Jinsi Mungu anavyoponya magonjwa sugu – Dr Lawi Mshana
Yapo magonjwa ambayo hayana tiba ya kibinadamu kv saratani na UKIMWI. Mungu pekee aliyemuumba mwanadamu ndiye anayeweza kuponya magonjwa ya aina hiyo. Yer 32:27 ‘Tazama, Mimi ni Bwana, Mungu wa wote wenye mwili, je! Kuna neno gumu lolote nisiloliweza?’
Ingawa vipimo vya wanadamu vinasema, ‘haiwezekani kupona ugonjwa ulio nao, Mungu anasema, ‘inawezekana kupona’. Matokeo ya maisha yako hayategemei taarifa uliyopewa kuhusu afya yako bali uchaguzi wako. Inategemea umechagua kuamini taarifa ya vipimo au Mungu asiyeshindwa. Kum 30:19,20 “Nazishuhudiza mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimekuwekea mbele yako uzima na mauti, baraka na laana; basi chagua uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako; kumpenda Bwana, Mungu wako, kuitii sauti yake, na kushikamana naye; kwani hiyo ndiyo uzima wako, na wingi wa siku zako; upate kukaa katika nchi Bwana aliyowaapia baba zako, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kuwa atawapa.” Ni uchaguzi wako utakaokupeleka kwenye UZIMA au KIFO. Vyote viwili vimewekwa mbele yako.
Kabla sijakuandaa au kukupa mafundisho ya kumuuandaa mgonjwa ili apone ugonjwa sugu, napenda ujue Mungu anavyoweza kuponya kwa sababu ambazo ziko nje ya imani ya mgonjwa mwenyewe.
1. Mungu anaweza kumponya mtu kama uponyaji huo utasababisha watu wampe utukufu. Mungu hapendi mtu yeyote aguse utukufu wake. Yn 11:4 “Naye Yesu aliposikia, alisema, Ugonjwa huu si wa mauti, bali ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu, ili Mwana wa Mungu atukuzwe kwa huo.”
2. Mungu anaweza kumponya mtu kama waliompeleka mgonjwa kwake wanaamini kwamba Mungu anaponya kimuujiza. Unaweza kusababisha ndugu au rafiki yako apone. Lk 5:19,20 “Hata walipokosa nafasi ya kumpeleka ndani kwa ajili ya lile kundi la watu, walipanda juu ya dari wakampisha katika matofali ya juu, wakamshusha yeye na kitanda chake katikati mbele ya Yesu. Naye alipoiona imani yao, alimwambia, Ee rafiki, umesamehewa dhambi zako.”.
3. Mungu anaweza kumponya mtu kama anayeombea ana karama za kuponya na yuko tayari kutumiwa na Mungu. Petro hakutumiwa kuponya kwa vile tu ana karama bali kwa sababu siku hiyo alikuwa tayari kutumiwa na Mungu. Mdo 3:6,7 “Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende. Akamshika mkono wa kuume, akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikatiwa nguvu.”
Najua wapo wengi ambao hawaamini kama Mungu anaweza kuponya magonjwa sugu. Imani yao inaishia kwenye kuombea matatizo kama kuumwa kichwa, kuombea daktari awezeshwe kufanya upasuaji salama na kuiombea dawa ifanye kazi. Imani nayo ina viwango vyake. Warumi 1:17 “Kwa maana haki ya Mungu inadhihirishwa ndani yake, toka imani hata imani; kama ilivyoandikwa, Mwenye haki ataishi kwa imani.” Mtu anaweza kuwa muumini lakini mwenye imani haba. Luka 8:25 “Akawaambia, Imani yenu iko wapi? Wakaogopa, wakamaka, wakisema wao kwa wao, Ni nani huyu basi hata anaamuru upepo na maji, navyo vyamtii?”
Hata hivyo, mgonjwa mwenyewe anaweza pia kusababisha uponyaji wa mwili wake.
