Ticker

6/recent/ticker-posts

Kwanini mitume wa leo wanatiliwa mashaka

KWA NINI MITUME WA LEO WANATILIWA MASHAKA

Mtume ni mtu aliyetumwa na Mungu akiwa na ujumbe au agizo maalum. Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na watumishi wengi wanaosema Mungu amewapa huduma ya kitume na wakati huohuo kuna watu wengi wanaotilia mashaka utume wao. Baadhi ya sababu za mashaka hayo ni za msingi lakini nyingine hazina msingi wowote. 

Hata hivyo napenda kutumia maandiko na uzoefu wangu katika huduma katika kukupa sababu za mashaka hayo: 

1. Tafsiri isiyo sahihi kuhusu utume Kuna watu wanaamini kwamba utume ulikoma katika kipindi cha Biblia. Hivyo, wanasema hakuna tena mitume wakati huu. Ila kama utawauliza andiko linalothibitisha huo msimamo wao hawataweza kukuonyesha. Wengine wanaamini kwamba utume ni cheo kikubwa sana ambacho kinastahili kutumiwa na mtume Yesu na mtume Muhamad tu. Hivyo wanaona ni kufuru kumsikia mwingine akisema ni mtume. Wanasahau kwamba hata kipindi cha Biblia kulikuwa na mitume wa Mwanakondoo (Thenashara) na mitume wengine wa kanisa kv Barnaba nk. 

2. Mapokeo na mazoea Kuna kundi kubwa ndani ya kanisa ambalo linaamini kinadharia (theoretically) kwamba Bwana ametoa huduma tano kwa mujibu wa Efe 4:11 ikiwemo huduma ya utume. Lakini, kiutendaji (practically) linazikubali huduma tatu tu za uchungaji, ualimu na uinjilisti. Waefeso 4:11 “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu.” Hii imetokana na msingi uliojengwa na waasisi wa madhehebu ya kikristo hapa nchini. Hata pale walipotumiwa kwa upako wa kitume, waliuita upako wa kiinjilisti. Na hata mtu alipojaribu kuwaita mitume, walimjia juu na kukataa kwamba hawana huduma hiyo wakati matunda ya kazi zao yanadhihirisha kwamba huduma hiyo wanayo. 

3. Kutojua hatua na aina za utume Utume ni huduma inayoanza katika uchanga na kukua kama zilivyo zingine. Hivyo mtu anaweza kuwa na mbegu ya utume lakini bado hajawa na ishara zote za kitume zinazokubalika kimaandiko. 2 Kor 12:12 “Kweli ishara za mtume zilitendwa katikati yenu katika saburi yote, kwa ishara na maajabu na miujiza.” Paulo anayesema maneno hayo alianza kutumiwa katika huduma nyingine hadi Roho wa Mungu aliposema umefika wakati wa kuachiliwa kwa huduma ya kitume. Mdo 13:1-3 “Na huko Antiokia katika kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni Barnaba, na Simeoni aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa ndugu wa kunyonya wa mfalme Herode, na Sauli. Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia. Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao.” Katikati ya manabii na waalimu Roho akajipatia mitume. Vilevile, kuna aina mbali mbali za utume. Inategemea Mungu amekutuma kwa nani na amekupa ujumbe gani. Mfano, wapo mitume wenye upako wa KUANZISHA zaidi (mf kupanda makanisa, kuanzisha misheni nk) kama Paulo wakati wengine wana upako wa KUENDELEZA kama Apolo. 1 Kor 3:6 ‘Mimi nilipanda, Apolo akatia maji; bali mwenye kukuza ni Mungu’. Watumishi wengine katika Agano Jipya waliitwa mitume lakini hawakupanda makanisa bali waliendelea kuchunga makanisa. 

