UNAJUA MTU ALIYELAANIWA YUKOJE?
Ni ukweli usiopingika kwamba Neno la Mungu linasema Kristo ametukomboa kutoka katika laana. Gal 3:13 “Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti.” Kila tunachohitaji kipo kwa Yesu Kristo. Yesu alikufa kifo cha kikatili sana akaimwaga damu kwa ajili ya ukombozi wetu. Katika kifo chake alimshinda shetani jumla, akatupatia uzima wa milele, uponyaji kwa ajili ya magonjwa yetu yote na ukombozi kutoka katika laana za vizazi. Ingawa hakutenda dhambi yoyote, alifanyika laana kwa ajili yetu kwa kuangikwa juu ya mti. Isa 53:6 “Sisi sote kama kondoo tumepotea; Kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe; Na Bwana ameweka juu yake Maovu yetu sisi sote.”
Tunawezaje kupata laana?
1. Kutoka kwa Mungu mwenyewe (kutokana na dhambi zetu).
Kum 28:20 “Bwana atakuletea laana na mashaka, na kukemewa, katika yote utakayotia mkono wako kuyafanya, hata uangamie na kupotea kwa upesi; kwa ule uovu wa matendo yako, uliyoniacha kwayo.” Hata unapofanya kazi ya Mungu kwa ulegevu unalaaniwa. Yeremia 48:10a “Na alaaniwe mtu afanyaye kazi ya Bwana kwa ulegevu.” Usipotoa zaka na dhabihu pia unalaaniwa. Mal 3:8,9 “Je! Mwanadamu atamwibia Mungu? Lakini ninyi mnaniibia mimi. Lakini ninyi mwasema, Tumekuibia kwa namna gani? Mmeniibia zaka na dhabihu. Ninyi mmelaaniwa kwa laana; maana mnaniibia mimi, naam, taifa hili lote.”
2. Kutoka kwa wazazi wa kimwili.
Mwa 9:24,25 “Nuhu akalevuka katika ulevi wake, akajua mwana wake mdogo alivyomtendea. Akasema,Na alaaniwe Kaanani; Atakuwa mtumwa kabisa kwa ndugu zake.” Unapomdharau mzazi wako unaweza kulaaniwa hata kama uko sahihi kuliko yeye. Kuheshimu wazazi ni moja ya amri za Mungu. Mt 15:4 “Kwa kuwa Mungu alisema, Mheshimu baba yako na mama yako, na Amtukanaye baba yake au mama yake kufa na afe.” Uko salama kama tu umekataa kutii agizo la mzazi ambalo liko kinyume na Mungu aliyemuumba mzazi huyo.
3. Kutoka kwa wazazi wa kiroho au watumishi wa Mungu.
2 Fal 2:23,24 “Akakwea kutoka huko mpaka Betheli; naye alipokuwa akienda njiani, wakatoka vijana katika mji, wakamfanyizia mzaha, wakamwambia, Paa wewe mwenye upaa! Paa wewe mwenye upaa! Akatazama nyuma akawaona, akawalaani kwa jina la Bwana. Wakatoka dubu wawili wa kike mwituni, wakawararua vijana arobaini na wawili miongoni mwao.” Kuna watu wamedharau na kuwanenea mabaya watumishi wa Mungu waliowekeza vitu vingi ndani yao. Leo hii hawana upenyo wowote wa kiroho wala kiuchumi. Kibaya zaidi hawako tayari kuwaendea wazazi wao ili kuomba msamaha bali wanazunguka tu kuombewa na watumishi wengine. Laana inafanyiwa kazi tofauti na matatizo mengine.
