Ticker

6/recent/ticker-posts

Huduma ya kitume (sehemu ya kwanza)


HUDUMA YA KITUME (sehemu ya kwanza) 

Niliahidi katika somo lililopita la KWA NINI MITUME WA LEO WANATILIWA MASHAKA kwamba nitazungumzia huduma ya kitume inavyotenda kazi ili kanisa lijue linakosa nini kwa kutoijali huduma hii (hasa kwa wale wasioitambua). Ili uelewe vizuri somo hili ni muhimu sana usome somo lililopita. Narudia kusema kwamba mtume ni mtu aliyetumwa na Mungu akiwa na ujumbe au agizo maalum kwa watu maalum. 

Kwa ufafanuzi zaidi ni kwamba: 

1. Mtume anapewa ujumbe au agizo maalum. Mfano Mtume Paulo alijua agizo lake. Mdo 26:16,18 “Lakini inuka, usimame kwa miguu yako, maana nimekutokea kwa sababu hii, nikuweke wewe uwe mtumishi na shahidi wa mambo haya uliyoyaona, na wa mambo ambayo katika hayo nitajidhihirisha kwako; uwafumbue macho yao, na kuwageuza waiache giza na kuielekea nuru, waziache na nguvu za Shetani na kumwelekea Mungu; kisha wapate msamaha wa dhambi zao, na urithi miongoni mwao waliotakaswa kwa imani iliyo kwangu mimi.” Hivyo ni lazima mtu anapopewa utume ajue agizo maalum alilopewa. 

2. Mtume anatumwa kwa watu au kundi maalum. Mfano Mtume Paulo alitumwa kwa mataifa. Hii haimaanishi kwamba akimkuta mtu wa kundi jingine hamhubirii bali huduma yake kuu (major) ni kwa mataifa. Mdo 26:17 “nikikuokoa na watu wako, na watu wa Mataifa, ambao nakutuma kwao.” Wagalatia 2:9 “tena walipokwisha kuijua ile neema niliyopewa; Yakobo, na Kefa, na Yohana, wenye sifa kuwa ni nguzo, walinipa mimi na Barnaba mkono wa kuume wa shirika; ili sisi tuende kwa Mataifa, na wao waende kwa watu wa tohara.” Kwa hiyo hakuna mtu ni mtume wa watu wote. Watu wanaomkataa mtumishi wa Mungu kwamba sio mtume ni vile hana ujumbe wao na hakutumwa kwao. Hata hivyo watu wanaweza kumkataa mtume aliyetumwa kwao kwa sababu ya ujinga au kiburi. Paulo alitambua kwamba kuna watu hakutumwa kwao kama mtume na kuna watu ambao ni mtume wao. 1 Kor 9:1-3 “Je! Mimi si huru? Mimi si mtume? Mimi sikumwona Yesu Bwana wetu? Ninyi si kazi yangu katika Bwana? Kwa maana ikiwa mimi si mtume kwa wengine, lakini ni mtume kwenu ninyi; kwa maana ninyi ndinyi muhuri ya utume wangu katika Bwana. Hilo ndilo jawabu langu kwa wale wanaoniuliza.” 

Lakini pia lazima tujue kwamba hakuna mtu anaweza kuupokea utume bila kuwa na uhusiano na ushirika na Yesu anayetoa huduma mbalimbali. Efe 4:10,11 “Naye aliyeshuka ndiye yeye aliyepaa juu sana kupita mbingu zote, ili avijaze vitu vyote. Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu.” Kwa lugha nyepesi mtu hawezi kuwa na huduma za Yesu bila kumpokea kuwa Bwana na Mwokozi wake. Bwana Yesu anatoa huduma (ministries) na Roho Mtakatifu anatoa karama (spiritual gifts). 1 Kor 12:4,5 “Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule. Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni yeye yule.” Ila tusisahau kwamba kuna watu waliopewa utume na wanadamu au madhehebu yao. Wagalatia 1:1,12 “Paulo, mtume, (si mtume wa wanadamu, wala kutumwa na mwanadamu, bali na Yesu Kristo, na Mungu Baba aliyemfufua kutoka kwa wafu). Kwa kuwa sikuipokea kwa mwanadamu wala sikufundishwa na mwanadamu, bali kwa ufunuo wa Yesu Kristo.” Kwa hiyo mhusika mwenyewe ndiye anajua Bwana Yesu amempa nini kwa watu gani. Na hao aliotumwa kwao wanamtambua hivyo. Hata mafundisho haya ninayotoa sio wote wanaweza kuyapokea kwa vile sio wote nimetumwa kuwafikia kwa njia hii. 

