyingi na pengine alifanyika baraka kwako wakati fulani halafu hata kazawadi huna. Mwingine umepaki kabisa gari ili usalimie halafu unaondoka na kupungia watoto mikono bila aibu yoyote na bila kuwaachia chochote. Unakuwa kama uliyekuja kujionyesha tu kwamba umebarikiwa. Biblia inasema kama umepungukiwa hekima ukimuomba Mungu atakupatia. Yakobo 1:5 “Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu, awapaye wote, kwa ukarimu, wala hakemei; naye atapewa.”
13. Wazazi kukosa uelewa wa utendaji wa Mungu
Mst 55-58 “Ndugu yake na mama yake wakasema, Msichana na akae kwetu kama siku kumi, zisipungue, baadaye aende. Naye akawaambia, Msinikawilishe, mradi Bwana amefanikisha njia yangu; nipeni ruhusa niende kwa bwana wangu. Wakasema, Na tumwite huyo msichana, tumwulize mwenyewe. Wakamwita Rebeka wakamwuliza, Je! Utakwenda na mtu huyu? Akasema, Nitakwenda.”
Kuna wazazi wana mawazo ya kikoloni kiasi kwamba wanakwamisha vijana wao kuoa na kuolewa na mtu sahihi. Hawako tayari kubadilishwa walichokipanga utadhani wao ndio wanaenda kuishi naye. Utasikia mzazi anasema mpaka umalize shahada ya pili ndipo uoe. Wakati huohuo yeye alioa wakati hana kitu akafanya kujiendeleza kimasomo baadaye. Ndugu zake Rebeka walitaka akae zaidi ya siku kumi wamfunde vizuri maana imekuwa ni dharura sana. Lakini Eliezeri alipowasihi wakakubali na wakampa msichana fursa hadharani bila kumuita kwanza pembeni. Kwa vile lilikuwa ni hitaji kubwa la Rebeka hakusita kusema, ‘Nitakwenda’. Unapogundua ni wakati wa Bwana tii bila kutanguliza ubinadamu. Ukipishana na wakati wa Mungu utahaha sana. Kila jambo lina wakati wake katika kalenda ya Mungu kwa ajili ya maisha yako. Watu wengi ambao leo wanajuta kwa kutoolewa, walipochumbiwa walishindwa kusoma nyakati wakaiga maisha ya mtu mwingine. Kwa Mungu hakuna kuwahi wala kuchelewa. Mimi sikujali wachungaji wenzangu wameoa. Nilikuwa najiuliza jambo moja tu. Je Mungu uliponipa huduma hii kabla sijaoa ulikosa waliooa? Hivyo sikuona sababu ya kukimbilia kuoa ili tu nifanane nao. Nilijua wakati wake ukifika atanipa mke. Lakini pia ukoloni huu haupo kwa wazazi wa kimwili tu. Upo pia kwa viongozi wa dini. Kuna viongozi wa dini watadaiwa na kuhukumiwa kwa kusababisha waumini kuingia katika mahusiano yasiyo sahihi au kuwavurugia mahusiano sahihi. Hatupaswi kuchanganya hitaji la ndoa na mahitaji ya dini zetu. Ndoa za watu zisiwe kitega uchumi. Kama Mungu anampa mtu mwenzi wa mbali tusimzuie bali tumuachilie kwa amani.
14. Kutoachiliwa kwa baraka za wazazi
Mst 59,60 “Ndipo wakampeleka Rebeka ndugu yao, na yaya wake, na mtumishi wa Ibrahimu, na watu wake. Wakambarikia Rebeka, wakamwambia, Ndugu yetu, uwe wewe mama wa kumi elfu, mara elfu nyingi, na wazao wako waurithi mlango wa hao wawachukiao.”
Rebeka alifanyiwa ‘send-off’ ya baraka za kipekee. Sio lazima send off iwe sherehe kubwa ya madeni makubwa. Send off ya maana ni ibada yenye maneno ya baraka kutoka kwa wazazi wako. Kama una pesa lakini hujabarikiwa au kuachiliwa na wazazi unaweza usizifurahie hizo baraka. Lazima watu muhimu katika maisha yako wakutakie mema. Lakini pia inasaidia kuepuka maumivu yasiyo na sababu. Kuna vijana walikutana Dar wakaamua kuishi pamoja bila kutambulishana kwa wazazi. Siku moja wakaamua waanze kutembelea upande wa mke. Kilichotokea wakashangaa wameoana mtu na dada yake. Kumbuka waliamua kutembelea wazazi wakati wameshazaa mtoto tayari.