4. Kutoka kwa shetani na mawakala wake.
1 Samweli 17:43 “Mfilisti akamwambia Daudi, Je! Mimi ni mbwa hata umenijia kwa fimbo? Mfilisti akamlaani Daudi kwa miungu yake.” Watu wengi wana matatizo kwa vile hawakuyakataa maneno ya wachawi. Mchawi akitaka kukuloga lazima akupe kwanza maneno fulani ya kukufanya uogope au uyaamini. Mfano, anaweza kukuambia naona duka lako linaisha! Unachotakiwa kufanya ni kuyafuta maneno hayo tena ikiwezekana mbele yake. Umwambie, “Biashara yangu haifi katika Jina la Yesu, tena hili ni duka kubwa saana ni macho yako tu hayaoni!” Ila kama hujaokoka na kumuishia Bwana usitaje Jina hili bure usije ukapata matatizo. Kuna waliojaribu kufanya hivyo wakapata matatizo makubwa. Shetani anajua maisha yako yakoje mbele za Mungu. Mdo 19:13-16 “Baadhi ya Wayahudi wenye kutanga-tanga, nao ni wapunga pepo, wakajaribu kutaja jina la Bwana Yesu juu yao waliopagawa na pepo wachafu, wakisema, Nawaapisha kwa Yesu, yule anayehubiriwa na Paulo. Walikuwako wana saba wa mtu mmoja Skewa, Myahudi, kuhani mkuu, waliofanya hivyo. Yule pepo mchafu akawajibu, akawaambia, Yesu namjua na Paulo namfahamu, lakini ninyi ni nani? Na yule mtu aliyepagawa na pepo mchafu akawarukia wawili, akawaweza, akawashinda, hata wakatoka mbio katika nyumba ile hali wa uchi na kujeruhiwa.” Wapo pia waliolaaniwa na watumishi wa shetani baada ya kushiriki ibada zao na kula viapo kisha wakatoka bila kuvunja maagano.
5. Kutokana na dhambi za mababu.
Kum 5:9 “Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi Bwana, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu, nawapatiliza wana uovu wa baba zao; hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao.” Kuna watu wana matatizo yale yale yanayosumbua ukoo ingawa wao tayari wanamjua Mungu. Matatizo yao yataisha kama watayachukua kama ya ukoo kwa kuungama dhambi walizofanya babu zao. Mfano, katika kikao cha ukoo walisema atakayeoa kwenye ukoo fulani apate kisukari pamoja na kizazi chake. Kwa vile walifanya ibada maalum na kuchanjiana damu, huwezi kulikwepa hili kama hutavunja hayo maagano. Na kama unabisha jaribu kukiuka kienyeji uone! Ndiyo maana tunaambiwa TOKENI KATI YAO MKATENGWE NAO (2 Kor 6:17). Haina maana uwakimbie kabisa ndugu zako ila usishiriki ibada za maagano ya kishetani ambazo wanazifanya. 1 Kor 10:20 “Sivyo, lakini vitu vile wavitoavyo sadaka wavitoa kwa mashetani, wala si kwa Mungu; nami sipendi ninyi kushirikiana na mashetani. Hamwezi kunywea kikombe cha Bwana na kikombe cha mashetani.” Unakwama maisha kwa vile umekula hivyo vyakula. Hata kama utajaribu kukemea kwa Jina la Yesu hutafanikiwa kwa vile umesajiliwa tayari. Unakuwa umeshaingizwa (initiated) kwenye maagano hata kama hutaki.
Yn 9:2,3 “Wanafunzi wake wakamwuliza wakisema, Rabi, ni yupi aliyetenda dhambi, mtu huyu au wazazi wake, hata azaliwe kipofu? Yesu akajibu, Huyu hakutenda dhambi, wala wazazi wake; bali kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yake.” Ukilichunguza sana jibu la Yesu lina maana wapo ambao ni vipofu kwa sababu ya dhambi zao wenyewe au dhambi za wazazi wao ila kwa suala la huyu ni tofauti. Mungu ameruhusu hali hii impate ili atimize kusudi lake fulani.
