Ticker

6/recent/ticker-posts

Sisi wote tu viungo katika mwili wa Kristo ili tutegemezane na si kushindana

SISI WOTE TU VIUNGO KATIKA MWILI ILI TUTEGEMEZANE NA SI KUSHINDANA – Dr Lawi Mshana

Ukisoma vizuri maandiko utagundua kwamba tofauti tulizo nazo hazikukusudiwa kutugawa bali kutufanya tuhitajiane. Ukisoma 1 Kor 12:14-27 utagundua mambo ya msingi kuhusu UMOJA KATIKA TOFAUTI ZETU NDANI YA KRISTO (UNITY IN DIVERSITY IN CHRIST).

Andiko hilo linasema hivi “14 Kwa maana mwili si kiungo kimoja, bali ni vingi.15 Mguu ukisema, Kwa kuwa mimi si mkono, mimi si wa mwili; je! Si wa mwili kwa sababu hiyo? 16 Na sikio likisema, Kwa kuwa mimi si jicho, mimi si la mwili; je! Si la mwili kwa sababu hiyo? 17 Kama mwili wote ukiwa jicho, ku wapi kusikia? Kama wote ni sikio ku wapi kunusa?18 Bali Mungu amevitia viungo kila kimoja katika mwili kama alivyotaka. 19 Lakini kama vyote vingekuwa kiungo kimoja, mwili ungekuwa wapi? 20 Lakini sasa viungo ni vingi, ila mwili ni mmoja. 21 Na jicho haliwezi kuuambia mkono, Sina haja na wewe; wala tena kichwa hakiwezi kuiambia miguu, Sina haja na ninyi. 22 Bali zaidi sana vile viungo vya mwili vidhaniwavyo kuwa vinyonge zaidi vyahitajiwa zaidi. 23 Na vile viungo vya mwili vidhaniwavyo kuwa havina heshima, viungo vile twavipa heshima zaidi; na viungo vyetu visivyo na uzuri vina uzuri zaidi sana. 24 Kwa maana viungo vyetu vilivyo na uzuri havina uhitaji; bali Mungu ameuungamanisha mwili, na kukipa heshima zaidi kile kiungo kilichopungukiwa; 25 ili kusiwe na faraka katika mwili, bali viungo vitunzane kila kiungo na mwenziwe. 26 Na kiungo kimoja kikiumia, viungo vyote huumia nacho, na kiungo kimoja kikitukuzwa, viungo vyote hufurahi pamoja nacho. 27 Basi ninyi mmekuwa mwili wa Kristo, na viungo kila kimoja peke yake.”

MAMBO NINAYOJIFUNZA KUTOKANA NA KIFUNGU HIKI KUHUSU KANISA LA MUNGU:

1. Hakuna mtumishi au mtu wa Mungu aliyepewa huduma zote anayeweza kusema amejitosheleza. Kwa maneno mengine hakuna mtumishi ambaye ni mwili wote bali ni kiungo kimoja wapo tu katika mwili. Mst 14 “Kwa maana mwili si kiungo kimoja, bali ni vingi.”

2. Haiwezekani mtumishi wa kweli adharau viungo vingine katika mwili kwa vile mguu lazima utahitaji mkono wakati fulani. Labda kama mtumishi huyo sio sehemu ya mwili bali ni kiumbe kingine tofauti. Mst 15,16 “Mguu ukisema, Kwa kuwa mimi si mkono, mimi si wa mwili; je! Si wa mwili kwa sababu hiyo? Na sikio likisema, Kwa kuwa mimi si jicho, mimi si la mwili; je! Si la mwili kwa sababu hiyo?”

3. Mtumishi akijiona yeye ni mwili mzima lazima yeye na watu anaowasimamia watakosa huduma zingine kwa hiyo kuna matatizo hayataweza kuondoka kirahisi. Watakuwa wana maono makubwa kwa vile ni jicho lakini hawataweza kupambanua nyakati maana wao sio pua hivyo hawawezi kutambua kwa kunusa. Mst 17 “Kama mwili wote ukiwa jicho, ku wapi kusikia? Kama wote ni sikio ku wapi kunusa?”