Sasa nitaanza kuzungumzia mambo machache kuhusu mtume anavyotenda kazi: 

1. Katika mpangilio wa mamlaka ya Mungu mtume amepewa nafasi ya kwanza. 1 Kor 12:28, 29 “Na Mungu ameweka wengine katika Kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, wa tatu waalimu, kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa, na masaidiano, na maongozi, na aina za lugha. Je! Wote ni mitume? Wote ni manabii? Wote ni waalimu? Wote wanatenda miujiza?” Andiko hili linatuonyesha kwamba sio watu wote ni mitume lakini mitume wapo. Na katika mpangilio wa ki-Mungu mtume anatangulia na kufuatiwa na nabii kisha karama zingine zinafuata. Hata hivyo huduma zinategemeana. Mfano katika mpangilio huo, huduma ya masaidiano ni ya 6 lakini ni ya muhimu sana kwa mitume. Mtu mwenye huduma ya masaidiano amepakwa mafuta kuwa karibu na huduma zingine kv mtume na kumsaidia kibinafsi. Mitume wengi walikuwa na watu wa kuwasaidia kwa karibu. Mtu mwenye huduma ya masaidiano anajisikia fahari kumsaidia mtume, nabii nk bila kutafuta kumzidi au kumpindua katika nafasi yake. Na hapendi kujulikana kwamba ndiye aliyefanya jambo fulani. 

2. Kama Mtume hapokelewi kama mtume, hawezi kutumiwa kikamilifu katika upako huo. Hata kwa Bwana Yesu ilishindikana kuponya wengi katika mji wake kwa sababu walimuona kama mtoto wa seremala. Mk 6:1-6 “Akatoka huko, akafika mpaka nchi ya kwao; wanafunzi wake wakamfuata. Na ilipokuwa sabato, alianza kufundisha katika sinagogi; wengi waliposikia wakashangaa, wakisema, Huyu ameyapata wapi haya? Na, Ni hekima gani hii aliyopewa huyu? Na, Ni nini miujiza hii mikubwa inayotendeka kwa mikono yake? Huyu si yule seremala, mwana wa Mariamu, na ndugu yao Yakobo, na Yose, na Yuda, na Simoni? Na maumbu yake hawapo hapa petu? Wakajikwaa kwake. Yesu akawaambia, Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake mwenyewe, na kwa jamaa zake, na nyumbani mwake. Wala hakuweza kufanya mwujiza wo wote huko, isipokuwa aliweka mikono yake juu ya wagonjwa wachache, akawaponya. Akastaajabu kwa sababu ya kutokuamini kwao. Akazunguka-zunguka katika vile vijiji, akifundisha.” Nadhani hata wewe unajiuliza kwa nini mtumishi wa Mungu anaweza kutumiwa kwa miujiza mikubwa akiwa mbali na nyumbani kwao. Mtu ukimzoea sana au ukijua historia yake ni rahisi kumdharau na hivyo kushindwa kupokea baraka za huduma yake. Utendaji wa karama na huduma hautegemei tu mtu aliye nayo bali pia wapokeaji. Kwa vile walimuona Yesu kama mtoto wa seremala (Yusufu) badala ya Masihi, wakamuwekea mipaka. Neno la Mungu linasema WALA HAKUWEZA KUFANYA MWUJIZA WO WOTE HUKO, ISIPOKUWA ALIWEKA MIKONO YAKE JUU YA WAGONJWA WACHACHE, AKAWAPONYA. Kama hatutambui upako wa mtumishi wa Mungu, tunaweka mipaka ya nguvu ya Mungu kutiririka kupitia kwake. Matokeo yake wengine wataponywa na huduma yake wakati wewe unabaki na matatizo yako. Zaburi 78:41 “Wakarudi nyuma wakamjaribu Mungu; Wakampa mpaka Mtakatifu wa Israeli.” 

