Ticker

6/recent/ticker-posts

Kwanini inakuwa vigumu leo kupata mke/mume sahihi (sehemu ya pili)

KWA NINI INAKUWA VIGUMU LEO KUPATA MKE/MUME SAHIHI (SEHEMU YA PILI)

Vijana wa kike na wa kiume wanakuwa na wakati mgumu sana kipindi hiki katika kupata mwenzi sahihi wa maisha. Wengine wanaomba Mungu awape mchumba badala ya mwenzi wa maisha. Matokeo yake wanachumbiana kila kukicha bila kufikia ndoa takatifu. Uchumba ni mchakato tu kuelekea kwenye ndoa kamili. Mungu hajaahidi popote kwamba atakupatia mchumba mwema bali mume au mke mwema.

Nitatumia ndoa ya Isaka na Rebeka ilivyokuwa tangu uchumba hadi ndoa. Hata hivyo ninapozungumzia MWENZI SAHIHI sina maana ya MWENZI MKAMILIFU. Bado mwanadamu ana mapungufu yake ambayo yanaweza kutumiwa kama fursa za kuhitajiana. Mungu anaunganisha watu ili wakamilishane (complement each other).

Nimepata msukumo wa kuisoma Mwanzo 24 kiufunuo ili kukupa kanuni za msingi za kukusaidia. Sio lazima zimfae kila mtu. Bado wapo wenye maisha mazuri bila kanuni hizi zote. Huu ni mwongozo tu kwa wacha Mungu (wanaomhofu Mungu kuliko kufuata tamaa zao za mwili na wanaojua kuna siku tutatoa hesabu ya matendo yetu mbele za Mungu).

NB: HATA HIVYO HII NI SEHEMU YA PILI. FUATILIA SOMO LILILOPITA (NA 1-5) NA LITAKALOENDELEA (NA 11-16).

Sababu za ugumu wa kupata mwenzi sahihi:

6. Kutojua wakati sahihi wa kukutana na watu wa aina ya mwenzi unayemtaka

Mst 11 “Akawapigisha magoti ngamia nje ya mji karibu na kisima cha maji wakati wa jioni, wakati ambapo wanawake wanakwenda kuteka maji.”

Mtumishi wa Ibrahimu alipofika Mesopotamia hakwenda popote bali alikwenda kwenye kisima wakati wa jioni ambapo wanawake wanakwenda kuteka maji. Bilashaka alifanya utafiti kidogo. Unadhani ingekuwaje kama angeenda muda ambao wanawake hawaendi kuteka maji bali wanapika nyumbani? Au kama angeenda kwenye kisima muda ambapo wanaume wanaenda kunywesha mifugo yao au kuoga? Unaweza kumlaumu Mungu kwa makosa yako mwenyewe (kutotumia akili vizuri). Huwezi kutafuta kazi ya ualimu sokoni au hotelini. Lakini pia huwezi kwenda maofisi ya serikali siku za sikukuu au wikiendi. Hutakuta mtumishi zaidi ya walinzi. Vijana wanapatikana zaidi kwenye kambi za vijana na sio kwenye semina za wanandoa. Biblia inaturuhusu kutumia akili ila tusitende dhambi. 1 Wakorintho 15:34 “Tumieni akili kama ipasavyo, wala msitende dhambi; kwa maana wengine hawamjui Mungu. Ninanena hayo niwafedheheshe.” Lazima uwe na maono makubwa. Ni rahisi kumkosea Mungu kama una maono finyu ya hapo ulipo tu. Mungu alipotaka kumuonyesha Ibrahimu jinsi atakavyombariki alimtoa nje ya hema kwanza. Mwanzo 15:5 “Akamleta nje, akasema, Tazama sasa mbinguni, kazihesabu nyota, kama ukiweza kuzihesabu. Akamwambia, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako.” Kama bado uko ndani ya nyumba yako ukihesabu makenchi au balbu, sasa toka nje uangalie angani na kuzihesabu nyota. Panua wigo wa kumpata mwenzi wako wa maisha. Isaya 54:2 “Panua mahali pa hema yako, na wayatandaze mapazia ya maskani yako; usiwakataze; ongeza urefu wa kamba zako; vikaze vigingi vya hema yako.”