4. Hakuna mtumishi ana mamlaka ya kuzipangia huduma za Mungu zitende kazi kama anavyotaka. Hivyo ni kosa kubwa kukosoa huduma aliyopewa mtu kwa sababu tu hukuipewa. Sio rahisi jicho litambue utendaji na changamoto za sikio au mguu. Anayejua ni yule aliyeweka sikio au mguu ambaye ni Mungu mwenyewe. Mst 18 “Bali Mungu amevitia viungo kila kimoja katika mwili kama alivyotaka.”

5.  Kama wote tungekuwa kama wewe katika utumishi wetu umuhimu wa Kanisa ungekuwepo? Tofauti zetu za huduma na utendaji ndizo zinaleta ladha ya kanisa. Sikio akisikia sauti anamshtua jicho atazame ni kitu gani. Mkono akigundua macho yameshindwa kuleta taarifa kamili anaamua kupapasa. Kila kiungo kina uwezo wake na mipaka yake katika kutusaidia. Mst 19.20 “Lakini kama vyote vingekuwa kiungo kimoja, mwili ungekuwa wapi? Lakini sasa viungo ni vingi, ila mwili ni mmoja.”

6.  Mtumishi ambaye ni kiungo katika mwili wa Kristo hawezi kumkataa mtumishi mwenzake ambaye yuko katika mwili huohuo. Jicho haliwezi kuwa salama wala kushangilia kama mkono anaumwa. Mst 21 “Na jicho haliwezi kuuambia mkono, Sina haja na wewe; wala tena kichwa hakiwezi kuiambia miguu, Sina haja na ninyi.”

7.  Watu wengi wanadhani watumishi ni wale tu ambao wanasimama madhabahuni kuhubiri na kuimba.Wanasahau kwamba zipo huduma zilizowabeba ndiyo maana hawajaacha huduma. Unaweza kupuuza kidole kidogo cha mkono lakini siku ukiwashwa ndani ya sikio ndipo utagundua ni kidole pekee kinachoweza kuingia ndani zaidi sikioni. Viungo vingine ni aibu hata kuvitaja lakini huwezi kuishi bila hivyo. Viungo vingine vinaheshimiwa zaidi lakini kuna watu hawana na maisha yanaenda. Wapo watu wanaomtolea Mungu kwa sababu ya kazi na biashara zao na bila wao kuna huduma zingekwama kabisa. Kazi zao ni madhabahu pia muhimu sana kwa kanisa. Mst 22,23 “Bali zaidi sana vile viungo vya mwili vidhaniwavyo kuwa vinyonge zaidi vyahitajiwa zaidi. Na vile viungo vya mwili vidhaniwavyo kuwa havina heshima, viungo vile twavipa heshima zaidi; na viungo vyetu visivyo na uzuri vina uzuri zaidi sana.”

8.  Raha ya mtumishi wa Mungu aliyepona na kubarikiwa ni kuona wenzake nao wanainuliwa. Kwa bahati mbaya kuna watumishi ambao wanataka watumishi wenzao watumike kwa mateso kama wao walivyoteseka zamani. Wako tayari kumsaidia shetani kuwapitisha wenzao katika majaribu waliyopitia wao zamani. Mst 24,25 “Kwa maana viungo vyetu vilivyo na uzuri havina uhitaji; bali Mungu ameuungamanisha mwili, na kukipa heshima zaidi kile kiungo kilichopungukiwa; ili kusiwe na faraka katika mwili, bali viungo vitunzane kila kiungo na mwenziwe.”

9. Ni watumishi wachache wako tayari kushiriki mateso ya wengine. Wako tofauti kabisa na andiko hili. Wakisikia askari mwenzao ameanguka au amepata tatizo wanashangilia badala ya kulia. Wakisikia Mungu amembariki mtumishi mwingine wako tayari wamuite Freemason ili tu wahalalishe umasikini wao na kuharibu sifa ya baraka zake.Ukiwauliza Freemason ni nini hata hawana la kusema. Mst 26,27 “Na kiungo kimoja kikiumia, viungo vyote huumia nacho, na kiungo kimoja kikitukuzwa, viungo vyote hufurahi pamoja nacho. Basi ninyi mmekuwa mwili wa Kristo, na viungo kila kimoja peke yake.”