3. Mtume anakuwa na mamlaka na ushawishi kwenye eneo fulani tu na sio maeneo yote. 2 Kor 10:13-16 “Lakini sisi hatutajisifu zaidi ya kadiri yetu; bali kwa kadiri ya kipimo tulichopimiwa na Mungu, yaani, kadiri ya kufika hata kwenu. Maana hatujitanui nafsi zetu kupita kadiri yetu, kana kwamba hatuwafikii ninyi; kwa sababu tulitangulia kufika mpaka kwenu katika injili ya Kristo; wala hatujisifu zaidi ya kadiri yetu, yaani, katika taabu za watu wengine; bali tukiwa na tumaini ya kwamba, imani yenu ikuapo, tutakuzwa kwenu kwa kadiri ya kipimo chetu, na kupata ziada; hata kuihubiri Injili katika nchi zilizo mbele kupita nchi zenu; tusijisifu katika kipimo cha mtu mwingine kwa mambo yaliyokwisha kutengenezwa.” Mtume anakuwa na kipimo au mipaka aliyopewa na Mungu. Mara nyingi akijaribu kutoka nje ya kusudi hilo kwa huruma zake za kibinadamu anapata matatizo. Mdo 22:18,21 “nikamwona, naye akiniambia, Hima, utoke Yerusalemu upesi, kwa sababu hawatakubali ushuhuda wako katika habari zangu. Naye akaniambia, Enenda zako; kwa kuwa mimi nitakutuma uende mbali kwa watu wa Mataifa.” Ikiwa Mungu anakuambia watu fulani hawatakubali huduma yako unadhani nini kitatokea kama unang’ang’ana nao? Mtume Paulo hakufika Tanzania lakini akawa na ujasiri wa kusema mwendo ameumaliza. Unajua kwanini? Alijua mipaka ya huduma yake aliyowekewa na Mungu. 2 Timotheo 4:7 “Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda.” 

Maswali ya kujiuliza: 
Je wewe unajua ukubwa wa shamba lako? 
Na je unajua mipaka yako vizuri usije ukalima shamba la mwingine na kuacha la kwako? 

4. Mitume ni walengwa namba moja wa mashambulizi ya shetani Kwa vile shetani anajua kwamba mitume ni watangulizi na waanzishaji wa mambo mengi anawalenga sana katika mashambulizi. Kama hawaombi sana na kuombewa ulinzi wanakuwa hatarini. Mitume wanahitaji waombaji binafsi (personal intercessors) ili watumike kwa ufanisi na kulindwa na Bwana. 2 The 3:1-2 “Hatimaye, ndugu, tuombeeni, neno la Bwana liendelee, na kutukuzwa vile vile kama ilivyo kwenu; tukaokolewe na watu wasio haki, wabaya; maana si wote walio na imani.” Rum 15:30,31 “Ndugu zangu, nawasihi kwa Bwana wetu Yesu Kristo, na kwa upendo wa Roho, jitahidini pamoja nami katika maombi yenu kwa ajili yangu mbele za Mungu; kwamba niokolewe na wale wasioamini katika Uyahudi, na tena huduma yangu niliyo nayo huko Yerusalemu ikubalike kwa watakatifu.” Maombi ya juu juu yanayoombwa siku za ibada peke yake hayatoshi kumbeba mtumishi mwenye huduma ya kitume. Vita anazopata zinatoka ndani kwa ndugu wa uongo na zingine nje kwa wasiomjua Mungu. 