Yafuatayo ni mambo muhimu ya kuzingatia ili muujiza wa uponyaji utokee:
1. Kubali kweli (facts) za tatizo lako na kubadili tabia.
Lk 17:12,13 ’Na alipoingia katika kijiji kimoja, alikutana na watu kumi wenye ukoma wakasimama mbali wakapaza sauti wakisema, ee Yesu, Bwana mkubwa uturehemu!’. Lazima mtu mwenye ugonjwa sugu alikubali tatizo lake kwamba ni la kweli. Kulikataa tatizo hakusaidii kuliondoa bali kunasababisha lisishughulikiwe. Kabla Mungu hajatenda muujiza wa uponyaji, lazima pia tahadhari zote za kulipunguza tatizo zizingatiwe. Lazima kuepuka mambo yote yanayoongeza kasi ya tatizo mfano kama ni virusi vya UKIMWI mtu asichelewe kupata tiba ya magonjwa nyemelezi na ajikinge na maambukizi ya magonjwa mengine kama vile homa ya matumbo (kwa kuchemsha maji ya kunywa) na malaria (kwa kutumia chandarua) nk.
Hata wenye ukoma wa kipindi cha Yesu walipona kwa kuzingatia mambo haya mawili. Kwanza, walilikubali tatizo kwa kusema, ‘ni najisi, ni najisi’ (Law 13:45,46). Lakini pia waliamua kubadili tabia pale walipokutana na Yesu kwa kusema, ‘Ee Yesu, Bwana mkubwa, uturehemu!’ Kwa msingi huu, kubali kwamba una VVU kama umepima ukawa chanya (+ve) lakini kamwe usibakie kusema, ’mimi ni najisi’. Sema, ‘Ee Yesu unirehemu (uniponye UKIMWI) — yaani, Ee Yesu huruma yako na itende kazi ndani yangu. Rehema ni huruma itendayo kazi. Mtu akikuhurumia anaweza kubaki kwenye kukusikitikia bila kukupa msaada. Lakini akikurehemu atakuhurumia na kufanya chochote anachoweza.
2. Kubali ukweli (truth) wa Biblia kuhusu uponyaji
Zab 103:3 ‘Akusamehe maovu yako yote, akuponya magonjwa yako yote’. Uponyaji wa Mungu hauchagui magonjwa. Imani ya kutokupona inatokana na kuwaza ukubwa wa tatizo lako kuliko ukuu wa Mungu. Maneno unayosikia yana nguvu kubwa ya kukuharibu au kukuinua. Kumbuka imani chanzo chake ni kusikia Neno la Kristo (Rum 10:17). Neno la Kristo ni Neno lenye uvuvio wa Roho Mtakatifu linalokujia kwa wakati muafaka. Hapa nimetofautisha “fact” na “truth”. Ni ukweli usiopingika kwamba una tatizo na vipimo vimethibitisha (fact). Lakini pia ni ukweli usiopingika kwamba Mungu anaponya magonjwa yote (truth). Zaburi 103:3 “Akusamehe maovu yako yote, Akuponya magonjwa yako yote.”
3. Samehe wote unaowahusianisha na tatizo lako bila kusahau kujisamehe mwenyewe.
1 Yoh 3:21,22 ‘Wapenzi, mioyo yetu isipotuhukumu, tuna ujasiri kwa Mungu, na lolote tuombalo, twalipokea kwake’. Ni rahisi kuwa na uchungu moyoni unapofikiria kuhusu mtu unayedhani alikuambukiza, akakuachia wajibu mkubwa. Wakati mwingine unakuwa na majuto ukikumbuka kwamba ulijiingiza mwenyewe kwenye tatizo. Kama umetubu na kuacha uovu, usikubali mashitaka ya hukumu za shetani katika moyo wako. Mkumbushe shetani jinsi hati ya mashitaka yake ilivyofutwa na Yesu msalabani (Kol 2:14). Kumbuka unaweza kusamehewa na Mungu na ushindwe kujisamehe mwenyewe au kuupokea msamaha wa Mungu. Lakini pia samehe wote wanaokuhukumu au wanaoonyesha kuchoshwa na tatizo lako.