15. Kupenda kujuana sana kabla ya kuoana
Mst 63-65 “Isaka akatoka ili kutafakari kondeni wakati wa jioni; akainua macho yake, akaona, kuna ngamia wanakuja. Rebeka akainua macho, naye alipomwona Isaka, alishuka juu ya ngamia. Akamwambia mtumishi, Ni nani mtu huyu ajaye kondeni kutulaki? Mtumishi akasema, Huyu ndiye bwana wangu. Basi akatwaa shela yake akajifunika.”
Wachumba wanatakiwa kujuana kwa mambo ya msingi tu lakini wasiwe kama vile ni wanandoa. Rebeka alimkubali Isaka bila kumjua. Hata hivyo ni vigumu kuoa kwa njia hii kama mtu hamjui Mungu vizuri maana anaweza kuangukia pabaya zaidi. Asiyemjua Mungu anategemea zaidi kuchunguza tabia jambo ambalo ni gumu sana kwa vile tabia mbaya zinafichwa sana. Ndiyo maana nawashauri watu wa aina hii kwamba wajitahidi kugundua mwenzake akiwa amekasirika anaweza kujitawala kiasi gani. Lakini pia washirikishe watu kwa ajili ya uchunguzi kabla upendo haujazama sana moyoni. Kuna ndugu mmoja aliamua kumpima mwenzake kama atafaa kukabiliana na changamoto zake za kuchelewa kazini. Akapatana naye wakutane muda fulani halafu baadaye akampigia simu na kumwambia hataweza kuja kwa vile amepata dharura. Msichana alimtukana matusi ya ajabu mpaka yule ndugu akamshukuru Mungu kwa kuijua tabia yake mapema na kisha kuuvunja uchumba hapohapo.
Mimi sikuwa na fursa kubwa ya kumfahamu mke wangu mtarajiwa kwa jinsi ya kibinadamu kwa vile tulikuwa mbali sana. Tulitegemea zaidi msaada wa Mungu aliyeanzisha uhusiano wetu. Pamoja na hayo niliuliza baadhi wanaomjua pia wakanipa sifa nzuri kwa vile mtu mwenye tabia mbaya hata akiwa safarini ataendelea nazo. Na kweli Mungu amekuwa mwaminifu sana kwetu. Kuna bwana arusi alimjua sana mwenzake kiasi cha kutembea naye kabla ya ndoa. Matokeo yake siku ya sherehe ya ndoa yao akawa anawatamani waalikwa wa sherehe yao kwa vile mkewe aliyempewa hana jipya tena. Tujithamini ili ndoa iwe ya thamani.
16. Kutafuta kupendwa (kupokea upendo) badala ya kupenda (kutoa upendo)
Mst 67 “Isaka akamwingiza Rebeka katika hema ya mama yake, Sara, akamtwaa Rebeka, akawa mkewe, akampenda; Isaka akafarijika kwa ajili ya kufa kwa mamake.”
Rebeka aliweza kuziba pengo alilokuwa nalo Isaka alipofiwa na mama yake. Hata kama wazazi bado wako hai mnaweza kuwa wapweke kwa vile mnaanza maisha yenu. Muwe wanandoa mnaokamilishana na sio wanandoa wapweke (married singles). Mtu mwenye TAMAA anasema nitapata nini kwako, nitakufaidi vipi. Lakini mtu mwenye UPENDO anasema nitakufanyia nini, nitakusaidiaje, nitafanya nini ili ujisikie ninakuthamini. Hata hivyo ni jambo gumu sana kumuonyesha upendo mtu mpaka ajisikie kwamba unampenda. Unaweza kumpenda mtu lakini ashindwe kuhisi upendo wako kwake. Unahitaji kujua lugha ya upendo ya mwenzako ili usije ukalalamika tu kwamba mbona namfanyia mwenzangu kila kitu lakini hanipendi. Mungu akusaidie hata wewe ambaye tayari uko kwenye ndoa uwe faraja kwa mwenzako. Ajisikie kukamilishwa anapokuwa na wewe ili usibaki na cheti cha ndoa tu sandukuni wakati upendo umehamia mahali pengine.
Namuomba
Mungu akuongoze katika hatua zako zote ili uishi maisha uliyokusudiwa na Mungu.
Dkt Lawi Mshana, +255712924234, Korogwe, Tanga, Tanzania