Ticker

6/recent/ticker-posts

Nini kinasababisha tatizo lirudi baada ya mtu kuponywa

NINI KINASABABISHA TATIZO LIRUDI BAADA YA MTU KUPONYWA? – Dr Lawi Mshana Mungu tunayemuabudu anaponya pale maombi ya imani yanapofanyika. Zaburi 103:3 “Akusamehe maovu yako yote, Akuponya magonjwa yako yote.” Wakati mwingine uponyaji unatokea kwa wepesi ikiwa anayeombea ana karama za kuponya magonjwa. 1 Wakorintho 12:9 “mwingine imani katika Roho yeye yule; na mwingine karama za kuponya katika Roho yule mmoja.” Biblia iko wazi kwamba sio wote wamepewa karama za kuponya wagonjwa. 1 Wakorintho 12:30 “Wote wana karama za kuponya wagonjwa? Wote wanena kwa lugha? Wote wafasiri?” Hivyo wakati mwingine hata kama tunaishi maisha matakatifu tunaweza kuteseka na magonjwa kama hatutawatambua watu waliopewa karama za kuponya magonjwa. Lakini kuna wakati watu wanaponywa magonjwa, mapepo yanawatoka, vifungo vinafunguliwa nk halafu matatizo hayo yanarudi tena. Sababu yake ni nini? 1. Mtu kutolewa pepo halafu hampokei Yesu moyoni mwake. Lk 11:24-26 “Pepo mchafu amtokapo mtu, hupitia mahali pasipo maji, akitafuta mahali pa kupumzika; asipoona, husema, Nitairudia nyumba yangu niliyotoka. Hata afikapo, akaiona imefagiwa na kupambwa, ndipo huenda akachukua pepo wengine saba, walio waovu kuliko yeye mwenyewe, wakaingia na kukaa humo; na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya kwanza.” Pepo anapomtoka mtu aliyekaa ndani yake kwa muda mrefu, mara nyingi hapati mazingira mazuri (ya starehe) kama hayo aliyokuwa nayo awali. Kwa hiyo anapokosa mazingira mazuri anakumbuka makazi yake ya zamani na kujaribu kurudi tena. Akirudi na kukuta “nafasi ni tupu” yaani alipotolewa nafasi yake haikuchukuliwa na Bwana Yesu, anaenda kuita wenzake saba waovu kuliko yeye ili mtu huyo asiweze tena kufunguliwa. Kama mtu ana pepo na hataki kuokoka, (labda kama amepagawa na kushindwa kufanya maamuzi) afadhali aachwe na pepo lake moja kuliko kulitoa na kumsababishia matatizo makubwa zaidi. Tusipende kufanya kazi za kutoa mapepo kama maonyesho bali tufuate kanuni za Mungu ili watu wasije wakaharibikiwa zaidi. Kumbuka sio watu wote wana haja ya kuponywa hata kama wanaumwa. Kuna watu wameridhika na maisha yao ila ni wewe tu unawahurumia. Luka 9:11 “Na makutano walipojua walimfuata; akawakaribisha, akawa akisema nao habari za ufalme wa Mungu, akawaponya wale wenye haja ya kuponywa.” 2. Kutenda dhambi tena (kurudia ile uliyoiacha au kutenda dhambi nyingine mpya) Yohana 5:14 “Baada ya hayo Yesu akamkuta ndani ya hekalu, akamwambia, Angalia, umekuwa mzima; usitende dhambi tena, lisije likakupata jambo lililo baya zaidi.” Huyu ni mtu aliyekuwa mgonjwa kwa miaka 38 akaponywa na Yesu na kutahadharishwa na Yesu mwenyewe. Dhambi ni mlango wa magonjwa na mateso. Hivyo mtu anapoponywa halafu akarudia dhambi zake au akaanza dhambi mpya, anampa shetani nafasi ya kurudisha tatizo lililokuwa limeondoka. Ndiyo maana tunaonywa kwamba tusimpe Ibilisi nafasi (mlango). Waefeso 4:27 “wala msimpe Ibilisi nafasi.” Ni kweli kwamba tunapewa mamlaka tulipomwamini Yesu lakini mamlaka hiyo haifanyi kazi kama tumemuasi Mungu. Lazima tutunze vazi la wokovu wetu lisichafuke. Tukijilinda shetani hataweza kutugusa. 