Mungu atusaidie ili tusije tukawa vibao vinavyoelekeza mahali lakini vyenyewe havijawahi kufika na havina mpango huo. Hebu jiulize kile kibao cha shule uliyosoma kimefika lini shuleni tangu umalize masomo yako!  

Mungu atusaidie tusije tukafanana na waandishi na mafarisayo ambao Yesu aliwasema kwa mambo yafuatayo:

1. Wanawazuia watu kuingia katika ufalme wakati wao wenyewe hawaingii.

Mathayo 23:13 “Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnawafungia watu ufalme wa mbinguni; ninyi wenyewe hamwingii, wala wanaoingia hamwaachi waingie.”

2. Wanatumika kwa kujionyesha na kutafuta faida binafsi lakini sio kwa ajili ya kutatua shida za watu.

Mathayo 23:14 “Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnakula nyumba za wajane, na kwa unafiki mnasali sala ndefu; kwa hiyo mtapata hukumu iliyo kubwa zaidi.”

3. Wanajitahidi kuongeza waumini na wakishaingia zizini ni wa kwanza kuwakwaza na kuwaangusha dhambini.

Mathayo 23:15 “Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnazunguka katika bahari na nchi kavu ili kumfanya mtu mmoja kuwa mwongofu; na akiisha kufanyika, mnamfanya kuwa mwana wa jehanum mara mbili zaidi kuliko ninyi wenyewe.”

4. Wanakazia utoaji kuliko uponyaji wa roho za watu. Wanachothamini ni pesa ya mtu lakini sio kuona ameshinda dhambi na mateso aliyo nayo.

Mathayo 23:23 “Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnalipa zaka za mnanaa na bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu ya sheria, yaani, adili, na rehema, na imani; hayo imewapasa kuyafanya, wala yale mengine msiyaache.”

5. Wanajali mwonekano wa nje (utauwa) na sio utakatifu wa moyo. Hata kama muumini anapiga mkewe au mke hajali kumhudumia mumewe, ili mradi anawajibika katika majukumu ya kanisani sio tatizo kwao.  

Mathayo 23:25 “Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnasafisha nje ya kikombe na chano, na ndani yake vimejaa unyang'anyi na kutokuwa na kiasi.”

6. Wanaridhika na taswira na umaarufu wao wanapokuwa katika huduma kwa waumini na kusahau wanayoyafanya sirini wakati Yesu akiwatazama.

Mathayo 23:27 “Ole wenu, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mmefanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, nayo kwa nje yaonekana kuwa mazuri, bali ndani yamejaa mifupa ya wafu, na uchafu wote”.

7. Wako tayari kuwatukuza watumishi waliowatangulia kwa kujengea makaburi yao na kusahau kuiga matendo yao mema. Hawana tofauti na watu wanaoacha wazazi wao wafe na Kwashakoo (kukosa lishe) halafu kwenye mazishi wananunua majeneza ya kifahari na kujenga makaburi ya kifahari. 

Mathayo 23:29 “Ole wenu, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnayajenga makaburi ya manabii, na kuyapamba maziara ya wenye haki”.

 Hatutapona tusipoujali wakovu mkuu namna hii. Waebrania 2:3 “sisi je! Tutapataje kupona, tusipojali wokovu mkuu namna hii? Ambao kwanza ulinenwa na Bwana, kisha ukathibitika kwetu na wale waliosikia.” Unaweza kuwa hujaokoka na hujali kumpokea Yesu. Lakini pia unaweza kuwa umeokoka lakini hujali kuutunza wokovu wako – uko ndani (zizini) lakini uko uchi. Ufunuo wa Yohana 3:18 “Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.”

CHUKUA HATUA KADIRI MUNGU ALIVYOSEMA NA WEWE. KWA VILE NI KWA UPENDO WA MUNGU TU UMEFIKIWA NA UJUMBE HUU. MUNGU ANAKUPENDA SANA NA ANAKUWAZIA MEMA. MAISHA YETU SIO MAREFU SANA HAPA DUNIANI BALI TUNAUTAFUTA MJI WENYE MISINGI. Waebrania 13:14 “Maana hapa hatuna mji udumuo, bali twautafuta ule ujao.”