Mara nyingi tunapata laana kwa uchaguzi wetu wenyewe. Kum 11:26-28 “Angalieni, nawawekea mbele yenu hivi leo baraka na laana; baraka ni hapo mtakapoyasikiza maagizo ya Bwana, Mungu wenu, niwaagizayo leo; na laana ni hapo msiposikiza maagizo ya Bwana, Mungu wenu, mkikengeuka katika njia niwaagizayo leo, kwa kuandama miungu mingine msiyoijua.” Shetani hawezi kuingia katika maisha yetu kama hakuna mlango tuliompa. Lazima apate “haki ya kisheria (legal right)” ndipo atafanya kazi. Waefeso 4:27 “wala msimpe Ibilisi nafasi.” Hivyo usijidanganye kwamba huwezi kulaaniwa wakati kuna sababu ya wewe kulaaniwa. Mit 26:2b “Kadhalika laana isiyo na sababu haimpigi mtu.”
LAZIMA TUTAMBUE MAMLAKA TULIYOPEWA NA JINSI YA KUITUMIA
Unaweza kuwa na Biblia na isikusaidie kama hujui jinsi ya kuitumia. Kuna watu wanaiweka Biblia chini ya mto (pillow) wakilala lakini bado wanakabwa na majinamizi. Unaweza kuimba nyimbo zinazotaja Jina la Yesu na bado uteswe na shetani kwa vile Yesu hayuko moyoni mwako. Unaweza kumilikiwa na kuteswa na mapepo ingawa Yesu alikufa na kufufuka kwa vile mapepo hayo hayajakemewa na mtu mwenye mamlaka au wewe mwenyewe umeyafungulia mlango. Unaweza kuteswa na matatizo yaleyale yaliyomtesa babu au bibi yako kwa vile maagano yaliyofanyika zamani hajavunjwa na mtu mwenye mamlaka. Kwa kifupi hakuna matatizo yataondoka yenyewe kwa vile tu una dini au umeamini. Lazima hatua ichukuliwe. Ndiyo maana Biblia imejaa maneno kama kemea, omba, tubu, vunja, haribu, tafuta nk. Hata Mungu ilimgharimu kumtuma Yesu (Adamu wa pili) ili kushinda yale ambayo Adamu wa kwanza alishindwa. Vinginevyo hatungepata ukombozi. Rum 5:14,15 “walakini mauti ilitawala tangu Adamu mpaka Musa, nayo iliwatawala hata wao wasiofanya dhambi ifananayo na kosa la Adamu, aliye mfano wake yeye atakayekuja. Lakini karama ile haikuwa kama lile kosa; kwa maana ikiwa kwa kukosa kwake yule mmoja wengi walikufa, zaidi sana neema ya Mungu, na kipawa kilicho katika neema yake mwanadamu mmoja Yesu Kristo kimezidi kwa ajili ya wale wengi.”
Kama mtu wa Mungu au mtumishi wa Mungu anapougua anaombewa uponyaji, anaweza pia kuwa katika laana na kuhitaji kuvunja maagano yaliyosababisha laana hiyo. Pamoja na kwamba Yesu alisema IMEKWISHA miaka zaidi ya 2000 iliyopita bado tuna watu tena wanaomuamini ambao bado hawajanufaika kikamilifu na uhuru uliotangazwa. Tusipende kulitumia Jina la Yesu kutoa mapepo ya wengine tu wakati sisi wenyewe tunatumikishwa.
Kama unakataa kwamba hakuna shida ngoja nikupe mifano michache uone kama hatuabudu na watu wenye vifungo na laana katika dini zetu:
1.Je hakuna watu ambao ndoa zao zina migogoro isiyoisha ingawa zilifungwa kwa kanuni zote za kimaandiko?
2.Je hakuna watu ambao hata sadaka ya kutoa hawana na wala hawana uhakika watakula nini nyumbani ingawa wana bidii ya kazi?
3.Je hakuna watu tena wanaotumika madhabahuni wanazini huku wanaimba kwaya, wanahubiri na kushiriki maombi na mikesha?