1 Yohana 5:18 “Twajua ya kuwa kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi; bali yeye aliyezaliwa na Mungu hujilinda, wala yule mwovu hamgusi.” Shetani hawezi kuingia katika maisha ya mtu bila kufunguliwa mlango. Mara nyingi atakushawishi mpaka ufungue mwenyewe kwa hiari yako. 3. Kuwa na mashaka na hofu Tunaishi kwa imani na si kwa kuona. 2 Wakorintho 5:7 “(Maana twaenenda kwa imani, si kwa kuona.)” Mara nyingi mtu aliyezoea ugonjwa au tatizo kwa miaka mingi ni rahisi kuruhusu mashaka hasa anapoona dalili fulani kama alizokuwa nazo awali. Siku moja mtu alikemewa pepo likatoka. Baada ya muda akasema, “Sijui limerudi?” Hapohapo pepo likarudi. Hofu ni imani katika tatizo lako hivyo inafungua mlango wa tatizo lako. Hutakiwi kuongozwa na hisia zako bali na Neno la Mungu lisiloshindwa. Mtu wa kusitasita hawezi kupokea uponyaji wa kudumu. Kupona ni suala moja na kutunza uponyaji ni suala jingine. Unaweza kupona lakini ushindwe kutunza uponyaji ulioupokea. Yak 1:6,7 “Ila na aombe kwa imani, pasipo shaka yo yote; maana mwenye shaka ni kama wimbi la bahari lililochukuliwa na upepo, na kupeperushwa huku na huku. Maana mtu kama yule asidhani ya kuwa atapokea kitu kwa Bwana.” Kumbuka roho ya woga haitoki kwa Mungu bali kwa shetani. 2 Timotheo 1:7 “Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi.” Zaburi 91:5 “Hutaogopa hofu ya usiku, Wala mshale urukao mchana.” 4. Kutoombewa mahali sahihi na kuishia njiani Si wakati wote Bwana Yesu aliponya matatizo kwa mara moja (instantaneous). Wakati mwingine aliponya kwa mchakato au kwa hatua. Mk 8:22-26 “Wakafika Bethsaida, wakamletea kipofu, wakamsihi amguse. Akamshika mkono yule kipofu, akamchukua nje ya kijiji, akamtemea mate ya macho, akamwekea mikono yake, akamwuliza, Waona kitu? Akatazama juu, akasema, Naona watu kama miti, inakwenda. Ndipo akaweka tena mikono yake juu ya macho yake, naye akatazama sana; akawa mzima, akaona vyote waziwazi. Akampeleka nyumbani kwake, akisema, Hata kijijini usiingie.” Kuna watu wakishaona mtu ameanguka wakati akiombewa wanadhani matatizo yote yameisha. Mara nyingi kuanguka kunakuwa ni ishara kwamba kuna roho fulani imekutana na nguvu za Mungu au Mungu anataka kufanya operesheni fulani (inategemea uangukaji ukoje). Hata hivyo kuna wakati mtu anaweza kuanguka kwa vile ameguswa na mtu anayeombea ambaye amevaa pete fulani ya kuzimu (uangalifu unahitajika). Mara nyingi mapepo yanapotoka yanaanza yale madhaifu maana yanazidiana uwezo. Mkuu wa pepo anaweza kukaa kwa muda mpaka aone wenzake wametoka wote. Kama maombi hayatafanyika kwa mfululizo mkuu wa pepo anaweza kukaribisha wengine. Bwana Yesu alimtoa huyu kipofu nje ya kijiji ndipo akaanza mchakato wa kumponya. Alimuuliza kujua hatua za uponyaji. Hakumlazimisha kwamba akiri amepona. Alipoelezea mabadiliko Yesu