7. Kutokuomba maombi ya kufunga macho yote mawili na kutoweka ishara zenye maana

Mst 12-15 “Naye akasema, Ee Bwana, Mungu wa bwana wangu Ibrahimu, nakuomba mambo yangu uyajalie yawe heri leo, ukamfadhili bwana wangu Ibrahimu. Tazama! Nimesimama karibu na kisima cha maji, na binti za watu wa mjini wanatoka kuteka maji, basi na iwe hivi; yule msichana nitakayemwambia, Tua mtungi wako, nakuomba, ninywe; naye akasema, Unywe, nami nitawanywesha na ngamia zako pia; basi huyu na awe ndiye uliyemchagulia mtumishi wako Isaka; na kwa hayo nitajua ya kuwa umemfadhili bwana wangu. Ikawa, kabla hajaisha kunena, tazama, Rebeka anatokea, binti wa Bethueli mwana wa Milka, mkewe Nahori, ndugu wa Ibrahimu, naye ana mtungi begani pake.”

Huyu mtumishi wa Ibrahimu akiwa eneo sahihi, aliomba maombi yenye ishara za kumrahisishia kutambua yupi ni mke mtarajiwa wa Isaka. Kuna vijana hawamuombi Mungu na kama wanamuomba Mungu hawatambui ishara za majibu yao. Unatakiwa utambue njia nyepesi ya wewe kujua majibu ya maombi yako. Pia unatakiwa uombe wakati huna mtu yeyote uliyemuweka moyoni. Ukiomba wakati tayari una mtu unayemfikiria, utakuwa unaomba ukiwa umefunga jicho moja tu na sio yote mawili. Utakuwa unalazimisha Mungu akupe huyo. Nilipokuwa kwenye semina mbali sana na Korogwe na kujisikia ishara moyoni kwamba yule aliyeketi pale ni mke wangu mtarajiwa, nilimwomba Mungu na kusema, “Ikiwa ni Wewe Mungu unayesema nami, naomba useme na mchungaji mwenyeji aliyenialika.” Nilijua sio busara kuongea naye moja kwa moja ukizingatia mimi ni mgeni tu katika kanisa hilo. Ningeweza hata kuzushiwa mabaya kwamba naongea nini na huyo msichana. Lakini pia nilikuwa sijui kama ana mchumba au la. Nilipomaliza kufundisha nikashangaa mchungaji mwenyeji akiniambia anataka nipate faragha na yeye. Akaniuliza swali, “Mtumishi wa Mungu unalo hitaji la kuoa?” Ikawa ni mara yangu ya kwanza kuulizwa swali lenye mtazamo chanya. Watumishi wengi walikuwa wananiambia, Mbona huoi? Walikuwa wananilaumu kwa kutokuoa. Nikamjibu, Ndiyo ninalo hitaji la kuoa. Akaniambia kuna binti yuko hapa kwa wiki chache. Najisikia moyoni kwamba anafaa kuwa mke wako. Nilichoshangaa ni yuleyule ambaye nilipata ishara nikiwa nafundisha madhabahuni. Mchungaji mwenyeji akatengeneza mazingira ya kuongea naye kisha tukaagana na kuendelea kumuomba Mungu, kupima afya zetu (kila mtu kwa wakati wake) na kushirikisha wazazi wetu wa kimwili na wa kiroho. Nashauri wachumba wapime afya mapema kabla upendo haujakua sana ili iwe rahisi kuvunja uchumba inapobidi. Mkisubiri mpime afya karibu na ndoa inaweza kuwagharimu. Kutokana na aibu au kupofushwa macho na upendo/tamaa mnaweza kupuuza kifo na kusema MIMI NIKO TAYARI TU NIKAFE NAYE. Lakini pia itakuwa rahisi kuhesabu gharama na kufanya maamuzi makini hata kama uko tayari kuishi na mtu mwenye tatizo ili usije ukajuta na kujilaumu ukipata changamoto baadaye. Lakini pia mimi ni mwezeshaji (facilitator) wa masuala ya UKIMWI hasahasa kwa viongozi wa dini. Kwa vipimo tulivyo navyo katika zahanati zetu, hutapata uhakika kwamba huna virusi kwa kupima siku chache kabla ya ndoa. Ingefaa zaidi upimaji uanze miezi 6 hadi 9 kabla ya ndoa kufungwa ili muweze kurudi kila baada ya miezi 3 kwa ajili ya kupata uhakika. Hata hivyo kurudia kupima kuna maana kwa wale tu waliotulia. Kwa wanaoendelea kufanya uasherati mpaka karibu na ndoa kufungwa, haiwezi kuwasaidia sana.

