Ticker

6/recent/ticker-posts

Huduma ya kitume (sehemu ya pili)


HUDUMA YA KITUME (sehemu ya pili)

Katika somo lililopita nilizungumzia HUDUMA YA KITUME. Naendelea kukupa mambo mengine ya msingi kuhusu huduma hii. 

1. Inachukua muda mtu kuwa mtume. Hata katika kipindi cha Biblia mitume walianza na huduma zingine kabla ya kuwa mitume. Barnaba na Paulo walitumika kama manabii na waalimu kabla ya kuwa mitume. Mdo 13:1,2 “Na huko Antiokia katika kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni Barnaba, na Simeoni aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa ndugu wa kunyonya wa mfalme Herode, na Sauli. Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia.” Kwa hiyo usishangae kuona mtu aliyekuwa mchungaji au mwinjilisti akisema sasa ni mtume. Mara nyingi mtume anaweza kutumika katika huduma zingine uhitaji unapokuwepo. Ndiyo maana utume unahusianishwa na dole gumba. Dole gumba linaweza kugusa vidole vingine vyote ambavyo vinawakilisha unabii, uinjilisti, uchungaji na ualimu. 

2. Ili mtume atumike katika upako unaohitajika anatakiwa kuachiliwa na kanisa lake pamoja na viongozi wake wa imani wanaotambua huduma yake (baba wa kiroho). Ingawa Mungu aliwaita Paulo na Barnaba alilitaka kanisa liwaachilie kwa maombi maalum. Na kanisa lilipoagizwa hivyo likafunga na kuomba na kuwaachilia. Mdo 13:2,3 “Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia. Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao.” Pia Paulo aliripoti kwa wakuu na kubarikiwa. Wagalatia 2:9 “tena walipokwisha kuijua ile neema niliyopewa; Yakobo, na Kefa, na Yohana, wenye sifa kuwa ni nguzo, walinipa mimi na Barnaba mkono wa kuume wa shirika; ili sisi tuende kwa Mataifa, na wao waende kwa watu wa tohara.” Mungu aliposema nami kuhusu huduma aliyonipa nilisubiri aseme na kanisa. Nilipoachiliwa na kanisa nikasafiri kilomita zaidi ya 1000 hadi Tunduma Mbeya kuachiliwa na baba yangu kiroho. Tangu nifuate kanuni za kibiblia nimeona upenyo mkubwa. Mtume ambaye hajaachiliwa kwa kanuni za kibiblia anapata UJUMBE lakini hapati UPENYO (FEDHA ZA HUDUMA ALIYOPEWA) kwa vile anatembea kwa upako wa huduma ya awali. 

3. Mtume anaweza kuwanusuru wachungaji katika matatizo mengi. Anaweza kuwasaidia wachungaji kuwa na muundo wa uongozi wa ki-Mungu badala ya kidhehebu, kuwasaidia kuwa na maono makubwa, kuwasaidia kuchagua viongozi sahihi, kuwasaidia watembee kwa imani na sio kwa kiburi, kuwasaidia kuzaa wana na sio watumishi tu, kuwasaidia wagawe madaraka badala ya kuonekana wao ndio kila kitu (one man show) na kuwasaidia wasiwaze tu kuwa na waumini wengi bila mikakati ya kufikia ulimwengu. Mdo 20:17-19,29-31 “Toka Mileto Paulo akatuma watu kwenda Efeso, akawaita wazee wa kanisa. Walipofika kwake, akawaambia, Ninyi wenyewe mnajua tangu siku ya kwanza nilipokanyaga hapa Asia, jinsi nilivyokuwa kwenu wakati wote, nikimtumikia Bwana kwa unyenyekevu wote, na kwa machozi, na majaribu yaliyonipata kwa hila za Wayahudi. Najua mimi ya kuwa baada ya kuondoka kwangu mbwa-mwitu wakali wataingia kwenu, wasilihurumie kundi; tena katika ninyi wenyewe watainuka watu wakisema mapotovu, wawavute hao wanafunzi wawaandamie wao. Kwa hiyo kesheni, mkikumbuka ya kwamba miaka mitatu, usiku na mchana, sikuacha kumwonya kila mtu kwa machozi.” Mtume anafunuliwa matatizo wanayopitia watumishi ambao ameunganishwa nao na kutumiwa na Mungu kwa neema ya pekee kuwasaidia. 

4. Mtume anazaa wachungaji, wainjilisti, waalimu na viongozi wengine ili wamsaidie kutimiza agizo alilopewa. Kama mchungaji alivyo na upako wa kuvuta MAKUSANYIKO, mtume ana upako wa kuwavuta VIONGOZI. 2 Timotheo 4:11 “Luka peke yake yupo hapa pamoja nami. Umtwae Marko, umlete pamoja nawe, maana anifaa kwa utumishi.” Kwa vile mtume ana mvuto mkubwa kwa viongozi anaweza kuwapa malezi viongozi na kuwafanya wajisikie kuwa salama wakiwa naye tofauti na viongozi ambao wanawatisha watumishi walio chini yao. Hana wivu anapoona Mungu anawainua watoto wake kwa vile anatumika nao kama baba na mtoto wake na sio bosi na mtumishi wake. 1 Wakorintho 4:17 “Kwa sababu hii nimemtuma Timotheo kwenu, aliye mwanangu mpendwa, mwaminifu katika Bwana, atakayewakumbusha njia zangu zilizo katika Kristo, kama vile nifundishavyo kila mahali katika kila kanisa.” 