5. Mitume wanatoa uongozi wa kimkakati kwa kanisa Wakati viongozi wengine wanawaza kukusanya mapato tu na kutoa maagizo kwa walio chini yao, mitume wa kweli wanawapatia walio chini yao uongozi wa kimkakati. Wanawasaidia wajue mbinu za kuwawezesha kutekeleza wito wao kwa ufanisi. 2 Kor 10:3-6 “Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;) tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo; tena tukiwa tayari kupatiliza maasi yote, kutii kwenu kutakapotimia.” Mitume walitoa maelekezo mengi ya kuwasaidia watu kupata mbinu badala ya kuwakataza tu kuacha mabaya. Watu wengi tayari wanajua wanatakiwa kuacha dhambi lakini hawajui wafanyeje ili waache dhambi. Wapo wanaojua ni masikini na wanauchukia umasikini lakini hawajui watajinasua vipi. Ni kazi ya viongozi kutumia upako kuwawezesha (empower) watu ili wasitumie nguvu za kibinadamu bila maarifa ya ki-Mungu. 

6. Mitume wanazaa makanisa, wana na huduma bila kutumia akili za kibinadamu Kazi ya mitume sio kupanda makanisa peke yake kama wengi wanavyofikiri. Mtu anaweza kupanda makanisa lakini sio mtume. Mitume pia wanaimarisha makanisa na kuyasimamia. 1 Wakorintho 3:6 Mimi nilipanda, Apolo akatia maji; bali mwenye kukuza ni Mungu.Matendo ya Mitume 15:41 “Akapita katika Shamu na Kilikia akiyathibitisha makanisa.” Makanisa yanayopandwa na mitume mara nyingi yanajitokeza yenyewe bila kujiandaa sana kibinadamu. Leo unaweza kusikia mtumishi akisema ‘Mji fulani hatuna kanisa letu hivyo tunatakiwa kupanda kanisa. Ila ukitazama kwa macho ya kiroho makanisa tayari yapo ila tu dhehebu lao ndilo halipo.’ Mtume Paulo alipanda makanisa lakini pia alianzisha madarasa ya kufundisha, alihubiri Injili nk. Pale makanisa yanapokuwa yapo tayari, huduma ya mtume inaweza kuwa ya kuyaimarisha zaidi na kuzaa wana wa kuendeleza kazi. 1 Timotheo 1:2 “kwa Timotheo, mwanangu hasa katika imani.” 1 Wakorintho 16:10 “Lakini, Timotheo akija, angalieni akae kwenu pasipo hofu; maana anaifanya kazi ya Bwana vile vile kama mimi mwenyewe.” 

7. Mitume wana uwezo wa kufanya waliloagizwa na Mungu kwa wepesi Kuna watu wengi leo ambao wanadai Mungu amewatuma lakini hawapati upenyo mpaka wakope pesa. Kukopa sio dhambi lakini sio njia nzuri ya kutumia katika kumtumikia Mungu kwa mtu anayeishi kwa imani. Kumbuka anayekopa ni mtumwa wake akopeshaye. Mithali 22:7 “Tajiri humtawala maskini, Naye akopaye ni mtumwa wake akopeshaye.” Najua kuna dharura mtu anaweza kupata zimlazimu kukopa kv magonjwa nk. Lakini kwa wengi kukopa kumekuwa ni mtindo wa maisha kiasi kwamba hata kabla hajaanza kumuomba Mungu ameshapanga tayari kwamba akitoka kwenye maombi ataenda kumkopa nani. Kukopa ni adui wa imani kwa kiasi kikubwa. Yesu alipotuma mitume aliwapa mahitaji ya misheni hiyo. Luka 22:35 “Akawauliza, Je! Hapo nilipowatuma hamna mfuko, wala mkoba, wala viatu, mlipungukiwa na kitu? Wakasema, La!” 

Kwa nini inalazimu kukopa mpaka kwa kazi ya Mungu mwenye vitu vyote? 

1. Huduma nyingi tunazofanya hazikuanzishwa na Mungu bali ni utashi wetu wenyewe. Waefeso 4:1 “Kwa hiyo nawasihi, mimi niliye mfungwa katika Bwana, mwenende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa.” Unaweza kulazimisha huduma ambayo sio wewe uliyetumwa kuifanya. Mungu anapoanzisha kitu anakikamilisha. Waebrania 12:2 “tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu.” 