4.Je hakuna watu ambao misiba na magonjwa yanafanya kusubiri pesa zao ili yazitafune kila zinapopatikana?
5.Je hakuna watu ambao mahubiri yakianza tu wanalala usingizi utadhani walikuwa kwenye mkesha?
6.Je hakuna watu wana tabia na magonjwa yale yale waliyokuwa nayo babu na bibi zao ambao hawakumwamini Yesu?
7.Je hakuna watu hawasalimiani na hawawezi kukaa pamoja hata wanapokutana ibadani?
8.Je hakuna watumishi wa Mungu wanaohukumu wenzao utadhani wao walienda mbinguni wakarudi?
9.Je hakuna watu wanavaa nguo za kukosesha wenzao tena wakiwa wanahudumu madhabahuni au wanaporikodi DVD zao na wala hawahukumiwi moyoni? Je hawajafundishwa adhabu ya dhambi ya kukosesha? (Mt 18:7-9 “Ole ni wa ulimwengu kwa sababu ya mambo ya kukosesha! Maana hayana budi kuja mambo ya kukosesha; lakini ole wake mtu yule aliletaye jambo la kukosesha! Basi mkono wako au mguu wako ukikukosesha, ukate ukautupe mbali nawe; ni afadhali kuingia katika uzima hali umepungukiwa na mkono au mguu, kuliko kuwa na mikono miwili au miguu miwili, na kutupwa katika moto wa milele. Na jicho lako likikukosesha, ling'oe, ukalitupe mbali nawe; ni afadhali kuingia katika uzima una chongo, kuliko kuwa na macho mawili, na kutupwa katika jehanum ya moto.”)
10.Je hakuna watu wanaiba mpaka fedha zilizotolewa kwa ajili ya kazi ya Mungu?
11.Je hakuna watu wanawakiana tamaa na kufanya uzinzi wa moyoni na wameshindwa kuacha tabia hizo?
12.Je hakuna watu wenye pesa lakini wameshindwa kumtolea Mungu inavyotakiwa na michango yao inaishia kwenye arusi za kifahari, misiba na kuhonga watu?
13.Je hakuna watumishi wamelazimika kukopa kwa ajili ya kazi ya Mungu na kushindwa kulipa deni? Je Bwana Yesu alipowatuma wanafunzi wake hakutimiza mahitaji yao? Luka 22:35 “Akawauliza, Je! Hapo nilipowatuma hamna mfuko, wala mkoba, wala viatu, mlipungukiwa na kitu? Wakasema, La!”
14.Je hakuna watumishi ambao milango ya uchumi imefunga kiasi kwamba wanalazimika kutumia hila na ujanja katika mahubiri yao ili pesa zipatikane?
Hii ni mifano michache tu ya kuthibitisha kwamba tunahitaji kufunguliwa ili tule mema ya nchi na mwisho tukakae na Bwana milele.
BIBLIA INASEMA MTU ALIYELAANIWA YUKOJE?
Tambua kwamba nakupa maandiko haya ili utambue laana na kuchukua hatua ya kutoka katika laana na sio kukata tamaa au kulaumu mtu mwingine. Kumbuka pia kwamba si kila tatizo ni laana. Laana ni pale tatizo linapojirudia sana na kushindikana kupata ufumbuzi hata pale raslimali zinapokuwepo. Mfano, hata mtu apewe mtaji mara nyingi bado biashara zake zinafilisika tu.
Kutokana na Kumbukumbu 28, mtu aliyelaaniwa:
1.Hata atoke kijijini na kuhamia mjini hafanikiwi. Mst 16,19: “Utalaaniwa mjini, utalaaniwa na mashambani. Utalaaniwa uingiapo, utalaaniwa na utokapo.”
2.Njia zake za kipato hazimpi faida. Mst 17: “Litalaaniwa kapu lako na chombo chako cha kukandia.”
3.Kila anachoanzisha hakiendelei. Mst 18 “Utalaaniwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, maongeo ya ng'ombe wako, na wadogo wa kondoo zako.”