alijua bado kuna kitu kimebaki. Na alipoona amepona kabisa akamwambia KIJIJINI USIIINGIE. Bwana Yesu anajua yote lakini alipenda kutufundisha kwamba sio wakati wote tunagundua matatizo ya watu kwa ufunuo (revelation). Kuna wakati tunagundua kwa kwa utafiti (spiritual diagnosis). Kuna watu hawataweza kupona kikamilifu kama wataombewa na kurudi nyumbani kila siku kwa vile kuna maagano ambayo yako kwenye nyumba zao. Kuna watu nalazimika kuwahamishia nyumbani pale inapowezekana ili waponywe kwa uhakika zaidi. (Kwa sasa tuna kituo ambacho mtu anaweza kuombewa mpaka afunguliwe ikiwa tatizo lake linahitaji aina hiyo ya maombezi). Ni kosa kubwa kumlazimisha mtu akiri uponyaji wakati kuna mapepo yalikuwa hayajatoka bado! 5. Kutofuata maelekezo na kuvunja masharti 2 Fal 5:13,14 “Watumishi wake wakamkaribia, wakamwambia, wakasema, Baba yangu, kama yule nabii angalikuambia kutenda jambo kubwa, usingalilitenda? Je! Si zaidi basi, akikuambia, Jioshe, uwe safi? Ndipo akashuka, akajichovya mara saba katika Yordani, sawasawa na neno lake yule mtu wa Mungu; nayo nyama ya mwili wake ikarudi ikawa kama nyama ya mwili wa mtoto mchanga, akawa safi.” Kuna wakati mtumishi anayeombea anaweza kupewa maelekezo fulani. Mfano nabii Elisha alimwambia mwenye ukoma akaoge mara saba. Mwanzoni alisita kwa vile hajui kanuni za Mungu. Aliposhauriwa na watumishi wake na kutii, akapona ukoma wake. Bwana Yesu pia aliwahi kuwaagiza watu wenye ukoma wakajionyeshe kwa makuhani wakapona wakiwa njiani. Luka 17:14 “Alipowaona aliwaambia, Enendeni, mkajionyeshe kwa makuhani. Ikawa walipokuwa wakienda walitakasika.” Hata hivyo maelekezo utakayopewa na mtumishi hayapaswi kupingana na Neno la Mungu na lazima utakuwa na amani moyoni. Lakini pia lazima mtu azingatie mambo yaliyosababisha tatizo lake. Mfano kama mtu ameponywa kisukari, na alipata ugonjwa huo kwa ulaji mbovu, lazima abadili mtindo wake wa maisha. Vinginevyo anaweza kusababisha ugonjwa urudi tena. Kama tatizo la mtu lilitokana na kushinda njaa mchana kutwa, akiponywa aanatakiwa kujali kula kwa wakati. Kama mtu alipata matatizo ya kifua kwa kunywa vinywaji vya baridi sana lazima abadilike. Kwa kifupi tuangalie sana isije ikawa pia tunapata matatizo kwa sababu ya mtindo mbovu wa maisha. Shetani anaweza kudhoofisha maisha ya mtu bila kumuingia bali kwa kumfanya akiuke kanuni za Mungu za maisha. 6. Kupokea uponyaji ambao ni “kiinimacho” Kum 13:1-4 “Kukizuka katikati yako nabii, au mwotaji wa ndoto, akikutolea ishara au ajabu, ikatukia hiyo ishara au hiyo ajabu aliyokuambia akisema, Na tuifuate miungu mingine usiyoijua, tuitumikie hiyo; wewe usiyasikize maneno ya nabii yule, au yule mwotaji wa ndoto, kwa kuwa Bwana, Mungu wenu, yuawajaribu, apate kujua kwamba mwampenda Bwana, Mungu wenu, kwa mioyo yenu yote na roho zenu zote. Tembeeni kwa kumfuata Bwana, Mungu wenu; mcheni na kushika maagizo yake na kuisikia sauti yake, nanyi mtumikieni na kushikamana naye.” Tusiangalie tu MATOKEO bali pia NJIA ILIYOTUMIKA katika kufikia matokeo