8. Kutoona uzuri wa nje na wa ndani (uzuri uliofichika)

Mst 16 “Naye yule msichana alikuwa mzuri sana uso wake, bikira, wala mwanamume hajamjua bado; akashuka kisimani, akajaza mtungi wake, akapanda.”

Katika utamaduni wao, pamoja na uzuri wa sura ya nje ilitakiwa pia kwamba ithibitike kwamba msichana ni bikira na hajui mume. Hata hapa kwetu zamani wasichana walikuwa wanachunguzwa kwanza na bibi zao ndipo waolewe. Hata hivyo la muhimu sio uchunguzi wa mwili wake (kuwa bikira) tu bali uchunguzi wa mahusiano na wanaume (kujua wanaume). Uzinzi haufanyiki kwa kujamiiana peke yake. Kuna wazinzi wengi kwa njia za mawazo (fantasy) kv punyeto (masturbation), kutazama picha za ngono, kuchungulia watu wanaofanya ngono, kupenda watu wakuone ukiwa uchi, kushikanashikana kingono (heavy petting), ngono kwa simu na mitandao nk. Kuna watu hawajui baadhi ya wapenzi wanaowasiliana nao kwa mtandao sio watu bali ni majini au wachawi. Wana uwezo wa kumuoa mtu kimtandao na kumzuia asiweza kuoa au kuolewa kabisa. Hata hivyo ni muhimu sana kuoa mke au kuolewa na mume umpendaye na kujua taswira yake katika jamii kabla ya kumuoa au kuolewa naye. Ni hatari sana kama utaijua tabia yake mbaya ambayo ina madhara makubwa baada ya kumuoa au kuolewa naye halafu ukaipuuzia. Mhubiri 9:9 “Uishi kwa furaha pamoja na mke umpendaye, siku zote za maisha yako ya ubatili, ulizopewa chini ya jua; siku zote za ubatili wako, kwa maana huo ni sehemu yako ya maisha; na katika taabu zako ulizozitaabika chini ya jua.” Kumbuka hapa hasemi UISHI KWA FURAHA NA MKE WA KUONYESHA WATU BALI MKE UMPENDAYE. Huwezi KUMPENDA kila mwanamke au mwanaume ila unaweza KUMTAMANI kila mwanamke au mwanaume. Inasemekana baadhi ya watu ambao wanadhaniwa au wanajiona ni wazuri sana wa sura hawawi na uwezo mkubwa wa kuonyesha upendo. Unajua kwanini? Kwa vile anajiona ni mzuri sana na kwamba wengi wanamtamani, anaona kwamba mumewe au mkewe anapaswa kumpenda maana amebahatika sana kumpata. Kinyume chake, wengi wanaoitwa wenye sura mbaya au za wastani ndio wako ndani ya ndoa zao wakifurahia maisha kwa vile wanajua kupenda. Hata kama umejaliwa kuwa mzuri kwa nje jitahidi na kwa ndani pia uwe mzuri na ulinde sana ushuhuda wako kwa jamii. 