2. Kukosa subira na kutoisikia vizuri sauti ya Mungu. Yohana 5:3 “Ndani ya hayo jamii kubwa ya wagonjwa walikuwa wamelala, vipofu, viwete, nao waliopooza, wakingoja maji yachemke.” Kwa vile tuna haraka sana kuliko Mungu inatulazimu tukope badala ya kusubiri Mungu atupe njia. Lakini pia inawezekana hatukusikia vizuri maelekezo kwamba tutapataje mahitaji ya huduma. Petro aliwahi kuelekezwa namna watakavyopata pesa. Mathayo 17:27 “Lakini tusije tukawakwaza, enenda baharini ukatupe ndoana, ukatwae samaki yule azukaye kwanza; na ukifumbua mdomo wake utaona shekeli ichukue hiyo ukawape kwa ajili yangu na kwa ajili yako.” 

3. Kujaribu kutumika kwa upako wa wengine. Matendo ya Mitume 19:13-16 “Baadhi ya Wayahudi wenye kutanga-tanga, nao ni wapunga pepo, wakajaribu kutaja jina la Bwana Yesu juu yao waliopagawa na pepo wachafu, wakisema, Nawaapisha kwa Yesu, yule anayehubiriwa na Paulo. Walikuwako wana saba wa mtu mmoja Skewa, Myahudi, kuhani mkuu, waliofanya hivyo. Yule pepo mchafu akawajibu, akawaambia, Yesu namjua na Paulo namfahamu, lakini ninyi ni nani? Na yule mtu aliyepagawa na pepo mchafu akawarukia wawili, akawaweza, akawashinda, hata wakatoka mbio katika nyumba ile hali wa uchi na kujeruhiwa.” Hawa watu walijaribu kutembea kwa upako wa mtume Paulo mwisho wakaaibika. Kuna watu hawataki kupandishwa taratibu na Bwana hivyo wanataka wakope ili mkutano uwe mkubwa kama wa mhubiri fulani. Matokeo yake wanaanza kuwalemea washiriki wa mkutano ili waweze kulipa madeni. 

4. Kuwa na mipango na kukosa mikakati. Kuna watu wana mipango mizuri sana lakini inashindikana kutekelezeka kwa vile hakuna mkakati. Lk 14:28-30 “Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia? Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki, wakisema, Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za kumaliza.” Bwana Yesu anatukumbusha kwamba katika mipango yetu tuhesabu gharama na kulinganisha na nguvu yetu ili tusije tukachekwa. Mkakati unaweza kusaidia kugundua raslimali zilizopo ili pesa zisitumike kununua kila kitu au kubana matumizi ili kufikia lengo nk. 

5. Kuamua kutumia imani ibadani peke yake Watu wengi tunapenda kuzungumzia imani katika mahubiri, maombi na mikesha lakini tumeshindwa kuitumia imani kujibu haja zetu. Ukisoma Waebrania 11 utaona karibu mara 20 mwandishi akisema KWA IMANI, FULANI AMEFANYA JAMBO FULANI. Wewe umefanya mazoezi ya kufanya jambo gani kwa imani bila kumtegemea mwanadamu? Kumbuka mwanadamu hana tofauti na shetani kama imani yake ni ya kusimulia tu na haina matokeo dhahiri. Shetani anaamini lakini hayuko tayari kuifanyia kazi. Yakobo 2:19 “Wewe waamini ya kuwa Mungu ni mmoja; watenda vema. Mashetani nao waamini na kutetemeka.” Haya ni baadhi tu ya mambo muhimu ya kutusaidia ili tuzitumie vizuri huduma tulizopewa na tujue tunaweza kushiriki vipi katika kuujenga mwili wa Kristo. Ubarikiwe na Bwana! 

Dr Lawi Mshana, +255712924234, Korogwe, Tanga, Tanzania