4.Hanufaiki na taabu yake kuanzia kwenye ndoa, watoto na shughuli zake. Mst 30,32-34,41 “Utaposa mke na mume mwingine atalala naye; utajenga nyumba usiikae; utapanda mizabibu usitumie matunda yake. Wanao na binti zako litapewa taifa lingine, na macho yako yataangalia, na kuzimia kwa kuwatamani mchana kutwa; wala hapatakuwa na kitu katika uwezo wa mkono wako. Matunda ya nchi yako, na taabu yako yote, vitaliwa na taifa usilolijua; utaonewa tu, na kupondwa chini daima; hata uwe mwenye wazimu kwa yaonwayo na macho yako, utakayoyaona. Utazaa wana na binti, lakini hawatakuwa wako wewe; kwa sababu watakwenda utumwani.”
5.Anapata hasara zisizoisha katika shughuli zake. Mst 38-40 “Mbegu nyingi utazichukua nje shambani, lakini utavuna haba, kwa kuwa nzige watazila. Utapanda mizabibu na kuitengeza, wala hutakunywa katika divai yake, wala kuichuma kwani italiwa na mabuu. Utakuwa na mizeituni katika mipaka yako yote usijipake mafuta yake; kwa kuwa mzeituni wako utapukutika.”
6. Anapokuja mgeni anainuka wakati yeye habaki tu palepale bali anadidimia. Mst 43, 44 “Mgeni aliye kati yako atazidi kupaa juu yako; nawe utazidi kushuka chini. Yeye atakukopesha, wala wewe usimkopeshe; yeye atakuwa ni kichwa, wewe utakuwa mkia.”
7.Kila anapopata tu pesa panatokea walaji ili asifanye chochote. Mst 50,51 “taifa lenye uso mkali, ambalo haliangalii uso wa mzee, wala halipendelei kijana; naye atakula uzao wa ng'ombe wako wa mifugo, na uzao wa nchi yako mpaka utakapokwisha kuangamizwa; wala hatakuachia nafaka, wala divai, wala mafuta, wala maongeo ya ng'ombe wako, wala wana-kondoo wako, hata atakapokwisha kukuangamiza.”
Kwa kifupi kulaaniwa ni KUWEZESHWA KUSHINDWA (TO BE EMPOWERED TO FAIL)! Yaani kutembea na nguvu ambayo inasababisha kila unachofanya hata kama mazingira fanikishi yapo kisifanikiwe.
Hebu fanyia kazi mambo yafuatayo:
1. Je kuna maneno ya laana umewahi kusikia mzazi au mlezi wako akitamka au mtu alikuambia amesikia mzazi wako akitamka juu yako?
2. Je kuna maneno yoyote ya laana yamewahi kutamkwa juu yako na mtu mwenye mamlaka kv mwalimu, mchungaji, mkuu wa kazi nk?
3. Je kuna maneno yoyote ya laana umewahi kusikia jirani yako au mtu yeyote mwenye sifa mbaya akitamka kwako au kwa mwanao?
USIYAPUUZIE. YANAWEZA KUWA CHANZO KIKUU CHA MATATIZO YAKO! MENGINE YANAKUTAKA UFUNGE SAFARI UKAYAFANYIE KAZI KAMA ALIYEYATAMKA NI NDUGU NA BADO YUKO HAI. MENGINE YANAHITAJI KUOMBA AU KUOMBEWA NA MWENYE MAMLAKA ZAIDI YAKO INAPOBIDI.
Usisahau kwamba tumepewa mamlaka kwa viwango tofauti. Mwingine ni balozi wa nyumba kumi, mwingine kiongozi wa kijiji, mwingine wa kata, mwingine wa wilaya, mwingine wa mkoa nk. Tambua kiwango cha mamlaka yako ulinganishe na ukubwa wa tatizo lako.
Lawi Mshana, +255712924234, Korogwe, Tanga, Tanzania