9. Kutochukua hatua yoyote unayoiweza na kutokuwa mkarimu kwa marika yote

Mst 17-21 “Ndipo yule mtumishi akapiga mbio kwenda kumlaki, akasema, Tafadhali unipe maji kidogo katika mtungi wako ninywe. Naye akasema, Unywe, bwana wangu, akafanya haraka, akatua mtungi wake mkononi mwake, akamnywesha. Hata alipokwisha kumnywesha akasema, Na ngamia zako nitawatekea, hata watakapokwisha kunywa. Akafanya haraka, akamwaga maji ya mtungi wake katika birika, akapiga mbio kisimani ateke, akawatekea ngamia zake wote. Basi yule mtu akamkazia macho, akanyamaza, ili ajue kwamba Bwana ameifanikisha safari yake ama sivyo.”

Eliezeri (mtumishi wa Ibrahimu) alifanya majaribio kuona kama kweli mke amepatikana. Hakuendelea kuzama kwenye maombi bila kuchukua hatua. Kumbuka aliweka ishara za kumsaidia kutambua mke atakayefaa kufanya kazi za Isaka na ambaye ni mchapa kazi. Eliezeri alisafiri na ngamia kumi na ngamia mmoja anakunywa wastani wa galoni 30 za maji kwa muda usiozidi dakika 15. Haikuwa rahisi kwa msichana kuwanywesha ngamia wote tena wa mpita njia. Huyu msichana pia alikuwa mkarimu sana tena kwa mtu ambaye si wa rika la kumuoa. Leo hii vijana wengi wanadhani watapata mwenzi sahihi kwa kuwachekea vijana wa marika yao tu. Hawajui kuna watu wazima ambao wanaweza kueleza sifa njema za msichana au mvulana waliyemuona. Watu wazima wanaweza kuelezea sifa za mtu mpaka apate mwenzi kwa wepesi. Nimekutana na wasichana wengi kwenye huduma ambao nadhani wanaomba Mungu awape wenzi wa maisha lakini hawawezi hata kukupokea mzigo ulioubeba wala kukusalimia kwa heshima. Wanafanya hivyo kwa vile wanajua wewe umeshaoa tayari. Ila wakiona mvulana wanayempigia mahesabu ndipo wanaanza kujinyenyekeza. Hakuna mtu mwenye busara anayeoa au kuolewa bila ushauri wa watu wazima.

Nilipoongea na mchungaji mwenyeji kabla hajamuita msichana ambaye baadaye nilimuoa, nikawa nje asubuhi napiga mswaki. Nilichoshangaa ingawa msichana huyo ni mgeni katika kanisa hilo alikuja kwa mchungaji kusaidia kazi kv kuchota maji nk wakati wasichana wenyeji wanaonekana tu muda wa semina jioni. Kwa sehemu nikaweka tiki kwamba atanifaa katika utumishi akiwa mama mchungaji kwa vile katika huduma zetu tunapokea wageni wengi.  Dada mmoja aliitwa na mvulana ili akamtambulishe kwa wazazi wake. Wakati akiwa kwenye basi akapanda babu mmoja akasimama karibu naye kwa vile hakupata siti. Yule babu akawa anamuangukia mara kwa mara kwa vile amechoka kusimama muda mrefu. Yule dada akawa anamtukana na kumsukuma bila kujali. Alipofika kituo cha kushukia akashangaa yule kijana anampokea pamoja na yule babu. Kumbe ni baba yake mzazi. Msichana akaanza kunyong’onyea. Walipofika nyumbani, kijana akamtambulisha kwa baba yake. Dada akawa hana la kusema (speechless). Baba alipoeleza yaliyotokea njiani, kijana akashangaa sana. Wakampa nauli akarudi kwao. Uchumba ukafia hapo. Ukikuta mtu anauliza habari zako tu lakini hajali kuuliza kuhusu ndugu zenu uwe macho naye sana. Eliezeri hakuwa na haraka alisubiri aone kama ishara zake zinatimia au asubiri mwingine pale kisimani. 