4. Amini kwamba Yesu ni ufufuo na uzima (Yn 11:25)
Yn 11:43,44 ‘Naye akiisha kusema hayo, akalia kwa sauti kuu, Lazaro, njoo huku nje. Akatoka yule aliyekufa, amefungwa sanda’. Ikiwa Bwana Yesu alimfufua Lazaro aliyekuwa maiti siku nne, Je! Anashindwa kuponywa mtu mwenye virusi tu ambaye bado hajafa? Lazima wakati wote ukumbuke kwamba Yesu ameshinda kifo na mauti na amemnyang’anya shetani funguo za kuzimu na mauti. Kwa kupigwa kwake (Yesu) tumeponywa (1 Pet 2:24). Hata hivyo Bwana Yesu hakufanya mambo yote katika mchakato wa kumfufua Lazaro. Aliwaagiza waondoe jiwe. Yn 11:39 “Yesu akasema, Liondoeni jiwe. Martha, dada yake yule aliyefariki, akamwambia, Bwana, ananuka sasa; maana amekuwa maiti siku nne.” Kinachozuia wengi kuponywa kimuujiza ni kuingiza mawazo ya kibinadamu kwenye masuala ya kiroho. Yesu hasemi uondoe jiwe kaburini ili aone maiti bali ili amfufue. Bwana Yesu ni zaidi ya mponyaji. Yeye ni UFUFUO NA UZIMA. Anaweza kufufua vilivyokufa katika mwili wako. Inawezekana unatembea lakini kuna viungo vimekufa. Natangaza ufufuo katika mwili wako katika Jina la Yesu.
5. Ombewa na mtumishi mwenye karama za kuponya au matendo ya miujiza na ambaye ana ufunuo wa tatizo lako.
Lk 11:52a ‘Ole wenu, enyi wana-sheria, kwa kuwa mmeuondoa ufunguo wa maarifa’. Mungu amewapa watumishi wake funguo mbalimbali. Mtumishi mmoja anaweza kutumiwa katika kufungua matatizo ya aina fulani na asitumiwe kwa mengine. Tatizo litaondoka upesi kama mtumishi wa Mungu, ana neema ya kuponya matatizo sugu kama la kwako na amepewa ufunuo wa tatizo lako. Usije ukashangaa mtumishi akitumiwa kuponya UKIMWI na asitumiwe kuponya homa ya malaria. Mungu anaponya kulingana na Neno alilompa mtumishi wake kwa wakati huo. Isa 55:11 ‘Ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu, halitanirudia bure bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma’. Hii haina maana uwadharau baadhi ya watumishi kwa vile hawakuweza kutumiwa kwa ajili yako. Kila mtu amepewa sehemu yake. Mtu anaweza kutumiwa kwa miujiza ya uponyaji lakini yeye mwenyewe inakuwa ngumu sana kupata pesa. Tunahitajiana ili yeyote asiwe na kiburi.
6. Fuata maelekezo ya kiufunuo unayopewa
2 Fal 5:10 ‘Naye Elisha akampelekea ujumbe, akisema, Enenda ukaoge katika Yordan mara saba, na nyama ya mwili wako itakurudia, nawe utakuwa safi’. Kama Naaman, mwenye ukoma, angeoga mara sita au mara kumi, hangetakasika ukoma wake. Hata ukuta wa Yeriko haukuanguka kwa sababu ya kuuzunguka tu bali kwa kufuata maelekezo ya jinsi ya kujipanga, idadi ya siku na idadi ya mizunguko (Yos 6:3-9). Hata Bwana Yesu hakuponya watu wote kwa njia moja. Mfano, aliwaambia wenye ukoma, Mkajionyeshe kwa makuhani (Lk 17:14), mwingine akamwambia, Kanawe katika birika la Siloamu (Yn 9:7). Usipunguze wala kuongeza kitu katika maagizo unayopewa na Bwana. Bwana anaangalia utii wako kabla ya kuangalia hitaji lako. Usipende kukiri tu uponyaji wakati hufuati maelekezo unayopewa na mtumishi wa Mungu.