4. Kudhani utume ni kupanda daraja katika utumishi Kuna watu wanadhani kwamba upako unapoongezeka ni ishara ya kupokea huduma nyingine. Si lazima mtu akipokea huduma ya kitume, huduma yake ya awali ifutike. Hata hivyo, Mungu anaweza kuongeza huduma ya kitume na kumfanya mtu awe Mchungaji-Mtume au Mtume-Mwalimu nk. Vilevile, Mungu anaweza kumtumia Mchungaji katika upako mkubwa bila kumbadilishia au kumuongezea huduma nyingine. Hivyo kuna watu wanapopewa huduma ya kitume wanaanza kudharau huduma zingine kwa kudhani wako juu zaidi. Na kuna watu wanamchukulia mtu anayesema ni mtume kwamba amejikweza. Kilicho cha msingi kwa mtume sio karama (gift) bali agizo (commission) alilopewa. Yesu alipochagua kutumia jina MTUME hakuchagua jina lenye heshima sana. Alichagua jina ambalo kwa kipindi hicho lilikuwa na maana ya MTU ALIYETUMWA KAZI FULANI LAKINI MAMLAKA YAKE INATOKANA NA HUYO ALIYEMTUMA. Hakuchagua majina makubwa yaliyotumiwa na viongozi wa dini katika kipindi chake. 

5. Desturi ya kutanguliza zaidi uchungaji Muundo wa madhehebu mengi unampa mchungaji nafasi ya juu kuliko mtume jambo ambalo ni kinyume cha mpangilio uliowekwa katika maandiko. 1 Kor 12:28 ‘Na Mungu ameweka wengine katika kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, wa tatu waalimu…’. Hapa haina maana kwamba utume ni bora kuliko huduma zingine bali Mungu anataka mtume asaidie kuweka msingi. Makanisa mengi hayana msingi mzuri kwa vile huduma ya kitume haipewi nafasi yake. Nikisema msingi mzuri nina maana ya kuandaa wanafunzi na watumishi na sio kuwa na washirika wengi. Yesu aliwekeza kwa wanafunzi wachache kuliko makutano (makusanyiko) na kazi yake imedumu. Leo kuna makanisa yenye washirika wengi lakini hawajaokoka, wengine wamemuacha Mungu na wengine hata kumuomba Mungu hawajui. Kama hoja yetu ya kutilia mashaka utume wa leo ingekuwa ya kimaandiko, tungetilia mashaka zaidi uchungaji kwa sababu jina mchungaji (pastor) katika umoja (singular) halikutajwa katika Agano Jipya. Limetumika mara moja tu katika wingi (wachungaji) wakati mitume wametajwa zaidi ya 20. Tunatumia zaidi mapokeo kuliko maandiko. Katika Biblia kuna mitume wengi waliochunga makanisa bila kupanda makanisa na bado hawakuitwa wachungaji. Ni mapokeo tu yamesababisha kutumia zaidi jina mchungaji kuliko mtume. 

6. Mwenendo mbaya wa baadhi ya mitume Mtume anaweza kukosea kama mchungaji anavyoweza kukosea. Sio tu kwamba mitume wa kipindi cha Biblia walikosea, bali pia walikuwepo mitume wa uongo. 2 Wakorintho 11:13 “Maana watu kama hao ni mitume wa uongo, watendao kazi kwa hila, wanaojigeuza wawe mfano wa mitume wa Kristo.” Kuwepo kwa baadhi ya wachungaji matapeli hakusababishi huduma ya kichungaji ifutike. Kila mtu atachukua mzigo wake mwenyewe. Wagalatia 6:4,5 “Lakini kila mtu na aipime kazi yake mwenyewe, ndipo atakapokuwa na sababu ya kujisifu ndani ya nafsi yake tu, wala si kwa mwenzake. Maana kila mtu atalichukua furushi lake mwenyewe.” Hata Paulo ambaye leo ana mashabiki wengi, katika kipindi chake wapo watu walitilia mashaka utume wake ikamlazimu kuutetea utume wake. 1 Kor 9:1-3 ‘Je! Mimi si huru? Mimi si mtume? mimi sikumwona Yesu Bwana wetu! Ninyi si kazi yangu katika Bwana? Kwa maana ikiwa mimi si mtume kwa wengine, lakini ni mtume kwenu ninyi; kwa maana ninyi ndinyi muhuri ya utume wangu katika Bwana. Hilo ndilo jawabu langu kwa wale wanaoniuliza.’ 