hayo. Ni vizuri kuangalia mwenendo wa mtu anayetoa huduma ukoje. Shetani ndiye anayepandikiza magonjwa hivyo akitaka kumfanya mtu apate ahueni anatuma pepo kubwa kuliko lile lililopo ili kulidhibiti. Kitakachotokea mtu ataona amepona lakini ataanza utumwa wa aina nyingine. Mfano mtu anaweza kujihisi hana ugonjwa lakini biashara zake zianze kwenda vibaya. Shetani hawezi kumpa mtu kitu chochote bure. Lazima akigharamie hata kama ni kwa njia nyingine. Kuna watu wameenda kuombewa na manabii wa uongo ambao tabia zao ziko wazi kabisa kwamba hazimpi Mungu utukufu na matatizo yao hayaishi. Watumishi hawa wanapenda sana viapo ili anayehudumiwa aogope kusema ukweli kuhusu maovu aliyofanyiwa. Kama mwombaji ni wakala wa shetani anaweza kumuingiza mtu (initiate) kwenye ufalme wa giza matokeo yake kama alihitaji mtoto anapata mimba ya mtoto wa kuzimu ambaye atamkosesha amani maisha yake yote au akifikia umri fulani atapotea katika mazingira tatanishi. Mtu mwenye pepo la uaguzi (spirit of divination) anaweza kukujulisha mambo yako ambayo yako sahihi. Tatizo wengi hawajui tofauti ya pepo la uaguzi na unabii wa Mungu. Mdo 16:16-19 “Ikawa tulipokuwa tukienda mahali pale pa kusali, kijakazi mmoja aliyekuwa na pepo wa uaguzi akatukuta, aliyewapatia bwana zake faida nyingi kwa kuagua. Akamfuata Paulo na sisi akipiga kelele, akisema, Watu hawa ni watumishi wa Mungu aliye juu, wenye kuwahubiria njia ya wokovu. Akafanya hayo siku nyingi. Lakini Paulo akasikitika, akageuka akamwambia yule pepo, Nakuamuru kwa jina la Yesu Kristo, mtoke huyu. Akamtoka saa ile ile. Basi bwana zake walipoona ya kuwa tumaini la faida yao limewapotea, wakawakamata Paulo na Sila, wakawakokota mpaka sokoni mbele ya wakuu wa mji.” Pepo wa uaguzi alisema ujumbe sahihi kuhusu huduma ya Mtume Paulo lakini Paulo akajisikia vibaya moyoni kwa vile chanzo hakikuwa sahihi. Mganga wa kienyeji anaweza kutabiri kitu sahihi ili baada ya kumuamini ndipo aanze taratibu kukudanganya. Hata hivyo hakuna maana yoyote mtu kukuambia amefunuliwa kwamba umevaa sidiria ya rangi nyekundu. Hata waganga wa kienyeji wanafanya sana mambo kama hayo. Unabii wa Mungu unakuambia mambo ya msingi ya hatima yako na makusudi ya Mungu juu ya maisha yako. Moja ya ishara ya wazi ya kutiliwa mashaka ni UTOAJI WA HUDUMA ZA KIROHO KWA KULIPISHA WATU PESA. Biblia imeweka wazi kwamba Mungu amezitoa karama zake bure hivyo zisilipiwe. Mathayo 10:8 “Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure.” Watu wanaruhusiwa kutoa sadaka tena bila kupangiwa kiasi lakini sio kulipia au kulazimishwa kununua vitu fulani ndipo waombewe. Luka 1:37 “kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu.” La msingi tuzingatie kanuni za Mungu katika kutatua matatizo. Wengine hawahitaji maombezi bali wanahitaji tu ushauri na mafundisho maana ufumbuzi wa matatizo yao uko mikononi mwao. Ubarikiwe na Bwana unapochukua hatua hizi za kupokea uponyaji kamili na wa kudumu katika maisha yako na familia yenu. Dr Lawi Mshana, Korogwe, Tanga, Tanzania