7. Pima tena ili kuthibitisha uponyaji wako
Mt 27:54 ‘...walipoliona tetemeko la nchi na mambo yaliyofanyika, wakaogopa sana, wakisema, Hakika huyu alikuwa ni mwana wa Mungu’. Bwana hakupenda kufufuka kimya kimya bila kufanya jambo linaloonekana kibinadamu. Kwa vile ni vipimo vya hospitali vilisema una VVU au ugonjwa ulio nao, lazima vipimo hivyohivyo vikubali kwamba hakuna tena VVU. Usikiri tu kwa watu bila kupima kwa sababu ya mhemko. Lazima ijulikane kama umeongezewa miaka ya kuishi na virusi bila kuumwa au umeponywa kabisa na virusi vimesalimu amri (havipo tena). Mungu anaweza kuvifanya virusi visiondoke lakini visiwe na madhara kwako. Mtume Paulo alipoomba kwamba Mungu amuondolee mwiba, Mungu aliamua kumpa NEEMA ya kuishi na mwiba huo badala ya kumpa UPONYAJI. 2 Kor 12:7-9 “Na makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi, kwa wingi wa mafunuo hayo nalipewa mwiba katika mwili, mjumbe wa Shetani ili anipige, nisije nikajivuna kupita kiasi. Kwa ajili ya kitu hicho nalimsihi Bwana mara tatu kwamba kinitoke. Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu.” Mungu anajua nini kitatokea akikuponya kabisa tatizo lako. Kwa Paulo aliona atajivuna kwa huduma kubwa aliyopewa. Wewe Mungu anaweza kuona kwamba utarudi kwenye dhambi au utahukumu wengine.
8. Vipimo visiathiri uhakika wako wa kupona
Mit 23:7 “Maana aonavyo nafsini mwake ndivyo alivyo”. Huwezi kuwa tofauti na mawazo yako (you are what you think). Usivunjike moyo kama bado vipimo vinasema virusi vipo. Katika ukweli wa kimwili (fact) virusi vipo lakini katika ukweli wa kiimani (truth), havipo. Amini kwamba ipo siku havitaonekana tena ndani yako. Unavyoendelea kukiri hatimaye majibu dhahiri yatatokea. Niliwahi kupata ushuhuda fulani. Kuna mtu alimuombea mwanae aliyeota nyama kwenye jicho ili Mungu amponye. Siku moja saa 4 usiku akajisikia moyoni kwamba ameponywa. Akaenda kitandani kumuona akakuta bado uvimbe upo. Kesho yake wakiwa mezani wanakula chakula, akaona bado upo. Lakini yeye akawa anasema NAJUA MWANANGU ALIPONA TANGU JANA SAA NNE USIKU. Aliendelea kuona uvimbe na kukiri uponyaji mpaka akasahau. Siku moja alipomuangalia mwanae akashangaa ile nyama imeondoka. Hata Bwana Yesu alipoulaani mtini mizizi yake ilinyauka hapohapo lakini majani yalichukua muda. Mk 11:20-24 “Na asubuhi walipokuwa wakipita, waliuona ule mtini umenyauka toka shinani. Petro akakumbuka habari yake, akamwambia, Rabi, tazama, mtini ulioulaani umenyauka. Yesu akajibu, akamwambia, Mwaminini Mungu. Amin, nawaambia, Ye yote atakayeuambia mlima huu, Ng'oka ukatupwe baharini, wala asione shaka moyoni mwake, ila aamini kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake. Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.” Yesu aliposema mwaminini Mungu alimaanisha IWENI NA IMANI YA KIMUNGU. Mpendwa unayeamini haya, uponyaji ni wa kwako kuanzia sasa unaposoma ujumbe huu!