10. Kupendana njiani bila kufikishana nyumbani kwa wazazi

Mst 22-25 “Ikawa, ngamia walipokwisha kunywa, yule mtu akatwaa pete ya dhahabu, uzani wake ulikuwa nusu shekeli, na vikuku viwili kwa mikono yake, uzani wake ulikuwa shekeli kumi za dhahabu. akasema, U binti wa nani wewe? Tafadhali uniambie. Je! Iko nafasi katika nyumba ya baba yako tupate mahali pa kukaa kwa muda? Akasema, Mimi ni binti wa Bethueli mwana wa Milka, aliyemzalia Nahori. Tena akamwambia, Kwetu kuna majani na malisho ya kutosha, na mahali pa kukaa wageni.””

Eliezeri alipoona dalili nzuri akatoa zawadi zake lakini akauliza baba yake ni nani na kama kuna nafasi kwao ili apeleke posa. Mnapowasiliana wenyewe bila kushirikisha wazazi wa kiroho na kimwili itawagharimu sana pale mtakapopata kikwazo. Upendo unapokua unapofusha macho kwa hiyo hamtasikia la mtu. Si busara kuruhusu mtu aingie sana moyoni wakati wazazi wako bado hawajui na bado hujamjua vizuri. Unaweza kudhani anafaa kuwa mume wako au mke wako bila wazazi kuhusika lakini usisahau kwamba kuna leo na kesho. Ipo siku mtahitaji msaada wa ndugu hata kama mna pesa kiasi gani. Lakini pia kama kutatokea dosari kwenye ndoa yenu unaweza kuteseka sana na kushindwa kuwashirikisha ndugu kwa vile uliwadharau. Matokeo yake unaweza kufanywa kilema kwa kupigwa au kuonewa na usipate pa kukimbilia. Utaona aibu kueleza matatizo yake kwa vile ulipuuza ushauri na nafasi ya ndugu zako. Mtu ambaye mmeamua kuishi pamoja mkiwa kwenye basi (njiani) mtaachana pia kwenye basi (mkiwa njiani). Kutaneni mahali sahihi pasipo na maswali kwa watu (msitiliwe mashaka) na ambapo sio mazingira hatarishi kwenu wenyewe. Mtu fulani aliwahi kuniambia msemo huu: ‘HUWEZI KUMPA MBWA KAZI YA KULINDA MSHIKAKI!’ Mkijaribiwa mkaanguka kuna uwezekano mkubwa wa kutoolewa au ndoa yenu kutokuwa imara hata kama itafungwa baadaye. Mtakuwa hamuaminiani. Mwenzako atakuona kwamba hushindwi kutembea na wengine kama ulishindwa kukataa na kusubiri. Ndiyo maana ndoa nyingi leo ni za kuwindana maana zimekuwa ndoana. Wanandoa ambao walitembea kabla ya ndoa kufungwa wanatakiwa kutubu dhambi hiyo ili ndoa yao iwe imara. Vinginevyo hata kama watu hawajui, shetani atawatesa kwa vile ni mshitaki wetu mbele za Mungu. Ufu 12:10 “Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu, mchana na usiku.” 

Kipindi hiki wengi hawataki wajulikane vizuri wala nyumbani kwao. Ndiyo maana hata katika mtandao hawaweki majina yao halisi, sura zao halisi na wala maelezo halisi. Mtu yuko tayari apige picha kwenye sofa za hoteli fulani ili adanganyie kwamba ndiyo sebule yake. Yuko tayari atafute wazazi bandia wa kukutambulisha kwao ili iwe rahisi kukuacha kwa wepesi anapotaka. Tuwe macho sana katika hatua hii muhimu sana ya safari ya maisha yetu.

………………………………somo litaendelea (Na 11-16)………..

Dkt. Lawi Mshana, +255712924234; Korogwe, Tanga, Tanzania