5. Mitume wanafanya kazi za kipato ambazo haziwatoi kwenye wito ili wasiwalemee waumini kwa vile huduma yao ni pana yenye mahitaji mengi yakiwemo kusaidia wanyonge. Mdo 20:33-35 “Sikutamani fedha wala dhahabu, wala mavazi ya mtu. Ninyi wenyewe mnajua ya kuwa mikono yangu hii imetumika kwa mahitaji yangu na ya wale waliokuwa pamoja nami. Katika mambo yote nimewaonyesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi alivyosema mwenyewe, Ni heri kutoa kuliko kupokea.” Mtume Paulo hakutegemea sadaka za waumini ingawa alifundisha umuhimu wa kumtolea Mungu. Hakutamani mali za waumini bali alishona mahema ili kuhudumia maisha yake na ya timu yake. Mdo 18:1-3 “Baada ya mambo hayo, Paulo akatoka Athene akafika Korintho. Akamwona Myahudi mmoja, jina lake Akila, mzalia wa Ponto; naye amekuja kutoka nchi ya Italia siku za karibu, pamoja na Prisila mkewe, kwa sababu Klaudio amewaamuru Wayahudi wote watoke Rumi, naye akafikilia kwao; na kwa kuwa kazi yao ya ufundi ilikuwa moja, akakaa kwao, wakafanya kazi pamoja, kwa maana walikuwa mafundi wa kushona hema.” Hata leso aliyotumia mtume Paulo sio kama hizi tunazonunua na kuwaambia watu wapepee wakati wa kipindi cha sifa bali ilitumika kuzuia jasho akishona mahema. Mdo 19:12 “hata wagonjwa wakaletewa leso na nguo zilizotoka mwilini mwake, magonjwa yao yakawaondokea, pepo wachafu wakawatoka.” Mungu ameniwezesha kufanya huduma za kuwafikia wengi bila kulilemea kanisa ninalolichunga. Niliwahi kumwambia Mungu mimi ndiye uliyeniita na sio kanisa hili hivyo sitaki mtu alemewe maana safari zangu haziishi na nina majukumu ya kuyafikia makundi yaliyo pembezoni kv wazee. Mtume ambaye hajishughulishi kuongeza kipato ni rahisi kuthamini waumini wenye kipato tu au kubebesha waumini michango isiyokoma. Lakini pia anaweza kujikuta anashindwa kuwasaidia wanyonge kama alivyofanya mtume Paulo na wengine. 

6. Mitume wanaona picha kubwa na wanaweza kuongozwa kufanya jambo ambalo viongozi wengine wanaona haliwezekani. Wanachozingatia ni agizo walilopewa na Mungu. Hivyo wanaweza kuanzisha miradi mikubwa kwa imani na bila kukopa na ifanikiwe. Mdo 27:21-25 “Na walipokuwa wamekaa wakati mwingi bila kula chakula, Paulo akasimama katikati yao, akasema, Wanaume, iliwapasa kunisikiliza mimi na kutokung'oa nanga huko Krete, na kupata madhara haya na hasara hii. Sasa nawapeni shauri, iweni na moyo mkuu, kwa maana hapana hata nafsi mmoja miongoni mwenu atakayepotea, ila merikebu tu. Kwa maana usiku huu wa leo malaika wa Mungu yule ambaye mimi ni wake, naye ndiye nimwabuduye, alisimama karibu nami, akaniambia, Usiogope, Paulo, huna budi kusimama mbele ya Kaisari; tena, tazama, Mungu amekupa watu wote wanaosafiri pamoja nawe. Basi, wanaume, changamkeni; kwa sababu namwamini Mungu, ya kwamba yatakuwa vile vile kama nilivyoambiwa.” Wakati mchungaji anawaona waumini kama KONDOO, mtume anawaona waumini kama MWILI WA KRISTO. Hivyo mchungaji anatamani kila anayemhudumia ajiunge kuwa mshirika wake wakati mtume anatamani kumsaidia aende akaujenge mwili wa Kristo. Mchungaji anawaza KUKUSANYA wakati mtume anawaza KUFIKIA. Wote wako sahihi kulingana na huduma walizopewa na Bwana. Ni Mungu amewapa watumishi mioyo tofauti kwa kusudi lake na kwa utukufu wake. 

Mungu akubariki. 

Dr Lawi Mshana, +255712924234, Korogwe, Tanga, Tanzania