9. Usimlazimishe Mungu
Ebr 11:1 “Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo”. Kama Mungu hajakupa uhakika (assurance) kuhusu uponyaji, usijitengenezee imani yako mwenyewe. Afadhali uombe kuongezewa imani. Luka 17:5 “Mitume wakamwambia Bwana, Tuongezee imani.” Lazima Mungu akujalie kwanza kuweza kutarajia yasiyoweza kutarajiwa. Ibrahimu alikuwa na miaka 100 na akatarajia kupata mtoto. Rum 4:18, 19 “Naye aliamini kwa kutarajia yasiyoweza kutarajiwa, ili apate kuwa baba wa mataifa mengi, kama ilivyonenwa, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako. Yeye asiyekuwa dhaifu wa imani, alifikiri hali ya mwili wake uliokuwa umekwisha kufa, (akiwa amekwisha kupata umri wa kama miaka mia), na hali ya kufa ya tumbo lake Sara.”. Usiache matibabu ya hospitalini kwa kumuiga mtu fulani. Pata uhakika wa ki-Mungu ndipo imani yako itatenda kazi. Rum 4:21 “huku akijua hakika ya kuwa Mungu aweza kufanya yale aliyoahidi.” Fanya lile ambalo unajisikia uhakika moyoni bila kuchelewa.
10. Usimjaribu Mungu
Lk 9:11 “...Akawaponya wale wenye haja ya kuponywa”. Hakikisha hitaji la kuponywa kwa imani ni la kwako mwenyewe na hukushinikizwa na watu. Wala usiombewe kama mtu anayejaribisha dawa. Hakikisha unaamini kwamba hakuna jambo lisilowezekana kwa Mungu (Lk 1:37). Usikiri tu uponyaji wakati hutaki kuacha dhambi. Dhambi ni mlango wa kuingiza au kurudisha magonjwa. Yn 5:14 ‘….Angalia, umekuwa mzima, usitende dhambi tena, lisije likakupata jambo lililo baya zaidi’. Pia usimuendee mtumishi wa Mungu kama vile unamuendea mganga wa kienyeji. Mtumishi anaweza kuongozwa na Roho Mtakatifu akuombee tofauti na unavyotaka. Mfano Mungu anaweza kumwambia mtumishi wake usimuombee huyu uponyaji kwa vile hana utii kwangu. Muombee roho ya toba au muonye. Yeremia 11:14 “Basi, usiwaombee watu hawa, wala usipaze sauti yako, wala kuwaombea dua watu hawa; maana sitawasikia wakati watakaponililia kwa ajili ya taabu yao.” Yeremia 14:11 “Naye Bwana akaniambia, Usiwaombee watu hawa wapate heri.”
Naomba Mungu atumie ujumbe huu kuponya tatizo lako lolote lililoshindikana hata kama sio ugonjwa wa mwili kama vile ndoa yako, familia yako, kazini kwako nk. Napenda kusisitiza kwamba usihusianishe ujumbe huu na watu wengine. Na kama kwa bahati mbaya umekutana na ujumbe huu na unaona sio wa kwako, acha kuusoma na kuwakatisha tamaa walengwa wa ujumbe huu. Siku zote Mungu analituma Neno lake kwa ajili ya mtu fulani. Kumbuka Mungu hatafuti watu, anatafuta mtu. Eze 22:30 “Nami nikatafuta mtu miongoni mwao, atakayelitengeneza boma, na kusimama mbele zangu mahali palipobomoka, kwa ajili ya nchi, nisije nikaiharibu, lakini sikuona mtu.”
Natamka uponyaji na ufufuo katika maeneo yote ya maisha yako katika Jina lipitalo majina yote la YESU KRISTO!
Dr Lawi Mshana, Korogwe, Tanga, Tanzania
Unauthorized use and/or duplication of this material without express and written permission from this site’s author and owner is strictly prohibited.
Excerpts and links may be used, provided that full and clear credits is given to Lawi Mshana and www.lawimshana.com with appropriate and specific direction to the original content.