7. Upeo mdogo wa baadhi ya mitume Wapo watumishi ambao wanalazimisha kuitwa mitume kabla hawajapata kibali Rum 15:31 “kwamba niokolewe na wale wasioamini katika Uyahudi, na tena huduma yangu niliyo nayo huko Yerusalemu ikubalike kwa watakatifu”. Si busara kujiita mtume kabla Mungu hajasema wazi, kabla baadhi ya watu uliotumwa kwao hawajaanza kuuona utume ndani yako na kabla hujaachiliwa kwa maombi rasmi. Usipoachiliwa unaweza kujikuta unatembea na upako wa huduma ya awali – hutapata upenyo wa huduma hiyo mpya. Hata hivyo si lazima watu ambao hukutumwa kwao wakuite mtume. Paulo hakujiita mtume wa ulimwengu mzima bali alisema, ‘kwa maana ikiwa si mtume kwa wengine, lakini ni mtume kwenu ninyi’ (1 Kor 9:2). Kwa mfano, mimi sipati shida nisipoitwa mchungaji na mtu ambaye simchungi. Vilevile wapo baadhi wananiita mtume lakini silazimishi kila mtu anione ni mtume kwake wakati sijatumiwa kuweka msingi wowote maishani mwake na wala haoni mguso wowote wa huduma yangu ya kitume kwake. Hizi huduma sio vyeo ambavyo vinatumika kila mahali na kwa kila mtu. Hata nyumbani sio wote wananiita baba, wengine wananiita mjomba na wengine babu kutegemeana na uhusiano wangu na wao. 

8. Ugumu wa kupokea mambo mapya ‘Kwa kila jambo kuna majira yake, na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu’ (Mhu 3:1). Hiki ni kipindi cha kurejezwa kwa huduma zilizosahaulika ikiwa ni pamoja na utume na utumishi wa wanawake. Ni kweli kwamba Mungu habadiliki lakini anabadilisha utendaji kutegemeana na uhitaji unaojitokeza kwa wakati husika. Katika Agano la Kale aliwatumia manabii, waonaji na waamuzi. Katika Agano Jipya akainua huduma tano za mitume, manabii, wainjilisti, wachungaji na waalimu (Efe 4:11). Tuache tabia ya kumuwekea mipaka Mungu katika utendaji wake. Zab 78:41 ‘..Wakampa mpaka Mtakatifu wa Israeli.’ Tufanyie kazi lile tulilofunuliwa na Mungu bila kusahau kwamba Mungu ana siri nyingi ambazo anafunulia watu wake kama apendavyo. Usilizungumzie jambo ambalo bado ni SIRI kwako. Subiri liwe UFUNUO ndipo uliseme. Kum 29:29 ‘Mambo ya siri ni ya BWANA, Mungu wetu; lakini mambo yaliyofunuliwa ni yetu sisi na watoto wetu milele, ili tuyafanye maneno yote ya sheria hii.’ Kimsingi, tusiupuuze wala kuuogopa utume lakini vilevile tusiurahisishe sana kiasi cha kupoteza maana yake ya kibiblia. Biblia haisemi wote ni mitume bali inasema, ALITOA WENGINE kuwa mitume (Efe 4:11). Kama hukupewa utume, umepewa huduma nyingine. Hivyo, itumie kwa kulijenga kanisa la Mungu bila kupinga huduma ambayo huijui. Tutahukumiwa kwa kuwa wapinzani wa mambo tusiyoyajua. Yakobo 3:1 “Ndugu zangu, msiwe waalimu wengi, mkijua ya kuwa mtapata hukumu kubwa zaidi.” Siku zijazo nitazungumzia zaidi huduma ya kitume inavyotenda kazi na mambo ambayo kanisa linayakosa kwa kukataa huduma hii. 

Dr Lawi Mshana, +255712924234, Korogwe, Tanga, Tanzania